Biden v Trump: Wana mitazamo gani kuhusu Urusi, China, Ukraine na Israeli-Palestina?

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Wamarekani wanakaribia kumchagua rais wao ajaye, uchaguzi huo unafuatiliwa karibu kote ulimwenguni. Kwani sera za nje za Marekani, huathiri sehemu mbalimbali za dunia.

Joe Biden na Donald Trump watakuwa na mjadala wa kwanza siku ya Alhamisi, kuelekea uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu.

Waandishi wa BBC wanaeleza matarajio na sera za nje za Marekani panapohusika uchaguzi huu na wagombea wake.

Pia unaweza kusoma

Urusi itafuatilia uchaguzi huu kwa ukaribu

Steve Rosenberg, mhariri wa Urusi

Fikiria wewe ni Vladimir Putin. Je, ungependelea nani katika Ikulu ya White House? Mtu aliyekuita "muuaji" na kuahidi kusimama na Ukraine? (huyo ni Joe Biden).

Au mgombea ambaye amekosoa usaidizi wa kijeshi wa Marekani kwa Kyiv na kusema ataihimiza Urusi kufanya "chochote kile inachotaka," kwa nchi yoyote mwanachama wa Nato, ambayo haitimizi makubaliano ya malipo ya ulinzi (huyo ni Donald Trump).

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amenukuliwa akisema, anapendelea Joe Biden aendelee na kazi yake kwa sababu "anatabirika."

Ikulu ya Urusi, Kremlin ilitamaushwa na muhula wa kwanza wa urais wa Trump.

Mwaka 2016 afisa mmoja wa Urusi alikiri kwangu, kusherehekea ushindi wa Trump kwa sigara na chupa ya shampeni. Urusi ilitarajia kuboreka uhusiano kati ya Urusi na Marekani – jambo ambalo halikutokea.

Yeyote atakayeshinda kinyang'anyiro cha kuwania Ikulu ya Marekani, Urusi itakuwa ikifuatilia kwa karibu dalili za kukosekana utulivu wa kisiasa baada ya uchaguzi na mgawanyiko ili kutafuta njia za kufaidika.

Tofauti kubwa kati yao ni juu ya Taiwan

Laura Bicker, mwandishi wa China

Wagombea wote wawili watakuwa wakali kwa Beijing na wana sera sawa za kiuchumi za kukabiliana na ushawishi wa China ikiwa ni pamoja na kuongeza ushuru kwa bidhaa za bei nafuu za China.

Tofauti kubwa kati ya watu hawa wawili ni juu ya Taiwan. Biden amesisitiza ahadi ya kukitetea kisiwa hicho kinachojitawala ikiwa Rais Xi wa China, atataka kutimiza ahadi yake ya kuiunganisha kwa nguvu Taiwan na China Bara.

Lakini Trump ameishutumu Taiwan kwa kuhujumu biashara za Marekani na amepinga mswada wa Marekani wa kutuma msaada Taiwan. Hilo lilifanya wengi watilie shaka ikiwa atakuwa tayari kuisaidia Taipei ikihitajika.

Wakati Marekani inapiga kura, hakuna uwezekano wa China kuwa na mgombea kipenzi katika pambano hilo.

Kwa maoni ya Beijing, Trump asiyetabirika anaweza kudhoofisha na kuwagawanya washirika wa Marekani katika eneo hilo - lakini pia anaweza kuanzisha vita vingine vya kibiashara.

Hawatatamani pia miaka mingine minne ya Biden. Wanaamini muungano wa washirika wake katika eneo hilo unaweza kuunda Vita vipya Baridi.

Ukraine ni mtazamaji katika uchaguzi huu

Gordon Corera, mwandishi wa usalama, Ukraine

Hakuna nchi ya kigeni ambayo uchaguzi wa Marekani ni muhimu zaidi kuliko Ukraine. Kila mtu anajua msaada wa Marekani wa fedha na silaha umekuwa muhimu katika vita vya Ukraine.

Kuna wasiwasi mkubwa wakati huu miji ikishambuliwa na mabomu ya Urusi na vikosi vya Ukraine vikipambana kuzuia Urusi kusonga mbele.

Wanafahamu sana kile kinachosemwa kuhusu Ukraine wakati wa kampeni. Kwa Donald Trump, wachambuzi wa hapa wanajua amezungumzia kuhusu kumaliza vita na kauli zake za kukata misaada.

Wengine wanahofia anaweza kuilazimisha Ukraine kuingia katika makubaliano ambayo haiyapendi. Wataalamu wanasema kitu muhimu kwa mwanasiasa ni kile anachofanya akiwa madarakani, si kile anachosema wakati wa kampeni au kwenye mjadala.

Na Ukraine inaelewa kuwa hata ushindi wa Joe Biden hautazuia changamoto, ikizingatia kuwa ilichukua muda mrefu msaada wa mwisho kuidhinishwa na Bunge la Congress.

Kwa hivyo hatari kwa Ukraine ni kubwa lakini inabaki kuwa mtazamaji tu, na Marekani kutotabirika ni jambo ambalo Waukraine wamejifunza kuishi nalo kwa muda mrefu.

Waisraeli wengi wanamuunga mkono Trump

Yolande Knell, mwandishi wa Mashariki ya Kati

Rais Biden anaiunga mkono Israel baada ya mashambulizi ya kushtukiza ya tarehe 7 Oktoba na ameendelea kuipatia nchi hiyo silaha hata kama amekuwa mkosoaji wa vita na idadi kubwa ya raia wa Palestina wanaouawa.

Kwa jumla, kura za maoni zinaonyesha sehemu kubwa ya Waisraeli wanafikiria Trump angekuwa bora kwa Israel kuliko Biden. Wengi hawakubaliani na jinsi Biden alivyoshughulikia vita. Na Wapalestina wengi wanamwona kuwa anapuuza wanayopitia.

Waisraeli wanakumbuka vyema jinsi Trump alivyoitambua rasmi Jerusalem kama mji mkuu wao na kuweka mikataba mipya ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi yao na mataifa ya Kiarabu.

Anaunga mkono vita vya Gaza lakini pia ameitaka Israel "kumaliza vita," akisema vinaharibu taswira ya Israel.

Wapalestina wana matumaini madogo katika muhula wa pili wa Biden, lakini Trump anaweza kuwa ni mbaya zaidi. Rais huyo wa zamani ameahidi, iwapo atachaguliwa, atasitisha misaada yote ya Marekani kwa Wapalestina.

Kwa muda mrefu, Rais Biden anaendelea kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili - ingawa hajatoa mpango madhubuti wa kufanikisha jambo hilo. Trump ametilia shaka uwezekano wa kuwepo kwa taifa huru la Palestina.

Kuna ukweli kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu angependa kumuona Trump akirejea madarakani. Lakini, rais huyo wa zamani anasemekana kumchukia Netanyahu kwa kutambua ushindi wa Biden wa 2020.

Maneno mabaya ya Trump yanakumbukwa Mexico

Will Grant, mwandishi wa Mexico

Wananchi wa Mexico hivi karibuni wamefanya uchaguzi wao wa urais na kufanya chaguo la kihistoria; kumchagua Claudia Sheinbaum kama rais wa kwanza mwanamke nchini humo.

Mshirika wake wa karibu, Rais anayeondoka Andres Manuel Lopez Obrador, alianzisha ushirikiano mgumu na Donald Trump alipokuwa katika Ikulu ya White House.

Ingawa uhusiano wa Mexico na Biden wakati fulani umekuwa wa wasiwasi, majirani hao wamepata maelewano katika maeneo muhimu kama vile uhamiaji na biashara ya mipakani.

Mara tu atakapokuwa madarakani, Sheinbaum atahitaji kuonyesha kuwa yeye sio tu nyongeza ya utawala uliopita - na njia bora ya kufanya hivyo ni kujenga uhusiano na Washington.

Kwa hivyo, anaweza kujaribu kuwa tofauti kwa kauli na mbinu za mtangulizi wake - linapokuja suala la kufanya kazi na Biden au Trump.

Akizungumza na BBC kwenye kampeni, Claudia Sheinbaum alisema hatishwi na matarajio ya mwanaume yeyote katika Ikulu ya White House. "Nitapigania watu wa Mexico."

Wamexico wenyewe, wanakumbuka urais wa Trump na kauli mbaya,"wauzaji wa dawa za kulevya, wahalifu, wabakaji," alivyowaita wahamiaji wa Mexico wakati akizindua kampeni zake mwaka 2016.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na Kuhaririwa na Yusuf Jumah