‘Mama yangu aliambiwa nitafariki dunia ndani ya wiki mbili’

ggg

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

  • Author, Veronica Mapunda
  • Nafasi, Mwandishi BBC
  • Akiripoti kutoka Dar es Salaam

Ulikuwa ni usiku wa kawaida kama zilivyo siku nyingine, kitandani binti wa umri wa miaka mitano ambaye hakuwa na ulemavu wowote ule akiwa amelala, alishtuka ghafla na kuhisi kwenda msalani.

Jambo la kushangaza, Zena Akuwa, alishindwa kusimama siku hiyo na kuamua kuomba msaada kutoka kwa mama yake.

“Nilimuita mama yangu ili aniinue lakini kwa sababu mimi ni mtoto wa mwisho mama aliniambia acha kudeka nenda msalani, ile nasimama tu nikaanguka chini”. Anasema Zena.

‘’Nilipoteza uwezo wa kusimama,miguu yangu ilikuwa inalegea kabisa. Kila mtu alishangaa na hata mimi mwenyewe sikuelewa nini kinanitokea, nilikuwa nikisimama sisikii kama nina miguu’’anaeleza zaidi.

Wazazi walipigwa na butwaa na kuamua kumpelekea hospitali na kumhangaikia kwa kila hali ili kupata ufumbuzi wa hali iliyompata.

‘Nilipoteza fahamu tukiwa Mlimba Morogoro, nilipoamka nilijikuta tayari nipo hospitali ya taifa Muhimbili Dar es Salaam’.

Baada ya vipimo vya wataalam, tatizo la Zena halikuweza kubainika chanzo chake kwani hali yake ilikuwa ikibadilikabadilika na ilifika mahali alipoteza uwezo wa kuona.

Hali ya Zena ilifika wakati hata madaktari walikata tamaa iwapo angeendelea kuishi. “Kuna daktari mmoja alimwambia mama inawezekana ndani ya wiki moja au mbili mtoto wako akafariki dunia kwa sababu hata sisi hili tatizo tunashindwa kuelewa ni kitu gani”.

‘’Mama yangu alihangaika sana ili kupata ufumbuzi wa tatizo langu. Alihangaika hospitali, misikitini makanisani ilimradi tu nipate uponyaji”, anasimulia Zena.

Na hapo ndipo safari yake ya ulemavu ilipoanzia, akawa mtu wa kubebwa kila mahali.

Alipoteza matumaini ya kuishi, alikata tamaa na hakuwa akielewa chochote kinachoendelea. Kwa msaada wa madaktari alipata tena uwezo wa kuona.

‘”Nilifumbua macho na fahamu zilirudi na kitu cha kwanza nilimwambia mama yangu naomba chakula. Huenda ndiyo maana napenda sana kupika’’, anasema Zena huku akitabasamu.

Unaweza pia kusoma
Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Kuishi na Ulemavu

“Wazazi na ndugu zangu walinipenda sana na kunijali na baba yangu aliiweka sheria pale nyumbani kwamba ndugu zangu wakitaka kwenda matembezini lazima wanichukue” .

Anaeleza kwamba: Kiukweli kuna wakati nilitamani kucheza na kuishi kama watoto wengine lakini mama alinizuia akisema usiende huko utajiumiza, niliona ananipenda ananilinda nisiumie.’’

“Wakati mwingine alizuia nisichangayike sana na watu ni katika ile hali ya kunijali, lakini nilivyopata akili nilikuwa namsumbua mama sana kwa maswali kwanini mimi niko hivi? mama alinitia moyo kuwa ananipenda na kunijali”. Anaongeza.

Zena anasema mama yake alifanya vile kwa mapenzi lakini baadaye alikuja kugundua kwamba mama yake hakumuandaa kuishi na uhalisia wa ulimwengu kwani baada ya mama yake kufariki dunia Zena anasema aliona rangi halisi za dunia zilizvyogeuka.

Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Safari ya ufukweni ilivyobadili maisha yake

“Wazazi wangu walinipenda sana hawakuruhusu mimi nikutane na changmoto yeyote ile, mtu akiniita jina baya halinifikii lilikuwa linaishia kwa mama yangu, hivyo alivyofariki nilichanganyikiwa”.

Anasema kuwa alikuwa hajikubali kabisa, hata kuweka picha katika mitandao ya kijamii alikuwa anaogopa hata kuhudhuria harusi au mikusnayiko. Aliamua kujitenga na ulimwengu.

“Siku moja tu niliamua, nikasema leo natoka peke yangu na ninakwenda kupanda daladala mwenyewe nataka niende ufukweni”

Anasema alianza kuhisi kukataliwa mara tu baada ya daladala kufika ‘Konda (kondakta wa gari) aliniambia panda haraka haraka watu wengine wapo kama maiti, nilitaka kurudi lakini nikapiga moyo konde’.

Akiwa ufukweni, alifurahia sana upepo wa bahari na mawazo yake papo hapo yalibadilika.

Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Mapishi

Alipata fursa ya kusomea mapishi baada ya kusikia tangazo la kufundisha watu wenye ulemavu bure.

“Mapishi mimi nilikuwa napenda lakini pia mama yangu alikuwa mpishi mzuri nilikuwa namuangalia sana, hivyo nilivyoona hii nafasi nikasema nijaribu”

Anasema anapenda sana vyakula vya baharini: “Napenda kula na nikikupigia vyakula hivyo utafurahia sana na utajirambana na kurudi tena”

Ndoto zake katika mapishi ilikuwa ni kufanya kazi katika hotel kubwa za nyota tano baada ya kumaliza masomo hayo.

Hivyo baada ya kumaliza alianza kutafuta kazi katika hoteli kubwa za jijini Dar es Salaam, lakini alikumbana na changangamoto za kukataliwa kutokana na hali yake ya ulemavu.

“Hoteli ya kwanza waliniambia hapa hatutoi msaada, ya pili waliniambia hatufanyi kazi na watu kama wewe, wateja watasema tunakuonea, ya tatu waliniambia mazingira haya hayakufai kwanini usifume vitambaa?” anaeleza kwa masikitiko.

Hali hii ilimsukuma kuanzisha mradi wake wa kupika huku akiwa na mtaji mdogo tu.

Alianza kwa kupika vyakula vya baharini, hivyo ilimpasa kufunga safari hadi eneo la Feri jijini Dar es Salaam kila siku ili kupata samaki.

Alianza kupika vyakula na kuchapisha katika mitandao ya kijamii huku akitoa elimu ya vyakula vya baharini.

“Nilikuwa mbunifu katika mitandao ya kijamii na jina la Chef Zeny likakua, wapo walioniamini na kuniunga mkono, lakini kuna wengine walihisi kuna ulemavu hadi kwenye chakula changu”

Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Unyanyapaa

“Nilishawahi kupeleka chakula cha watu kama 50, niliambiwa fanya haraka sitaki watu waone chakula kimetoka kwa mtu wa aina gani”

Zena anasema kauli kama hizi zinarudisha nyuma watu wenye ulemavu, kwani chakula hakina ulemavu “Unaponihukumu niambie dagaa kamba hajaiva na si kwa ulemavu wangu”

Akiwa kama mwanaharakati wa walemavu anasema hakusita kumuelewesha mteja wake huku akimsihi kutumia lugha nzuri kwani haamini kama chakula chake kina ulemavu

Zena anasisitiza kwake kuwa uoga hauna nafasi kwenye maisha yake na alishaukataa tangu alipoamua kwenda ufukweni kwa mara ya kwanza.

Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Zena Akuwa ni nani?

Zena Akuwa, 30, almaarufu Chef Zenny ni mtoto wa mwisho katika familia ya Watoto sita. Zena ni mtaalamu wa kupika vyakula mbalimbali ikiwemo vya baharini kama kamba na samaki wengine, vitafunwa na mapishi mengine. Pia ni muandishi wa vitabu vya mapishi vilivyosheheni ujuzi wa aina mbalimbali wa mapishi tofauti tofauti.

Kupitia ukurasa wake katika mitandao ya kijamii pia anatoa elimu kuhusu ulaji sahihi wenye afya kama kula vyakula vya kudhibiti sukari mwilini, kuujua mwili wako na kupangilia milo.

Ni mwanzilishi wa Parachef, Taasisi ya walemavu wanaojihusisha na upishi katika shughuli mbalimbali, pia wanatoa mafunzo ya upishi kwa watu wenye ulemavu. Alianzisha taasisi hiyo baada ya kukataliwa mara nyingi katika kazi.

“Nilipoanza ilikuwa ngumu sana kukubalika, Parachefs inafanyakazi na walemavu wenzangu, nilikuwa nakataliwa kazini na nilirudi chuoni kuangalia ni walemavu wangapi walipata kazi baada ya kumaliza mafunzo nikagundua takribani asilimia 99 hawajapata kazi hivyo nikaanza kuwatafuta ili kuwaunganisha” anaelezea Zena.

Kwa sasa Zena pia ni mwanaharakati wa masuala ya watu wenye ulemavu ambapo amepata fursa ya kushiriki katika majukwaa mbalimbali ya kutetea haki za watu wenye ulemavu ndani na nje ya Tanzania

“Nilienda kwenye mkutano Nairobi, nilialikwa na nilizungumza katika mkutano ule, niliwaambia wasitufanyie maamuzi kama watu wenye ulemavu, watuingize ndani ya mfumo tuseme wenyewe”

Mwaka 2023 Zena ‘Chef Zen’ kwa kushirikiana na chuo kikuu kilichopo Marekani na Tanzania waliwezesha miradi miwili iliyoandaliwa na vijana wenye ulemavu na kuandaa shindano maalumu ambapo lilikuwa na lengo la kufundisha watu wenye ulemavu kuonesha uwezo wao kupitia mitandao ya kijamii.

Zena Akuwa

Chanzo cha picha, Zena Akuwa - Instragram

Ushauri

Watoto ni baraka, mtoto mwenye ulemavu ana haki sawa na mtoto na asiye na ulemavu, hivyo mshirikishe kila kitu katika maamuzi lakini pia mtoe mtoto nje usiamini kuwa dunia itakuwa inampiga tu.

“Mfundishe namna ya kukabiliana na changamoto atakazokubali na, mfundishe mtoto wako namna ya kujipenda mwenyewe na anaweza kuwa kitu chochote” anamaliza Zena

Unaweza pia kusoma

Imehaririwa na Florian Kaijage