Mauaji ya halaiki yasiyotajwa yaliyotekelezwa na Ujerumani barani Afrika

cx

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wafungwa wa jamii ya Herero waliofungwa minyororo 1904.

Tarehe 27 Januari ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi (Holocaust), tarehe iliyowekwa na Umoja wa Mataifa kukumbuka ukatili uliofanywa na Wanazi dhidi ya Wayahudi na jamii nyingine za walio wachache.

Januari 27, 1945, askari wa ki-Soviet waliikomboa kambi ya mateso ya Auschwitz.

Mwaka huu, sherehe hizo zilichukua uzito mkubwa kutokana na vita vya Gaza na shambulio la Hamas dhidi ya Israel mwezi Oktoba mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu 1,300 na mateka 240.

Majibu ya Israel yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 25,000 huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.

Mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague, Afrika Kusini inaishutumu Israel kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Pia unaweza kusoma

Kilichofanywa na Ujerumani

CX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Swakopmund ni mojawapo ya fukwe zinazotembelewa zaidi nchini Namibia.

Mwaka 2021, baada ya zaidi ya miaka 100, Berlin ilikiri kufanya mauaji ya kimbari nchini Namibia. Wakoloni wa Ujerumani waliwaua zaidi ya Waherero na Wanama 70,000 kati ya 1904 na 1908. Yanaelezwa kuwa ndio mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20.

Rais wa Namibia, Hage Geingob alisema hivi karibuni, "serikali ya Ujerumani bado haijalipa kikamilifu fidia kwa mauaji ya kimbari iliyofanya katika ardhi ya Namibia."

Baada ya Ujerumani kukiri ukatili ilioufanya, iliipa Namibia kiasi cha pesa kama fidia. Ujerumani ilikubali kulipa zaidi ya dola bilioni moja.

"Kwa kuzingatia wajibu wa kimaadili na historia, tutaomba radhi kwa Namibia na vizazi vya waathiriwa," Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani wa wakati huo Heiko Maas alisema 2021.

Waziri huyo aliongeza kuwa nchi yake, katika kutambua mateso makubwa waliyopata waathiriwa, itaunga mkono maendeleo ya taifa hilo la Afrika kupitia mpango unaotarajiwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3.

Kiasi hiki kitalipwa kwa muda wa miaka 30 na kuwekezwa katika miundombinu, matibabu na programu za mafunzo kwa manufaa ya jamii zilizoathirika.

Ukoloni wa Ujerumani Afrika

dc

Chanzo cha picha, GETTY/BBC

Maelezo ya picha, Laidlaw Peringanda katika makaburi ya halaiki ya wahanga wa kambi ya mateso.

"Katika ufukwe huu kulijaa kambi za mateso," anaelezea Laidlaw Peringanda, mwanaharakati na mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Mauaji ya Kimbari.

"Senyenge zenye miba zilikuwepo sehemu ambayo leo kuna maegesho ya magari."

Miaka 1904-1908, Namibia ya sasa ilikuwa ni koloni la Ujerumani kusini-magharibi mwa Afrika. Maelfu ya watu waliuawa wakati majeshi ya kikoloni yalipokandamiza kikatili maasi ya jamii mbili za nchi hiyo, Waherero na Wanama.

Waliwauwa wengi wao na kuwafukuza wengine katika Jangwa la Omaheke, mashariki mwa nchi, ambako wengi walikufa kwa njaa. Walionusurika waliishia kwenye kambi na walitumiwa kama watumwa.

Inakadiriwa kuwa takribani watu 65,000 kati ya Waherero 80,000 walioishi kusini-magharibi mwa Afrika chini ya utawala wa Wajerumani walikufa, pamoja na Wanama wapatao 10,000 kutoka idadi jumla ya watu 20,000.

Ikiwa hawakufa kwa njaa, walikuwa wanakufa kwa uchovu, kiu au risasi. Ubakaji wa wanawake ulikubalika.

Mamia ya mafuvu ya waathiriwa yalipelekwa Ujerumani kwa ajili ya masomo kuhusu tofauti ya rangi - yaliyolenga kuonyesha ubora wa wazungu. Ishirini kati ya mafuvu haya yalirudishwa kutoka hospitali ya Berlin hadi Namibia mwaka 2011.

Ukatili uliofanywa umeelezewa na wanahistoria kama "mauaji ya halaiki yaliyosahaulika" ya mwanzoni mwa karne ya 20.

Ujerumani ilikuwa inazifukuza jamii kutoka katika ardhi zao katika maeneo waliyoyatawala katika bara la Afrika, na zilikabidhiwa kwa walowezi wa Kijerumani.

Mwaka 1903, wapiganaji wa Herero na Nama waliasi na kuanzisha mashambulizi ambayo yaliua makumi ya walowezi.

Ujerumani ilijibu kwa ukatili

X

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Treni ya kusafirisha wafungwa wa Herero kwenda katika kambi ya mateso 1904.

Mwaka 1904, mfalme wa Ujerumani, Kaiser Wilhelm II, alituma askari wapatao 14,000 kwenda Namibia chini ya uongozi wa Lothar von Trotha, jenerali ambaye alikandamiza kikatili uasi nchini China na Afrika Mashariki.

Wale walionusurika waliuawa au kulazimishwa kuishi katika Jangwa la Kalahari, ambapo askari wa Ujerumani walitia sumu visima vya maji.

Sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo iligawanywa katika mashamba ya kibinafsi na kupewa walowezi wa Kijerumani.

"Mimi jenerali wa wanajeshi wa Ujerumani natuma barua hii kwa Waherero. Taifa la Herero lazima liondoke nchini. Wakikataa nitawapiga mizinga. Mherero yeyote, akiwa na silaha au bila silaha, atauawa," ujumbe wa Von Trotha kwa Waherero.

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Jeshi la wanamaji la Ujerumani likiwa tayari kushambulia 1904.

Profesa Reinhart Koessler kutoka idara ya sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Freiburg na aliyebobea katika kumbukumbu za kisiasa, ambaye amesoma historia ya ukoloni wa Ujerumani barani Afrika kwa miongo miwili, anaeleza:

"Von Trotha aliwaambia askari wake kwamba hawatapoteza heshima yao kwa kuwapiga risasi wanawake na watoto. Waliwapiga risasi ili kuwatisha na kuwalazimisha kukimbia jangwani, ambako wengine walikufa kwa kiu na njaa.’’

Ubakaji wa wanawake wa Herero na Nama ulikuwa wa kawaida sana – kiasi kwamba kuna vizazi vingi leo vina asili ya Wajerumani.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah