Je, Urusi inatafuta silaha za aina gani Korea Kaskazini?

fg

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Vladimir Putin na Kim Jong-un, walipokutana 2019

Vladimir Putin na Kim Jong-un wana mengi yanayofanana. Wote hawatembei sana. Kiongozi wa Kremlin hajaondoka Urusi mwaka sasa. Kwa upande wa Kim, imepita miaka minne bila kusafiri.

Wote wawili wako chini ya vikwazo vizito vya kimataifa. Urusi na Korea Kaskazini zimekuwa zikishutumiwa kuwa ni mataifa hatari. Serikali zote mbili zinakosoa ukuu wa Marekani.

Adui anaweza kuleta viongozi pamoja, na ndivyo inavyotokea kwa Putin na Kim. Ndoa yao sio ya mbinguni, imekuja kutokana na hali halisi ya mazingira ya kisiasa ya 2023.

Tofauti na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ambaye aliwahi kutangaza kwamba yeye na Kim Jong-un ni marafiki. Viongozi wa Urusi na Korea Kaskazini hawaoyeshi kupendana kwao hadharani. Lakini wanaona faida zinazowezekana katika uhusiano wao wa karibu.

Faida Gani?

Kremlin inafaidika nini kutokana na ukaribu huu? Kwa kuanzia, Korea Kaskazini ina sekta kubwa ya ulinzi yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji. Wakati vita vya Urusi nchini Ukraine vikiendelea, Pyongyang inaweza kuwa chanzo muhimu cha silaha kwa Moscow.

Washington inashuku mazungumzo ya silaha kati ya Urusi na Korea Kaskazini yamekuwa yakiendelea na Urusi inaripotiwa kutafuta silaha na mizinga.

Hakuna uthibitisho kutoka kwa maafisa wa Urusi. Lakini kuna ishara nyingi zisizo wazi kwamba Urusi na Korea Kaskazini zinakusudia kuongeza ushirikiano wa kijeshi.

Julai, Sergei Shoigu – alikuwa Waziri wa Ulinzi wa kwanza wa Urusi kutembelea Korea Kaskazini tangu kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti, alipohudhuria hafla za kuadhimisha miaka 70 ya uwekezaji wa silaha wa Korea.

Kim Jong-un aliigiza kama mwongoza watalii wakati akimwonyesha Shoigu maonyesho ya silaha. Waziri wa Ulinzi pia alidokeza kuwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi yanatayarishwa.

"Kwa maoni yangu, ikiwa wanatafuta silaha huko Korea Kaskazini, moja ya nchi masikini na iliyotengwa, huku ni kudhalilika kwa nguvu za Urusi," anasema Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Urusi, Andrei Kozyrev.

Kozyrev alizungumza na BBC kupitia simu ya video kutoka Marekani, ambako anaishi kwa sasa.

"Nchi kubwa haiwezi kwenda Korea Kaskazini kutafuta mshirika au vifaa vya kijeshi," aliongeza.

Vikwazo

Ushirikiano wa kijeshi na Korea Kaskazini unaweza kuwa ishara nyingine ya Urusi ya kujaribu kupindua ushawishi wa Kimagharibi. Mkataba wa silaha kati ya Moscow na Pyongyang unaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Hadi hivi karibuni, Urusi ilikuwa inaunga mkono vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Pyongyang kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia. Miongoni mwa mambo mengine, vikwazo hivyo vinakataza biashara ya silaha na Korea Kaskazini.

"Moscow ilikuwa imetia saini maazimio hayo ya Baraza la Usalama,"gazeti la udaku la Urusi Moskovsky Komsomolets liliwakumbusha wasomaji wake wiki iliyopita. "Haijalishi. Saini inaweza kubatilishwa."

Gazeti hilo lilimnukuu mwenyekiti wa Baraza la Sera za Kigeni na Ulinzi la Urusi, Fyodor Lukyanov, akisema: "Swali limeulizwa kwa muda mrefu: kwa nini sisi [Urusi] tunatii vikwazo hivyo? Mfumo mzima wa uhusiano wa kimataifa uko katika hali ya sintofahamu."

"Kwa kweli, vikwazo vya Umoja wa Mataifa ni halali. Ni vigumu kukataa. Tulivipigia kura. Lakini hali imebadilika. Kwa nini tusifute kura yetu?"

Pamoja milele?

gf

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha vikwazo dhidi ya Korea ya Kaskazini na Urusi ikaunga mkono vikwazo hivyo.

Korea Kaskazini inatarajia nini kutoka Urusi? Hakika ni msaada wa kibinadamu ambao utasaidia kupunguza uhaba wa chakula katika ardhi ya Korea Kaskazini.

Pia kuna uvumi kwamba Pyongyang imekuwa ikitafuta teknolojia ya hali ya juu ya Urusi kwa satelaiti na matumizi ya kijeshi, zikiwemo nyambizi zinazotumia nyuklia.

Zaidi ya mwaka mmoja na nusu katika vita ambavyo Urusi imefanya vibaya sana, Moscow inaweza kuhitaji kujaza akiba yake ya silaha. Makubaliano na Pyongyang inaweza kuwa njia ya kusaidia kufanikisha hili.

Lakini hilo halimaanishi kwamba, bila ya msaada wa Korea Kaskazini, vita vya Urusi vinakaribia kusimama.

"Putin hajakata tamaa," anasema waziri wa zamani Andrei Kozyrev:

"Anaweza kuendeleza vita kwa muda mrefu na anaweza kubadilika. Anajifunza kila siku jinsi ya kukwepa vikwazo, jinsi ya kushirikiana na China, Korea Kaskazini na baadhi ya serikali za Afrika. Huo si mbadala kwa siku zijazo. Lakini ni mpango mbadala kwa wakati huu."