Watu watano waliopishana na Putin na hatima zao

SQ

Chanzo cha picha, TASS

Maelezo ya picha, Yevgeny Prigozhin
  • Author, Rashid Abdallah
  • Nafasi, BBC Swahili

Watawala kuwashughulikia wapinzani au wakosoaji sio jambo geni kwa serikali nyingi ulimwenguni, ingawa ugumu unakuja kwenye kuthibitisha kwamba mkuu fulani wa serikali ndio amehusika na mabaya yanayowakumba wakosoaji wake.

Vifo vyenye harufu ya mkono wa serikali mara nyingi vinakuwa na utata, wahusika wa mauaji hawajulikani na hubaki kuwa kitendawili cha milele kisicho na mteguaji. Matukio ya aina hii hufunikwa na taarifa za kushuku hapa na pale.

Yevgeny Prigozhin, mshirika wa muda mrefu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi anasemekana kuaga dunia katika ajali ya ndege. Bado kifo chake hakijathibitishwa, kwa sababu miili ni ya waliopata ajali imeungua vibaya na panahitajika vipimo vya vinasaba ili kuthibitisha mwili wake ni miongoni mwa maiti zilizopatikana.

Prigozhin mkuu wa Wagner kwa muda mrefu amekuwa swahiba wa Putin, uswahiba huo ulizidi kukuwa baada ya kumsaidia katika vita vyake nchini Ukraine. Lakini ghafla mambo yaligeuka baada ya Prigozhin kufanya uasi wa muda mfupi dhidi ya maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Urusi.

Hadithi ni ndefu, lakini Prigozhin alisitisha uasi huo. Na kwa hakika hapo ndipo urafiki wake na Putin ukaingia doa. Ikiwa Prigozhin ameaga dunia: Je, kifo chake ni ajali ya kawaida? Ama utawala wa Putin unahusika? Au wale aliowapiga kule Ukraine wamelipiza? Haya ni maswali ambayo – jawabu ya uhakika inahitaji muda na subra.

Lakini wapo watu wengine ambao walipishana na utawala wa Putin na hatima zao hazikuwa nzuri. Wengine waliponea chupuchupu kuuwawa na baadhi hawakuweza kukwepa mitego ya wale waliodhamiria kuwandoa duniani:

Boris Nemtsov

fewd

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Boris Nemtsov

Katika miaka ya 1990, Boris Nemtsov alikuwa nyota wa kisiasa wa Urusi ya baada Soviet. Akawa naibu waziri mkuu na baadaye alionekana kama anaweza kuwa rais - lakini Putin ndiye alirithi kiti cha urais 2000 kutoka kwa Boris Yeltsin.

Nemtsov akawa mwanasiasi wa kuukosoa utawala wa Putin. Aliongoza mikutano mikubwa ya mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa 2011 na aliandika ripoti kuhusu ufisadi.

Alikamatwa mara kadhaa wakati Kremlin ilipokandamiza mikutano ya upinzani. Februari 2015, saa chache baada ya kuwataka watu kujiunga na maandamano dhidi ya ushiriki wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine, Nemtsov alipigwa risasi nne mgongoni na mshambuliaji asiyejulikana karibu na Kremlin. Muuaji hajajulikana hadi leo.

Alexander Litvinenko

WEDCSX

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Alexander Litvinenko

Afisa wa zamani wa ujasusi wa Urusi aliyegeuka kuwa mwasi, Alexander Litvinenko, alikufa kifo cha polepole na cha uchungu katika hospitali ya London 2006 baada ya kuwekewa sumu ya Polonium-210.

Uchunguzi wa Uingereza uligundua kuwa Litvinenko alilishwa sumu na maafisa wa shirika la kijasusi la Urusi la FSB, Andrei Lugovoi na Dmitry Kovtun. Moscow ilikanusha kuhusika lakini ilikataa kuwasalimisha washukiwa wawili kwa ajili ya kesi.

Litvinenko alikuwa mkosoaji mkubwa wa Putin, akimshutumu kulipua jengo la ghorofa na kuamuru mauaji ya mwandishi wa habari Anna Politkovskaya.

Sergei Skripal

yhg

Chanzo cha picha, NEWS UK

Maelezo ya picha, Sergei Skripal na binti yake

Sergei Viktorovich Skripal ni afisa wa zamani wa intelijensia katika jeshi la Urusi aliekuwa akiitumikia pia idara ya ujasusi ya Uingereza katika miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000.

Mnamo mwaka 2018 yeye na binti yake Yulia waliponea kifo chupuchupu walipowekewa kemikali ya sumu inayoathiri mishipa ya fahamu huko Salisbury, Uingereza.

"Serikali baada ya Uchaguzi, imebaini kuwa Urusi ilihusika na tungependa tusikie kutoka kwao iwapo wana pingamizi yoyote," alisema Waziri Mkuu wa Uingereza wa wakati huo Theresa May.

Hata hivyo, Urusi imeendelea kukanusha madai ya kuhusika katika jaribio la kumuua jasusi huyo ambaye amepewa uraia nchini Uingereza.

Alexei Navalny

DW

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Alexei Navalny

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi Alexei Navalny alionekana kwa mara ya kwanza hadharani mwezi wa 9, 2020 baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya mjini Berlin, ambako alikuwa anatibiwa kutokana na sumu inayouwa mishipa ya fahamu.

Serikali ya Ujerumani ilisema vipimo vilivyofanywa nchini Ujerumani, Ufaransa na Sweden vimeonyesha kuwa alipewa sumu ya kemikali aina ya Novichok, ambayo inauwa mishipa ya fahamu.

Mpinzani na mkosoaji wa Rais Putin, alirejea Urusi na kwa sasa anatumikia kifungo jela katika kituo chenye ulinzi mkali huko Melekhovo, kilomita 250 mashariki mwa Moscow.

Boris Berezovsky

trgfdb

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha, Boris Berezovsky

Afisa wa zamani wa serikali na mfanyabiashara; akiwa uhamishoni, Boris Berezovsky alikuwa mkosoaji wa serikali ya Urusi, hadi kufikia kufadhili upinzani dhidi Putin na kutaka kupinduliwa kwake kwa nguvu. Serikali ya Urusi mwaka 2003 iliomba arejeshwe nchini humo. Hata hivyo, alipewa hifadhi Uingereza.

2007 alishtakiwa bila kuwepo mahakamani na mahakama ya Urusi na kupatikana na hatia ya ubadhirifu. Kulingana na Alexander Litvinenko, afisa wa Shirika la Kijasusi la Urusi (FSB) huko London alikuwa akijiandaa kumuua Berezovsky Septemba 2003. Njama hiyo iliripotiwa kwa polisi wa Uingereza

Machi 23, 2013, Berezovsky alipatikana amekufa nyumbani kwake nchini Uingereza. Mwili wake ulikuwa na kamba shingoni.

Kwa hakika kuna orodha ndefu ya Warusi walioingia katika vuta nikuvute na serikali ya Rais Putin, na wengi wao wameishia kubaya. Wakati maswali yakizidi kuibuka kuhusu Prigozhin, historia inaonesha kwamba siku zote Putin ni mshika mpini huku wapinzani na wakosoaji wake wakijikuta makalini.