Muswada wa fedha 2024:Mahakama yazuia Polisi kutumia maji, mabomu ya machozi dhidi ya waandamaji Kenya

Polisi wamepigwa marufuku kutumia maji ya kuwasha, mabomu ya machozi, risasi za moto, risasi za mpira, au silaha nyingine yoyote dhidi ya waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa sasa.

Muhtasari

  • Mwanamitindo wa Uganda aapa kukuza nywele zilizokatwa jela
  • Cameroon: Mchezaji wa zamani wa Celtic Nguemo aombolezwa
  • Mbunge aliyeunga mkono Muswada wa fedha Kenya aeleza alivyookolewa na Gen Z
  • Mwanahabari mkongwe wa Kenya Mutegi Njau afariki dunia
  • Marekani: Jimbo la Oklahoma laamuru shule kutoa mafunzo ya Biblia 'mara moja'
  • Betri ya gari la umeme yachaji chini ya dakika tano katika jaribio
  • Mgomo Tanzania: Serikali, wafanyabishara wafikia maazimio 15 nikoa 9 ikiathirika
  • Rais wa Afrika Kusini amsuta mshirika wake wa muungano katika mvutano mkali
  • Mdahalo kati ya Biden na Trump: Je ni nani aliyeibuka mshindi?
  • Mdahalo kati ya Biden na Trump: Yaliyojiri kwa mukhtasari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Muswada wa fedha 2024:Mahakama yazuia Polisi kutumia maji, mabomu ya machozi dhidi ya waandamaji Kenya

    Waandamanaji

    Chanzo cha picha, REUTERS/MONICA MWANGI

    Polisi wamepigwa marufuku kutumia maji ya kuwasha, mabomu ya machozi, risasi za moto, risasi za mpira, au silaha nyingine yoyote dhidi ya waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa sasa.

    Hii ni baada ya ombi lililowasilishwa na Saitabao Ole Kanchory ambapo Jaji Mugure Thande pia alipiga marufuku matumizi ya nguvu au aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya waandamanaji.

    "Nimeona mleta maombi amedhihirisha kuwa ombi hilo ni la msingi na si la kipuuzi. Pili, amedhihirisha kwamba ni kwa maslahi ya umma," aliamua Jaji Thande.

    Vilevile, mahakama imetoa amri ya kuwazuia polisi kufanya mauaji ya kiholela, ukamataji, utekaji nyara, kuwekwa kizuizini, unyanyasaji, vitisho, utesaji, ukatili, unyama na udhalilishaji wa watu wanaoandamana kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha.

    Unaweza kusoma;

  2. Watuhumiwa wa mauaji ya mtoto mwenye ualbino wafikishwa mahakamani Tanzania

    Watuhumiwa

    Chanzo cha picha, Mariam Emilly

    Watuhumiwa wa mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Bukoba, Kasikazini Magharibi mwa Tanzania.

    Mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, Elipokea Wilson, washtakiwa hao akiwemo Padre wa Parokia ya Bugandika, Elpidius Rwegoshora, Baba wa mtoto Asimwe , Novath Venant pamoja na washtakiwa wengine saba wamesomewa shtaka la mauaji ya kukusudia, shirika la utangazaji, TBC limeripoti.

    Mkuu wa mashtaka wa mkoa wa Kagera, Waziri Magumbo amesema kuwa uchunguzi wa shauri hilo umekamilika.

    Washtakiwa hao tisa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza shauri hilo.

    Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 12, 2024 huku washtakiwa wote wakirudishwa rumande.

    Mtoto Asimwe alichukuliwa nyumbani kwao kaskazini magharibi mwa nchi hiyo katika kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera Mei 30 majira ya saa mbili usiku.

    Baada ya tukio hili la mtoto Asimwe, polisi mkoani Kagera wanasema wameimarisha ushirikiano na wananchi kupata taarifa za wahalifu kwa haraka na kuimarisha ulinzi kwa watu wenye ualbino.

  3. Trump asema masharti ya Putin ya kumaliza vita hayakubaliki

    Trump

    Chanzo cha picha, CNN

    Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, wakati wa mjadala na kiongozi wa sasa wa Marekani Joe Biden, alisema kuwa masharti ya kumaliza vita nchini Ukraine, ambayo yalitolewa na Rais wa Urusi Vladimir Putin, hayakubaliki.

