Kim Jong Un: Mambo 5 ambayo hatuyajui kumhusu Kiongozi wa Korea Kaskazini

Kim Jong Un with a crowd of young female admirers behind him

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Inafikiriwa kuwa siku ya kuzaliwa ya Kim Jong Un ni tarehe 8 Januari - lakini je ni kweli? Na atakuwa na umri wa miaka mingapi?

Na Issariya Praithongyaem

Kim Jong Un wa Korea Kaskazini anatimiza umri wa miaka 40. Lakini ni kweli?

Siku ya kuzaliwa ya Kiongozi Mkuu inaaminika sana kuwa Januari 8, lakini wengi hawakubaliani kuhusu tarehe yake kamili ya kuzaliwa.

Na hili sio fumbo pekee kuhusu Kim - haya ni maswali matano ambayo hayajajibiwa kuhusu dikteta wa Korea Kaskazini aliyeingia madarakani mwaka 2011.

1. Kim Jong Un alizaliwa lini?

Hatujui kwa hakika.

"Kuna mijadala mingi kuhusu mwaka aliozaliwa, ikiwa ni 1982, 1983 au 1984," Dk Edward Howell, mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Oxford, aliambia BBC.

Siku yake ya kuzaliwa inayodhaniwa kuwa tarehe 8 Januari ni siku ya kawaida ya kufanya kazi katika nchi ya Kikomunisti, ambapo siku ya kuzaliwa ya babake Kim Jong Il huadhimishwa tarehe 16 Februari kila mwaka kama Siku ya Nyota Ing'aayo.

Siku ya kuzaliwa ya babu yake Kim Il Sung tarehe 15 Aprili pia imeainishwa kama Siku ya Jua.

Maelezo mengi ya familia yake pana yamembwa kwa siri, hata hivyo.

Mtaalamu wa Korea Kaskazini Dk Howell anasema kuwa tunajua Kim ana ndugu wa kambo, mmoja wao - Kim Jong Nam - aliuawa nchini Malaysia mwaka wa 2017.

Babake Kim Jong Un alidhaniwa kuwa na takribani wapenzi wanne tofauti - lakini mahusiano yake mara nyingi yaliwekwa nje ya macho ya umma.

Mama yake, Ko Young Hui, anafikiriwa kuwa alizaliwa Japani, alikuja Korea Kaskazini katika miaka ya 1960 kufanya kazi kama dansi.

Alisemekana kuwa kipenzi cha wake wote wa Kim Jong Il.

Mnamo 2018, picha za Ko Young Hui, zilizopigwa alipotembelea Japani mnamo 1973, zilipatikana.

Gazeti la Korea Times liliripoti kwamba Korea Kaskazini haijatangaza sana kuhusu Ko kwa sababu ya kazi yake kama densi na historia ya familia inayohusishwa na Japan.

"Kuzaliwa katika Japani, ambayo ilikuwa imechukua peninsula ya Korea wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, kwa kawaida ingemshusha mtu kwenye tabaka la chini la kijamii. Lakini kwa sababu aliolewa na Kim Jong Il, alikuwa na maisha ya anasa,” anasema Dk Howell.

2. Mke wa Kim Jong Un ni nani?

Ri Sol Ju and Kim Jong Un

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Habari zinasema kuwa Bw Kim huenda alimwona Ri Sol Ju kwenye maonyesho ya muziki

Tena, hatuna uhakika. Tunajua kuwa ana mke, Ri Sol Ju, lakini hatuna uhakika ni lini walifunga ndoa (kuna uvumi kwamba hii inaweza kuwa ilitokea mnamo 2009).

Machache yanajulikana kuhusu "Comrade Ri Sol Ju". Je, alikuwa mwimbaji wa zamani ambaye alivutia umakini wa Bw Kim wakati wa onyesho?

Kuna mwigizaji wa Korea Kaskazini kwa jina kama hilo, lakini haijawahi kuthibitishwa rasmi kuwa wao ni mtu mmoja.

Mbunge mmoja, akiwanukuu maafisa wa ujasusi, alisema wanaamini Ri Sol Ju alitembelea Korea Kusini mwaka wa 2005 kama sehemu ya timu ya ushangiliaji ya mashindano ya riadha ya Asia, na alisomea uimbaji nchini China.

Korea Kaskazini haijatoa maelezo yoyote zaidi ya kusema yeye ni mke wa Bw Kim.

3. Kim Jong Un ana watoto wangapi?

Kim Jong Un and Kim Ju Ae

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kim Jong Un ameonekana hadharani na Kim Ju Ae, lakini pia ana watoto wengine na ni machache sana yanayojulikana kuwahusu

Hapa tuna maelezo mengine ya familia ambayo ni vigumu kujua.

Uvumi kwamba Ri Sol Ju alikuwa mjamzito ulianza mnamo 2016 baada ya kutoweka kutoka kwa macho ya umma, lakini haujawahi kuthibitishwa rasmi.

Watoto wawili wa awali wanaaminika kuwa walizaliwa mwaka wa 2010 na 2013, lakini haijulikani ikiwa kuna wa kiume na kwa hivyo wanaweza kuwa mrithi. Kwa kweli, kuna machache ambayo tunajua kuwahusu.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini ameonekana hadharani na bintiye, Kim Ju Ae, anayeaminika kuwa mtoto wa pili kwa umri wa karibu miaka 10 na ndiye tunayemfahamu zaidi - alijitokeza hadharani angalau mara tano mnamo 2023.

"Bado hatujui hadithi kamili ya watoto wake," Dk Howell anaelezea, na kutukumbusha kwamba alikuwa nyota wa zamani wa mpira wa kikapu wa Marekani Dennis Rodman, rafiki wa karibu sana wa Kim Jong Un, ambaye alifichua jina la binti huyo katika 2013 mahojiano.

"Ana watoto wengine lakini machache sana yanajulikana kuwahusu. Hatujui mama zao ni akina nani," mtaalam wa Korea Kaskazini anaongeza.

Kinyume na wachambuzi wengi (na kwa hakika shirika la kijasusi la Korea Kusini), Dk Howell haamini kwamba Kim Ju Ae anaandaliwa kuwa kiongozi ajaye.

Bado ni mdogo, na dadake Kim Jong Un mwenye ushawishi mkubwa, Kim Yo Jong, ana uzoefu zaidi na uhusiano bora na viongozi wengine ambayo inaweza kumfanya awe mgombea zaidi wa kumrithi kaka yake.

"Kiongozi wa Korea Kaskazini anaonekana akiwa na binti yake mdogo wakati wa kurusha makombora, kwenye karamu au kwenye michezo ya kandanda kwa sababu anataka kuonekana kama mtu wa familia na kiongozi mkarimu," Dk Howell anaamini.

4. Je, Kim Jong Un anawezaje kuishi maisha ya anasa ikiwa nchi ni maskini sana?

Kim Jong Un

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Korea Kaskazini mara nyingi hutumia njia za kifahari za usafiri

Korea Kaskazini na kiongozi wake wamekabiliwa na vikwazo vikali vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi kwa miaka mingi kwa sababu ya utengenezaji wa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki.

Lakini Dk Howell anasema kwamba Kim Jong Un anafanya kila awezalo kukwepa vikwazo.

"Nchi ina hazina ambayo imeundwa mahsusi kwa matumizi ya serikali. Kim anataka kuendelea na haya kwani anataka yeye na familia yake waendelee kuwa na maisha ya anasa.”

Kuna mitandao ya nchi kote ulimwenguni ambayo iko tayari kuipatia Korea Kaskazini pesa, Dk Howell anaamini, na kuna madai kuwa inaweza pia kuja kwa fedha kwa njia zingine.

"Watu mara nyingi hufikiria kuwa Korea Kaskazini ni nchi iliyotengwa ambayo haina mtandao. Ina mtandao unaoendeshwa na serikali, na vita vya mtandao vimekuwa mkakati muhimu: Utawala wa Kim unadukua mifumo ya kompyuta ya nchi nyingine ili kuiba pesa za kuendesha uchumi wake na mpango wa nyuklia," Dk Howell anadai.

5. Je, Kim Jong Un anajali watu wake?

North Korean leader Kim Jong Un attends an event with students to celebrate the new year in Pyongyang

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wakosoaji wanasema mtindo wa maisha wa kiongozi huyo wa Korea Kaskazini unakinzana na tabia yake ya kujali umma

Hotuba kwenye gwaride la kijeshi mnamo 2020 ilituonyesha upande tofauti wa Kiongozi Mkuu.

Aliwashukuru wanajeshi wake kwa juhudi zao dhidi ya janga hili na majanga ya asili ya hivi karibuni. Wakati fulani, alifuta machozi alipokuwa akizungumzia mapambano ya nchi hiyo. Ilikuwa ni onyesho la nadra la hisia kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini.

Baadhi ya waangalizi wamedokeza kwamba huenda anajaribu kuonyesha unyenyekevu hata wakati nchi hiyo inakabiliwa na mzozo wa kiuchumi unaozidi kuongezeka.

Walakini, uchunguzi wa maisha ya kifahari ya kiongozi wa Korea Kaskazini unaonyesha kinyume.

Kim Jong Un anaendelea na desturi ya kusafiri umbali mrefu kupitia treni za kifahari, iliyoanzishwa na Kim II Sung - babu yake.

Kamanda wa jeshi la Urusi ambaye aliandamana na Kim Jong Il - babake Kim Jong Un- kwenye safari ya 2001 alizungumza juu ya utajiri wake katika kumbukumbu yake Orient Express.

"Iliwezekana kuagiza sahani yoyote ya vyakula vya Kirusi, Kichina, Kikorea, Kijapani na Kifaransa," aliandika. Samaki hai aina ya Kamba na mivinyo ya kifahari ya Bordeaux na Burgundy pia zilisafirishwa kwa ndege kutoka Paris.

Hii na aina nyingine za usafiri wa kifahari zikiwemo ndege za kibinafsi zinatofautisha sana maisha duni ya watu wa Korea Kaskazini.

Watu nchini Korea Kaskazini wameambia BBC kwamba chakula ni adimu sana majirani zao wamekufa kwa njaa. Wataalamu wanasema hali ni mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu miaka ya 1990.

Je, hii inasema nini kuhusu vipaumbele vya Kim?

"Anataka tu kuhifadhi sio tu utawala wake lakini uongozi wake mwenyewe dhalimu . Inaonekana hajali kuhusu watu milioni 26 nchini mwake, "anasema Dk Howell.

"Je, anafikiri huu ni mkakati mzuri wa kusonga mbele?"

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah