Afisa wa Serbia afumwa mshale nje ya ubalozi wa Israel
![Polisi huyo alimpiga risasi mshambuliaji huyo na kumuua baada ya kujeruhiwa shingoni](https://cdn.statically.io/img/ichef.bbci.co.uk/ace/ws/640/cpsprodpb/vivo/live/images/2024/6/29/539784ab-514b-470d-9624-d022df192643.jpg.webp)
Chanzo cha picha, Reuters
Afisa wa polisi wa Serbia amejeruhiwa katika shambulio la mshale nje ya ubalozi wa Israel mjini Belgrade.
Waziri wa Mambo ya Ndani Ivica Dacic aliwaambia waandishi wa habari kwamba afisa huyo alimpiga risasi na kumuua mshambuliaji.
Mshambuliaji huyo - ambaye bado hajatambuliwa na mamlaka - alimfuma polisi mshale shingoni, Bw Dacic alisema.
Afisa huyo amepelekwa hospitalini kufanyiwa upasuaji kutibu jeraha lake, na inasemekana yuko katika hali mbaya.
Shirika la utangazaji la Serbia B92 alimnukuu Bw Dacic akisema kwamba mshambuliaji alikaribia jengo dogo mbele ya ubalozi wa Israel mwendo wa 11:00 (09:00 GMT), akidaiwa kuuliza kuhusu jumba la makumbusho.
Mwanamume huyo alikuwa amefungua mlango wa jengo hilo dogo, akatoa upinde na na mshale na kumfuma afisa huyo, Bw Dacic aliripotiwa kusema.
Bw Dacic alisema tukio hilo linachunguzwa na waendesha mashtaka maalum na kwamba wengine kadhaa wamekamatwa kama hatua ya tahadhari.
Sio mara ya kwanza kwa mtu kujaribu kufanya shambulio kwenye ubalozi wa Israeli huko Belgrade tangu vita vya Gaza ambavyo Israeli ilianza baada ya shambulio la Hamas la 7 Oktoba kusini mwa Israel.