Jinsi zana hizi tatu zilivyotumiwa na Gen Z kuishinikiza serikali ya Kenya

TH

Chanzo cha picha, Getty Images

Imekuwa wiki ya matukio mengi nchini Kenya .

Mswada wa Fedha wa serikali uliokuwa ukipendekeza ushuru zaidi ili kufadhili bajeti ya mwaka mpya wa kifedha ulisababisha lalama za Wakenya wengi na hasa vijana walioamua kwenda barabarani kuandamana ili kuupinga .

Maafa,majeruhi na uharibifu wa mali vimetokea na kutilia doa kilichoanza kama vugu vugu la amani mtandaoni la kupaza sauti za vijana kueleza pingamizi zao dhidi ya mswada huo .

Hatahivyo wakati historia ya mwamko huo wa vijana kuhusiana na masuala ya utawala na kisiasa itakapoandikwa, mchango mkubwa kuhusu athari za mitandao ya kijamii na intaneti ni mambo ambayo yatakuwa na nafasi kubwa sana katika simulizi hiyo.

Katika maandamano hayo na harakati za kupinga mswada huo ,vijana waliibuka kuwa na silaha kali na wezeshi-Simu zao za mkononi,intaneti na mitandao ya kijamii.

Huo ulikuwa mseto wa zana ambazo hata serikali haikuwa imejitayarisha ifaavyo kukabiliana nazo .

Kwa mara ya kwanza katika taifa hilo la Afrika mashariki,vijana wa kizazi ambacho kiliitwa ‘Wapambanaji wa mitandao’ waliwashangaza wengi kwa kutumia weledi wao katika nyanja hiyo na mitandao ya kijamii kuungana ,kutoka majumbani na kuingia barabarani na mitaani kuandamana.

Waliotilia shaka uwezo wao huo walikiri kwamba hatua zao hizo zimepata ufanisi kwani Jumatano tarehe 26 rais William Ruto alisalimu amri na kuuondoa mswada huo ambao ulikuwa umepitishwa na bunge na kilichokuwa kimesalia ni sahihi yake tu .

Kwa vijana hao wa Gen Z,huo ulikuwa ushindi muhimu sana ikizingatiwa kwamba pingamizi za wananchi wengi dhidi ya mswada huo zilipuuzwa na kamati ya bunge ya mipango na fedha,wabunge na hata rais mwenyewe hadi pale lalama hizo zilipozaa zogo la Jumanne na kusababisha maafa .

Wengi hawakufahamu machungu yao hadi pale maandamano hayo yaliposambaa kote nchini na wenzao katika miji mbalimbali ya nchi kando na jiji kuu la Nairobi walipojitokeza katika sehemu zao kubeba mabango ili kulalamikia mswada huo wa fedha na sera nyingine za ushuru ambazo walidai serikali ya rais William Ruto imezitekeleza.

Unaweza Pia Kusoma

Mijadala na Hashitagi

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Katika kumbi za midahalo ya mitandao ya kijamii kama Twitter Space kwenye X na Tiktok,vijana ambao awali maudhui yaliyowavutia yalikuwa mambo ya burudani-ilianza kutawala mijadala kuhusu ukali wa maisha ,gharama ya juu ya bidhaa, ubadhirifu wa fedha za umma,ukosefu wa ajira,uhalifu na mambo mengi yaliyowakwaza.

Vijana walianza kuzungumza kuhusu yaliyomo katika mswada huo wa fedha na jinsi maisha yao yatakavyoathiriwa iwapo mswada huo ungekuwa sheria.

Baadhi ya vijana walitafsiri mswada huo kwa lugha nyepesi na hata lugha za mama na kusambaza video za mafunzo yao kwa wenzao kupitia mitandao ya kijamii.

Muda usiokuwa mrefu ,hashitagi ya #rejectfinancebill ilishika kasi katika mitandao ya kijamii.

Ujumbe uliwafikia wengi sio tu Kenya bali hata wananchi wengine wanaoishi ng’ambo.

Kupitia kampeni hizo kali, ujasiri uliwajaa na mwelekeo wa kuingia barabarani ili kulalamika wazi kuhusu mswada huo ukaonekana.

Mabango na maelekezo ya sehemu za kukutana na kwenda kuandamana yalichapishwa na kusambazwa mitandaoni.

Chombo chenye nguvu

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Mchambuzi wa masuala ya Kisiasa Calvin Muga anasema kuwa matumizi ya Mitandao ya Kijamii na intanteni yalikuwa chombo muhimu sana cha kupashana habari kabla ,wakati na baada ya maandamano ya vijana.

Anasema matumizi yake ni ya juu sana kwa kizazi cha Gen Z na hata miongoni mwa kile cha Millenial kwani makundi hayo yanatumia muda mwingi sana katika mitandao ya kijamii.

Intaneti na mitandao ya kijamii hutumiwa kwa kazi na hata mawasiliano ya kikazi yametegemea sana mitandao na hivyo basi kukifanya chombo hicho kuwa nguzo muhimu ya maisha ya kila siku ya vijana wengi nchini kenya .

‘Wengi wao wana uzoefu na ni watumizi wakubwa wa mitandao ya kijamii na hili lilirahisisha sana wao kuwasiliana na kupanga maandamano yaliyofanyika’ anasema Muga.

Jambo jingine ambalo liliwafanya vijana nchini Kenya kuwa na mvuto wa kushiriki kabisa katika pingamizi dhidi ya mswada huo wa fedha ni mapendekezo katika mswada huo kuongeza ushuru kwa huduma za intaneti na tozo zaidi kwa malipo ya miamala.

Muga anasema wengi wa vijana wanategemea kipato kutoka kwa mitandao kama Youtube na mapendekezo ya kutoza ushuru tasnia ya burudani na ubunifu wa mtandao pia haikupokelewa vyema .

Iwapo daalili hizo za jinsi hali ilivyokuwa ikishika kasi mtandaoni ni jambo ambalo serikali ililiona mapema na kupuuza ni kitu ambacho hakitajulikana kwa sasa ila ilikuwa wazi kwamba hamaki zilikuwa zimewachemka wengi .

Baadhi ya viongozi wa kisiasa waliojaribu kujiunga na vikao vya midahalo mtandaoni walikemewa na vijana na hata kufurushwa katika kumbi hizo mtandaoni.

Bunge lilipovamiwa na vijana siku ya Jumanne tarehe 25 ,yote yaliyokuwa yakifanyika yalinaswa mubashara katika mitandao ya kijamii na vituo vya runinga nchini .

Kupigwa risasi kwa waandamanaji,uporaji,wabunge wakikimbilia usalama wao,magari ya ambulansi yakiwachukua waliojeruhiwa ,moshi ukitanda baada ya sehemu la majengo ya bunge kuchomwa-yote yalinaswa na kupeperushwa mtandaoni.

Ilikuwa kama filamu na hapo ndipo uhalisia wa ukubwa wa kilichokuwa kikifanyika ulipodhihirika kwa maamlaka.

Wakenya na hasa vijana walikuwa wakiona moja kwa moja jinsi wabunge - ambao ni waakilishi wao walivyokuwa wakiujadili mswada huo na hata walifahamu misimamo ya kila mmoja wao.

Mwanzoni kabisa wa mswada huo kuwasilishwa bungeni,ishara zilikuwepo za jinsi pingamizi dhidi ya mapendekezo hayo zilivyokithiri.

Nambari za simu za wabunge zilivujisshwa na kusambazwa mitandaoni. Watu wakaztumia kuanza kuwatumia wabunge jumbe na kuwapigia simu ili waukate mswada huo.

Tume ya Data nchini ilionya dhidi ya kuvujishwa kwa maelezo ya kibinfasi ya viongozi mtandaoni lakini hilo lilipuuzwa na vijana.

Kubanwa kwa huduma za intaneti

TH

Chanzo cha picha, EPA

Ilipobainika wazi kwamba mtandao ulikuwa kiunganishi muhimu cha mawasiliano na uratibu wa shughuli za maandamano ya vijana ,palitokea usumbufu wa huduma za intaneti.

Inahofiwa na wadadisi kwamba huenda usumbufu huo ulikuwa hatua ya maamlaka kuingilia huduma za intaneti-lakini hilo halijathibitishwa

Hatahivyo maswali zaidi yameibuka baada ya kampuni za huduma za mawasiliano kutoa maelezo ambayo hayajaonekana kuwaridhisha wengi.

Kampuni kubwa ya mawasiliano nchini Safaricom ilitoa taarifa kusema kuwa usumbufu huo ulisababishwa na kukatika kwa nyaya za faiba chini ya bahari.

Lakini shirika linalochunguza kutatizika kwa matumizi ya intaneti la Netblocks lilisema baadaye katika tathmini yake kwamba ‘hapajakuwa na ushahidi hadi sasa kwamba kilichotokea ni kukatika kwa nyaya za chini ya bahari’.

Iwapo kulikuwa na mkono wa serikali katika kubinya kasi ya intanenti,basi hatua hiyo inatishia kuiweka Kenya katika orodha ya mataifa ya Afrika ambayo yametumia mbinu hiyo kupambana na upinzani au manung’uniko dhidi ya serikali .

Mbinu kama hizo zimetumiwa na nchi kama vile Senegal mwezi Februari wakati waandamanaji walipopinga hatua ya Rais wa wakati huo Macky Sall kuahirisha uchaguzi,DRC,Sudan na Somalia .

Kinachobainika wazi sasa ni jinsi mitandao ya kijamii inavyochukua nafasi kubwa sana katika kuendeleza mijadala kuhusu masuala ya siasa katika nchi kama Kenya na ushawishi au nguvu ya chombo kama hiki katika kuleta uajibikaji .

Muga anasema kuna hatari ya serikali za matifa ya Afrika kulifanya kuwa jambo la kawaida kubana matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii ili kukwepa kuajibishwa lakini vijana watazidi kuvumbua njia zaidi za kuweza kuwasilisha ujumbe wao na kutaka kusikilizwa .

‘ Vijana wa Kenya walitumia mitandao ya kijamii na intaneti kama nyenzo muhimu ya kudumisha utawala bora na kuwawajibisha viongozi na kutumia mamlaka yao.’