Urusi na Korea Kaskazini: kwa nini Putin na Kim wanaimarisha uhusiano wao?

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Urusi na Korea Kaskazini kwa sasa wanapitia mapenzi makubwa ambayo hayajawahi kutokea tangu Vita Baridi, wakati ambao utawala wa Kim una mshirika muhimu katika Umoja wa Kisovieti.

Rais wa Urusi Vladimir Putin aliapa "kupanua uhusiano wa kina na wenye kujenga kwa pande zote" katika barua ya hivi mkaribuni kwa mwenzake wa Korea Kaskazini Kim Jong-un.

Alijibu kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeongezeka"hadi kiwango cha juu" katika hali ya pamoja dhidi ya "vikosi vya uadui."

Viongozi wote wawili walipiga muhuri urafiki wao katika mkutano wa kihistoria mnamo 2019 huko Vladivostok (mashariki mwa Urusi) na tangu wakati huo Kim ameonyesha wazi kuunga mkono Moscow katika mzozo wowote unaomhusu.

MIKHAIL SVETLOV

Chanzo cha picha, MIKHAIL SVETLOV

Maelezo ya picha, Ishara za uaminifu za Korea Kaskazini kwa mshirika wake zimeongezeka katika uvamizi wa Ukraine: Julai ilikuwa nchi ya tatu kutambua jamhuri za Donetsk na Luhansk chini ya udhibiti wa Urusi kama nchi huru.

Kim pia amekuwa mwepesi kuisifu Urusi na rais wake, ambao ajenda zao za kisiasa zinachukua nafasi zaidi na zaidi katika vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini.

Nchi mbili zilizounganishwa na historia

"Uhusiano kati ya Pyongyang na Moscow ulizorota sana baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti. Kutokana na msingi huo sasa unaboreka," mwanachuoni Samuel Wells, kutoka Kituo cha Wilson huko Washington DC, anaelezea.

Uhusiano kati ya Pyongyang na Moscow ulianza tangu kuanzishwa kwa Korea Kaskazini mnamo 1948.

Baada ya Vita vya Dunia vya Pili, serikali ya Joseph Stalin iliunda na kumleta madarakani Kim Il-sung, babu wa kiongozi wa sasa, ambaye alisaidia kujenga mfumo unaofanana na ule wa USSR na sifa maalum za tamaduni na mila ya Kikorea.

Moscow iliunga mkono mshirika wake dhidi ya Kusini katika Vita vya Korea (1950-53) na katika miongo iliyofuata ilikuwa, pamoja na China, mfuasi wa serikali ya Kim, ambayo ilifadhili kwa rasilimali nyingi za kifedha na zana.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kim Il-sung alipata mafunzo katika Umoja wa Kisovieti kwa miaka kadhaa kabla ya kuanzisha Korea Kaskazini mnamo 1948.

"Wakati wa Vita Baridi, Kim Il-sung aliweza kudumisha usawa katika uhusiano wake na Beijing na Moscow, akiwa rafiki mzuri wa wote wawili bila kuegemea mmoja na kujaribu kufaidika na uadui kati ya mataifa hayo mawili baada ya kuingia madarakani kwa Khruschev (1953)," anasema Andrés Sánchez Braun, mwandishi wa wakala wa Efe nchini Korea.

Hata hivyo, kati ya washirika hao wawili ni Muungano wa Kisovieti uliotoa msaada mkubwa zaidi kwa Korea Kaskazini, kuanzia chakula au mafuta, mashine na mafunzo ya kiufundi, hata kufikia kutoa ruzuku ya uagizaji wa bidhaa za Korea Kaskazini ambazo hazikuwa na manufaa kwake. .

Mkakati wa Kim Jong-un

Lakini kila kitu kilibadilika baada ya kufutwa kwa kambi ya ujamaa mnamo 1991.

Kwanza na Boris Yeltsin na kisha Vladimir Putin mkuu wa Urusi mpya ya kibepari, uhusiano ulibaki baridi kiasi na Korea Kaskazini, ambayo sasa ilikuwa na China kama mshirika wake pekee mwenye nguvu.

Majaribio ya nyuklia na makombora yaliweka kando zaidi utawala wa Korea Kaskazini na Urusi, ambayo haikusita kuidhinisha vikwazo vikali zaidi ilivyowekewa Pyongyang mwaka 2017 kwa majaribio yake ya nyuklia na makombora ya masafa marefu.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Korea Kaskazini ina safu kubwa ya makombora ya kujitengenezea yenyewe, ikiwa ni pamoja na Taepodong 2, ambayo safu yake inakadiriwa kuwa kilomita elfu kadhaa na ni jambo linalotia wasiwasi katika jumuiya ya kimataifa.

"Korea Kaskazini ilikuwa ikifanya majaribio ya silaha za atomiki, makombora yalizidi kuwa makubwa, na wakati huo Urusi, ambayo haitaki wanachama zaidi katika klabu ya nchi zenye uwezo wa nyuklia, haikunufaika na hilo," anaelezea Sánchez Braun.

Vikwazo viliwekwa ili kuukandamiza kiuchumi utawala wa Kim kwa kuzuia biashara zake nyingi, karibu zote na China.

Na janga la mlipuko limeongeza kutengwa kwa serikali. Kim Jong-un alifunga kabisa mipaka, akizuia mtiririko wa pembejeo muhimu kwa uendeshaji wa kisekta katika nchi hiyo ili kuokoa wakazi wake takriban milioni 25.

"Korea Kaskazini inataka kuwa na Urusi upande wake. Kwa kuwa uchumi wake umesimama kwa miaka miwili, haihitaji kutegemea Beijing pekee bali pia Moscow, kwani zote mbili ni kitu cha karibu zaidi na washirika walio nao," anasema.

"Hii ndiyo sababu Kim Jong-un amechukua mkakati wa babu yake: kuweka mchezo wa usawa kati ya mamlaka ambazo anazitegemea."

Faida kwa ajili ya kitu fulani

Wote Kim Jong-un na Vladimir Putin wanatumai kufaidika na urafiki wao mpya. Lakini ni kwa namna gani? Wataalam wako wazi juu ya kile ambacho Urusi inaweza kuchangia Korea Kaskazini: mtiririko mkubwa wa mafuta na chakula ambayo inaruhusu nchi ya kikomunisti kupunguza mgogoro wake na kwa kiwango kidogo, mashine za viwandani, sehemu, silaha au vifaa vingine.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Barabara tupu za Pyongyang mwezi Mei mwaka jana zinaonyesha kutengwa kwa utawala wa Korea Kaskazini, ambao umepitisha mkakati wa kufunga mpaka kabisa.

Na Pyongyang, licha ya hali yake tete ya kiuchumi, pia ina mambo kadhaa ya kutoa.

"Korea Kaskazini tayari inaipatia Urusi msaada wa kidiplomasia katika Umoja wa Mataifa na maelfu ya watendaji wanaofanya kazi nchini Urusi. Inaweza kutoa wafanyakazi zaidi na pia madini adimu," Wells anasema.

Vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vya 2017 vinakataza kuajiriwa kwa wafanyikazi wa Korea Kaskazini, kwa sehemu kwa sababu ya hali ya unyanyasaji wanayopewa, na masaa mengi ya kazi na mishahara yao mingi uchukuliwa naserikali.

Hata hivyo, mashirika kadhaa yanakadiria kuwa baadhi ya Wakorea Kaskazini 20,000 wanafanya kazi katika maeneo ya mbali ya Urusi kinyume na vikwazo ambavyo nchi hiyo yenyewe iliidhinisha miaka mitano iliyopita. Zoezi hili linahakikisha manufaa ya pande zote, anasema Sergey Radchenko, mwanahistoria wa Vita Baridi katika Shule ya Johns Hopkins

"Urusi inapokea wafanyakazi wenye uwezo mkubwa na wa bei nafuu, na kwa Korea Kaskazini wao ni chanzo muhimu cha fedha za kigeni."

Ushawishi wa vita huko Ukraine

Uvamizi wa Ukraine, kulingana na wachambuzi wengi, umeimarisha muungano kati ya Moscow na Pyongyang.

"Korea Kaskazini ina historia ya kuwadanganya wabia na washirika wake. Katika kesi hii, Kim Jong-un, akiwa anafahamu kutengwa kwa Urusi (kutokana na vikwazo vya kimataifa baada ya uvamizi), alichukua fursa hiyo kuikumbatia Urusi," Radchenko anaelezea.

ggg

Chanzo cha picha, API

Balozi wa Urusi mjini Pyongyang, Alexander Matsegora, hivi karibuni alidai kwamba Kim Jong-un anaweza kuwatuma wafanyakazi kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na vita katika jamhuri zinazojiita za Donetsk na Luhansk mashariki mwa Ukraine.

Aliongeza kuwa Korea Kaskazini ina nia ya kupatia vipuri vya enzi ya Usovieti kwa ajili ya mashine nzito ambazo bado zinatengenezwa katika miji ya mashariki mwa Ukraine, kama vile Sloyansk na Kramatorsk, ambayo bado inashikiliwa na vikosi vya Kyiv.

Kwa upande mwingine, mwandishi wa habari anayeunga mkono Kremlin Igor Korotchenko alihakikisha mapema Agosti kwamba Korea Kaskazini ilipanga kutuma wanajeshi 100,000 kupigana upande wa Urusi katika vita vya Ukraine.

Hakuna serikali kati ya hizo mbili iliyotoa uamuzi juu ya uwezekano huu, huku wataalam wakitilia shaka.

"Sidhani Korea Kaskazini inaweza au itatuma wanajeshi Ukraine. Ni jambo ambalo hawajawahi kufanya," Wells anasema.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Korea Kaskazini, ambayo inatumia takriban theluthi moja ya bajeti yake katika ulinzi, ina moja ya majeshi makubwa zaidi duniani yenye wanajeshi milioni 1.2. Hata hivyo, haijawahi kutuma wanajeshi kupigana nje ya nchi.

"Urusi ni wazi inahitaji wanajeshi zaidi, lakini mafunzo kwa Wakorea Kaskazini yangechukua muda mrefu na Kim Jong-un anaweza kupinga kwa kuhofia wanajeshi wake wangeweza kutoroka," Radchenko alisema.

Kuhusu usafirishaji wa silaha kwenda Urusi, moja ya rasilimali chache ambazo sio haba nchini Korea Kaskazini, Sánchez Braun anaamini kwamba "Pyongyang haitatoa sehemu ya safu yake ya ushambuliaji kwa Moscow, kwa sababu inaihitaji kufanya mazungumzo kwa mustakhabali wa baadaye au kuhakikisha usalama wao wenyewe.

Mwanahabari huyo anaangazia jambo lingine, lisiloonekana sana lakini muhimu vile vile, ambalo Kim Jong-un anaweza kumpa Putin wakati huu: ukosefu wa utulivu wa kijiografia

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tofauti na mwaka 2017, mwaka huu Urusi ilikataa kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vipya kwa majaribio yake ya hivi punde ya makombora. Ishara hiyo ni ushahidi mwingine wa kukua kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

"Korea Kaskazini inachangia kukosekana kwa utulivu wa kikanda na tofauti na miaka michache iliyopita, sasa hakuna kitu ambacho Moscow inaweza kupenda zaidi ya hilo," anasema. "Kwamba Pyongyang ina silaha zaidi na zaidi, kwamba inaongeza kelele ya vitisho vyake na kwamba kuendelea kufanya majaribio ya makombora ni maumivu ya kichwa kwa Marekani wakati huu ambao inataka kuzingatia mzozo wa Ukraine, lakini pia Taiwan na Mashariki ya Kati".

Majibu ya China

Mshirika mkuu wa Korea Kaskazini bado ni China, nchi ambayo ilichangia zaidi ya 90% ya biashara yake ya nje mnamo 2019, mwaka mmoja kabla ya mipaka kufungwa kwa sababu ya janga la mlipuko la corona, kwa mujibu wa Observatory of Economic Complexity (OEC).

China inaiona Korea Kaskazini kama kingo muhimu katika eneo lake la kaskazini-mashariki, ambalo linaitenganisha na eneo la Korea Kusini, ambako Marekani ina kambi za kijeshi na takriban wanajeshi 28,000. Kadiri Korea Kaskazini inavyoitegemea zaidi China kiuchumi, ndivyo ushawishi mkubwa wa kisiasa ambao taifa hilo kubwa la Asia linao juu ya mshirika wake mdogo.

Na mara nyingi Beijing hutumia ushawishi huo kuzuia kadiri inavyowezekana hasira kali za utawala wa Kim, ambaye vitisho vyake, majaribio ya nyuklia na makombora huvutia uwepo wa kijeshi na operesheni zaidi kutoka Korea Kusini na Marekani katika eneo hilo.

ggg

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa China Xi Jinping anathamini thamani ya kijiografia ya Korea Kaskazini, lakini hafurahii kukosekana kwa utulivu katika eneo hilo.

Kwa hivyo, Radchenko anaamini kwamba "Wachina hawatafurahi" ikiwa mapenzi kati ya Pyongyang na Moscow yataongezeka.

"Siku zote wanaangalia kwa mashaka Urusi kuingilia Korea Kaskazini, na wanaelewa kuwa uboreshaji wowote katika uhusiano wao utampa Kim Jong-un faida zaidi dhidi ya China." Wells anafikiria kwa njia hiyo hiyo: "Ikiwa uhusiano unakuwa karibu zaidi, Beijing inaweza kuwasilisha kutoridhika kwa viongozi wake kidiplomasia na kwa kuchelewesha usambazaji wa chakula na nishati."