Je Urusi inaweza kutekeleza tishio lake la kutumia silaha za nyuklia huko Ukraine?

Rais Putin

Chanzo cha picha, EPA

Ni swali ambalo tumekuwa tukiuliza tangu Rais Vladimir Putin kuamuru uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Katika vita hivi je, Kremlin inaweza kutekeleza tishio la kutumia silaha za nyuklia?

Rais Joe Biden anahofia hilo.

"Nina wasiwasi Putin huenda akatumia silaha za nyuklia," rais wa Marekani alisema wiki hii. Anaamini hatari "ingalipo".

Sijui kama Rais Biden anasoma jarida la Urusi. Ikiwa amefanya hivyo, unaweza kuelewa kwa nini ana wasiwasi.

Wiki iliyopita, jarida hilo lilichapisha makala ya mtaalam mashuhuri wa sera za kigeni na ulinzi wa Urusi Sergei Karaganov. Bw Karaganov ni mwenyekiti wa Baraza la Sera ya Kigeni na Ulinzi la Urusi. Kwa kifupi, ana uhusiano wa karibu na walio madarakani nchini humo.

Hoja yake inakwenda hivi. Ili "kuvunja nia ya Magharibi", Urusi "italazimika kuangazia tena haja ya kuzuia nyuklia kuwa hoja ya kuridhisha kwa kupunguza kizingiti cha matumizi ya silaha za nyuklia".

"Adui lazima ajue kuwa tuko tayari kufanya mashambulizi katika hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya vitendo vyake vyote vya sasa na vya zamani vya uchokozi ili kuzuia kuzuka kwa vita vya nyuklia vya kimataifa.

"Lakini itakuaje endapo hawatarudi nyuma? Katika hali hii, tutalazimika kushambulia ngome tofauti katika nchi kadhaa ili kuwafanya wale ambao hawataki kuja kwenye meza ya majadiliano kutathmini upya msimamo wao."

Tangu mwaka jana, tumekabiliwa na vitisho vya Moscow kutumia nyuklia mpaka tumezoea.

Na Rais Putin amethibitisha kuwa Urusi tayari imepeleka sehemu ya kwanza ya silaha za kinyuklia huko Belarus, hatua ambayo kiongozi huyo wa Urusi anasema imewekwa kumkumbusha yeyote aliye na mawazo ya "kutushinda kimkakati".

Lakini ni wazi kwamba, sio kila mtu nchini Urusi anaunga mkono wazo kama hilo.

Toleo la leo la gazeti la kila siku la biashara la Kommersant lina makala yenye kichwa "Vita vya Nyuklia ni njia mbaya ya kutatua matatizo".

BBC/DARREN CONWAY

Chanzo cha picha, BBC/DARREN CONWAY

Maelezo ya picha, Mjadala wa Urusi kutumia au kutotumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine umeibuka nchini humo

Lakini kinachovutia kuhusu makala hayo ni kwamba yanadai mjadala umeibuka nchini Urusi kuhusu kutumia au kutotumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine. Na wahusika wakuu hawawezi kujiamulia kivyao kama ilivyodhaniwa.

Makala hayo ya Kommersant yaliyoandikwa na Imeandikwa na kundi la wataalam wa sera za kigeni na ulinzi wa Moscow, yanaeleza kwa nini wanaamini Sergei Karaganov amekosea katika suala hili.

"Wazo kwamba utumiaji wa silaha za nyuklia unaweza kusimamisha kuongezeka na kutatua shida za kimkakati ambazo zimeshindwa kutatuliwa kwa njia za kawaida za kijeshi ni za kutilia shaka sana na, ni makosa," Wanaandika Alexei Arbatov, Konstantin Bogdanov na Dmitry Stefanovich kutoka Kituo cha Usalama wa Kimataifa - Kitengo cha ushauri wa kitaalamu wa Chuo cha Sayansi cha Urusi.

"Wazo la kutumia 'tishio la nyuklia' huenda likajenga msingi mbaya zaidi wa siku za usoni. Wanaoshabikia wazo hilo la kusisimua bila kuzingatia athari yake wanatakiwa kukumbuka hilo."

Huenda pendekezo la Bw Karaganov la kutishia shambulio la nyuklia lilikuwa la kushtua sana kiasi kwamba baadhi ya wasomi nchini Urusi walihisi kwamba hawawezi kusalia kimya.

Ikiwa hilo lilifanyika, inaonyesha kwamba ingawa hali ya vyombo vya habari vya Urusi sasa imedhibitiwa sana na serikali, hata ndani ya mipaka ya sasa, bado kuna nafasi kwenye baadhi ya majukwaa yanajadili kuhusu mada fulani. Hasa mada muhimu kama vile vita vya nyuklia.

Ama kuna uwezekano huenda mjadala huu umeibuliwa kwa lengo la keteka mawazo ya tahadhari ya Magharibi, kumfanya Rais Putin kuonekana kama mtu mzuri huku lawama zikielekezwa kwa Bw Karaganov.

Licha ya yote hayo, kiongozi wa Kremlin mwenyewe hajatoa wito kutishia kutumia silaha za nyuklia ilikuzitikisa nchi za Magharibi. Hatua ambayo huenda - ikatoa nafasi ya majadiliano - bora kukaa chini na kufanya amani naye, badala ya kumuacha mtu mwenye misimamo mikali kama Karaganovites kumshawishi abonyeze kitufe cha silaha za nyuklia.

Jambo moja ni wazi: huku matamshi dhidi ya nchi Magharibi nchini Urusi yakiongezeka, na huku jeshi la Ukraine likikabiliana na mashambulizi yanayoendelea, swali la matumizi ya silaha za nyuklia litaendelea kuibuka.