Hospitali ya watoto ya Kyiv miongoni mwa maeneo yalioshambuliwa na Urusi na kuua watu kadhaa

Watu wawili wameuawa katika hospitali ya watoto ya Okhmatdyt baada ya mashambulizi makali ya Urusi, maafisa wanasema.

Muhtasari

  • Msanii aliyefunguwa jela kwa kuchoma picha ya Rais Samia aachiwa huru
  • Mahakama ya Kenya yaamuru malipo kwa mjane wa mwandishi wa Pakistani
  • Vikosi vya Israel vyashambulia mji wa Gaza huku vifaru vikiingia tena katikati ya mji
  • Kampuni ya ndege ya Boeing kukiri mashtaka ya ulaghai wa jinai
  • Wanachama zaidi waandamizi wa chama cha democratic wamtaka Biden kutowania urais
  • Takriban watu 20 wauawa katika shambulizi la Urusi katika miji ya Ukraine
  • Uchaguzi wa Marekani 2024: Ni Wanademocrat gani wamemtaka Biden kusitisha kampeni yake?
  • Wamachinga wafanya mgomo na kufunga barabara Dar ea Salaam
  • Zanzibar: Mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika Mashariki wakutana kujadili amani na usalama
  • Jeshi la Ukraine laboresha ujuzi wa kutumia ndege zisizo na rubani - ISW
  • Bastola za Napoleon zinauzwa kwa €1.69m kwenye mnada
  • Uchaguzi Ufaransa: Muungano wa mrengo wa kushoto waongoza bila kutarajiwa
  • Afisa mkuu wa Hamas auawa huku Israel ikiwaamuru upya watu kuhama

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi, Seif Abdalla & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Msanii aliyefungwa jela kwa kuchoma picha ya Rais Samia aachiwa huru

    .

    Chanzo cha picha, Nation Media Group

    Msanii wa picha nchini Tanzania Shadrack Chaula, aliyefungwa jela kwa kuchoma moto picha ya Rais Samia Suluhu Hassan, ameachiwa huru.

    Msanii huyo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela au faini ya $2,000 (£1,600) baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa mtandaoni.

    Kufuatia hukumu yake, watumiaji wa mitandao wa kijamii wa X, walichangisha shilingi milioni 5.6 za Tanzania ndani ya saa sita.

    Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, wakili Peter Kibatala alisema,"Shadrack Yusuph Chaula ameachiwa huru. Mumemlipia uhuru wake na uhuru wa kujieleza kwa nchi hii".

    Mchoraji huyo mwenye umri wa miaka 24 alikiri kutenda uhalifu huo na kushindwa kutetea hatua yake mahakamani.

    Kukamatwa kwake kulizua utata wa kisheria, huku baadhi ya mawakili wakisema kuwa hakuna sheria iliyovunjwa katika kuchoma picha hiyo.

    Soma zaidi:

  3. Mahakama ya Kenya yaamuru malipo kwa mjane wa mwandishi wa habari wa Pakistani aliyeuawa na polisi nchini humo

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Mahakama nchini Kenya imetoa shilingi 10m ($78,000; £61,000) kama fidia kwa mjane wa mwanahabari maarufu wa Pakistani aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi kwenye kizuizi cha barabarani karibu miaka miwili iliyopita.

    Arshad Sharif alikuwa mtangazaji wa televisheni anayejulikana kwa ukosoaji wake wa wazi dhidi ya viongozi wenye nguvu wa kijeshi wa Pakistani na ufisadi katika siasa.

    Baba wa watoto watano alipokea vitisho vya kuuawa ambavyo aliviashiria kwa jaji mkuu wa Pakistan, kabla ya kutoroka nchi yake kutafuta usalama nje ya nchi.

    Mauaji ya Sharif miezi miwili baadaye mikononi mwa polisi katika mji wa Kajiado nchini Kenya yalisababisha ghadhabu, na jibu la polepole la maafisa lilifanya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuzikosoa Kenya na Pakistan.

    'Afueni kwangu na kwa familia yangu'

    Polisi wa Kenya walidai kuwa ni kisa cha utambulisho kimakosa lakini mjane wa Sharif, Javeria Siddique, alisema ni mauaji yaliyopangwa yaliyotekelezwa kwa niaba ya mtu ambaye hakutajwa jina nchini Pakistan.

    Siku ya Jumatatu, Mahakama Kuu ya Kajiado iliamua kwamba mamlaka ya Kenya ilitenda kinyume cha sheria na kukiuka haki ya kuishi ya Sharif. Ilitoa uamuzi wa Bi. Siddique kupewa fidia pamoja na riba hadi malipo yakamilike.

    "Hasara ya maisha haiwezi kufidiwa kwa njia za kifedha wala uchungu na mateso ambayo familia imepitia. Lakini kuna maafikiano kwamba fidia ni suluhu mwafaka kwa kukiuka haki za kimsingi," alisema Jaji Stella Mutuku alipokuwa akitoa uamuzi huo.

    Jaji huyo pia aliamua kwamba mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini Kenya na mamlaka huru ya kusimamia polisi walikiuka haki za Sharif kwa kukosa kuwashtaki maafisa wawili wa polisi waliohusika. Mahakama imeamuru asasi zote mbili kukamilisha uchunguzi na kuwafungulia mashtaka maafisa hao.

    Wakili anayemwakilisha mjane wa Sharif, Ochiel Dudley, alisema "huu ni ushindi kwa familia na ni ushindi kwa Wakenya katika harakati zao za kuwajibika kwa polisi".

    Mjane wa Sharif, Bi Siddique, alitoa shukrani zake kwa mahakama ya Kenya lakini akaongeza kuwa kazi yake bado haijakamilika.

    Soma zaidi:

  4. Vikosi vya Israel vyashambulia mji wa Gaza huku vifaru vikiingia tena katikati ya mji

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Wapalestina katika mji wa Gaza wanasema wamepitia moja ya mashambulizi makali zaidi ya Israel tangu ilipoanzisha vita vyake dhidi ya Hamas baada ya kundi hilo kufanya shambulizi la Oktoba 7.

    Vifaru vya Israel vinaripotiwa kukaribia katikati ya mji kutoka pande mbalimbali.

    Huduma ya Dharura ya Kiraia ya Gaza inasema inaamini idadi ya watu wameuawa lakini hadi sasa haijaweza kuwafikia kwa sababu ya mapigano katika wilaya kadhaa mashariki na magharibi mwa Jiji la Gaza.

    Hospitali ya Al-Ahli Baptist inaripotiwa kuhamisha wagonjwa wake wakipelekwa katika mojawapo ya vituo vya matibabu ambavyo bado vinafanya kazi katika eneo hilo - hospitali ya Indonesia ambayo tayari ina watu wengi kupita uwezo wake.

    Kabla ya shambulio hilo, jeshi la Israel lilitoa maagizo ya kuhama kwa vitongoji kadhaa katikati mwa jiji.

    Lakini moja ya maeneo ambayo yamekumbwa na mashambulizi makali zaidi, Tel al-Hawa, haikujumuishwa katika amri ya kuwahamisha watu iliotumwa mtandaoni pamoja na ramani na msemaji wa Kiarabu wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Jumapili jioni.

    Soma zaidi:

  5. Kampuni ya ndege ya Boeing kukiri mashtaka ya ulaghai wa jinai

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kampuni ya Boeing yakubali kukiri shtaka la kula njama ya ulaghai baada ya Marekani kupata kampuni hiyo ilikiuka makubaliano yaliyokusudiwa kuifanyia marekebisho baada ya ajali mbili mbaya za ndege zake 737 Max zilizoua abiria 346 na wafanyakazi.

    Wizara ya Sheria ilisema mtengenezaji huyo wa ndege pia alikubali kulipa faini ya $243.6m (£190m).

    Hata hivyo, familia za watu waliofariki katika safari za ndege miaka mitano iliyopita wameikosoa faini hiyo wakisema kuwa ni "adhabu kidogo" ambayo ingeruhusu Boeing kuepuka kuwajibika kikamilifu kwa vifo hivyo.

    Makubaliano hayo lazima sasa yaidhinishwe na jaji wa Marekani.

    Kwa kukiri kuwa na hatia, Boeing itaepuka kesi ya jinai - jambo ambalo familia za waathiriwa zimekuwa zikishinikiza.

    Kampuni hiyo imekuwa katika mgogoro kutokana na rekodi yake ya usalama tangu ajali mbili zinazokaribiana kufanana zilizohusisha ndege za 737 Max mwaka 2018 na 2019. Ilisababisha kusimamishwa kwa ndege hizo duniani kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Mnamo 2021, waendesha mashtaka walishtaki Boeing kwa shtaka moja la kula njama za kuwalaghai wasimamizi, wakidai kuwa ilidanganya Utawala wa Usafiri wa Anga (FAA) kuhusu mfumo wake wa kudhibiti ndege, ambao ulihusishwa na ajali zote mbili.

    Ilikubali kutoshtaki Boeing ikiwa kampuni hiyo italipa faini na kukamilisha kwa mafanikio kipindi cha miaka mitatu cha kuongezeka kwa ufuatiliaji na utoaji wa taarifa.

    Lakini mnamo Januari, muda mfupi kabla ya muda huo kukamilika, mlango wa ndege ya Boeing inayoendeshwa na Shirika la Ndege la Alaska ulifunguka mara baada ya kupaa na kuilazimisha ndege hiyo kutua.

    Hakuna aliyejeruhiwa wakati wa kisa hicho lakini ilizidisha uchunguzi juu ya maendeleo kiasi gani Boeing ilikuwa imefanya katika kuboresha rekodi yake ya usalama na ubora.

    Mnamo mwezi Mei, Wizara ya Sheria ilisema imepata Boeing ilikiuka masharti ya makubaliano, na kuongeza uwezekano wa kampuni hiyo kufunguliwa mashtaka.

    Soma zaidi:

  6. Wanachama zaidi waandamizi wa chama cha democratic wamtaka Biden kutowania urais

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wabunge wengine kadhaa waandamizi wa chama cha Rais Joe Biden cha Democratic wamejiunga na wito wa kumtaka akabidhi ugombea wake katika uchaguzi wa Novemba kwa mgombea mwingine, vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.

    Wakati wa mazungumzo na Kiongozi wa walio Wachache Bungeni Hakeem Jeffries, wabunge wanne walizungumza wazi kumtaka Bwana Biden ajiondoe, kulingana na vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na mshirika wa BBC wa Marekani CBS News.

    Wanne hao waliungwa mkono na wengine ambao walionyesha wasiwasi wao juu ya uwezo wa Bw Biden kuendelea kushikilia ofisi hiyo baada ya utendaji mbaya wa mjadala wa hivi majuzi, lakini hawakumuomba rais kujiondoa, CBS iliongeza.

    Bw Biden ameapa kuendelea kuwa kinyang’anyironi, na amedumisha uungwaji mkono wa Wanademokrasia wengine ambao wanasisitiza kuwa yeye ndiye mtu atakayemshinda Donald Trump katika kura ya Novemba.

    Maoni mbalimbali juu ya kugombea kwa Bw Biden yanatarajiwa kujitokeza zaidi siku ya Jumatatu baada ya wabunge kurejea Capitol Hill.

    Rais pia ataangaziwa katika siku zijazo huku akiandaa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Nato huko Washington.

    Soma zaidi:

  7. Takriban watu 24 wauawa katika shambulizi la Urusi katika miji ya Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 20 wameuawa baada ya Urusi kufanya shambulizi kubwa la kombora dhidi ya miji kote Ukraine, kulingana na maafisa.

    Katika mji mkuu, Kyiv, takriban watu saba waliuawa katika shambulio la nadra la mchana.

    Meya wa jiji hilo alisema hospitali ya watoto imeshambuliwa kwa makombora na wagonjwa wanahamishwa.

    Mkuu wa utawala wa kijeshi katika mji wa kati wa Ukraine wa Kryvyi Rih amesema takriban watu 10 wameuawa huko, huku watatu wakiuawa katika mji wa mashariki wa Pokrovsk.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye anazuru Poland, alisema kuwa Urusi imefyatua takriban makombora 40 kulenga shabaha kote nchini.

    Bw Zelensky, ambaye anatazamiwa kusafiri hadi Marekani kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Nato wa wiki hii mjini Washington, alisema Urusi "imeishambulia kwa kiasi kikubwa" Ukraine.

    "Miji tofauti: Kyiv, Dnipro, Kryvyi Rih, Sloviansk, Kramatorsk. Zaidi ya makombora 40 ya aina mbalimbali. Majengo ya makazi, miundombinu na hospitali ya watoto yaliharibiwa, "alisema.

    Moshi mwingi ulionekana katika mji mkuu wa Kyiv, huku video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha uharibifu ndani na nje ya hospitali ya watoto ya Okhmadyt. Haijabainika iwapo mtu yeyote ndani alijeruhiwa.

