Je, bosi wa akili mnemba (AI) atakuwa bora zaidi kuliko bosi binadamu?

dfc

Chanzo cha picha, Hannu Rauma

Maelezo ya picha, Hannu Rauma anasema kutumia akili mnemba kumemsaidia katika kusimamia wafanyakazi wake
  • Author, MaryLou Costa
  • Nafasi, BBC

Hannu Rauma, ni meneja katika kampuni inayoitwa Student Marketing Agency, Vancouver, Canada, huajiri wanafunzi wa vyuo vikuu ili kutoa msaada wa masoko kwa biashara ndogo ndogo.

Novemba mwaka jana, kampuni hiyo ilianza kutumia meneja anayejiendesha kwa akili mnemba, aliyetengenezwa na kampuni ya Inspira yenye makao yake makuu nchini Marekani.

Akili mnemba huwasaidia wafanyikazi, wanaofanya kazi kwa saa tofauti wakiwa nyumbani, kuweka ratiba zao na kupanga majukumu yao ya kazi mapema.

Hufuatilia ratiba zao, huwakumbusha kuhusu makataa, na kuwatumia jumbe fupi, na kurekodi muda wanaotumia kwa wateja tofauti, ili waweze kutoza bili kwa usahihi.

Akili mnemba pia hutoa mapendekezo ya kuboresha maneno ya maandishi yaliyoandikwa, kujibu maswali yanayohusiana na kazi, na kuboresha maendeleo ya kazi ya kila mtu.

Pia unaweza kusoma

Mafaniko katika utafiti

xc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dell ni kampuni ambayo imepunguza wafanyakazi kwa kuongezeka matumizi ya akili mnemba

Rauma anasema mabadiliko ya kutumia meneja wa akili mnemba hayajapunguza tu kiwango cha hamkani, lakini yamewezesha wafanyikazi wake kufanya kazi haraka na kuwa na tija zaidi.

Rauma anaongeza kuwa uhusiano wake na wafanyikazi wake pia umeboreka sana. "Hapo awali, ulikuwa kama uhusiano wa baba na mtoto. Sasa, ni kama tuko usawa. Hapo awali, ilikuwa ni kutatua tu shida. Lakini sasa tunaweza kuwa na majadiliano zaidi.”

Rauma na wafanyakazi wake 26 kati ya 83 walikuwa sehemu ya utafiti ulioendeshwa na Inspira na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Columbia, Chuo Kikuu cha Jimbo la Arizona, na Chuo Kikuu cha Wisconsin kulinganisha utendajikazi wa meneja wa akili mnemba na wenzao wa kibinadamu.

Washiriki waligawanywa katika vikundi vitatu: kikundi kimoja, kilisimamiwa na meneja wa kibinadamu, chingine na meneja wa akili mnemba, na kundi la mwisho, likasimamiwa na meneja wa akili mnemba na meneja wa kibinadamu.

Meneja wa akili mnemba alipata kiwango cha mafanikio cha 44% katika kuwafanya wafanyakazi kupanga mapema siku zao za kazi, na aliweza kuwahamasisha wafanyakazi kuingia kwenye akaunti zao kwa 42% ya wakati. Takwimu hizi zililinganishwa na meneja wa kibinadamu, ambaye alipata alama za 45% na 44% kwa maeneo hayo mawili.

Meneja wa akili mnemba alipofanya kazi kwa ushirikiano na meneja wa kibinadamu, kwa pamoja walipata kiwango cha mafanikio cha 72% katika kuwafanya wafanyakazi kupanga mapema siku zao za kazi, na waliweza kufikia 46% ya ufanisi katika suala la wakati.

Licha ya utafiti kuwa mdogo kitakwimu, na unaozingatia aina maalumu ya wafanyakazi na uwanja wa kazi, matokeo yake yanavutia kwa kampuni zinazoanzisha zana za akili mnemba.

Akili mnemba isimamie kila kitu?

Prof wa masuala ya uongozi, Paul Thurman, kutoka Chuo Kikuu cha Columbia huko New York, anasema kubadilishana kabisa majukumu ya usimamizi kwa akili mnemba, litakuwa ni kosa.

