Kenya kukopa zaidi baada ya muswada wa fedha kugonga mwamba

Rais wa Kenya William Ruto anasema nchi italazimika kukopa zaidi ili kuendelea kuendesha serikali kufuatia kukataliwa kwa muswada wa fedha ambao haukupendwa na watu wengi ambao ungeongeza fedha zaidi za ushuru.

Muhtasari

  • Mrengo wa kulia wa Ufaransa washerehekea uongozi na sasa unatafuta wingi wa viti
  • Roketi ya China yaanguka baada ya kurushwa 'kwa bahati mbaya'
  • Wapalestina zaidi waliojeruhiwa waiambia BBC jeshi la Israel liliwalazimisha kuingia katika magari yao kikatili
  • BET 2024: Tyla ashinda tuzo ya Msanii Bora Mpya
  • Marekani kuipa kampuni ya ndege ya Boeing 'adhabu ndogo'
  • Washirika wanamtetea Biden huku kura ya maoni ikionyesha kuongezeka kwa wasiwasi kwa umri wake
  • Euro 2024: Uhispania na England zatinga robo fainali ya Euro
  • Serikali mpya ya muungano ya Afrika Kusini yatangazwa

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Yusuf Jumah

  1. Mamlaka nchini Kenya yakana taarifa kuwa askari wake wameuawa Haiti

    Askari

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mkuu wa huduma za polisi nchini Kenya amekana taarifa alizoziita za uongo, zisizo za kizalendo na zisizo za msingi zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa, askari wake wameuawa nchini Haiti.

    ''Tunapenda kuufafanulia Umma kuwa maafisa wetu waliondoka Kenya tarehe 24 mwezi Juni mwaka 2024 na si tu kuwa walikaribishwa kwa ukarimu na watu wa Haiti, lakini pia wako na tayari wako kwa ajili ya kutekeleza jukumu lao, Ilisema sehemu ya taarifa.

    ''Tunapenda kurejelea tena kuwa misheni yetu nchini Haiti ni kwa ajili ya raia wa Haiti, na tunapenda kuomba wakenya wenzetu kuwaunga mkono kwa kupeperusha juu bendera ya nchi yetu, sambamba na kutekeleza majukumu yao kimataifa. Ilisema taarifa hiyo.

    Unaweza kusoma;

  2. Usher ahutubia kwa hisia baada ya kupokea tuzo ya mafanikio BET

    Usher

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Usher alitoa hotuba ya hisia alipopokea tuzo ya mafanikio ya maisha yake katika Tuzo za BET siku ya Jumapili.

    Mwimbaji-mtunzi wa nyimbo aliwaambia watazamaji wakati akipokea tuzo hiyo kwamba "kufika hapa kwa hakika haikuwa rahisi, lakini imekuwa na thamani yake".

    Usher mwenye umri wa miaka 45 anafahamika zaidi kwa vibao vikiwemo Yeah! na You make me wanna.

    Usher pia alitwaa tuzo ya msanii bora wa R&B na hip-hop kwenye tamasha hilo.

    Alifungua hotuba kwa muda wa dakika 15 kwa kusema: "Tuzo hii ya mafanikio ya maisha, sijui, jamani, ni mapema sana kuipokea? Kwa sababu bado ninakimbia kama nilivyofanya nilipokuwa na umri wa miaka minane.”

    Mwimbaji aliendelea kuzungumza kuhusu baba yake kuacha familia yake alipokuwa mtoto. "Nilikuwa nikijaribu kuelewa jina hili ambalo mwanaume alinipa ambalo halikudumu kwa sababu hakunipenda," alisema. "Lazima uwe na moyo wa kusamehe ili kuelewa mitego na magumu ya kweli ya mtu mweusi Marekani na baba yangu, alikuwa zao la hilo."

    Pia alitafakari maana ya sasa kuwa baba mwenyewe. “Huu ni mwaka wa baba. Simama kwa ajili ya binti zako na watoto wako na uongoze," aliwaambia watazamaji katika ukumbi wa michezo wa Peacock huko Los Angeles. "Ni muhimu kuelewa kwamba baba ni muhimu sana.

    "Kwa akina baba wote usiku wa leo nyumbani au kwenye hadhira ningependa ninyi nyote msimame kwa sekunde mbili tu kwa ajili yangu.

    Wanaume kadhaa kwenye hadhira waliposimama, Usher alisema: "Hatuna nafasi ya kusema vya kutosha, kwa hivyo hii ni ya wanaume wote huko nje, majenerali wa watoto wao. na motisha kwa viongozi wetu weusi wa baadaye, vijana."

  3. Kenya kukopa zaidi baada ya muswada wa fedha kugonga mwamba

    Polisi wa Kenya wameshutumiwa kwa ukatili wakati wakiwakabili waandamanaji

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Kenya William Ruto anasema nchi italazimika kukopa zaidi ili kuendelea kuendesha serikali kufuatia kukataliwa kwa muswada wa fedha ambao haukupendwa na watu wengi ambao ungeongeza fedha zaidi za ushuru.

    Rais alisema ataondoa muswada huo wenye utata wa nyongeza ya ushuru Jumatano iliyopita baada ya maandamano mabaya ambayo yalisababisha sehemu ya jengo la bunge kuchomwa moto.

    Lakini Jumapili alisema kutupilia mbali mswada huo kumeirudisha nchi nyuma miaka miwili, kwani alieleza ugumu wa kutoweza kuongeza ushuru wa ziada huku ikikabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni.

    Alisema hii ina maana kwamba Kenya italazimika kukopa shilingi trilioni moja ($7.6bn; £6.1bn) "ili tu kuweza kuendesha serikali yetu".

    Hili ni ongezeko la 67% zaidi ya kilichokuwa kimepangwa. Lakini pia alisema anazingatia kubana matumizi katika serikali nzima, ikiwa ni pamoja na ofisi yake mwenyewe, na pia kupunguza mgao kwa idara ya mahakama na serikali za kaunti.

    Waandamanaji wengi walipinga kuongezwa kwa ushuru kwa kusema kuwa pesa za ziada zingepotea.

    Kulingana na rais, hatua zilizopendekezwa za ushuru zilikuwa sehemu ya juhudi za kupunguza mzigo wa deni wa zaidi ya $80bn (£63bn).

    Takribani 60% ya mapato yanayokusanywa nchini Kenya huenda kwenye kulipia deni. "Nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii kuiondoa Kenya kutoka kwenye mtego wa madeni... Ni rahisi kwetu, kama nchi, kusema: 'Hebu tukatae muswada wa fedha.' Ni sawa na nimesema tutaondoa muswada wa fedha, lakini itakuwa na madhara makubwa,” rais alisema alipokuwa akizungumza na wanahabari Jumapili usiku.

    Bw Ruto alisema kukataliwa kwa bajeti hiyo kutaathiri ajira kwa walimu 46,000 wa shule za msingi na sekondari ambao wamekuwa kwenye mikataba, pamoja na utoaji wa huduma za afya.

    Unaweza kusoma;

  4. Familia yamtaka Biden abaki katika mbio za kuingia Ikulu

    Biden akielekea Camp David mwishoni mwa juma

    Chanzo cha picha, Reuters

    Familia ya Rais wa chama cha Democratic Joe Biden imemtaka kupuuza wito wa kujiuzulu baada ya mjadala dhidi ya Donald Trump wa chama cha Republican.

    Jumapili alikaa na jamaa zake ambao walimtia moyo kuendelea kupigana, kulingana na mshirika wa BBC wa Marekani CBS News.

    Wasiwasi umekumba sehemu fulani za chama chake kufuatia kufanya vibaya kwenye mdahalo huko Atlanta. Kura za maoni tangu wakati huo zinaonesha wasiwasi kuhusu umri wake.