    Katika Mkutano wa Amani nchini Uswizi, Putin alisema kuwa sharti la mazungumzo hayo ni kuondolewa kwa wanajeshi wa Kiukreni katika eneo linalokaliwa na Urusi, pamoja na Kiev kuachana na nia yake ya kujiunga na NATO.

    "Hapana, hazikubaliki," Trump alijibu swali la moja kwa moja.

    Wakati wa mdahalo huo, Trump alisema tena kwamba atasuluhisha mzozo huo ikiwa atashinda uchaguzi huo kabla ya kushika wadhifa huo rasmi, lakini hakubainisha ni kwa namna gani alikusudia kufanya hivyo.

    Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan mwaka wa 2021, Trump aliitaja kuwa "wakati wa aibu zaidi katika historia ya nchi hii" na kusema kwamba uzembe wa Marekani wakati huo pia ulisukuma Urusi kuivamia Ukraine.

    "Sijawahi kusikia ujinga mwingi maishani mwangu," Biden alijibu. Alimwita Vladimir Putin mhalifu wa kivita na akasema hataishia Ukraine.

  4. Mwanamitindo wa Uganda aapa kukuza nywele zilizokatwa jela

    Latif Madoi

    Chanzo cha picha, Latif Mado

    Maelezo ya picha, Latif Madoi anasema hii ni mara ya kwanza kwa bintiye kumuona bila dreadlocks

    Mbunifu mashuhuri wa mitindo wa Uganda ambaye nywele zake (dreadlocks) zilikatwa baada ya kukamatwa ameambia BBC kuwa ana mpango wa kuzikuza tena "muda wote [atakapoishi]".

    Latif Madoi, ambaye ametengeneza nguo za watu mashuhuri kama vile msanii maarufu wa reggae wa Afrika Kusini Lucky Dube na Busy Signal wa Jamaica, alikaa kizuizini kwa zaidi ya wiki sita.

    Hajapatikana na hatia ya uhalifu wowote lakini wakuu wa magereza hata hivyo walisisitiza kukata nywele za nywele ambazo amekuwa akikuza kwa miaka 17.

    Siku ya Jumatatu aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja za Uganda sawa na dola 269 za Kimarekani.

    Baada ya kutulia nyumbani, Bw Madoi aliambia BBC kwamba hatua ya kunyolewa nywele zake "ilikuwa tukio la kuvunja moyo".

    Mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 47 alipata umaarufu wake kupitia "matamasha ya mtindo" ambapo angetengeneza nguo 10 hadi 15 kwa saa mbili tu.

    Lakini sasa, bila nywele ambazo zilikuwa sehemu muhimu ya utambulisho wake wa Rastafari, anahisi "aibu ... siwezi kutembelea maeneo. Huenda hata nitahisi aibu kurudi jukwaani".

    Bw Madoi amekuwa akikuza dreadlocks zake kwa miaka 17

    Chanzo cha picha, Latif Madoi

    Maelezo ya picha, Bw Madoi amekuwa akikuza dreadlocks zake kwa miaka 17

    Polisi walisema walivamia shule yake ya mitindo na kumkamata kwa kuvalia "sare zilizotangazwa kuwa za matumizi ya kipekee" ya wanajeshi na polisi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za Uganda.

    Lakini Bw Madoi, wakili wake na wafuasi wengi wa Uganda mtandaoni wanashawishika kuwa alifungiwa kwa uhusiano wake na Bobi Wine, kiongozi wa upinzani na mwimbaji ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu.

  5. Cameroon: Mchezaji wa zamani wa Celtic Nguemo aombolezwa

    Kiungo wa zamani wa Celtic Landry Nguemo

    Chanzo cha picha, SNS

    Kiungo wa zamani wa Celtic Landry Nguemo amefariki dunia baada ya kuhusika katika ya barabarani nchini Cameroon.

    Mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Cameroon alikuwa amekaa kwa mkopo kwa msimu mmoja Parkhead katika maisha yake ya soka ambayo yalianza akiwa na Nancy ya Ufaransa na kujumuisha soka la Uturuki na Norway.

    Mamlaka ya soka ya Cameroon imethibitisha leo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 amepoteza maisha katika ajali.

    "Shirikisho la Soka la Cameroon limepokea taarifa za kusikitisha za kifo cha aliyekuwa mchezaji wa Indomitable Lion Landry Nguemo katika ajali ya barabarani.

    “Nguemo, ambaye alikuwa mchezaji muhimu wa timu ya taifa ya Cameroon kuanzia 2006 hadi 2014 na mchezaji wa zamani wa Girondins de Bordeaux, atakumbukwa kwa mchango wake katika soka.

    "FECAFOOT inatuma rambirambi kwa familia yake, marafiki na jumuiya nzima ya soka."

    N'Guemo alicheza zaidi ya mara 40 chini ya Tony Mowbray na Neil Lennon kama kiungo mkabaji wakati wa msimu wa 2009-10, akifanya mechi yake ya kwanza ya ushindani katika mechi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa dhidi ya Dynamo Moscow.

    "Kila mmoja katika Klabu ya Soka ya Celtic ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kuaga dunia kwa Landry N'Guemo akiwa na umri wa miaka 38," klabu hiyo ilisema katika taarifa.

  6. Mbunge aliyeunga mkono Muswada wa fedha Kenya aeleza alivyookolewa na Gen Z

    .

    Chanzo cha picha, Facebook/Kosgei

    Maelezo ya picha, Mbunge mteule Jackson Kosgei

    Askofu na Mbunge Mteule Jackson Kosgei Jumanne aliachwa na wenzake wakati waandamanaji wa Gen Z walipovamia bunge na kuteketeza eneo moja.

    Kulingana na gazeti la The Star, Mbunge huyo mwenye matatizo ya kimwili alikumbuka matukio ya Jumanne, Juni 25, wakati wa maandamano ya #OccupyParliament kupinga Muswada wa Fedha wa 2024.

    Wabunge wengine walilazimika kukimbilia usalama wao wakati vijana wa Gen Z walipovunja uzio wa bunge na kuingia kwa nguvu licha ya vizuizi vya usalama vilivyokuwa vimewekwa.

    Takriban watu 5 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa wakati polisi walipowafyatulia risasi waandamanaji.

    Mbunge huyo aliyezungumza na runinga moja mjini Nairobi na kunukuliwa na gazeti la The Star alisimulia siku hiyo akihofia usalama wake.

    Hata hivyo, alinusurika baada ya umati wa Vijana hao kumhakikishia kuwa hawatamdhuru."Licha ya ya kwamba ilikuwa katika hali ya hasira, walionyesha sura ya kibinadamu. Walipoingia walisema mzee tunakujua, ulikopiga kura, na tunakujua kama mtu mwema," alisimulia.

    Katika video zilisosambaa mtandaoni, mbunge huyo alisindikizwa nje na kikundi kilichomuhakikishia usalama.

    "Kwa hiyo walisema suala la wapi ulipiga kura na kadhalika sio hoja. 'tunataka kukusaidia kwa sababu kinachoweza kutokea hapa kinaweza kisiwe kizuri kwako," Kosgei alisema.

  7. Mwanahabari mkongwe wa Kenya Mutegi Njau afariki dunia

    Tasnia ya habari nchini Kenya inaomboleza kufuatia kifo cha mwanahabari mkongwe Mutegi Njau.

    Mtandoa wa Citizen Digital umenukuu familia ikisema Bw. Mutegi alifariki kwa amani Alhamisi jioni Juni 27, 2024, mwendo wa saa saba usiku.

    Mutegi, ambaye taaluma yake ya uandishi ilidumu kwa miongo kadhaa, alifanya kazi katika mashirika mashuhuri ya vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Royal Media Services.

    Mutegi, alijulikana kwa umakini wake na ustadi kazini.

    Safari yake ya uandishi ilianza mwaka wa 1979, tangu enzi za rais mwanzilishi wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

  8. Marekani: Jimbo la Oklahoma laamuru shule kutoa mafunzo ya Biblia 'mara moja'

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Afisa mkuu wa elimu wa jimbo la Oklahoma nchini Marekani ameamuru shule kuanza kujumuisha Biblia katika masomo, katika agizo la hivi punde ya kuhusu mafunzo ya kidini shuleni.

    Agizo lililotumwa na Msimamizi wa jimbo la Republican Ryan Walters lilisema sheria hiyo ni ya lazima, inayohitaji "kuzingatiwa kikamilifu".

    Sheria hiyo itadumishwa kwa wanafunzi wote wa shule za umma walio na umri wa kuanzia miaka 11-18.

    Inakuja wiki moja baada ya gavana wa Louisiana kutia saini sheria inayoagiza shule zote za umma katika jimbo hilo kuonyesha Amri Kumi.

    Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Bw Walters alielezea Biblia kama "msingi wa kihistoria na kitamaduni".

    "Bila ujuzi wa kimsingi juu yake, wanafunzi wa Oklahoma hawawezi kuweka msingi wa taifa letu ipasavyo, ndiyo maana viwango vya elimu vya Oklahoma vinatoa mafundisho yake," aliongeza.

    Bw Walters, mwalimu wa zamani wa historia ya shule ya umma, alichaguliwa kwa wadhifa wake mwaka wa 2022 baada ya kuegemeza ampeni kwenye jukwaa la kupinga "itikadi iliyolegea" na kuwaondoa "walio na msimamo mkali wa kushoto" kutoka kwa mfumo wa elimu wa Oklahoma.

    Tangazo lake, ambalo linajumuisha darasa la tano hadi la 12, lilikosolewa vikali na mashirika ya haki za kiraia na vikundi vinavyotetea utengano mkali wa kanisa na serikali.

  9. Betri ya gari la umeme yachaji chini ya dakika tano katika jaribio

    Aina hii ya chaja inaweza kurahisisha mambo katika siku zijazo

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Aina hii ya chaja inaweza kurahisisha mambo katika siku zijazo

    Betri ya gari ya umeme iliyotengenezwa na kampuni ya Nyobolt ya Uingereza imechaji kwa ufanisi kutoka 10% hadi 80% katika dakika nne na sekunde 37 katika onyesho lake la kwanza la moja kwa moja.

    Iliafikiwa na gari la michezo lenye dhana iliyoundwa mahususi kwenye wimbo wa majaribio huko Bedford, na ni sehemu ya juhudi za sekta nzima kupata magari ya umeme (EVs) yanayochaji kwa haraka zaidi.

    Kwa kulinganisha, supercharger iliyopo ya Tesla inaweza kuchaji betri ya gari hadi 80% katika dakika 15-20. Wataalamu wanasema kuondoa kile kinachoitwa "wasiwasi wa aina mbalimbali" ni muhimu katika kuongeza matumizi ya EVs - lakini pia wanasisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya malipo.

    "Kutengeneza teknolojia ambayo inawawezesha watu kuchaji haraka zaidi, ambayo inaambatana na wakati unaochukua sasa kupaka gari tena - ni muhimu sana," Paul Shearing, Profesa wa Uhandisi Endelevu wa Nishati katika Chuo Kikuu cha Oxford, aliiambia BBC.

    Lakini aliongeza kuna haja ya kuwa na chaja zaidi za aina zote.

    "Watu watataka miundombinu inayochaji haraka, bila kujali gari wanalotumia - kila mtu anataka kufanya hivi haraka zaidi," alisema. Gari la michezo ambalo betri ya Nyobolt liliwekwa - ambalo lilijaribiwa kwa siku mbili wiki hii - lilifanikiwa umbali wa maili 120 baada ya dakika nne.

    Tesla inayotozwa hadi 80% kwa kawaida inaweza kuwa na masafa ya hadi maili 200.

  10. Mgomo Tanzania: Serikali, wafanyabishara wafikia maazimio 15 mikoa 9 ikiathirika,

    Waganyabiashara

    Serikali ya Tanzania imesema mazungumzo kati yake na jumuiya ya wafanyabiashara yaliyodumu kwa takriban siku nne yamekamilika na kukubaliana kusimamia maazimio 15. Hoja za wafanyabiashara zilikuwa 41.

    Masemaji Mkuu wa serikali ya Tanzania Thobias Makoba amesema mjini Dodoma kuwa mazungumzo hayo yamekamilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya mazungumzo mengine yaliyofanyika kwa ngazi ya mawaziri wa sekta husika.

    Hatua hii imekuja huku mgomo wa wafanyabiashara wenye maduka nchini Tanzania ukishuhudiwa katika baadhi ya miji mikubwa yakiwemo majiji mengi.

    Hadi kufikia jioni ya Alhamisi Juni 27 tayari kulikuwa na uthibitisho wa mgomo wa kufungua maduka kuyakumba majiji ya Dar es Salaam eneo la Kariakoo, Mwanza, Dodoma, Mbeya na Arusha huku miji mingine minne ya makao makuu ya mikoa ya Songwe, Iringa Mtwara na Kagera nayo ikikumbwa na mgomo.

    Maazimio hayo 15 yanayolenga kuudhibiti mgomo ni TRA kusitisha mara moja mazoezi yote ya kamata kamata pamoja na kusitisha mazoezi mengine yote ya ufuatiliaji wa risisti za EFD katika maeneo yote nchini hadi mwezi Agosti, 2024. Aidha, pamoja kusitishwa huko wafanyabishara wanahimizwa kuelendelea kutoa risiti za mauzo.

    Pia TRA imeagizwa kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa nchini kuanzia Julai, 2024. Aidha, utekelezaji wake utawekewa utaratibu mzuri kwa kushirikisha wadau wote muhimu huku serikali ikiiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania kuongeza haraka bandari kavu (ICD) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.

    Kadhalika TRA imeelekezwa kuongeza nguvu kwenye kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho ya kodi yanayofanyika ili kuwezesha kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi nchini. Aidha, Taasisi husika za Serikali pamoja na mabaraza ya biashara yashirikishwe kikamilifu katika ngazi zote.

    Mamlaka hiyo ya mapato pia imeelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.

    Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara.

    Maazimio mengine ni kuwa katika kipindi cha muda wa kati, serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi tulivyo navyo kwa sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa amani na haki kulingana na thamani ya biashara zao; serikali itashughulikia changamoto zote za wafanyabishara zilizowasilishwa serikalini hususan zile ambazo hazihitaji mabadiliko ya sera au sheria; na serikali kuiagiza TRA ikamilishe maboresho ya mfumo wa TANCIS ambao utajumuisha moduli ya Auto valuation itakayoweka wazi na usawa katika ukokotoaji wa kodi kufikia Januari 2025

    Pia kuna maazimio yanayogusa mamlaka na utendaji wa shirika la viwango TBS na TRA na matumizi ya namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN); Uchambuzi, tathimini na mapitio ya ushuru wa huduma (Service Levy); wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania; mawaziri kukutana na wafanayabiashara wote nchini kusikikliza kero; wataalamu wa forodha kukutana na wafanyabiashara kusikiliza kero zao na uratibu wa mrejesho kuhusu utekelezaji wa maazimo kati ya wafanabiashara na serikali.

    Mgomo wa wafanyabishara na kufunga maduka yao ni suala lililoanza taratibu Jumatatu juma Juni 24 baada ya matangazo kupitia mitandao ya kijami kuhusu mgomo huo kusambaa kwa kasi Jumapili Juni 23, huku viongozi wa serikali na vyombo kadhaa vya dola likiwemo jeshi la polisi vikitoa matamko na maonyo kwa wafanyabiashara kutokushiriki mgomo.

    Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo alisema Jumatatu kuwa walikuwa wamekubaliana na wafanyabiashara juu ya masuala ya msingi yanayolalamikiwa ikiwemo TRA kuweka mfumo mpya wa nyaraka na kusitisha operesheni zake ikiwemo kamatakamata.

    Lakini sasa ni dhahiri kuwa suluhisho lililoelezwa na Waziri Kitila Mkumbo halikuwa halisi kwani mgomo umeendelea na kusambaa zaidi.

    Kilicho wazi ni kuwa kuna upotevu mkubwa wa mapato kwa upande wa wafanyabiashara na serikali. Kwa mujibu wa takwimu za TRA za mwaka 2023, makusanyo ya mkoa wa kikodi wa Kariakoo Dar es Salaam pekee kwa siku ni shilingi milioni 472.

    Bado haijulikani ni upi mustakabali wa mgomo huu hususan iwapo wafanyabiashara watafungua maduka baada ya maazimio yaliyofikiwa kati ya serikali na jumuiya ya wafanayabishara.

  11. Rais wa Afrika Kusini amsuta mshirika wake wa muungano katika mvutano mkali

    Rais Cyril Ramaphosa aliongoza ANC kwa matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Rais Cyril Ramaphosa aliongoza ANC kwa matokeo mabaya zaidi ya uchaguzi

    Washirika wakuu wa muungano wa Afrika Kusini wanazozana wiki chache tu baada ya kukubaliana kugawana madaraka, huku Rais Cyril Ramaphosa akimshutumu kiongozi wa chama cha Democratic Alliance (DA) John Steenhuisen kwa kujaribu kuunda "serikali nyingine" inayokiuka katiba.

    Inasemekana alitoa madai hayo katika barua aliyomwandikia Bw Steenhuisen tarehe 25 Juni, ambayo imeonekana na vyombo vya habari vya ndani.

    Masoko yamedorora kutokana na habari za kuongezeka kwa mpasuko, wakati ambapo chama cha Bw Ramaphosa cha African National Congress (ANC) na DA zinapaswa kugawana nyadhifa za baraza la mawaziri na kutulia ofisini.

    Wakati ANC iliposhindwa kupata wingi wa kura katika uchaguzi wa mwezi uliopita, chama kikuu cha upinzani DA kilikubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ambayo ingemweka Rais Ramaphosa madarakani - badala ya wanasiasa wa DA kupata nyadhifa za baraza la mawaziri.

    Kilipata 40% ya kura, wakati DA ilipata 22%

    Hapo awali, wachambuzi waliiambia BBC kwamba pande hizo mbili zinaweza kuzozana wakati zitakapokuwa zikijaribu kufikia makubaliano bora, lakini mawasiliano ya hivi punde yaliyofichuliwa yanaashiria mpasuko ambao baadhi wanahofia huenda ukaathiri makubaliano ya muungano yaliyotiwa saini tarehe 14 mwezi Juni.

    Taarifa za uwezekano wa kusambaratika kwa muungano huo ziliifanya sarafu ya Afrika Kusini, rand, kuporomoka dhidi ya dola.

    Sekta ya biashara imetetea vikali makubaliano kati ya pande hizo mbili, ikiamini kuwa yatasaidia kufikia utulivu wa uchumi.

  12. Mdahalo kati ya Biden na Trump: Je ni nani aliyeibuka mshindi?

    xx

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wanachama wa Republican na Democratic waliotazama mjadala huo kwa karibu wameshiriki mawazo yao na wanahabari wetu.

    Stephanie Murphy, mbunge wa zamani wa Democrat, aliambia BBC kwamba ni wakati ambapo Joe Biden alionyesha umri wake. "Ilikuwa vigumu kumuelewa."

    Lakini kwa upande mwingine, anasema Donald Trump alitoa maoni ambayo "hayakuwa kweli kabisa" na ambayo yangehitaji kukaguliwa.

    Anaongeza kuwa alikuwa na wasiwasi kuhusu kutokuwa tayari kwa Trump kusema atakubali matokeo ya uchaguzi.

    Maelezo ya video, Wanachama wa Republican na Democratic waliutazama mjadala huo

    Anasema kwa ujumla, mjadala uliangazia uzee wa Biden, wakati muundo uliodhibitiwa ulisaidia Trump kutoa utendaji uliopimwa zaidi.

    Rodney Davis, mbunge wa zamani wa chama cha Republican, aliiambia BBC kwamba mjadala huo ulikuwa "ushindi wa wazi kwa Donald Trump," akiongeza kuwa alijiimarisha kama mgombea wa wazi. "Kwa bahati mbaya kwa wafuasi wa chama cha Democratic kote nchini Marekani, muundo huo ulimsaidia Trump," anasema.

    Biden alikuwa na kipindi bora cha pili na hatimaye alipata nguvu ya kumkabili Trump, lakini ilikuwa imechelewa.

    Wadadisi wanahisi Donald Trump "alishinda" mjadala huu.

    Lakini itamsaidia kushinda uchaguzi?

    Soma zaidi:

  13. Mdahalo kati ya Biden na Trump: Yaliyojiri kwa mukhtasari

    Trump na Biden

    Chanzo cha picha, reu

    Rais wa Marekani Joe Biden na mtangulizi wake Donald Trump wamemaliza mdahalo wa Urais wa CNN baada ya takriban saa moja na dakika 40.

    Iwapo uliikosa, haya ndio yaliyojiri:

    • Wagombea wote wawili wamemshutumiana kwa kusema uwongo kwenye mada kuanzia masuala ya maslahi ya Wamarekani, mipaka hadi hali ya uchumi wa Marekani na mfumuko wa bei.
    • Trump alimshambulia Biden mara kwa mara juu ya utunzaji wake wa uchumi na rekodi yake ya sera za kigeni, pamoja na idadi ya wahamiaji.
    • Biden, kwa upande wake, alilenga hukumu za hivi majuzi za uhalifu dhidi ya Trump na kile anachosema ni tishio kwa demokrasia.
    • Biden, wakati mmoja, alionekana kupoteza msururu wa mawazo na kujikwaa katika sehemu mbalimbali, na kusababisha kile ambacho baadhi ya waangalizi wanasema ni "hofu" ndani ya Chama cha Democratic na kampeni ya Biden-Harris.
    • Katika barua pepe za kuchangisha pesa, Trump alidai ushindi katika mdahalo wa usiku wa kuamkia leo, ingawa wakaguzi wa ukweli walitilia shaka madai yake mengi.

  14. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.