Utafiti: Usingizi wa mchana ni mzuri kwa ubongo

mtu

Chanzo cha picha, Getty Images

Kupata muda wa kulala kidogo mara kwa mara ni vizuri kwa ubongo wetu na husaidia kuuweka ubongo kuwa mkubwa kwa muda mrefu, wanasema watafiti wa Chuo Kikuu cha London.

Watafiti hao wamebaini kuwa ubongo wa watu wanaopata muda kidogo wa kualala ulikuwa na sentimita za ujazo wa 15 sawa na inchi 0.9 na hali hiyo pia inachelewesha kuzeeka kwa kati ya miaka mitatu na sita.

Lakini, wanasayansi wanapendekeza kulala kwa chini ya nusu saa.

Wameongeza kuwa kwa wale wanaofanya kazi mchana, usingizi wao ni wa nadra sana kutokana na kubanwa na kazi nyingi, huku utamaduni wa kufanya kazi mara nyingi ukipinga suala zima la kulala mchana maeneo ya kazini.

"Tunapendekeza kwamba kila mtu anaweza kupata faida fulani kutokana na kulala," Daktari Victoria Garfield anasema. Alielezea matokeo hayo kama "riwaya kabisa na ya kusisimua kabisa".

Kulala usingizi kumeonekana kuwa muhimu kwa maendeleo ya ukuaji hasa kipindi cha utoto, na hali hiyo hupungua kwa kasi kubwa kwenye utu uzima sana kisha kupata umaarufu tena baada ya kustaafu, huku asilimia 27 ya watu walio na umri wa zaidi ya miaka 65 wakiripoti kupata usingizi wakati wa mchana.

Daktari Garfield anasema ushauri wa kulala usingizi ni "jambo rahisi sana" kwa kulinganisha na kupunguza uzito au mazoezi ambayo "ni kazi ngumu na hatua kubwa kwa watu wengi".

Ubongo kwa kawaida hupungua kwa umri, lakini ikiwa unapata usingizi unaweza kusaidia kuzuia magonjwa kama vile Alzheimers tatizo linalomfanya mtu kutoshiriki katika mazungumzo kwa muda mrefu, japo utafiti zaidi bado unahitajika.

Kwa ujumla afya ya ubongo ni muhimu kwa ajili ya kukulinda dhidi ya shida ya akili na hali hiyo inahusishwa na usingizi usio na wasiwasi.

Watafiti wanapendekeza kuwa tabia ya kutolala kwa wakati kunaathiri afya ya ubongo kwa kuathiri miunganisho kati ya seli za ubongo.

"Kwa hivyo, kulala mara kwa mara kunaweza kusaidia kukulinda dhidi ya kuzorota kwa mfumo wa neva kwa kufidia usingizi duni," mtafiti Valentina Paz alisema.

Hata hivyo, Daktari Garfield huwa hapendi sana kutafuta eneo zuri la kukalala mchana akiwa kazini lakini badala yake huwa anatumia njia mbadala za kutunza ubongo wake.

"Kusema kweli, ningependa kutumia dakika 30 kufanya mazoezi kuliko kulala, labda nitajaribu na kupendekeza kwamba mama yangu afanye hivyo."

Jinsi ya kupata jibu?

Kusoma somo la usingizi kunaweza kuwa changamoto.

Kulala kunaweza kuimarisha afya, lakini kinyume chake pia ni kweli kwani afya yako inaweza kukuacha umechoka sana unahitaji kulala zaidi.

Kwa hivyo watafiti walitumia mbinu ya busara ili kudhibitisha kuwa kulala kuna faida.

Walitumia jaribio kubwa la asili kulingana na vinasaba vya kanuni ya maumbile ambayo tunazaliwa nayo. Tafiti za awali zimebainisha vijisehemu 97 vya vinasaba yetu ambavyo vinatufanya tuwe na uwezekano mkubwa wa kuwa walala hoi au kuwa na nguvu siku nzima.

Kwa hivyo watafiti hao walichukua data kutoka kwa watu 35,000, wenye umri wa miaka 40 hadi 69, walioshiriki katika mradi wa Biobank wa Uingereza na kulinganisha kwa urahisi wale wanaolala na wale "wasiolala".

Matokeo, yaliyochapishwa katika jarida la Afya ya Kulala, yalionyesha tofauti ya sentimita 15 za ujazo sawa na miaka 2.6 hadi 6.5 ya uzee. Jumla ya ujazo wa ubongo ulikuwa takriban sentimita 1,480 za ujazo katika utafiti.

"Ninafurahiya kulala kwa muda mfupi wikendi na utafiti huu umenishawishi kwamba nisijisikie mvivu wa kulala, huenda hata unalinda ubongo wangu," Prof Tara Spires-Jones, kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh na rais wa British Neuroscience. Anasema

Alisema utafiti wa "kuvutia" wa matokeo ulionyesha "ongezeko ndogo lakini kubwa la ujazo wa ubongo" na "kuongeza kwa data inayoonyesha kuwa kulala ni muhimu kwa afya ya ubongo".

Watafiti hawakusoma moja kwa moja kuwa na usingizi mkubwa katikati ya mchana, lakini walisema sayansi ilielekeza kukatwa kwa nusu saa.