    Lakini Bw Zelensky alisema katika ujumbe wa mtandao wa kijamii kwamba watu walinaswa chini ya vifusi vya hospitali hiyo. Aliongeza kuwa idadi ya watu waliojeruhiwa katika hospitali ya Okhmadyt haijulikani.

    Vitaliy Klitschko, meya wa Kyiv, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba shambulio hilo lilikuwa baya zaidi katika mji mkuu huo tangu kuanza kwa vita.

    Kwingineko, Oleksandr Vilkul, mkuu wa utawala wa kijeshi huko Kryvy Rih, alichapisha kwenye programu ya Telegram ujumbe kwamba watu wasiopungua 10 waliuawa na 31 kujeruhiwa kufuatia shambulio la mji huo. Kati ya hao, alisema 10 walijeruhiwa vibaya.

    Kryvy Rih ni mji alikozaliwa Bw Zelensky na umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na Urusi tangu ilipoanzisha uvamizi wake huko Ukraine mnamo Februari 2022.

    Soma zaidi:

  8. Uchaguzi wa Marekani 2024: Ni Wanademocrat gani wamemtaka Biden kusitisha kampeni yake?

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Idadi inayoongezeka ya Wademocrat katika Bunge la Marekani wanamtaka Rais wa Kidemokrasia Joe Biden kusitisha azma yake ya kuchaguliwa tena baada ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 kusitisha mjadala dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump.

    Hii ni orodha ya wabunge wa Democrats waliomuambia wazi Joe Biden asigombee urais;

    Mwakilishi Lloyd Dogget

    Doggett, ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kutoka wilaya yenye uungani mkono zaidi wa chama cha Democrat ya Texas, alikuwa mwanademokrasia wa kwanza kumtaka Biden ajiuzulu.

    Mwakilishi Raul Grijalva

    Mwanaliberali ambaye anawakilisha wilaya ya kusini mwa Arizona kwenye mpaka na Mexico. Grijalva aliliambia gazeti la New York Times kuwa ni wakati wa Biden kumaliza kampeni yake, akisema, "Ikiwa yeye ndiye mgombea, nitamuunga mkono, lakini nitamuunga mkono. nadhani hii ni fursa ya kuangalia mahali pengine." Wawakilishi wa Grijalva hawakujibu maombi ya maoni.

    Mwakilishi kutoka Seth Moulton

    Moulton alisifu huduma ya Biden kwa nchi lakini akamtaka afuate "nyayo za George Washington na kujitenga ili kuwaacha viongozi wapya wasimame dhidi ya Donald Trump," Mwanademokrasia anayewakilisha wilaya ya Massachusetts aliambia kipindi cha redio cha ndani.

    Mwakilishi Mike Quigley

    Mwakilishi kutoka Illinois, Quigley aliiambia MSNBC kwamba Biden lazima aondoke na "kumwacha mtu mwingine afanye hivi" au ahatarishe "janga kubwa."

    Mwakilishi Angiel Craig

    Craig, ambaye wilaya yake inachukuliwa kuwa kipaumbele cha juu kwa Republican kushinda tena mnamo Novemba, alikuwa mwanzilishi wa kwanza kutoka wilaya yenye ushindani mkubwa kumtaka Biden ajiuzulu.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Wamachinga wafanya mgomo na kufunga barabara Dar ea Salaam

    g

    Chanzo cha picha, Ngaira

    Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu wamachinga katika Soko la Simu2000, katika manispaa ya Ubungo, ijini Dar eS Salaam wameingia kwenye mgomo asubuhi ya leo na kufunga barabara.

    Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, wamachinga hao wanalalamikia mpango wa kukabidhiwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), sehemu ya eneo lao kwa ajili ya kujenga karakana ya mabasi yake.

    Mbali na kufunga biashara zao, pia wameweka vizuizi katika barabara kuelekea Sinza na kuzuia magari kuingia na kutoka katika kituo hicho cha daladala.

    Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko alifika eneo hilo na polisi, lakini wafanyabiashara hao walimtaka aondoke.

    Mgomo huu umekuja wiki chache tangu kumalizika kwa mgomo wa kufunga biashara uliofanywa na wamiliki wa maduka katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, na kuenea katika mikoa mengine, wakilalamikia mrundikano wa kodi.