"Tabaka la uongozi wa kati ndio safu muhimu zaidi katika shirika lolote. Ndio safu ambayo, ikianza kuanguka, uko kwenye hali mbaya. Watu wako wa chini hawaoni mwendelezo, hawapati ushauri na mafunzo. Mambo yote ambayo wasimamizi wa kibinadamu wanayafanya bora zaidi kuliko akili mnemba, yanapaswa kuachwa hivyo."

Prof Thurman anaongeza, akili mnemba inaweza kuwakumbusha wafanyakazi, ili kuzingatia njia za kibunifu zaidi za kufanya kazi. Kwa mfano, wasimamizi wanaweza kuchagua timu na mradi, na kisha kuiacha akili mnemba isimamie makataa.

Akili mbemba inaweza pia kutambua ni nani kwenye timu bado yuko nyuma na anahitaji kusimamiwa kwa karibu zaidi na binadamu.

"Lakini makampuni yanapaswa kujiepusha kutumia akili mnemba kama chombo cha uchunguzi," anasema.

"Isifikie hatua ya kuchunguza kwamba wafanyakazi wanachukua muda mwingi wakati wa chakula cha mchana, na hawali saladi ya kutosha. Isiende mbali hivyo,” anasema Prof Thurman. "Tumia njia sahihi kuhimiza tabia zinazofaa."

“Akili mnemba pia inaweza kuwasaidia watu ambao wamekuwa mameneja kwa bahati mbaya, watu wanaofanya vyema katika majukumu yao na hatimaye wanajikuta wanasimamia watu wengine, licha ya suala la usimamizi kutokuwa sehemu ya ujuzi wao kiasili,” anasema Tina Rahman, mwanzilishi wa ofisi ya ushauri kuhusu rasilimali watu, HR Habitat, London.

"Tulifanya utafiti uliangalia sababu za watu kuacha kazi. Takribani 100% ya waliohojiwa walisema ni kwa sababu ya usimamizi mbaya."

"Baadhi yao walisema hawakupenda jinsi walivyosimamiwa, na wengi walisema ni kwa sababu hawakujua ni nini kilitarajiwa kutoka kwao au ikiwa walikuwa wakifanya kazi nzuri," anasema Bi Rahman.

"Unadhani meneja wa akili mnemba ataundwa kutoa maagizo sahihi, kutoa uwazi juu ya mahitaji na matokeo. Watu ni bora zaidi kuliko akili mnemba, ikiwa watajua kile kinachohitajiwa kutoka kwao.”

“Kuegemea kupita kiasi katika usimamizi wa akili mnemba, ni dalili kwamba makampuni yanajali tu matokeo na si watu,” anasema Bi Rahman.

"Itakuwa vigumu kwa makampuni kuwaambia wafanyikazi wao, tunaleta mfumo huu mpya wa akili mnemba ambao utawasimamia kwa kila kitu, kisha useme hapo hapo, 'tunajali uzoefu wako wa kazi," anasema.

sx

Chanzo cha picha, James Bore

Maelezo ya picha, James Bore

“Wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya akili mnemba, sio kuhusu mtazamo wa watu, bali ni suala la usalama wa mtandao,” anasema James Bore, mwandishi na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya ushauri kuhusu usalama mtandaoni, Bores.

"Ikiwa una meneja wa akili mnemba, na umempa taarifa zote za kampuni, na ghafla meneja huyo amedukuliwa na kutekwa nyara, atashikiliwa hadi ulipe fidia,” anasema Bore.

"Ikiwa utaitegemea sana akili mnemba, na zikachukua nafasi ya wanadamu na kisha akili mnemba ikakwama, utakuwa huna chaguo la kurudi kwa wanadamu, kwa sababu hunao tena."

Badala ya makampuni kutafuta ufanisi zaidi kupitia matumizi makubwa ya akili mnemba, Bore anasema kunaweza kuwa na matokeo mabaya zaidi katika kutegemea mifumo ambayo inaweza kushindwa.

"Kadiri unavyotumia akili mnemba, na kadiri unavyoondoa watu kwenye biashara yako, ndio, utapunguza gharama. Lakini utazidi kuifanya kampuni yako iingiliwe zaidi.”

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah