Uhaba wa maji: Ni wakati wa jiji la Dar es salaam kufunga mkanda?

Yusuph Mazimu, BBC Swahili

DSM

Chanzo cha picha, Getty Images

Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linakadiria kwamba tatizo la uhaba wa maji, litakuwa moja ya janga kubwa duniani katika muongo mmoja ujao. Hata Ripoti ya tano ya tathimini ya mabadiliko ya tabia nchi ya mwaka 2015 ilionya kuhusu upungufu wa rasilimali ya maji duniani. Huenda sasa athari zimeanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Afrika Mashariki kama Somalia, Ethiopia mashariki na kati, maeneo ya Pwani ya Kenya na Tanzania, likiwemo jiji la Dar es Salaaam. Jiji hilo linalokadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 6 linapitia kwenye majaribu ya uhaba wa maji katika kipindi cha hivi karibuni huku upatikanaji wa maji ukipungua mpaka asilimia 64%, kwa mujibu wa mamlaka za mkoa huku mahitaji halisi ya maji ya jiji hilo kwa siku ni lita zaidi ya milioni 450.

Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka ni kwamba kiwango cha uzalishaji maji katika mitambo ya Ruvu juu na chini inayotumika kusambaza maji katika jiji hilo na maeneo ya Pwani kimepungua kutoka lita milioni 466 kwa siku mpaka 300.

Hali hii inakuja ikiwa ni miezi mitatu tu imepita tangu Mamkala ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) itoe tathimini yake ikisema jiji hilo linajitosheleza kwa maji kwa karibu asilimia 96. Kulikoni sasa?

Nini kimetokea na kwanini kina kipungue?

DAWASA

Chanzo cha picha, DAWASA

Maelezo ya picha, Kazi za kusafisha chanzo cha mto Ruvu zikiendelea, mto unaotumika kuzalisha asilimia 90 ya maji ya jiji la Dar es Salaam kupitia mitambo ya Ruvu juu na Chini

Kupungua kwa kina cha maji kunakotajwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Bwana Makalla kunatokana na upungufu wa mvua ambao pamoja na sababu zingine unahusishwa pia na athari za moja kwa moja za mabadiliko ya tabia nchi.

Na upungufu huu haugusi jiji hili pekee, karibu maeneo mengi ya nchi hiyo japo makali yake hayawezi kufanana. Kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara ya maji kwa mwaka huu wa fedha hadi kufikia Aprili, 2022 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji mijini ilipungua kwa kutoka asilimia 86.5 hadi 86.

Ruka Twitter ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Mkuu wa mkoa anasema hakuna hila katika upungufu huo wa maji. “Hakuna makusudi yoyote iliyofanyika labda tuweze kukosa maji, suala ni mvua, ni kwamba kina cha maji kimeshuka’, alisema na kuongeza, ‘Upatikanaji wa maji katika chanjo ni asilimia 64% sio mia kwa mia, kwa hiyo kwa vyovyote vile lazima kutakuwa na kamgao ka maji kwa sababu maji hayapatikani inavyotakiwa’.

Makali ya mgao yanonekana. Harusi Masanja, mkazi wa Salasala anasema ‘Ninapoishi ni mita chache kutoka tanki kubwa la maji la DAWASA, lakini nyumbani hatuna maji, na haijaanza jana na sijui itaisha lini’.

Je wakati wa kufunga mikanda kwa uhaba wa maji?

Dawasa

Chanzo cha picha, Dawasa

Maelezo ya picha, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akizungumza na wanahabari kuhusu tatizo la maji Dar es Salaam

Kwa wiki mbili sasa, wakazi wa jiji hilo na maeneo ya pwani wamekuwa katika ‘mgao’ wa maji usio rasmi kutokana na kupungua kwa kina cha maji katika mitambo tegemezi ya uzalishaji wa maji ya Ruvu chini na Ruvu juu.

Huenda hali hiyo ikaendelea kwa vipindi tofauti vya ukame katika kipindi cha miezi 6 ijayo, kufuatia taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA).

‘Kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali’ sehemu ya taarifa ya TMA kuhusu utabiri wa mvua za masimu (Novemba 2022 mpaka April, 2023).

Ruka Twitter ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

Mwisho wa Twitter ujumbe, 2

Na hilo linawasukuma wakazi wa jiji hilo kuanza kufikiria kuhusu kufunga mkanda katika kipind hiki.

‘Nimejiandaa kwa lolote, ingawa naamini Serikali itafanya kitu’, anasema Harusi.

Mpaka sasa hatua za muda mfupi zinazochukuliwa na Serikali kupitia mamlaka ya maji ya DAWASA ni kukamilisha mradi wa maji wa Kigamboni utakaozalisha takribani lita milioni 60 kwa siku.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi huu.

Cop27 kuiokoa Dar es salaam na miji mingine Afrika?

Dawasa

Chanzo cha picha, dawasa

Viongozi wa dunia wakiwa sehemu ya waalikwa 200 wanajiandaa kukutana mwezi ujao huko Misri katika mkutano wa 27 wa mabadiliko ya tabia nchi (COP27) chini ya Umoja wa Mataifa.

Ni moja ya mikutano ya kilele ya Umoja wa mataifa inayoangazia namna ya kupunguza joto duniani ili kuondoa athari zake, ikiwemo ukame na kupunguza vina vya maji.

Ingawa matokeo yake si ya haraka, nchi zinazoendelea kama Tanzania zinatarajiwa kuwekewa mipango ya fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake.

Mwaka 2009, nchi zilizoendelea zilijitolea kutoa dola bilioni 100 kwa mwaka, ifikapo mwaka 2020, kwa nchi zinazoendelea ili kuzisaidia kupunguza utoaji wa gesi hizo na kujiandaa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Fedha hizi ni kupunguza shughuli zinazochangia ongezo la joto duniani. Jiji kama Dar es salaam litakuwa moja ya mnufaika kama hilo litafanyiwa kazi ipasavyo. Hata kama litakua ni la muda mrefu.

Kwa mujibu wa DAWASA, hatua za sasa za muda mfupi, mradi wa kigamboni utakua msaada ukitarajia kupunguza uhaba wa maji hasa katika wilaya za Ilala na Kigamboni.

Wakati ikiendelea kusubiri kina cha maji kiongezeke kwenye mitambo yake kwa "kudra za mvua" mambo mengine ambayo yanatajwa kufanywa na Dawasa sasa ni kutumia visima virefu zaidi ya 170 vilivyopo ambavyo mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amepanga kuvitembelea ijumaa hii.