Kwanini Bollywood bado inatengeneza filamu zenye 'kudhalilisha wanawake na mawazo ya kizamani'

.

Chanzo cha picha, SCREENSHOT FROM YOUTUBE

Bollywood, tasnia maarufu ya filamu ya Kihindi nchini India, mara nyingi hufafanuliwa kama ulimwengu wa mwanamume.

Ni jambo ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu, lakini sasa utafiti mpya unaonyesha jinsi usawa wa kijinsia ulivyo – kwenye skirini na nyuma ya pazia.

Sekta ya $2.1bn (£1.5bn) huzalisha mamia ya filamu kila mwaka na ina wafuasi wengi miongoni mwa Wahindi duniani kote.

Nguvu ya filamu na waigizaji nyota kwenye mawazo ya mashabiki wao haiwezi kuelezeka.

Lakini kwa miaka mingi, filamu nyingi za Bollywood zimekuwa zikikosolewa kwa kuangazia mambo ya kizamani, yanayokuza chuki dhidi ya wanawake na upendeleo wa kijinsia.

Katika utafiti wake wa kwanza wa aina yake, watafiti kutoka Tiss (Taasisi ya Tata ya Sayansi ya Kijamii) huko Mumbai walijaribu kubainisha jinsi unyanyapaa wa mfumo dume ulivyokithiri kwenye sinema ya Kihindi.

Walichagua filamu 25 kati ya zile maarufu zaidi kutoka 2019, mwaka uliopita wa kabla ya janga, na filamu 10 zinazozingatia wanawake kati ya 2012 na 2019 - kipindi hicho kilichaguliwa ili kuona ikiwa kulikuwa na mabadiliko yoyote katika simulizi za filamu kufuatia genge la 2012- kubakwa kwa mwanafunzi wa kike kwenye basi huko Delhi, na ghasia zilizotokana na uhalifu huo na kuanzishwa kwa sheria mpya kali za kushughulikia uhalifu dhidi ya wanawake.

Orodha ya filamu ilijumuisha War, Kabir Singh, Mission Mangal, Dabangg3, Housefull4 na Ibara ya 15 na filamu zinazolenga wanawake ni pamoja na Raazi, Queen, Lipstick Under My Burkha na Margarita with a Straw, miongoni mwa zingine.

Watafiti walifuatilia karibu wahusika 2,000 kwenye skrini ili kuona nafasi zilizochezwa na waigizaji na kuchanganua filamu hizo kwa vigezo kadhaa kama vile dhana potofu ya ngono, ridhaa na ukaribu na unyanyasaji.

Walihesabu idadi ya filamu za LGBTQ+ na wahusika wake na jinsi walivyoonyeshwa, na kuchunguza ni wanawake wangapi walifanya kazi nyuma ya skrini kwenye filamu hizi.

Wamehitimisha kuwa ingawa filamu zinazowahusu wanawake zinatoa sababu fulani ya matumaini, filamu zilizotazamwa sana zinaendelea kuwa za udhalilishaji wa wanawake na za mawazo ya kizamani na uwakilishi wa wanawake na watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja unasalia kuwa wa chini.

Kwa mfano, 72% ya wahusika katika filamu ambazo zilichanganuliwa ziliigizwa na wanaume, 26% wanawake na 2% ni waigizaji wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Watazamaji wengi wa filamu wanaaminika kuwa wanaume nchini India

Prof Lakshmi Lingam, kiongozi wa mradi wa utafiti huo, anasema "wanaopata pesa nyingi ni wanaume katika filamu za Bollywood" na watayarishaji wa filamu wanasema "mhusika wa kike mwenye nguvu sana hatashirikiana na watazamaji".

"Kuna hatua chache sana zinazochukuliwa kubadilisha hali kwa sababu kanuni za mfumo dume hubadilisha mawazo ya watu kuhusu hadithi au simulizi na wanaamini kwamba hii ndiyo inaweza kuwapa pesa," aliiambia BBC.

Kwa hivyo, anasema, wanashikamana na "mfumo" huo.

"Mhusika mkuu lazima awe mwanamume kutoka tabaka la juu, kiongozi wa kike awe mwembamba na mrembo. Anapaswa kuwa mcheshi na mwoga anayeonyesha ridhaa yake kwa ishara badala ya maneno, lakini anavaa mavazi yanayoonyesha umbo lake la kuvutia na lazima awe wa kisasa kumruhusu kuwa katika uhusiano wa kabla ya ndoa ambayo ni uvunjaji sheria."

Ajira kwenye filamu pia inafikiriwa kupitia mtazamo finyu wa kijinsia - Prof Lingam anasema ingawa "asilimia 42 ya viongozi wa kike waliajiriwa katika filamu hizi - [juu zaidi ya takwimu halisi za ajira za India za 25.1%] - walikuwa katika taaluma zenye dhana potofu".

"Wanaume tisa kati ya 10 walikuwa katika majukumu ya kufanya maamuzi wakichukua nafasi za maafisa wa jeshi, polisi, wanasiasa na wakuu wa uhalifu; wanawake wengi walikuwa madaktari na wauguzi, walimu na waandishi wa habari na ni mmoja tu kati ya 10 alikuwa katika majukumu ya kufanya maamuzi," anasema.

Taswira ya wahusika wa LGBTQ+, utafiti unaonyesha, bado imesalia kuwa tatizo kubwa - hawakuwa katika jukumu la kufanya maamuzi na mara nyingi walikuwa tu kwenye uoande wa ucheshi hasa masuala ya ngono.

Walemavu pia uwakilishi wao ulikuwa wa chini sana - walifikia 0.5% tu ya wahusika wote na wengi walitumiwa kama kuonyesha huruma au katika vichekesho.

"Watengenezaji filamu wanasema huo ndio ukweli. Lakini kuna ukweli mwingine mwingi ambao hawaonyeshi. Upo kati ya ukweli na kufirika ili kuhalalisha hali hii," Prof Lingam anasema.

Taswira ya wanawake na watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja katika tasnia, anaongeza, lazima ibadilike kwa sababu "maisha halisi pia yanaamriwa na kile tunachokiona kwenye sinema".

"Nchini India, ambapo familia na shule hazifundishi juu ya elimu ya ngono na ridhaa, majibu yetu yote yanaathiriwa na vitabu na sinema," anasema, akiongeza kuwa ni shida wakati filamu kama Kabir Singh inamwonyesha kiongozi wa kiume akimvizia na kumnyanyasa shujaa ili kumtongoza.

"Inaonesha kuwa kawaida wanaume kuchukuliwa wenye nguvu. kwa hivyo mwanamke anaponyemelewa au kunyanyaswa mitaani, kila mtu anasema inatokea. Na huwa hakuna msukumo wowote."

.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, Vidya Balan alihoji mfumo dume katika filamu yake Mission Mangal

Filamu chache ingawa, anadokeza, zinatoa taswira tofauti - kwa mfano, Mission Mangal, wakati mwanasayansi wa roketi, nafasi iliyochezwa na Vidya Balan, anazomewa na mkewe kwa kutumia muda mwingi kazini na kuwapuuza watoto wao na yeye na anageuka na kumuuliza ikiwa watoto sio jukumu lake pia.

Filamu za Queen na Lipstick Under my Burkha zilikuwa miongoni mwa filamu chache ambazo ziliongozwa na waigizaji wanawake na zilihusu wahusika wa kike wenye nguvu.

Lakini idadi ya filamu kama hizo bado ni ndogo sana.

Kwa upande mwingine, mfumo unaotumiwa na Bollywood haufanyi kazi tena.

"Filamu nyingi zinatawaliwa na wanaume zikiongozwa na baadhi ya waigizaji nyota wakubwa kama vile Salman Khan na Akshay Kumar zimefanya vizuri sana."

Kwa hivyo tasnia, anasema, inahitaji kufikiria tena maoni haya.

"Mawazo ya kawaida ni kwamba watazamaji wengi ni wanaume kwa hivyo filamu zinatengenezwa kwa ajili yao. Hatusemi usifanye filamu hizo, lakini fanya filamu nyingi ili kuwe na aina nyingi."

Sababu moja, anasema, kwa nini mwonekano wa Bollywood unajumuisha wanaume wengi, ni kwa sababu kuna wanawake wachache wanaofanya kazi nje ya skrini kwenye tasnia na wachache zaidi katika idara kuu za utengenezaji wa filamu - filamu ambazo Tiss ilifanya utafiti na kubaini zilikuwa na zaidi ya wanaume 26,300 na wanawake 4,100 pekee wafanyakazi.

"Ikiwa filamu zitatengenezwa kwa ajili ya hadhira tofauti, na watu mbalimbali nyuma ya skrini, simulizi pia zitakuwa tofauti," anasema Prof Lingam.