'Sina damu mikononi mwangu,' asema Ruto

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Kenya William Ruto sasa anadai kuwa hana damu mikononi mwake kufuatia mauaji ya watu yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

Kulingana na Ruto ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kikao na wanahabari katika Ikulu Jumapili, Juni 30, maafisa wa polisi walitekeleza majukumu yao kwa njia huru wakati wa maandamano hayo.

Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) katika rekodi, imesema watu 23 walifariki kwa kupigwa risasi na polisi kote nchini. Zaidi ya hayo, kulikuwa na zaidi ya watu 50 waliokamatwa, 22 kutekwa nyara, na zaidi ya 300 kujeruhiwa.Rais Ruto hata hivyo alishikilia kuwa ni watu 19 ndio waliofariki.

Kuhusu hashtag inayovuma ya 'Ruto lazima aende', rais alisema kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake.

TH
Unaweza Pia Kusoma

Matamshi ya Ruto yanakuja kutokana na maandamano ya nchi nzima kupinga nyongeza ya ushuru iliyopendekezwa katika Mswada wa Fedha wa 2024, ambao umeondolewa na wasiwasi ulioibuliwa kuhusu utawala duni.

Kenya Kukopa shilingi trilioni moja baada ya kukataliwa kwa Mswada wa Fedha

Rais Ruto alitoa taswira ya kutisha ya mustakabali wa nchi siku ya Jumapili, kufuatia kukataliwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 uliopendekezwa.

Kulingana na Mkuu wa Nchi, Kenya imerudi nyuma miaka miwili na itahitaji kukopa Takriban Ksh.1.2 trilioni mwaka huu ili kuendesha

"Tumetupilia mbali Mswada wa Fedha. Hiyo inamaanisha nini? Ina maana kwamba tumerudi nyuma kwa takriban miaka 2," Rais Ruto aliambia wanahabari katika Ikulu Jumapili.

TH

Rais alisema kwamba kutupilia mbali Mswada wa Fedha kunamaanisha kuwa serikali haitaweza kuwaajiri walimu 46,000 wa Shule za Sekondari za JSS kwa kandarasi za kudumu na za pensheni.

Alisema kuwa bila fedha ambazo utawala wake ulitarajia kupata, haitawezekana kuwasaidia wakulima wa Kenya katika kuhakikisha wanapokea angalau Ksh.50 kwa lita moja ya maziwa.

Rais Ruto alitangaza Jumatano iliyopita kwamba hatatia saini Mswada tata wa Fedha kuwa sheria, kufuatia siku kadhaa za machafuko na maandamano katika zaidi ya kaunti 15.

Mswada huo ulikusudiwa kukusanya shilingi bilioni 346 za Kenya (dola bilioni 2.68), au 3% ya Pato la Taifa, katika mapato ya ziada.

Kenya ilikubali mkopo wa miaka minne na IMF mnamo 2021, na kutia saini kwa mkopo wa ziada kusaidia hatua za mabadiliko ya hali ya hewa mnamo Mei 2023, na kufanya jumla ya mkopo wake wa IMF kufikia $3.6 bilioni.

Kupunguza matumizi ya fedha serikalini

Afisi za Mke wa Rais Rachel Ruto na mke wa naibu wake Rigathi Gachagua , Dorcas Rigathi hazitajumuishwa katika bajeti mpya, Rais William Ruto ametangaza.

Rais aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Ikulu Jumapili, Juni 30.

“Ofisi kama ile ya Mke wa Rais zilikuwepo hapo awali, lakini kuanzia kesho tunakwenda kuzifuta ofisi hizo na nyinginezo ili tuangalie matumizi yetu,” alisema.

Zaidi ya hayo, rais alisema nafasi za Katibu Mkuu Tawala (CAS) zitaondolewa.

"Kuhusu CASs, mahakama ilitoa tamko kuhusu hilo na tumeheshimu hilo. Hakuna CAS atakayeteuliwa hadi tuwe na uchumi unaounga mkono fursa zaidi," alisema.

Rais alikuwa ameteua maafisa hao 50 kuhudumu afisini lakini ombi lililowasilishwa mahakamani lilipinga kubuniwa kwa nyadhifa hizo.

Kuhusu utajiri wa baadhi ya viongozi washirika wa muungano tawala wa Kenya Kwanza, Ruto alisema; "Nawaahidi, angalieni kitakachofuata. Tukisonga mbele mtaona mabadiliko kwa sababu ni lazima tufanye kitu kuhusu utajiri wa aina hii na ubadhirifu. Tunakwenda kuchukua hatua ambazo zitatuweka mahali pazuri," alisema.

TH

Rais alisema mali ya thamani ya Sh bilioni 2.4 iliharibiwa na ofisi za Jaji Mkuu, Bunge na Ukumbi wa Jiji kuteketezwa wakati wa ghasia za wiki nzima.

“Maisha yoyote ya Mkenya yaliyopotea yananisumbua, na ndiyo sababu nilipochaguliwa nilisema kwamba hakutakuwa na mauaji ya kiholela nchini Kenya. Pia nilihakikisha kuna Huduma Huru ya Polisi na kutia sahihi vyombo vinavyofaa kwa polisi kufanya kazi kwa uhuru,” alisema Ruto.

Rais alisema watoto wamekuwa wahanga wa maandamano,.

Mazungumzo na vijana

TH

Rais William Ruto ameeleza nia yake ya kujihusisha na vijana kwenye X Space.

Hii inafuatia wito wa Wakenya, hasa Gen Z, kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ambao wamesema kwamba ikiwa mazungumzo yoyote yatafanyika na serikali, yafanywe kwenye X space.

Katika mahojiano na wanahabari Jumapili, Rais alisema yuko tayari kujadili masuala yoyote ambayo wanaweza kuwa nayo.

“Nasikia vijana wanasema hatutaki jukwaa la sektambalimbali labda tufanye mazungumzo na Rais kwenye X. Mimi niko tayari kufanya mazungumzo na vijana kwenye jukwaa hilo. Wakitaka nishirikiane nao kwenye X, nitakuwepo," alisema.

"Nataka tujadili kuhusu kodi, nataka tujadili ukosefu wa ajira, rushwa na masuala yote."

Vijana wamekuwa wakiandaa maandamano nchini kote kwa wiki mbili kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024, ambao Ruto alioundoa kujibu shinikizo zinazoongezeka.