Ukimya unavyofanya saratani ya uke iwe vigumu kugundulika

edc

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Saratani hii inajumuisha sehemu ya nje ya uchi wa mwanamke; mashavu madogo, mashavu makubwa, kinena na mlango wa uke.

Watu wengi wanajua kuhusu saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya ovari, na ya mfuko wa kizazi. Lakini kuna aina moja ya saratani ya uzazi ambayo haijuulikani na wengi; saratani ya nje ya uke.

Shirika la Uingereza la Utafiti wa Saratani linasema 69% ya kesi za saratani ya uke zinaweza kuzuiwa. Ingawa kutibu aina hii ya saratani ikiwa imefikia hatua kubwa, inaweza kujumuisha kuondolewa kabisa uke.

Saratani ya uke inajumuisha sehemu ya nje ya uchi wa mwanamke; mashavu madogo, mashavu makubwa, kinena na mlango wa uke.

Saratani ya uke inachukuliwa kuwa ya nadra. Ni 1% miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake wa Uingereza. Lakini hiyo haimaanishi kuwa sio hatari.

Watu wanne hugunduliwa na saratani kila siku nchini Uingereza na makadirio yanaonyesha kuwa viwango vya vifo vinatarajiwa kuongezeka kwa 20% katika miongo ijayo.

Kesi nyingi za saratani ya uke huhusiana na maambukizi kutokana na virusi vya papilloma vya binadamu (HPV) au maambukizi ya ngozi.

Wataalamu huamini saratani ya uke inawapata zaidi wanawake wakubwa. Lakini kesi zinaongezeka miongoni mwa wanawake wachanga - baadhi yao hutokana na ongezeko la maambukizi ya HPV.

Watu wengi wanajua HPV inaweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi. Lakini ukweli ni kwamba HPV inaweza pia kusababisha aina nyingine za saratani, kama vile sehemu ya haja kubwa, uume na sehemu ya ndani ya uke.

Chanjo ya HPV hulinda dhidi ya aina zote za saratani zinazohusiana na virusi, pamoja na saratani ya uke.

Hali nyingine inayosababisha saratani ya uke ni maambukizi sugu ya ngozi ambayo huleta muwasho mkali na mabaka meupe au kijivu.

Uchunguzi

Utafiti uliofanywa nchini Denmark ulitazama aina zote za saratani za uzazi na kugundua kuwa saratani ya uke ndiyo inachukua muda mrefu zaidi kugunduliwa.

Wanasayansi waneleza kwamba hii ni kutokana na dalili zake za hatua ya awali, mara nyingi zinachanganya. Lakini pia ukosefu wa elimu na tabia ya aibu hufanya wanawake kuchelewa kutafuta msaada.

Zaidi ya hayo, wanawake wanaotafuta msaada kwa dalili za saratani ya uke nyingi hugunduliwa na aina nyingine ya magonjwa.

Ikiwa una wasiwasi kuhusu dalili za saratani ya uke, unaweza kusisitiza kwa daktari uhitaji wako wa kuchunguzwa aina hiyo ya saratani.

Uingereza, kwa mfano, haina mpango wa uchunguzi wa saratani ya uke kwa sababu ni nadra sana. Lakini wakati wa uchunguzi wa kizazi, mgonjwa anaweza kumwomba muuguzi pia kuchunguza uke ikiwa kuna ishara yoyote inayoonekana ya kansa.

Dalili na ishara zake

Kuwasha mara kwa mara kwenye uke.

Maumivu au kuvimba katika uke.

Mabaka kwenye ngozi, ambayo yanaweza kuwa mekundu, meupe, au meusi.

Mapunye au chunjua kwenye uke.

Kutokwa na damu katika uke au michirizi ya damu kati ya hedhi.

Vidonda katika uke.

Kuungua wakati wa kukojoa.

Mapunye yanayobadilika rangi katika uke.

Ikiwa una mojawapo ya dalili hizi, unapaswa kutafuta msaada. Lakini usiogope. Zinaweza pia kusababishwa na hali nyingine, ambazo zinaweza kuwa mbaya.

Ni muhimu kufahamu uke wako. Ndiposa Chuo Kikuu cha Manchester, nchini Uingereza, kiliunda jarida ili kuwafundisha wanawake jinsi ya kujichunguza uke zao.

Matibabu

Ikigunduliwa katika hatua ya awali, saratani ya uke inaweza kutibiwa kwa ukataji, kuondoa seli za saratani na seli za kawaida zinazozizunguka. Lakini kutibu saratani ya uke ya hatua mbaya inaweza kuwa ya kikatili kidogo.

Hutegemea sehemu saratani hiyo ilipo na ukubwa wake, upasuaji unaweza hata kuondoa sehemu yote ya mashavu makubwa au madogo ya uke na hata kuondoa kinena.

Kupona huchukua muda mrefu na katika kipindi chote mwanamke hawezi kukaa - anaweza tu kusimama au kulala. Na shughuli za ngono zinaweza zisivutie tena.

Umri ambao wanawake hugunduliwa na saratani ya uke ni takriban miaka 10 hadi 15 katika nchi za kipato cha chini, kama vile Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikilinganishwa na nchi tajiri. Kwa sababu katika nchi hizo kuna kesi nyingi za maambukizi.

Kesi za saratani ya uke nchini Uingereza 74% hutokea kwa watu wa kipato cha chini. Dalili za saratani ya uke hazipaswi kuchukuliwa kuwa za kawaida.

Hivyo ni muhimu kuchukua maumivu na kuwasha katika uke kwa uzito, kuzungumza juu ya saratani ya uke na kusisitiza umuhimu wa chanjo ya HPV.