  10. Zanzibar: Mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika Mashariki wakutana kujadili amani na usalama

    g

    Chanzo cha picha, @RwandaMFA

    Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) wanakutana Zanzibar, kujadili amani na usalama katika kanda, uhusiano kati ya nchi washirika na mchakato wa ushirikiano wa EAC, kwa lengo la kutafuta suluhisho halisi la changamoto zilizopo.

    Mkutano huu unafanyika huku kukiwa mahusiano kati ya nchi za Rwanda na majirani zake Burundi na DRC ukiwa na dosari, kila upande ukimlaumu mwenzake kwa kuwaunga mkono waasi wa upande mwingine.

    Nchi washirika zitajadili kati ya wengine hali ya amani na usalama wa kikanda pamoja na mchakato wa ushirikiano wa kikanda.

    ''Ni heshima kwetu kuwakaribisha hapa Zanzibar kwa ajili ya mapumziko(Retreat) haya muhimu. Nimefurahishwa sana na namna ya busara ambayo tumejihusisha na masuala nyeti sana ya amani, usalama na uhusiano wa nchi washirika katika eneo yetu.’’, Ameandika Kwenye mtandao wa kijami wa X, Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Januari Makamba:https://x.com/JMakamba/status/1809813106664620376

    Katika Ujumbe wao kuhusiana na mkutano huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameelezea kufurahishwa na mwaliko wa Tanzania wa mkutano huo wa Zanzibar

  11. Jeshi la Ukraine laboresha ujuzi wa kutumia ndege zisizo na rubani - ISW

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waendeshaji wa ndege zisizo na rubani za Ukraine wanaboresha uwezo wao wa kunasa ndege zisizo na rubani za Urusi za masafa marefu, Taasisi ya Amerika ya Utafiti wa Vita (ISW) inaandika katika ripoti ya kawaida ya kila siku.

    Kulingana na wataalamu hao, uvumbuzi huo wa kiteknolojia unaweza kuviruhusu vikosi vya Ukraine kupunguza mzigo kwenye mifumo ya ulinzi wa anga ikiwa itatumika kwa ufanisi kote nchini.

    Picha zilizotolewa mnamo tarehe 1 Juni zinaonyesha vikosi vya Ukraine vikitumia ndege zisizo na rubani za aina ya FPV kushambulia ndege isiyo na rubani ya Urusi ya upelelezi aina ya Zala na ndege nyingine isiyo na rubani ya masafa ya kati aina ya Orlan-10.

    Mwishoni mwa mwezi Juni, jeshi la Ukraine pia lilichapisha picha za ndege isiyo na rubani yaUkraine ikinasa ile ya Urusi aina ya Lancet UAV angani katika iliyokua ikielekea Kharkov.

    Vikosi vyote vya Ukraine na Urusi vinaonekana kuboresha uwezo wao wa ndege zisizo na rubani katika kiwango cha mbinu, lakini ISW bado haijapata ushahidi wa vikosi vya Urusi vinavyotumia ndege zisizo na rubani za FPV kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya droni za kamikaze au UAV za masafa marefu za upelelezi.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

  12. Bastola za Napoleon zinauzwa kwa €1.69m kwenye mnada

    f

    Chanzo cha picha, Osenat auction house

    Maelezo ya picha, Baadaye Napoleon alitoa bastola kwa mmiliki wa ardhi yake Armand de Caulaincourt, ambaye aliwakabidhi wazao wake.

    Bastola mbili zilizomilikiwa na mfalme wa Ufaransa Napoleon Bonaparte, ambazo hapo awali alikusudia kuzitumia kujiua, zimeuzwa kenye mnada kwa thamani ya €1.69m (£1.4m).

    Silaha hizo, ambazo ziliundwa na mtengenezaji wa bunduki wa Paris Louis-Marin Gosset, zilitarajiwa kuuzwa kati ya €1.2m na €1.5m.

    Ziliuzwa katika jumba la mnada la Osenat siku ya Jumapili - karibu na jumba la Fontainebleau ambapo Napoleon alijaribu kujiua kufuatia kutekwa nyara kwake mnamo 1814.

    Uuzaji wa bastola hizo unakuja baada ya wizara ya utamaduni ya Ufaransa hivi majuzi kuziainisha kuwa hazina za kitaifa na kupiga marufuku usafirishaji wake.

    Hii inamaanisha kuwa serikali ya Ufaransa sasa ina miezi 30 kufanya ofa ya ununuzi kwa mmiliki mpya, ambaye hajatajwa jina. Pia inamaanisha bastola hizo zinaweza kuondoka kwa muda tu Ufaransa.

