Je, machozi ya wanasiasa huwaweka karibu na wananchi?

fd

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama
  • Author, Nicola Bryan
  • Nafasi, BBC

'Wanaume hawalii' ni msemo wa zamani. Lakini hali ikoje kwa wanasiasa katika suala hili? Watu hufikiria nini wanasiasa wanapotokwa na machozi?

Hivi karibuni, Waziri wa kwanza wa Wales, Vaughan Gething, alionekana akitokwa na machozi kabla ya hoja ya kutokuwa na imani nae kujadiliwa katika Bunge la Wales. Na alishindwa katika kura hiyo.

Gething alijiunga na orodha ya viongozi wa dunia ambao wamemwaga machozi hadharani, kutoka Winston Churchill hadi Obama.

Je, watu wanawaona viongozi wanaomwaga machozi hadharani ni watu wenye utu? Au wanadhani ni dalili ya udhaifu wao?

"Viongozi hutaka kuonesha hisia zao. Kuzielewa hisia ni mhimu,'' anasema Guto Harry, mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson.

“Lakini ukweli ni kwamba watu hawapendi kuwaona viongozi wao ni dhaifu. Hata uwe mwema na mwenye huruma kiasi gani, ukionekana unalia, unaonekana ni dhaifu,” anasema Harry.

Pia unaweza kusoma

Matukio ya Viongozi Kulia

ZX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwendazake Malkia Elizabeth wa Uingereza

Viongozi wengi katika nyanja ya kisiasa na nje ya siasa, wamenaswa na kamera wakimwaga machozi. Winston Churchill alikuwa akilia hadharani.

Malkia wa Uingereza alionekana akipangusa machozi wakati boti aliyoipenda ilipoondolewa katika matumizi mwaka 1997. Mwaka 2019, alionekana pia akitokwa na machozi wakati wa ibada ya Jumapili ya Ukumbusho.

Mwaka 2013, Kansela George Osborne alitoa machozi kwenye mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher.

Wakati wa uongozi wake, Obama ameonekana mara kadhaa akitokwa na machozi hadharani. Baada ya mauaji ya Sandy Hook ya 2012, alitokwa na machozi. Pia alitokwa na machozi katika maonyesho ya Aretha Franklin 2015.

as

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Theresa May

Mwaka 2019, Theresa May alimwaga machozi alipotangaza kujiuzulu kama Waziri Mkuu wa Uingereza.

Video ya Gething akibubujikwa na machozi, akimfariji Mnadhimu Mkuu wa Serikali ya Wales, Jane Hutt na kufuta machozi yake kwa tishu ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Wapo wanaoamini machozi haya ya mbele ya kamera ni ya uongo. Ingawa Harry, anaamini ni machozi ya kweli. Anasema katika hali kama hizi, hisia zao huwa ni za kweli.

Kulia sio udhaifu tena

l

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi

Hapo zamani wanaume walichukuliwa kuwa dhaifu wanapolia, lakini sio sasa.

“Kulia hadharani ni hatari sana. Kwa sababu watu hudhani ni machozi ya uongo, kwamba wanalia mbele ya watu ili upate huruma kutoka kwao,'' anasema Harry.

"Mara nyingi katika siasa au maisha, watu hulia ili kuondoa msongo wa mawazo wa mfadhaiko. Kwa mfano, mpenzi wako amekuacha. Kwa sababu unataka huruma kutoka kwa wengine. Unalia, ila kulia hakushawishi watu vya kutosha kuwafanya wakuamini.

"Katika historia, maoni ya watu kuhusu kulia hadharani yamebadilika," anasema Bernard Kapp, profesa mstaafu wa historia katika Chuo Kikuu cha Warwick, Uingereza.

''Wakati wa Ugiriki ya kale, au Roma, na Uingereza wakati wa Enzi ya Kati, wanaume walionyesha hisia zao waziwazi. Miongoni mwa hisia hizo ni kulia. Pia walikuwa wakionyesha hasira zao waziwazi," anasema.

"Baadaye, yaani, karne ya 18 na mapema ya 20, ilianza kuonekana kuwa kudhibiti hisia zako na usizioneshe hadharani ndilo jambo bora."

"Lakini siku hizi watu kutoka nyanja kama vile siasa na michezo wanaonyesha hisia zao waziwazi," anaelezea Bernard Kapp.

"Huwezi kuona mfanyabiashara maarufu akilia wakati anaondolewa kwenye bodi ya kampuni. Lakini katika siasa, Mawaziri Wakuu wa Uingereza, Thatcher na Theresa May walimwaga machozi walipojiuzulu. Pia, Waziri Mkuu, Winston Churchill alilia katika Baraza la Commons. Pia alitoa machozi alipokwenda kwenye miji ya Uingereza iliyoshambuliwa na Ujerumani," anasema Kapp.

Hakuna haja ya kujificha

xc

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Kansela George Osborne (katikati) akiomboleza kifo cha Margaret Thatcher

David Cameron, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, alionekana akitabasamu wakati wa kujiuzulu. Kwa kufanya hivyo alitaka kuonyesha kwamba alikuwa na uwezo wa kudhibiti hisia zake.

Mark Borkowski ni mshauri kuhusu migogoro, anaefanya kazi na mashirika ya kimataifa, anasema, “ikiwa atatakiwa kutoa ushauri kuhusu kulia hadharani, anasema hakuna haja ya kuficha machozi.”

“Ondoa maumivu yako kwa kulia. Lakini usitegemee sana kilio kama njia ya kuondoa maumivu. Unaweza pia kuondoa maumivu kwa njia zingine.”

“Watu wa Uingereza kwa sasa wako huru zaidi kueleza hisia zao hadharani kuliko wanasiasa,” anasema Mark.

“Wanasiasa wakati mwingine hujaribu kuonyesha uwezo wao mbele ya umma na kuficha udhaifu wao. Lakini, sisi ni binadamu na ni dhaifu pia. Tunafanya makosa. Hakuna aliye mkamilifu," anaeleza Mark.

Anasema suala muhimu ni kuacha maumivu yako nyuma na kusonga mbele.

i

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa zamani wa India, Indira Gandhi amevalia miwani ya jua wakati akiomboleza kifo cha Sanjay Gandhi Juni 25, 1980.

Waziri Mkuu wa zamani wa India Indira Gandhi hakupenda kulia, au kuonekana akilia hadharani.

Wenzake waliokwenda kuomboleza kifo cha mwanawe Sanjay Gandhi, walishangaa kuona macho yake hayatoi machozi licha ya msiba huo mkubwa.

Watu wa India hawatasahau tukio la Indira Gandhi kuvaa miwani ya jua (miwani nyeusi) wakati wa ibada ya mwisho ya mwanawe, ili asionekane kwa umma ikwia macho yake yatalowa machozi.

Lakini Waziri Mkuu wa sasa Narendra Modi ameonyesha hisia zake katika mahojiano kadhaa ya TV. Modi amezungumza kwa sauti ya kutetemeka mara kadhaa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah