Tunawezaje kukabiliana na joto kali?

DSX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Joto kali hupiga maeneo mbalimbali ya dunia
  • Author, James Gallagher
  • Nafasi, BBC

Joto linaweza kumuathiri kila mtu, lakini baadhi ya watu wako hatarini zaidi. Wazee na watoto wachanga wanakabiliwa na hatari na madhara makubwa zaidi.

Joto la mwili linapoongezeka, mishipa ya damu hupanuka. Hilo husababisha kupungua kwa shinikizo la damu, na huufanya moyo kufanya kazi kubwa kusukuma damu sehemu mbalimbali za mwili.

Hali hiyo inaweza kusababisha upele wa joto na kuwasha au miguu kuvimba. Vilevile, jasho likitoka husababisha kupotea maji na chumvi.

Hayo yakichanganyika na shinikizo la chini la damu, yanaweza kusababisha kile kinachoitwa uchovu unaotokana na joto.

Dalili zake ni pamoja na: Kizunguzungu, kichefuchefu, kuzimia, misuli kuuma, maumivu ya kichwa, kutokwa na jasho kupita kiasi, uchovu, ngozi kuwa baridi na kubadilika rangi.

Ikiwa shinikizo la damu litapungua sana, kuna hatari ya kupata mshituko wa moyo.

Pia unaweza kusoma

Joto katika Mwili

Miili yetu huliweka joto la mwili liwe nyuzi joto 98°F (37°C), hata tukiwa kwenye dhoruba ya theluji au katika joto kali.

Ndilo joto mbalo mwili wetu unaweza kufanya kazi. Lakini hali ya hewa inapozidi kuwa moto, mwili hufanya kazi sana ili kupunguza joto.

Hufungua mishipa zaidi ya damu karibu na ngozi ili kupoza joto na kuanza kutoa jasho. Jasho linapotoka, joto hupungua kwa kasi.

Ushuari wa kufuata

DSC

Chanzo cha picha, Getty images

Maelezo ya picha, Kunywa maji mengi husaidia kukabiliana na joto

Ukiwa katika joto kali, unashauriwa kufuata mambo haya:

Vaa nguo nyepesi na zinazopitisha hewa.

Kaa mahali penye kiyoyozi kadri uwezavyo. Ikiwa nyumba yako haina kiyoyozi, nenda kwenye maduka makubwa au maktaba ya umma.

Punguza kutoka nje wakati wa joto.

Kunywa maji mengi na usinywe pombe nyingi.

Kaa kivulini, tumia kinga dhidi ya jua, mfano kofia yenye ukingo mpana.

Watunze watu walio hatarini, kama wazee, wagonjwa na wanaoishi peke yao.

Usiache mtu yeyote, hasa watoto wachanga, watoto wadogo, na wanyama, katika gari lililofungwa.

Wataalamu wanakushauri ziweke soksi zako kwenye jokofu kabla ya kuzivaa na lala muda wako wa siku zote unaolala.

Kwa mtu ambaye amepata uchovu kutokana na joto; poza ngozi yake kwa kunyunyizia maji. Mpe maji mengi ya kunywa.

Lakini ikiwa hatopata nafuu ndani ya dakika 30. Unahitajika kupiga namba ya dharura katika nchi yako ili kupata msaada au kumpeleka hospitali.

Watu wanao athiriwa na joto, huacha kutokwa na jasho ingawa miili yao ina joto kali. Halijoto yao inaweza kufikia 104°F (40°C) na wanaweza kupata kifafa au kupoteza fahamu.

Makundi yaliyo hatarini

Wazee na watu walio na magonjwa ya muda mrefu kama vile ugonjwa wa moyo hawana uwezo wa kukabiliana na joto kali.

Ugonjwa wa kisukari unaweza kufanya mwili kupoteza maji kwa haraka zaidi, na joto kali linaweza kubadilisha hali ya mishipa ya damu na uwezo wa kutoa jasho.

Watoto wanaweza kuwa hatarini pia na watoto walio na magonjwa ya ubongo, kama vile shida ya akili, wanaweza kubaki juani na wasijue la kufanya.

Watu wasio na makazi pia wanakabiliwa na hatari. Wale wanaoishi katika vyumba kwenye ghorofa ya juu wanakabiliwa na joto kali.

Baadhi ya dawa huongeza joto mwilini. Lakini watu wanapaswa kuendelea kutumia dawa zao kama kawaida na wanapaswa kufanya jitihada za ziada ili kukaa katika baridi na unyevu.

Joto linaweza kusababisha kifo?

D

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwanamke akiwa amebeba mwavuli kujikinga na joto kali katika jiji la Uturuki la Istanbul.

Zaidi ya watu 700 hufa nchini Marekani kila mwaka kutokana na joto kali, kulingana na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti Magonjwa.

Vifo vingi hutokana na mshtuko wa moyo au kiharusi. Kiwango cha juu cha vifo huanza mara tu kipimajoto kinapozidi 77-79°F (25-26°C).

Ushahidi unaonyesha ongezeko la vifo hutokea zaidi ndani ya saa 24 za kwanza pale wimbi la joto kali linapoanza.