    Bunduki hizo zimepambwa kwa dhahabu na fedha, na zina picha ya kuchonga ya Napoleon mwenyewe.

    Inasemekana alitaka kuzitumia kujiua usiku wa tarehe 12 Aprili, 1814 baada ya kushindwa kwa jeshi lake na majeshi ya kigeni jambo ambalo lilimaanisha kwamba alilazimika kuachia madaraka.

  13. Uchaguzi Ufaransa: Muungano wa mrengo wa kushoto waongoza bila kutarajiwa

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa mrengo wa kushoto Jean-Luc Mélenchon alikuwa mwepesi wa kudai ushindi baada ya makadirio ya kwanza

    Ulikuwa ni usiku ambao hakuna mtu nchini Ufaransa alitarajia kushuhudia kupata matokeo ya uchaguzi kinyume na matarajio. Matokeo haya ya uchaguzi wa ubunge yalikuwa ya mshtuko.

    Muungano wa mrengo wa kushoto uliobuniwa haraka na Jean-Luc Mélenchon kufuatia Macron kuititisha kwa uchaguzi ulikua juu kwenye chati ya kura.

    Wajumbe wa chama cha Emmanuel Macron walikuwa wamepata matokeo ambayo hayakutarajiwa, na kura za mrengo wa kulia National Rally (RN) zilishuka kutoka kwa zile zilizotabiriwa na mrengo huo ukashuka hadi nafasi ya tatu.

    Lakini hakuna aliye na viti vya kutosha kutawala, na Ufaransa sasa inakabiliwa na bunge lisilo na walio wengi.

    Kundi la mrengo wa kulia la National Rally lilitabiriwa kwa kiasi kikubwa kushinda uchaguzi wa Ufaransa - lakini inaonekana wamejipata katika nafasi ya tatu.

    Muungano wa mrengo wa kushoto, The New Popular Front, uko mbioni kupata ushindi, baada ya uchaguzi wenye mashtaka mengi na uliofupishwa ulioitishwa wiki nne tu zilizopita na Macron.

    Yote yalikuwa yameonekana tofauti baada ya duru ya kwanza, huku National Rally ikitabiriwa ushindi katika duru ya pili.

    Badala yake, Ufaransa inaelekea kwenye bunge ambalo litakuwa halina chama chenye wingi wa wabunge bungeni.

  14. Afisa mkuu wa Hamas auawa huku Israel ikiwaamuru upya watu kuhama

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kifo cha Al-Ghussein hakichukuliwi kuwa pigo kwa Hamas kijeshi.

    Afisa mkuu wa utawala wa Hamas alikuwa miongoni mwa watu wanne waliouawa katika shambulizi la anga la Israel lililofanyika katika shule moja katika mji wa Gaza, duru za Palestina zinasema.

    Afisa mmoja wa eneo hilo ameiambia BBC kwamba Ehab Al-Ghussein aliteuliwa kusimamia maswala ya serikali ya Hamas katika mji wa Gaza na kaskazini mwa Gaza miezi mitatu iliyopita.

    Jeshi la Israel linasema kuwa lilifanya shambulizi katika eneo la jengo la shule katika mji wa Gaza ambapo linasema "magaidi walikuwa wakiendesha shughuli zao na kujificha".

    Linasema kwamba lilichukua hatua hiyo ili kupunguza hatari ya kuwadhuru raia.

    Walioshuhudia wanasema shambulio hilo lililenga Shule iliyo karibu na Kanisa la Holy Family, magharibi mwa mji wa Gaza. Idadi kubwa ya watu walikuwa wamejihifadhi katika jengo hilo, BBC inafahamu.

    Shambulio hilo la anga ulilenga vyumba viwili vya madarasa kwenye ghorofa ya chini, walisema.

    Ehab Al-Ghussein aliwahi kuwa naibu waziri wa kazi katika utawala wa Hamas na kabla ya hapo alikuwa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani.

    Kifo chake hakichukuliwi kuwa pigo kwa Hamas kijeshi, lakini alichukuliwa kuwa mtu muhimu katika utawala wa Hamas.

    Watu wengine wengi wameuliwa katika utawala wa Hamas katika muda wa miezi tisa iliyopita.

    Unaweza pia kusoma:

  15. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya mushara leo ikiwa ni tarehe 08.07.2024