Biden amkaribisha kiongozi wa Kenya huku Marekani ikikabiliwa na shinikizo barani Afrika

Barbara Plett Usher ,

Mwandishi wa BBC News Africa, Nairobi

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa Kenya William Ruto atakuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika katika zaidi ya miaka 15 kufanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Marekani.

Hii ni fursa kwa Rais Joe Biden kudhihirisha kujitolea kwa Afrika wakati ambapo Washington inaonekana kuwa na ushawishi katika ushirikiano wake na bara hilo.

Lakini uhusiano na washirika wengine wa Kiafrika unakabiliwa na mvutano, kwani wapinzani wa kimkakati ikiwa ni pamoja na Urusi na China zinaonyesha upinzani katika maeneo ya jadi ambayo yamekuwa na ushawishi wa Magharibi.

Katika fulani Bw Ruto hangekuwa mtu ambaye angepokelewa, kusifiwa katika Ikulu ya Marekani huku sherehe za heshima alizopewa zikitolewa kwa washirika wachache tu wa karibu kwa mwaka.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilimshtaki kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhusiana na ghasia zilizofuatia uchaguzi wa 2007 nchini Kenya. Lakini kesi hiyo ilisambaratika na tangu wakati huo Bw Ruto amejipanga upya kama mshirika wa muhimu wa Marekani.

Tuhuma zinazoendelea rekodi zake za kidemokrasia sio sababu kwamba bunge liliamua dhidi ya kumualika kuhutubia kikao cha pamoja, anasema balozi wa Marekani nchini Kenya, Meg Whitman. Kwa kadiri ajuavyo, ni suala la upangaji wa ratiba.

Bi Whitman, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa makampuni kama vile eBay na Hewlett Packard Enterprises, ni muungaji mkono na mtetezi wa Kenya na uwezekano wake wa uwekezaji kama kitovu cha teknolojia, kinachojulikana kama Silicon Savannah.

"Ikiwa kweli unataka kuegemea Afrika, basi ni nani atakuwa chaguo sahihi kuja kwenye chakula cha jioni cha serikali?" anauliza.

“Kenya imekuwa mshirika wa muda mrefu wa Marekani kwa miaka 60. Hakika ni demokrasia imara zaidi katika Afrika Mashariki. Rais Ruto amejitokeza na ni kiongozi wa kweli.”

Chini ya Bw Ruto, Kenya imeendeleza jukumu lake kama kituo cha kidiplomasia na biashara katika eneo hilo, "nchi kuu" kwa Marekani katika kitongoji kigumu.

Ingawa ndani ya nchi amekabiliwa na maandamano kuhusu jinsi anavyoshughulikia uchumi unaosuasua, duniani kote amekuwa mtetezi wa Afrika katika masuala yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na msamaha wa madeni.

Kenya pia ni mshirika muhimu wa usalama katika Afrika Mashariki, na imeifurahisha Washington kwa kuahidi kutuma polisi wa Kenya nchini Haiti.

Simu pekee iliyopigwa na Rais Biden kwa kiongozi katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika mwaka jana ilikuwa kwa Bw Ruto, kuhusu ahadi ya Nairobi ya kuongoza kikosi cha kimataifa katika nchi hiyo yenye matatizo.

Wachambuzi wanashuku kuwa ziara hiyo ya serikali kwa kiasi fulani inakusudiwa kufidia ukweli kwamba Bw Biden ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuzuru Afrika.

Alitoa ahadi hiyo katika mkutano mkuu wa viongozi wa Afrika mjini Washington miaka miwili iliyopita, ambapo aliwahakikishia wageni wake kwamba yuko tayari kwa ajili ya bara hilo. Lakini tangu wakati huo, ameelekeza juhudi zake katika machafuko mahali pengine, kama vile vita vya Ukraine na Gaza.

Unaweza pia kusoma:
f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Joe Biden aliwakaribisha viongozi wengi wa Afrika mjini Washington mwaka 2022 lakini hajafika Afrika kama rais

Mkutano huo wa Biden na viongozi wa Afrika ulifuatia tangazo la utawala la mkakati mpya unaolenga kubadilisha uhusiano wake na nchi za Kiafrika kuwa ubia sawa zaidi ambao unaendeleza maslahi ya kimkakati ya pande mbili.

Kwa njia fulani Bw Ruto ndiye mtoto anayewakilisha mbinu hiyo, lakini wakati akiwasili Washington lengo hilo la Marekani limekuwa likikabili vikwazo vya Marekani katika Afrika Magharibi.

Ikiwa kuna nchi moja ambayoinaonyesha vyema changamoto zinazoikabili Marekani barani Afrika, lhuenda ni Niger.

Kwa miaka mingi ilikuwa ni makao ya zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Marekani, wakiwa kwenye kambi mbili za kijeshi ambazo zilitumiwa kuanzisha operesheni za usalama dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika eneo hilo.

Lakini mapinduzi ya mwaka jana yalibadilisha hali ya uhusiano - huku watawala wa kijeshi wa Niger wakizidi kuwa karibu na Urusi na Iran.

Juhudi za Marekani kutafuta njia ya kuendeleza ushirikiano wa kiusalama zilivunjika mwezi Machi.

Waziri mkuu wa serikali ya kijeshi aliliambia gazeti la Washington Post kwamba ujumbe wa ngazi ya juu wa Marekani ulikuwa na "sauti ya kudharau" na kuonyesha "kutokuwa na heshima". Aliishutumu kwa kujaribu kulazimisha uhusiano wa Niamey na nchi nyingine.

Wiki hii Pentagon ilithibitisha kuondoka kikamilifu kwa wanajeshi wake ifikapo Septemba - na kufungua mlango wa uhusiano wa karibu zaidi kati ya Niger na Moscow.

Molly Phee, afisa mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje anayehusika na masuala ya Afrika, anasema haikuwezekana kuweka sawa maslahi na maadili ya Marekani, ambayo pia yalijumuisha ratiba ya kurejea katika utawala wa kiraia, pamoja na utawala wa kijeshi.

"Tulikuwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa majadiliano [ya Niger] na Urusi na Iran," aliiambia BBC.

"Mwishowe, hatukuweza kufikia maelewano ambayo yalishughulikia vipaumbele vyetu vikuu," alisema, akibainisha kuwa uhusiano huo unapaswa kuwa wa usawa.

"Tunakusudia kudumisha ushirikiano wa kidiplomasia, pamoja na mambo mengine ya uhusiano wetu."

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Marekani imekubali kuwaondoa wanajeshi wake, waliokuwa wakifuatilia shughuli za makundi ya jihadi kutoka Niger

Kuvunjika huko kunafuatia Niger kuwafukuza Wafaransa, wakoloni wa zamani.

Inaonyesha mvutano huo wakati Marekani inajaribu kusawazisha ushirikiano wa usalama na maadili ya kidemokrasia, vikwazo ambavyo Warusi hawashiriki.

Kilichotokea Niger kimesisitizwa katika nchi nyingine za Sahel – huku Moscow ikiwa na furaha kutoa ulinzi kwa wale walionyakua mamlaka katika msururu wa mapinduzi, mara nyingi kwa ajili ya fidia ya kupata rasilimali.

Katika wiki za hivi karibuni kikosi kidogo cha wanajeshi wa Marekani walilazimishwa kuondoka jirani ya Niger Chad, wakati maafisa huko walitilia shaka mustakabali wa uwepo wa Marekani.

Marekani pia inakabiliwa na kuongezeka kwa ushindani kutoka kwa mataifa mengine barani. China imekuwa ikiwekeza barani Afrika kwa miongo miwili, lakini kuna wahusika wengi wapya wenye nguvu ya kati.

Kura ya maoni ya Gallup mwaka jana iligundua kuwa Marekani ilikuwa imepoteza nguvu zake laini huku China ikipata mashabiki. Lakini mabadiliko makubwa yalikuwa ni kuongezeka kwa umaarufu wa Urusi.

"Kihistoria nchi za Magharibi zimeiona Afrika kama tatizo la kutatuliwa. China na Uturuki, na mataifa mengine ya Ghuba ya Uarabuni, wanaiona kama fursa ,” anasema Muritha Mutiga, mkurugenzi wa programu barani Afrika wa Kundi la Kimataifa la Migogoro.

"Kwa hivyo, ushiriki wa China, Uturuki na Ghuba umekubalika , kwa sababu inaonekana kama dau la muda mrefu, inaonekana kama wamelichukulia bara hili kwa uzito."

Utawala wa Biden unaonyesha mafanikio fulani katika juhudi zake za kuichukulia Afrika kama mshirika wa kimkakati.

Msururu wa ziara za ngazi ya juu umeweka umuhimu wa Afrika kama "bara la siku zijazo", na idadi yake ya vijana inayokua kwa kasi, wingi wa maliasili na ushawishi unaoongezeka katika jukwaa la kimataifa.

Uungwaji mkono wa Marekani umeyasaidia mataifa ya Afrika kupata uwakilishi bora katika vikao vya kimataifa, kama vile G20, IMF na Benki ya Dunia, ingawa Marekani imejitahidi kupata uungwaji mkono wa Afrika kwa misimamo yake kuhusu vita vya Israel huko Gaza, na vita vya Urusi na Ukraine.

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mke wa Rais wa Marekani Jill Biden alikuwa nchini Kenya mwaka jana - moja ya mfululizo wa ziara za Marekani katika bara hilo.

Utawala wa Marekani pia umeshinda sifa kwa kuwekeza katika Ukanda wa Lobito, njia ya reli inayopitia Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia ambayo itatumika kusafirisha malighafi muhimu.

"Kwa njia hiyo ya Lobito Corridor, [Wamarekani] waliamua kuzungumza katika lugha ambayo Waafrika wanaielewa," anasema Kingsley Moghalu, mwanauchumi wa kisiasa wa Nigeria na gavana wa zamani wa benki kuu.

"Ikiwa unaonekana kuwa unatoa miradi mikubwa yenye manufaa kwa uchumi wa Afrika, na kwa watu wa Afrika, basi nyuma ya hilo una uwezo wa kuzungumza kuhusu demokrasia na mambo kama hayo."

Alex Vines, mkuu wa Mpango wa Afrika katika ktaasisi ya Chatham House mjini London, anarudisha nyuma mtazamo kwamba mamlaka ya Magharibi yanafifia barani Afrika.

"Kiongozi mmoja wa Afrika aliniambia: 'Tunachoshwa nadhifa za Kichina, tungependa kwenda la carte, tunataka chaguo," anasema.

"Kwa hivyo, nadhani tunachozidi kuona ni [kwamba] nchi nyingi za Kiafrika zinataka Marekani kidogo, lakini zitataka Urusi au UAE au Uturuki."

Changamoto ni "uongozi dhaifu wa Kiafrika" wenye maono makubwa , ya muda mrefu ambayo yanaweza kufaidika zaidi na ushindani.

Rais Ruto anaonekana kama mmoja wa watu wanaoweza, lakini wote, ikiwa ni pamoja na Niger, wana chaguo.

"Kuna mchezo wa chess unaendelea," Dk Vines anasema. "Kuna kinyang'anyiro kipya kwa Afrika. Tofauti ni kwamba bodi ya chess, bara la Afrika ni hai, ya kukubali mambo tu. Inaweza kuwavuta watu ndani na kuwashangaza sana.”

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi