Wajue nguli wa tano wa soka walioaga dunia hivi karibuni

Hh

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mario Zagallo, mchezaji pekee aliyekuwa sehemu ya ushindi mara nne wa kombe la dunia
  • Author, Rashid Abdallah
  • Nafasi, BBC Swahili

Katika kipindi cha mwaka 2023 na mwanzoni mwa 2024 - kuna wachezaji wengi wameaga dunia kwa sababu mbalimbali. Katika ulingo wa soka pia wapo manguli walioondoka katika dunia hii.

Makala hii ina lengo la kuwataja wachache miongoni mwa wengi - ambao wameweka historia kadhaa wa kadhaa; kuanzia kufunga magoli mengi na kuchukua kombe la dunia mara nyingi na wengine wamevunja rekodi ambazo bado hazijaweza kufikiwa.

Mario Zagallo - Brazil

Jj

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Zagallo akipiga shuti dhidi ya Uingereza wakati timu yake iliposhinda 3-1 robo fainali kwenye Kombe la Dunia la 1962

Wachezaji wengi wenye vipaji na mameneja wameshinda makombe mengi, lakini hakuna anayeweza kufikia rekodi ya Mbrazil huyo ya ushindi mara nne katika kombe la dunia; mara mbili akiwa mchezaji 1958 na 1962, mara moja akiwa meneja 1970 na mara nyingine akiwa msaidizi meneja mwaka 1994.

Mario Zagallo amefariki akiwa na miaka 92 mwezi huu. Ni mchezaji wa zamani wa Brazil - alishinda Kombe la Dunia mwaka 1958. Brazili iliifunga timu mwenyeji Sweden na kuchua kombe kwa mara ya kwanza.

Tena 1962, ilishinda kwa mara ya pili kombe la dunia huko Chile. Brazil ilicheza dhidi ya Czechoslovakia na kubeba ubingwa kwa ushindi wa 3-1.

Mario Zagallo alibeba tena ubingwa wa kombe la dunia akiwa kocha wa Brazil. Wababe wa soka walicheza fainali huko Mexico 1970 - Brazil na Italy na Brazil ikaibuka kidedea 4:1.

Ilionekana angeshinda Kombe la Dunia mara ya tano mwaka 1998 - akiwa meneja wa Brazil, kabla ya Ronaldo Luís Nazário de Lima, nyota wa timu hiyo, kupata kifafa asubuhi ya fainali na kuvunja ari ya timu.

Franz Beckenbauer - Ujerumani

Hh

Chanzo cha picha, Bayern Munich

Maelezo ya picha, Franz Beckenbauer akicheza nusu fainali katika Kombe la Dunia la 1970 kati ya Ujerumani na Italia licha ya kuumia bega.

Franz Beckenbauer, anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji nguli wa kandanda, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Alishinda Kombe la Dunia akiwa nahodha wa Ujerumani Magharibi mwaka 1974. Mechi hiyo ilichezwa kati ya Netherlands na Ujerumani Magharibi na timu ya Beckenbauer ikashinda 2–1.

Beckenbauer alinyanyua tena kombe la dunia akiwa meneja mwaka 1990. Ujerumani Magharibi iliishinda Argentina 1 - 0 katika fainali zilizochezwa huko Italy.

Taarifa kutoka familia yake Januari mwaka huu kwenda shirika la habari la Ujerumani DPA ilisomeka: "Kwa huzuni kubwa tunatangaza kwamba mume wangu na baba yetu, Franz Beckenbauer, amefariki dunia kwa amani usingizini jana, Jumapili, akiwa amezungukwa na familia yake."

Gianluca Vialli - Italia

Hh

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vialli mwenye fulana la buluu akicheza dhidi ya Genoa, 1984

Gianluca Vialli alikuwa mchezaji wa Italia na kocha. Alicheza katika safu ya ushambuliaji. Vialli alianza maisha yake ya soka katika klabu ya mji wa Cremonese mwaka 1980.

Uchezaji wake ulivutia Sampdoria ambao walimsajili 1984, alifunga mabao 85, akashinda vikombe vitatu vya Italia, Serie A na Kombe la Mabingwa Ulaya.

Vialli aliacha shughuli za soka mwezi Disemba, akielezea hitaji lake la kufanyiwa matibabu ya saratani ya kongosho. Mshambulizi huyo wa zamani wa Italia na Chelsea aligundulika na ugonjwa huo kwa mara ya pili mwaka 2021, baada ya kutibiwa mara ya kwanza mwaka 2017.

Vialli alimaliza maisha yake ya uchezaji mwishoni mwa msimu wa 1998-99. Aliichezea Italia mara 59, akifunga mabao 16, na hivi karibuni alikuwa mkuu wa wajumbe wa timu hiyo.

Vialli alifariki Januari 2023 akiwa na umri wa miaka 58.

François Bracci - Ufaransa

Y6

Chanzo cha picha, Max Colin/Icon Sport

Maelezo ya picha, François Bracci, mbele, akiwa na klabu yake Olympique de Marseille, Aprili 14, 1984

Disemba 2023, mchezaji wa tatu aliyecheza mara nyingi zaidi katika historia ya Olympique de Marseille (OM) - François Bracci, akiwa na mechi 343 nyuma ya Steve Mandanda (613) na Roger Scotti (452), alifariki akiwa na umri wa miaka 72 baada ya kuugua muda mfupi.

Mzaliwa wa Beinheim (Bas-Rhin) alishinda Coupe de France akiwa na OM 1972 na kushinda tena miaka minne baadaye. Akiwa beki alichezea timu ya Ufaransa (mechezaji 18) na kucheza miongoni mwa wengine, Kombe la Dunia la 1978.

Ni beki mwenye mechi zisizopungua 342 akiwa na OM kuanzia 1971 hadi 1979 kisha 1983 hadi 1985. Bracci pia alipata kuchezea vilabu vya Girondins de Bordeaux, RC Strasbourg, FC Rouen na AS. Béziers.

Alicheza kwenye Kombe la Dunia la 1978 huko Argentina. Baadaye, aliamua kuwa kocha msaidizi wa Jean Tigana kisha akawa kocha namba moja wa klabu ya MC Alger, CS Constantine na Olympique Khouribga.

Just Fontaine - Ufaransa

88

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Just Fontaine aliinuliwa na wachezaji wenzake baada ya kuifungia Ufaransa dhidi ya Ujerumani kwenye Kombe la Dunia la 1958 nchini Sweden.

Just Fontaine alizaliwa Agosti 18, 1933 na kufariki Machi 1, 2023. Hakuna aliyeweza kuifikia rekodi ya ufungaji wa Just Fontaine katika Kombe la Dunia enzi za uhai wake.

Mwanasoka huyo amefariki akiwa na umri wa miaka 89, alikuwa mmoja wa watu walioshangaza fainali za Kombe la Dunia za 1958 nchini Sweden. Alipofika akiwa na kikosi cha Ufaransa kama mshambulizi wa akiba akiwa na matarajio madogo - lakini aliishia kufunga jumla ya mabao 13 - rekodi ambayo haijafutwa.

Kifo cha Fontaine kimethibitishwa na klabu yake ya zamani ya Reims na shirikisho la soka la Ufaransa: "Just atasalia kuwa gwiji wa timu ya Ufaransa," kocha wa Ufaransa Didier Deschamps alisema.

Fontaine aliweka rekodi hiyo wakati FIFA ilikuwa haitoi tuzo mahususi kwa mfungaji bora wa michuano hiyo - ambapo sasa kunatolewa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu.

"Kifo cha Just Fontaine kinaliingiza soka la Ufaransa katika huzuni kubwa," Philippe Diallo, rais wa muda wa shirikisho la Ufaransa alisema. "aliandika moja kati ya historia nzuri zaidi katika timu ya taifa ya Ufaransa."

Pia unaweza kusoma

Imeandikwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi