Vita vya Ukraine: Marekani yatuma kwa siri makombora ya masafa marefu kusaidia Kyiv

Na Kathryn Armstrong ,

BBC News

th

Chanzo cha picha, Reuters

Ukraine imeanza kutumia makombora ya masafa marefu yaliyotolewa kwa siri na Marekani dhidi ya Urusi, maafisa wa Marekani wamethibitisha.

Silaha hizo zilikuwa sehemu ya msaada wa $300m (£240m) ulioidhinishwa na Rais wa Marekani Joe Biden mwezi Machi na ziliwasili mwezi huu.

Tayari zimetumika angalau mara moja kulenga shabaha za Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea, ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinasema.

Bwana Biden sasa ametia saini kifurushi kipya cha msaada cha $61bn kwa Ukraine.

Hapo awali Marekani iliipatia Ukraine toleo la masafa ya kati la Mifumo ya silaha za Makombora (ATACMS) lakini ilikuwa ikisita kutuma kitu chochote chenye nguvu zaidi, kwa sababu ya wasiwasi wa kuhatarisha utayari wa kijeshi wa Marekani.

Hata hivyo, Bw Biden anasemekana kuidhinisha kwa siri kutuma mfumo wa masafa marefu - ambao unaweza kurusha makombora umbali wa hadi 300km (maili 186) - mnamo Februari.

"Naweza kuthibitisha kwamba Marekani iliipatia Ukraine ATACMS ya masafa marefu kwa maelekezo ya moja kwa moja ya rais," msemaji wa idara ya serikali Vedant Patel alisema.

Unaweza Pia Kusoma

Marekani "haikutangaza hili mwanzoni ili kudumisha usalama wa oparesheni za vita nchini Ukraine kwa ombi lao", aliongeza.

Haijabainika ni silaha ngapi ambazo tayari zimetumwa, lakini Mshauri wa Usalama wa Kitaifa wa Marekani Jake Sullivan alisema Washington inapanga kutuma zaidi.

"Zitaleta mabadiliko. Lakini kama nilivyosema hapo awali kwenye jukwaa hili... njia rahisi," alisema.

Makombora hayo ya masafa marefu yalitumiwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita kushambulia uwanja wa ndege wa Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea, shirika la habari la Reuters lilimnukuu afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutajwa jina akisema.

Na makombora hayo mapya pia yalitumiwa katika shambulio dhidi ya wanajeshi wa Urusi katika mji wa bandari wa Berdyansk unaokaliwa usiku wa kuamkia Jumanne, kulingana na New York Times.

Miezi ya hivi karibuni imeshuhudia Kyiv ikiongeza wito wake wa kutaka usaidizi wa nchi za Magharibi huku akiba yake ya risasi ikipungua na Urusi ikipata mafanikio ya kutosha.

Kifurushi kipya cha msaada kinafuatia miezi kadhaa ya kukwama huku kukiwa na upinzani wa msaada kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Congress.

"Itafanya Amerika kuwa salama zaidi, itafanya ulimwengu kuwa salama," Bw Biden alisema baada ya kutia saini kuwa sheria.

Akijibu maswali kuhusu kifurushi hicho, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema: "Sasa tutafanya kila kitu kufidia nusu mwaka iliyotumika katika mijadala na mashaka.

"Kile Urusi inachoweza kufanya wakati huu, anachopanga Putin sasa, lazima tumpinge."

Bw Zelensky hivi majuzi alionya kwamba mashambulizi ya Urusi yanatarajiwa katika wiki zijazo baada ya Ukraine kupoteza mji wa Avdiivka wakati wa majira ya baridi.

Vikosi vya Ukraine vimekumbwa na uhaba wa risasi na mifumo ya ulinzi wa anga katika miezi ya hivi karibuni na maafisa wamelaumu kucheleweshwa kwa msaada wa kijeshi kutoka kwa Marekani na washirika wengine wa Magharibi kwa kupoteza maisha na sehemu ya nchi yao.

Bw Sullivan alisema siku ya Jumatano "inawezekana kwa hakika kwamba Urusi inaweza kupata mafanikio zaidi katika wiki zijazo".

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine tarehe 24 Februari 2022, makumi ya maelfu ya watu, wengi wao wakiwa wanajeshi, wameuawa au kujeruhiwa kwa pande zote mbili na mamilioni ya watu wamekimbia makazi yao.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah