Waridi wa BBC: ‘Sitasahau ule wasiwasi uliopitiliza wakati wa kesi ya sheria ya ndoa Tanzania’

Rebeca Gyumi

Chanzo cha picha, Rebeca Gyumi-Instagram

  • Author, Veronica Mapunda
  • Nafasi, BBC Swahili

“Nilikuwa naambiwa waziwazi, msichana gani huyu? atashindana na serikali? Jamii imekaa na ndoa za utotoni muda wote huo, wewe ndiye utabadilisha? Nani atamuoa binti huyu, hayo nilikuwa naambiwa waziwazi” .

January 2016 Rebeca Gyumi aliteka vyombo vya habari baada ya kufungua kesi dhidi ya serikali ya Tanzania akipinga kifungu cha 13 na 17 vya sheria ya ndoa vinavyoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa kibali cha mahakama, na miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi.

Alikuwa kinara na shujaa kwa wengi lakini baadhi walimuona kama mtu anayepinga na asiyefaaa katika jamii huku wengine wakienda mbali zaidi na kumshambulia kwa uamuzi wake huo.

“Hakuna wakati ambao nilielewa kwa undani kuhusu namna mifumo kandamizi inavyofanya kazi kama kipindi ambacho tupo mahakani, nilikuwa naona ilivyokuwa inanichakata na kunichambua” Anasema Rebeca Gyumi.

Akiwa na umri wa miaka 29 wakati huo, Rebeca na wakili Jebra Kambole waliibuka washindi wa kesi hiyo July 08, 2016 baada ya Mahakama Kuu kutoa hukumu ikikubali kwamba vifungu hivyo vya sheria ya ndoa vinapingana na Katiba ya Tanzania kwa kuweka umri tofauti wa kuoa/kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.

Ushindi huu mkubwa kwake ulimfanya kuwa kinara wa kupinga ndoa za utotoni kwa wasichana lakini nyuma ya pazia alikabiliana na mashambulizi mengi ambayo aliweza kuyashinda.

Rebeca anasema “Hakuna wakati nilimuelewa Nelson Mandela kama kipindi kile. Ule usemi wake unaosema ‘kuwa na ujasiri haimaanishi mtu hana hofu, lakini ni kuweza kuishinda ile hofu” anaeleza Rebeca akitabasamu.

Alipigania yote haya ili kumweka mtoto wa kike salama kwa sababu Rebeca anasema kwa Tanzania watoto 3 kati ya 7 wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18.

Je Rebeca Gyumi ni nani

Rebeca Gyumi

Chanzo cha picha, Rebeca Gyumi-Instagram

Rebeca Gyumi ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji katika taasisi ya Msichana Initiative inayolenga kumwezesha mtoto wa kike kupitia elimu, na kushughulikia changamoto muhimu ambazo hupunguza haki ya msichana ya kupata elimu.

Miaka 37 iliyopita, mwanaharakati huyu wa masuala ya wanawake na kinara wa kupinga ndoa za utotoni, alizaliwa katika mji mkuu wa Tanzania Dodoma.

Safari yake katika harakati za wanawake haikuanza tu kwa bahati mbaya bali ina mizizi kutoka katika familia yake enzi za bibi yake.

Bibi yake mzaa baba mwenye jina kama lake Rebeca alikuwa alipigania haki za watoto wake kupata elimu tangu enzi hizo

Rebeca anasema bibi yake huyo alikuwa akitembea umbali mrefu na kuvuka milima na mabonde ili kutafuta shule kwa ajili ya watoto wake.

“Nimekuwa hivi kwa sababu ya wanawake wenye nguvu na imara ambao wamekuwepo kwenye ukoo wangu na wengine ndiyo ambao nimerithi majina yao na wanasema vya kurithi vinazidi, hivyo harakati ni kitu kipo ndani kabisa ya maisha yangu”.

Anasema ameishi na kuona matokeo chanya kwa wazazi wanapoamua kutochagua kusomesha mtoto wa kike au kiume lakini pia namna ambavyo mifumo inapokuwa kandamizi inavyokwaza wasichana kufikia ndoto zao.

Amelelewa na kukua akiona wanawake wachache katika uongozi wa Tanzania kama Dkt. Asha-Rose Migiro aliyekuwa waziri wa sheria na katiba wakati huo ambaye alimvutia na kumpenda.

“Nilimpenda kwa sababu hakukuwa na idadi kubwa ya viongozi wanawake, nilipenda uthabiti wake, nia yake kwamba anaweza kutumia elimu kusimamia haki.

Msukumo wa kutetea haki za msichana pia aliupata kupitia malezi na makuzi kutoka kwa wazazi wake ambao walimlea bila kumkataza kujielezea “Ilikuwa sehemu ya kunijenga kwamba kama nikiona kitu hakiko vizuri nitasema kwa sababu si dhambi”, anaeleza Rebeca

"Lazima mjione kuwa zaidi ya wake za watu" Ni kauli iliyompa hamasa sana ya kuwa na ndoto fulani katika maisha.

Licha ya kuwa maeneo kama ya kanisani wakati mwingine yanaweza kuwa yanaendeleza mifumo kandamizi lakini kwake anasema wanawake wa kanisani waliweza kuchochea kufikia ndoto zake.

“Namkumbuka mama mmoja wa kanisani kwetu "mama Mdendema" alipenda sana kutufundisha wanawake kwamba tuwe watu wenye maono”.

Harakati za wanawake

Safari ya harakati za kumtetea msichana zilichochewa haswa na kazi ya kujitolea aliyoianza katika taasisi ya kiraia Fema iliyowakusanya vijana mbalimbali nchini Tanzania kwa lengo la kuwawezesha kujitambua kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa ikiwemo afya ya uzazi, Elimu jamii na kiuchumi.

‘Kupitia taasisi hiyo niliweza kuzunguka maeneo mengi ya nchi yetu nilikutana na vijana wengi lakini changamoto za wasichana kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito zilinikera na kuniudhi sana.

“Unakuta msichana kapata ujauzito akiwa darasa la 5 au 6 hapo ni kama miaka 14 au 16 ambayo ni mtoto kisha anaozeshwa kwa mwanaume huyo"ilikuwa inaniumiza sana”,anasema Rebeca.

Kupitia asasi ya kiraia ya Fema, Rebeca alibaini tatizo la wasichana kuacha shule kutokana na ndoa za utotoni na ujauzito ni kubwa.

“Nilifanya kazi na Femina nilizunguka mikoa mingi lakini kila nilipokuwa nakwenda nilikuwa nakutana na matatizo ya wasichana kuacha shule kisa kaozwa au mimba”

Hii ilimpa msukumo wa kusoma taaluma ya Sheria mwaka 2008 hadi 2012 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuchimba kwa undani sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo inaruhusu wasichana wenye umri wa miaka 14 kuolewa huku wavulana wakiruhusiwa kuoa wakiwa na umri wa miaka 18.

Hiyo ilimpa nafasi Rebeca kuangalia uwezekano wa kwenda kuipinga sheria hii ili ibadili umri huu kwa mtoto wa kike.

Akiwa ndiyo kwanza ameanzisha taasisi yake ya Msichana Initiative, pamoja na wakili wake Jebra Kombole, alifanya utafiti wa kina ili kupata nyaraka na hoja zitakazosaidia kesi yao.

‘Nilifungua lile shauri nikiwa na hasira sana kuona watoto wa kike wanaacha shule kwa sababu za kuozwa au ujauzito’.

Elimu

Rebeca Gyumi

Chanzo cha picha, Rebeca Gyumi

‘Elimu ni kila kitu kwangu, ndiyo nyenzo iliyoniwezesha kubadilika na kubadili jamii yangu’, anasema.

Baada ya kufaulu vizuri darasa la saba alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Kikuyu Dodoma ambapo baada ya miaka minne alifaulu kwa daraja la kwanza na kujiunga na shule ya wasichana wenye vipaji maalum Kilakala Morogoro alikohitimu kidato cha sita 2008 kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea sheria.

Kutambuliwa Kimataifa

Kupitia taasisi yake Rebeca ametambuliwa na kushinda tuzo mbalimbali kimataifa ikiwemo ile Tuzo ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa mwaka 2018.

Pia amepata fursa ya kukutana na viongozi wakubwa duniani kushiriki mijadala na watu mashuhuri duniani.

Novemba, 2023 alishiriki mjadala katika jukwaa moja na aliyekuwa mke wa rais wa Marekani Michelle Obama, Melinda Gates na mke wa mcheza filamu maarufu wa Marekani Amal Clooney.

‘’Kukutana na wanawake wenye ushawishi duniani, viongozi wakubwa ni jambo linaloninyenyekeza sana na kunihakikishia kwamba ninaweza kuwa chochote ninachotaka’’.

Kadhalika alikuwa miongoni mwa watu wanne walioalikwa kukutana na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Frank-Water Steinmeier na jopo lake na kuzungumza masuala mbalimbali kuhusu masuala ya jinsia na elimu.

“Mimi kukaa na watu mashuhuli sana duniani inanikumbusha kuwa nina wajibu mkubwa, nimekaa na kina Michelle Obama wananisikiliza ni kitu kikubwa kwangu”

Familia

Rebeca Gyumi na mumewe siku ya ndoa yao

Chanzo cha picha, Rebeca Gyumi

Rebeca anajivunia kuwa na mume ambaye amekuwa msaada mkubwa kwake katika kufanikisha shughuli zake.

Anasema katika familia yenye watoto watatu imekuwa ngumu kwake kujigawa muda wa kazi na nyumbani lakini kwa msaada wa mume wake na kumuelewa amekuwa akimpa moyo wa kuendelea kupigania watoto wa kike.

“Mume wangu ambaye wakati wa kesi alikuwa mpenzi tu allikuwa akinipeleka hadi mahakamani wakati wa kesi, ninamshukuru sana”

Ujumbe kwa jamii

‘Wasichana wajengewe kujitambua, wafundishwe ‘K’ tatu ambazo zinamaanisha: Kujitambua, Kujiamini na Kuwa na ndoto’, anaweka bayana.

Imehaririwa na Florian Kaijage