Bahari mpya itakayoigawa Afrika itaibuka mapema zaidi ya ilivyofikiriwa – Utafiti mpya

x

Chanzo cha picha, TEACHER. JR ROWLAND, UNIVERSITY OF AUCKLAND

Maelezo ya picha, Eneo la Afar, Ethiopia

Bahari mpya inaibuka barani Afrika, kulingana na utafiti mpya, ni mchakato ambao ulidhaniwa ungechukua kati ya miaka milioni 5 na 10, lakini utafiti mpya wa kisayansi unaonesha kuibuka huko kunaweza kutokea kwa kasi zaidi ya ilivyotarajiwa.

Cynthia Ebinger, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Tulane nchini Marekani na profesa wa jiolojia tangu miaka ya 1980, anasema "wakati bahari mpya ilipoanza kuibuka – ilitarajiwa kuchukua mamilioni ya miaka lakini sasa inaonekana itachukua chini ya hapo.’’

Kulingana na tovuti ya Google, Ebinger ameandika zaidi ya makala 16,000 katika majarida ya kisayansi na ndiye mtaalamu anayeaminika katika uwanja wa jiolojia na mazingira duniani.

Mwaka 2023, makala 17 zilichapishwa, zikieleza juu ya mkondo mpya wa bahari utakaoibuka katika eneo la Afar, Ethiopia ambalo liko kwenye mipaka ya nchi hiyo pamoja Eritrea na Djibouti.

Wanajiolojia wamesema bahari hiyo mpya itaonekana hasa katika nchi za Afrika Mashariki, na tafiti mbalimbali zimefanyika.

Tafiti zimechambua magma katika ardhi ya Ethiopia ambapo kulikuwa na mlipuko wa volkano uliodumu kwa miaka milioni 45.

Pia unaweza kusoma

Bahari ya Shamu na mabara mawili

cd

Chanzo cha picha, TEACHER. JR ROWLAND, UNIVERSITY OF AUCKLAND

Maelezo ya picha, Watafiti huko Ethiopia

Wakati bahari mpya inapoibuka, bara la Afrika litakuwa mabara mawili. Litatenganishwa na bahari mpya ndogo ambayo itaibuka kati yao.

Wataalamu wameeleza kuwa Bahari ya Shamu inasogea kwa sentimeta 2.5 kila mwaka kutoka ilipo sasa, huku ardhi ya jirani nazo zikisogea kwa nusu sentimita.

Maji mengi ya chumvi yatatoka Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden ili kuunda bahari bahari mpya kulingana na utafiti.

Tetemeko la ardhi lililotokea nchini Ethiopia mwaka 2005 limeripotiwa katika utafiti ambao umetoa ushahidi mwingi juu ya kugawika bara la Afrika.

Katika eneo la Afar nchini Ethiopia, inasemekana kwa sasa, eneo la kilomita 60 limeachana ikiwa ni ishara ya mgawanyiko huo.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2009, ukiongozwa na Atalay Ayele, kutoka Chuo Kikuu cha Addis Ababa, Ethiopia unaeleza kuwa kugawika kwa bara hilo kumekaribia.

Afrika inaweza kugawika mapema zaidi

k

Chanzo cha picha, TEACHER. JR ROWLAND, UNIVERSITY OF AUCKLAND

Maelezo ya picha, Eneo la Afar, Ethiopia

Mwezi uliopita, Ayele na Ebinger walikuwa sehemu ya kundi la wanasayansi tisa ambao walichapisha utafiti katika jarida la Tectonophysics.

Miongoni mwa matokeo ya utafiti huo, waligundua ukoko mpya ulioibuka kutoka ardhini na safu ya chini ya ardhi ya eneo la Afar ni laini.

"Matukio makubwa yanaweza kuharakisha mchakato wa kufungua nyufa na kupata maji ya chumvi," alisema mwanasayansi Cynthia Ebinger, katika mahojiano na BBC.

Anakadiria itachukua chini ya miaka milioni moja kwa bahari mpya kuibuka kutoka maji ya bahari ya Shamu.

"Tatizo ni kwamba sayansi ya sasa haiwezi kutabiri kwa usahihi matukio kama vile milipuko ya volkeno na matetemeko ya ardhi," anasema Ebinger.

Utafiti kuhusu ufa mkubwa katika Jangwa la Ethiopia unalenga kujibu maswali kuhusu matukio yanayotarajiwa kutokea maelfu ya miaka baadaye na kuunda mbinu zenye uwezo wa kutabiri kwa usahihi mazingira ya siku zijazo.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla