Korea Kaskazini yaonesha makombora yake ya masafa marefu

Kim Ju-ae akiangalia gwaride na Kim Jong-un

Chanzo cha picha, Reuters

Korea Kaskazini imeonesha onyesho lake kubwa zaidi kuwahi kutokea la makombora ya masafa marefu (ICBMs), idadi ambayo wachambuzi wanasema inaweza kuleta changamoto katika mfumo wa ulinzi wa Marekani.

Takribani dazeni za ICBM za masafa marefu zilioneshwa kwenye gwaride la kijeshi la Jumatano.

Kiongozi Kim Jong-un alionekana kwenye gwaride la usiku wa manane akiwa na bintiye mdogo.

Kuonekana kwa Kim Ju-ae kumechochea uvumi kwamba anapewa nafasi ya mrithi.

Idadi ya makombora ya masafa marefu iliyooneshwa kwenye gwaride hilo imezua wasiwasi. Wachambuzi wanasema idadi kama hiyo ya makombora - ambayo kwa nadharia inaweza kugonga hadi Marekani.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini havikutoa maelezo zaidi, lakini vilisema kwamba silaha kama hizo zilionesha "uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi na kushambulia".

Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Korea Kaskazini Alhamisi asubuhi zilionekana kuonyesha zaidi ya dazeni za ICBM zikipita katikati ya uwanja wa Pyongyang - zikiwa zimeambatana na jeshi la ardhini.

Virusha makombora vilivyoonyeshwa kwenye gwaride

Chanzo cha picha, Reuters

Baadhi ya wachambuzi wa Korea Kaskazini walisema kuwa onyesho hilo pia lilijumuisha kombora la ICBM.

Makombora ya mafuta imara yanaweza kurushwa kwa haraka zaidi.

Hata hivyo, utawala wa Kim haujawahi kufanyia majaribio makombora ya masafa marefu ya mafuta.

"Hili ni mojawapo ya malengo makuu ya Korea Kaskazini ya kuboresha nyuklia," alisema Ankit Panda, mtaalamu wa sera za nyuklia katika Shirika la Carnegie Endowment for International Peace.

"Tunapaswa kutarajia kuona majaribio ya kwanza ya ndege ya makombora ya masafa marefu ya mafuta katika miezi ijayo," aliiambia BBC.

Aliongeza upanuzi wa ghala la silaha la ICBM la Korea Kaskazini uliwasilisha uwezekano wa "changamoto kubwa za mipango ya kijeshi" kwa Marekani katika mzozo, kwani itakuwa vigumu kwa Marekani kupata na kuharibu ICBM zote za Korea Kaskazini.

Gwaride hilo linakuja baada ya mwaka wa rekodi wa majaribio ya kombora na Korea Kaskazini kukiuka vikwazo vya kiuchumi vya Umoja wa Mataifa. Hilo limesababisha kuzuka kwa mivutano kadhaa kwenye peninsula ya Korea.

Shirika la Habari la Korea liliripoti gwaride hilo lilisisitiza uwezo wa nchi hiyo kuwakabili maadui zake "nuke kwa nuke, makabiliano kwa makabiliano".

Picha zilizochapishwa zilionesha Bw Kim akiwa amevalia koti jeusi akikagua safu za wanajeshi walioshika bayoneti, na kutoa saluti huku wanajeshi na vitengo vya makombora vikipita.

Pia alipigwa picha akitazama gwaride kutoka roshani na Ju-ae kando yake.

Kuinuliwa kwa Ju-ae - ambaye anaaminika kuwa na umri wa miaka 10 - imekuwa jambo jingine muhimu la kuzungumziwa na waangalizi.

Kim Ju-ae akiwa na baba yake Kim Jong-un na mama Ri Sol Ju kwenye karamu

Chanzo cha picha, Reuters

Picha za vyombo vya habari vya serikali zilimuonesha akisimama katika karamu ya kabla ya gwaride na viongozi wa kijeshi, ambapo alikuwa ameketi katikati kati ya Bw Kim na mkewe Ri Sol Ju, sehemu ambayo kwa kawaida hupewa baba yake.

Watatu hao walipigwa picha wakitabasamu na pembeni yao wakiwa na makamanda wakuu wa kijeshi. Bi Ri pia alionekana akiwa amevalia mkufu wenye kidani chenye umbo la Hwasong-17 ICBM, kombora kubwa zaidi la Korea Kaskazini ambalo lilifanyiwa majaribio mwaka jana.

Huku wachambuzi wengine wakisema kuwa Ju-ae ndiye mrithi wa Bw Kim, wengine wanasema kuwa serikali hiyo huenda inamuonesha kiongozi huyo wa Korea Kaskazini kama "mtu wa familia".

"Kujumuishwa kwa bintiye Kim katika karamu ilikuwa jambo ambalo halikwepeki. Waeneza propaganda wa serikali ya Korea Kaskazini wanajaribu kuonesha Kim Jong-un kama mtu wa familia, lakini kutengwa kwa binti yake mwingine aliyeripotiwa ni jambo la kushangaza," alisema Martyn Williams, mwandamizi katika Kituo cha Stimson anayeangazia Korea Kaskazini.

Kim Jong-un anaripotiwa kuwa na takribani watoto watatu, akiwemo mtoto wa kiume mkubwa na binti mdogo. Ju-ae anaaminika kuwa mtoto wake wa pili.

Alionekana hadharani kwa mara ya kwanza miezi mitatu iliyopita mnamo Novemba, wakati baba yake alipompeleka kwenye uzinduzi mkubwa wa ICBM.

Ingawa nafasi ya urithi inaweza kuwa hivyo, ni "mapema sana" kufikia hitimisho, Bw Williams aliiambia BBC.

Bw Panda alisema umaarufu wa Ju-ae katika miezi ya hivi karibuni unaweza kuashiria kwamba Kim anatarajia biashara ya nyuklia ya nchi yake kuwa jambo la vizazi vingi.