    Kura ya maoni ya CBS News/YouGov iliyotolewa Jumapili ilionesha kuwa 72% ya wapiga kura wa Democratic waliojiandikisha wanaamini kuwa rais hana afya nzuri ya akili ya kuhudumu nafasi ya urais

    Karibu nusu walisema anapaswa kujiondoa. Lakini ujumbe kutoka kwa timu yake ya kampeni na familia yake ni kwamba anasalia kuwa tumaini bora la chama kumshinda Trump.

    Mkutano wa familia, Camp David huko Maryland ulikuwa umeratibiwa hapo awali kama upigaji picha na mpiga picha mashuhuri Annie Leibovitz.

    Mkewe Bw Biden Jill, watoto wake na wajukuu walikuwa miongoni mwa waliohudhuria. Kutiwa moyo kwa familia hiyo kusalia kwenye mbio hizo kuliripotiwa kwanza na New York Times na baadaye kuthibitishwa na CBS News.

    Unaweza kusoma;

  5. Watu 24 wameuawa, 32 wametekwa nyara wakati wa maandamano ya Kenya: Amnesty International

    Askari na muandamanaji

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wakenya 24 wamethibitishwa kufariki dunia Jumapili usiku kutokana na ukatili wa polisi katika maandamano ya hivi majuzi nchini kote, shirika la Amnesty International limesema.

    Katika taarifa siku ya Jumatatu, shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilisema kuwa aliyepoteza maisha ni mtoto wa miaka kumi na miwili aliyetambulika kama Kennedy Onyango.

    Zaidi ya hayo, watu 361 wamejeruhiwa, 627 wamekamatwa na utekaji nyara 32 uliofanywa tangu mwanzo wa harakati za kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha 2024 na maandamano dhidi ya serikali mnamo Juni 18.

    "Kutekwa nyara na kuwekwa kizuizini kunatofautiana na kukamatwa. Wengi wa waliotekwa nyara na maafisa wa serikali hawakusomewa mashtaka dhidi yao au kupelekwa katika kituo cha polisi. Makumi wameshikiliwa kwa siri na kunyimwa fursa ya kuonana na familia zao, uwakilishi wa kisheria na msaada wa matibabu," Amnesty ilisema.

    Shirika hilo lililaani matumizi ya nguvu ya polisi kupita kiasi dhidi ya timu za dharura na waandishi wa habari.

    "Wahudumu wa afya wameshutumiwa, wakikamatwa na maafisa wa serikali na kuibiwa orodha zao za wagonjwa kutoka kwenye vituo vya dharura vilivyohudumia waliojeruhiwa.

    Mawakili wamenyimwa nafasi ya kuwafikia wateja wao, kukamatwa, na kutishwa na maafisa wa serikali kufuta kesi," Amnesty ilisema. "Waandishi wa habari wanaoripoti maandamano hayo wamenyang'anywa kamera zao, kukamatwa na kupigwa mchana kweupe.

    Aidha waliitaka serikali kuzingatia matakwa yaliyotolewa na vijana wa Kenya ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa wale waliozuiliwa na mamlaka ya polisi na kuwajibika katika utawala.

    Unaweza kusoma;

  6. Mrengo wa kulia wa Ufaransa washerehekea uongozi na sasa unatafuta wingi wa viti

    .

    Chanzo cha picha, REUTERS/Yves Herman

    Mrengo wa kulia nchini Ufaransa uko katika nafasi nzuri baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge ambao ulithibitisha kutawala kwao katika siasa za Ufaransa na kuwafikisha kwenye milango ya utawala.

    Wafuasi wa chama cha Marine Le Pen kinachopinga uhamiaji National Rally (RN) walishangilia aliposema "kambi ya rais ya ‘Macronist’ imefutiliwa mbali".

    RN ilipata 33.1% ya kura, na muungano wa mrengo wa kushoto nyuma ukiwa na 28%, na kambi ya Macron nyuma kwa 20.76%.

    "Ninalenga kuwa waziri mkuu kwa watu wote wa Ufaransa, ikiwa Wafaransa watatupa kura zao," kiongozi wa chama cha RN mwenye umri wa miaka 28 Jordan Bardella alisema.

    Haijawahi kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa wabunge wa Ufaransa. Ukweli rahisi kwamba imewezekana ni historia, anasema mtoa maoni mkongwe Alain Duhamel.

    Wanachotaka Marine Le Pen na Jordan Bardella ni wingi kamili wa viti 289 katika Bunge la Kitaifa lenye viti 577.

    Hata hivyo, makadirio ya viti kwa ajili ya duru ya pili Jumapili ijayo yanapendekeza kuwa huenda wakapungukiwa.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Roketi ya China yaanguka baada ya kurushwa kwa 'bahati mbaya'

    Maelezo ya video, Watch: China rocket crashes after 'accidental' launch

    Roketi ambayo ilirushwa kwa bahati mbaya baada ya kutenganishwa na safu yake ya kurushia ilianguka nchini China siku ya Jumapili.

    Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha roketi ya Tianlong-3 ikianguka tena Duniani na kulipuka kwenye mlima katikati mwa mkoa wa Henan nchini China.

    Kampuni inayohusika na roketi hiyo, Tianbing Technology ilisema kwamba roketi hiyo "ilivunjika" kutoka kwa sehemu ya kurushia roketi wakati wa majaribio ya ardhini.

    Imeongeza kuwa hakukuwa na majeruhi kutokana na tukio hilo kwani watu katika eneo hilo walikuwa wameondolewa.

    Tianlong-3 ni ya roketi ya Kichina iliyoundwa na kutengenezwa na inakusudiwa kuwa roketi inayoweza kutumika tena

    Pia unaweza kusoma:

  8. Wapalestina zaidi waliojeruhiwa waiambia BBC jeshi la Israel liliwalazimisha kuingia katika magari yao kikatili

    .

    Wanaume wawili wa Kipalestina, waliojeruhiwa wakati wa operesheni ya kijeshi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa wiki jana, wameiambia BBC kwamba wanajeshi wa Israel waliwalazimisha kuingia kwenye boneti ya jeep ya jeshi na kuwaendesha - wakati mwingine kwa kasi - kwenye barabara za vijijini.

    Maelezo hayo yanawadia siku chache baada ya video ya Mujahid Abadi Balas mwenye umri wa miaka 23 akining’inia kwenye boneti ya jeep hiyo hiyo ya jeshi la Israel kuzusha hasira kimataifa.

    BBC sasa imezungumza na wanaume wawili wanaodai kutendewa kama hivyo wakati wa operesheni huko Jabariyat, viungani mwa Jenin, Jumamosi iliyopita.

    Samir Dabaya mwenye umri wa miaka 25, ambaye sasa yuko hospitalini huko Jenin, anasema alipigwa risasi mgongoni na wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni ya Jabariyat, na alilala kifudifudi na kuvuja damu kwa saa nyingi, hadi wanajeshi walipokuja kumtathmini hali yake.

    Walipomgeuza na kukuta yu hai, alipigwa na bunduki, anasema kabla ya kuokotwa, akabebwa hadi kwenye gari aina ya jeep na kutupwa juu yake.

    “Walinivua [suruali]. Nilitaka kushikilia gari, lakini [mwanajeshi mmoja] alinigonga usoni na kuniambia nisifanye hivyo. Kisha akaanza kuendesha gari,” alisema. "Nilikuwa nikingojea kifo tu."

    Samir alituonyesha picha za video kutoka kwa kamera ya ulinzi ambayo inaonekana ikimuonyesha akiwa nusu uchi, akiwa amelala kwenye jeep ya mwendo kasi, ikiwa na alama ya namba 1 ubavuni.

    Mahali panaonekana kuendana na mahali ambapo operesheni hiyo ilifanyika, lakini hakuna tarehe au saa inayoonekana kwenye rekodi.

    Mwanaume mwingine wa Palestina, Hesham Isleit, pia aliiambia BBC kwamba alipigwa risasi mara mbili wakati wa operesheni huko Jabariyat na kulazimishwa kupanda kwenye jeep hiyo hiyo ya kijeshi, iliyokuwa na nambari 1.

    Alielezea "kupigwa risasi kutoka pande zote" na kusema alijaribu kukimbia lakini alipigwa risasi ya mguu, na kisha kikosi cha jeshi kilifika kumchukua yeye na mtu mwingine.

    "Walituamuru tusimame, na wakatuvua nguo," alisema, "kisha wakalazimisha tupande mbele ya jeep."

    Gari lilikuwa moto sana, lilihisi "kama moto", anasema.

    “Nilikuwa peku na bila nguo. Nilijaribu kuweka mkono wangu kwenye jeep lakini sikuweza, ilikuwa inawaka moto. Nilikuwa nikiwaambia liko moto sana, na lakini wakinilazimisha kupanda - wakiniambia kwamba ikiwa sitaki kufa, nifanye hivyo."

    Tulitoa madai haya kwa jeshi la Israel; likasema kesi hizo zinaendelea kuchunguzwa.

    Soma zaidi:

    Maelezo ya video, CCTV inaonyesha Mpalestina Samir Dabaya aliyevaa nusu uchi kwenye jeep ya Israel
  9. BET 2024: Tyla ashinda tuzo ya Msanii Bora Mpya

    ,

    Chanzo cha picha, Epic / Fax Records

    Mwimbaji wa Afrika Kusini Tyla alitajwa kuwa Msanii Bora Mpya katika Tuzo za BET 2024, na hivyo kuashiria mafanikio makubwa katika kazi yake inayokua.

    Tyla anayejulikana kwa miondoko yake ya pop, amevutia haraka mioyo ya mashabiki kote ulimwenguni.

    Wimbo wake wa kwanza, "Water," ulivuma sana, ukionyesha ndoano zake za kuvutia na mtindo wa maonyesho yake ya kusisimua.

    Mchanganyiko wa muziki wa Tyla unaohusisha pop, R&B na Afrobeat umekuja na utofauti katika ulingo wa muziki.

    Katika hotuba yake, Tyla alitoa shukrani kwa mashabiki wake, familia, na jumuiya ya BET.

    “Jamani hii sasa imezidi, na ni kubwa sana..."Ni kitu cha pekee kuwa hapa... Nataka kuitoa tuzo hii kwa ajili ya Afrika. Nataka kuidhamiria zawadi hii kwa nyota wote wa Kiafrika kabla yangu ambao hawakupata fursa hizi ninazopata. Hii inapendeza sana. Kutoka Afrika hadi kwa ulimwengu.”

    Ushindi wa Tyla kama Msanii Bora Mpya unadhihirisha kipaji chake cha kipekee na mvuto wa kimataifa wa muziki wake. Mafanikio yake yanaashiria mustakabali mzuri na kuendelea kufanya vizuri katika tasnia ya muziki.

  10. Marekani kuipa kampuni ya ndege ya Boeing 'adhabu ndogo' - Mwanasheria

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wakili anayewakilisha waathiriwa wa ajali mbili mbaya za ndege aina ya Boeing 737 Max ameambia BBC kwamba serikali ya Marekani inapanga kuipa kampuni hiyo "adhabu ndogo".

    Paul Cassell, ambaye anasema alipata taarifa "moja kwa moja kutoka kwa Wizara ya Sheria", aliongeza kuwa mpango huo unajumuisha faini ndogo, miaka mitatu ya kuchunguzwa tabia na ukaguzi huru wa usalama.

    Boeing haikujibu mara moja ombi la BBC la kutoa maoni yake, huku Wizara ya Sheria ikikataa kutoa taarifa.

    Wiki iliyopita, waendesha mashtaka wa Marekani walipendekeza kwamba Wizara ya Sheria ifungue mashtaka ya jinai dhidi ya mtengenezaji huyo wa ndege.

    Hiyo ilikuwa baada ya wizara hiyo kusema kampuni ya Boeing ilikiuka suluhu la mwaka 2021 kuhusiana na ajali ambazo ziliua watu 346.

    "Kumbukumbu ya watu 346 wasio na hatia waliouawa na ndege aina ya Boeing inadai haki zaidi kuliko hii," alisema Bw Cassell, akiongeza kuwa "familia zitapinga vikali adhabu hii".

    Ajali za ndege hiyo - zote zikihusisha ndege aina ya Boeing 737 Max - zilitokea ndani ya miezi sita ya kila mmoja.

    Ajali iliyohusisha Lion Air ya Indonesia ilitokea Oktoba 2018, ikifuatiwa na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia iliyotokea Machi 2019.

    Soma zaidi:

  11. Washirika wanamtetea Biden huku kura ya maoni ikionyesha kuongezeka kwa wasiwasi kwa umri wake

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kura mpya ya maoni inapendekeza kwamba baadhi ya wapiga kura wa chama cha Democratic wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu iwapo Joe Biden yuko sawa kiakili kuhudumu kama rais baada ya kuyumba kwenye mjadala siku ya Alhamisi.

    Kura ya maoni ya CBS News/YouGov iliyotolewa Jumapili ilionyesha kuwa 72% ya wapiga kura waliojiandikisha wanaamini kuwa Biden hana uwezo wa afya ya kiakili ya kuhudumu kama rais - ongezeko kubwa kutoka 65% kwa waliokuwa na maoni kama hayo katika kura ya maoni ya awali.

    Asilimia 49 ya wapiga kura walikuwa na maoni kama hayo kwa Rais wa zamani Donald Trump.

    Hasa jambo la kutia hofu kwa kampeni ya Biden, 45% ya Wanademokrasia waliojiandikisha ambao walijibu kura hiyo walisema wanaamini kuwa rais anapaswa kujiondoa na mgombea mwingine kuchukua nafasi yake.

    Bw Biden ana miaka 81 na Trump ana miaka 78. Sauti ya kishindo ya Bw Biden na majibu ya kutatanisha, hata hivyo, yalizua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya Wanademokrasia kuhusu kugombea kwake na kuwaacha wengine wakitaka Bw Biden ajiondoe kwenye ugombeaji.

    Familia ya rais ilimtia moyo kusalia katika kinyang'anyiro hicho wakati wa ziara iliyopangwa kwa muda mrefu huko Camp David siku ya Jumapili, chanzo chenye kufahamu mazungumzo hayo kilithibitishwa na CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani.

    Bado, mbunge wa Maryland, Jamie Raskin ambaye pia ni mshirika wa Democrat na White House, alielezea mahojiano yake kama "wakati mgumu".

    Raskin alisema kuna "mazungumzo ya ukweli na mazito yanayofanyika katika kila ngazi ya chama chetu", ingawa alisisitiza kuwa uamuzi wa mwisho unasalia kuwa wa Bw Biden.

    "Licha ya uamuzi wowote utakaochukuliwa na Biden, chama chetu kitakuwa na umoja na pia kinamhitaji katikati mwa mijadala yetu katika kampeni," aliongeza.

    Soma zaidi:

  12. Euro 2024: Uhispania na England zatinga robo fainali ya Euro

    th

    Chanzo cha picha, REX FEATURES

    Maelezo ya picha, Nico Williams aliisaidia Uhispania kushinda mechi zao zote za kundi kwenye Euro 2024 - timu pekee iliyosonga mbele ikiwa na rekodi ya 100%.

    Uhispania walitinga hatua ya robo fainali na wenyeji wa michuano ya Euro 2024 Ujerumani kwa kunusurika na hofu ya mapema ya kuondolewa na Georgia baada ya kwa kupata ushindi wa maao 4-1.

    Wakicheza katika mchuano wao wa kwanza muhimu, Georgia ililazimika kupata presha kubwa kutoka kwa Uhispania mapema lakini ikawashangaza wengi katika Uwanja wa Cologne walipopata uongozi wa kushtukiza baada ya dakika 18.

    Beki wa Uhispania Robin le Normand alichombeza krosi ya Otar Kakabadze kwenye lango lake, akimalizia shambulizi la kushtukiza na kuwanyamazisha mashabiki nyuma ya lango lao.

    Wachezaji wa akiba waliokuwa wakipasha misuli motowalimkimbilia Khvicha Kvaratskhelia, ambaye aliongoza sherehe za Georgia kwenye kona.

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jude Bellingham alionyesha kipaji cha kipekee baada ya kuiokoa England kwa kuwabakiza katika katika Euro 2024 baada ya hofu ya kuyaaga mashindano hayo alipofunga bao ambalo liliwapa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Slovakia kwa mtindo wa ajabu na kutinga hatua ya nane bora.

    England walikuwa wamesalia sekunde chache kuyaaga mashindano hayo huku Slovakia wakilinda bao lao la kuongoza ambalo walikuwa wameshikilia tangu dakika ya 25 pale Ivan Schranz alipoingia kwenye eneo la hatari na kumshinda kipa wa Uingereza Jordan Pickford.

    Hapo ndipo Bellingham, ambaye alisherehekea siku yake ya kuzaliwa ya mwaka wa 21 siku ya Jumamosi, alionyesha umahiri wake ambao umemfanya kuwa supastaa mpya wa England kwa kupaa angani katika eneo la hatari kuusuka vyema mpira wa kichwa wa Marc Guehi kumpita Martin Dubravka kwa kiki ya ajabu .

    Unaweza pia kusoma

  13. Serikali mpya ya muungano ya Afrika Kusini yatangazwa

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza serikali mpya ya mseto, baada ya chama chake tawala cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wa wabunge katika uchaguzi wa mwezi Mei.

    Alisema "serikali ya umoja wa kitaifa... haijawahi kutokea katika historia ya demokrasia yetu".

    Chama cha ANC kitakuwa na nyadhifa 20 kati ya 32 za baraza la mawaziri, huku chama cha Democratic Alliance (DA) - hadi sasa chama kikuu cha upinzani - kitashikilia nyadhifa sita. Nyingine sita zitagawanywa kati ya vyama vidogo.

    Kupungua kwa uungwaji mkono wa chama cha ANC katika uchaguzi kulionyesha kufadhaika kwa umma juu ya rekodi yake mbaya ya kutoa huduma za kimsingi na kukabiliana na ukosefu wa ajira, umaskini na ufisadi.

    ANC chini ya Nelson Mandela ilifanikisha lengo lake la kukomesha utawala wa wazungu walio wachache nchini Afrika Kusini mwaka 1994, na imekuwa ikitawala nchi hiyo peke yake.

    Katika baraza jipya la mawaziri, ANC itashikilia wizara muhimu kama vile ulinzi, fedha na mambo ya nje.

    Huku chama cha DA kikishikilia nyadhifa kama wizara ya mambo ya ndani na ujenzi. Kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen ataongoza wizara ya kilimo.

    Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni siku ya Jumapili, Bw Ramaphosa alisema: "Serikali inayokuja itaweka kipaumbele ukuaji wa uchumi wa haraka na endelevu, na upatikanaji wa jamii yenye kuzingatia haki zaidi."

    ANC ilikaribisha hatua hiyo kama "hatua muhimu kusonga mbele, na ushahidi wa uthabiti wa demokrasia yetu".

    Wakati huo huo, DA ilisema "ni fahari kukabiliana na changamoto hiyo na kuchukua nafasi yetu, kwa mara ya kwanza, kuingia katika serikali ya kitaifa".

    Pia iliahidi "utawala bora, kutovumilia kabisa rushwa na utungaji sera kwa vitendo".

    Hata hivyo, licha ya makubaliano ya muungano wa baraza la mawaziri, malumbano makali ya kisiasa yameendelea kushuhudiwa kati ya vyama vya ANC na DA.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ikiwa ni tarehe 01/07/2024