Kutoroka Sudan: 'Niliachwa na maiti ya mama jangwani'

 Watu ndani na karibu na lori la wazi la juu jangwani
Maelezo ya picha,
  • Author, By Mohamed Osman
  • Nafasi, BBC News Arabic

"Waliniacha mimi na mama yangu aliyekufa jangwani," anasema Om Salma ambaye alitupwa na wasafirishaji wa binadamu mahali fulani akiwa njiani kutoka Sudan kwenda Misri.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 25 anasema mama yake aliuawa wakati lori la wazi walimokuwa wakisafiria lilipoanguka, na kumtupa mama yake nje ya gari.

"Tulijaribu kumwambia dereva apunguze mwendo," Om Salma anasema. Lakini walikuwa wamechelewa. Mama yake Om Salma, ambaye alikuwa na umri wa miaka 65, alikuwa amejigonga kichwa na kufariki.

Akiwa analia bila kujizuia, Om Salma alitolewa nje ya lori, pamoja na ndugu zake na vitu vichache walivyokuwa navyo.

Wasafirishaji haramu walikataa kusafirisha maiti na kwa hofu ya Om Salma wakaondoka.

Om Salma na familia yake walikuwa wakijaribu kutoroka mzozo nchini Sudan, ambao Umoja wa Mataifa (UN) unauelezea kama "mgogoro mkubwa zaidi duniani wa watu kuhama makazi yao".

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni nane wamelazimika kuyahama makazi yao tangu makabiliano makali kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) kuzuka mwezi Aprili.

Inakadiria watu 450,000 wameondoka Sudan katika muda wa miezi 10 iliyopita na kuvuka mpaka na kuingia Misri.

Mwaka jana mapigano makali yalizuka katika mji mkuu, Khartoum, kutokana na mzozo mkali wa madaraka ndani ya uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo. Ulienea haraka nchi nzima na kuwalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao.

Mapigano yalipokaribia karibu na mji wa Om Salma wa Omdurman, aliweza kusikia milio ya risasi na kusema: "Ilitubidi kuondoka. Maisha yetu yalikuwa hatarini."

Anasema watu wengi walimwambia kuwa "haiwezekani" kupata visa ya kusafiri kihalali kwenda Misri haraka, hivyo alimwendea mtu mmoja ambaye alitoza dola 300 kwa kila mtu kusafirisha familia yake kutoka Sudan.

Usafirishaji wa watu umeenea sana katika mpaka wa Misri na Sudan wenye urefu wa kilomita 1,200.

Wasafirishaji wa watu, wengi wao wakiwa wanaume, kwa kawaida wanahusika katika uchimbaji wa dhahabu katika maeneo ya kaskazini mwa Sudan na kusini mwa Misri. Tayari wanafanya kazi katika eneo hilo, wanajua ardhi ngumu ya jangwa na wanaweza kupata malori ya kusafirisha watu.

Om Salma na familia yake walikwenda katika mji wa Gabgaba kaskazini mwa Sudan. Hiki ni kituo kinachojulikana sana cha kuanzia kwa watu wanaosafirishwa kwa magendo kuvuka mpaka, kiasi kwamba, wenyeji wameupa jina la utani uwanja wa ndege wa Gabgaba.

Om Salma aliambiwa wangesafirishwa kuvuka jangwa na kuvuka mpaka hadi mji wa kusini mwa Misri wa Aswan. Tayari walikuwa wamesafiri kwa saa nane, na walisimama kulala usiku mmoja kabla ya ajali hiyo kutokea.

Sasa katika jangwa, na chakula kidogo na maji na maiti ya mama yake, Om Salma na ndugu zake walikuwa wamekwama.

Ramani ya Sudan na Misri

Hatimaye, baada ya saa nyingi za kusubiri jangwani, Om Salma alifanikiwa kumshawishi dereva aliyekuwa akisafirisha chakula na bidhaa za umeme kutoka Misri hadi Sudan, awapeleke pamoja na mwili wa mama yao hadi katika mji wa Abu Hamad ambako walikuwa wamekaa hapo awali.

Familia ilifika salama Abu Hamad, ambapo baadaye waliweza kumzika mama yake Om Salma.

Hapo awali watu walisitasita kuzungumza nasi, lakini walipofanya hivyo, tulikuta hadithi ya Om Salma haikuwa ya kawaida na ajali hutokea mara kwa mara katika eneo hilo.

Wasafirishaji wa watu kwa kawaida huendesha malori ya wazi kwa mwendo wa kasi ili kukwepa mamlaka, wanapovuka mpaka haraka.

Mtu mmoja anayeitwa Ibrahim, ambaye kwa sasa yuko Cairo, anasema aliposafirishwa kutoka Sudan kwa magendo, mtu aliyekuwa akisafiri naye alivunjika shingo na kufariki baada ya lori walimokuwa wamepanda kugonga mwamba.

Kwa upande wa Ibrahim, mtu huyo alikuwa akisafiri pekeyake na licha ya upinzani kutoka kwa kundi hilo, wasafirishaji haramu walisisitiza kuuacha mwili wake na kuuzika jangwani.

"Kila mtu alishtuka. Nilitazama kaburi lisilokuwa na alama kutoka dirishani tulipokuwa tunaendesha gari, huku wanawake na watoto kwenye lori wakilia," Ibrahim anasema.

Ujambazi pia ni wa kawaida. Halima, ambaye ana umri wa miaka 60, anasema alipatwa na hali ya kutisha aliposafirishwa kinyemela na familia yake katika jangwa la Sudan kabla ya kuwasili Misri.

"Tulivamiwa na watu wanne waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakati lori letu lilipoharibika. Walifyatua risasi hewani, wakampiga binti yangu makofi na kuiba vitu vyetu," asema, kabla ya wao kuogopa wakati gari lingine lilipokuja. Kwa bahati nzuri dereva wa gari hilo alikubali kuwasaidia na kuwavusha mpaka.

Lakini Halima anasema binti yake mwenye umri wa miaka 25 alitikiswa sana na akafa siku iliyofuata walipofika Misri. "Alipata mshtuko wa hofu na hakuweza kupumua," Halima anasema, akiongeza hawakuweza kupata msaada wa matibabu kwa wakati.

BBC imeona nakala ya cheti cha kifo, ambacho kinataja matatizo ya kupumua kuwa chanzo cha kifo.

 Watu wameketi nyuma ya gari katika jangwa la Sudan
Maelezo ya picha,

BBC imewasiliana na serikali ya Misri kuuliza inachofanya kukabiliana na watu haramu wanaosafirisha kutoka Sudan lakini hatujapata jibu.

Abdel Qader Abdullah kutoka ubalozi mdogo wa Sudan huko Aswan kusini mwa Misri aliiambia BBC kuwa ni kosa kisheria kuvuka mipaka ya jangwa bila visa na mamlaka imeanzisha kampeni ya kuonya juu ya hatari inayohusishwa na watu wanaofanya magendo.

Abdullah aliongeza: "Ubalozi mdogo wa Sudan huko Aswan unafanya kazi na serikali ya Misri kusaidia kuharakisha mchakato wa visa, kusaidia kuongeza idadi ya maombi yaliyoidhinishwa na kuruhusu watu wengi zaidi wa Sudan kuingia nchini kihalali."

Wanawake na watoto walikuwa wakiruhusiwa kuingia Misri bila visa lakini serikali ilileta vikwazo vipya baada ya mapigano nchini Sudan kuzuka. Mahitaji nchini Sudan ya kupata visa ya Misri ni makubwa, kwani watu wanataka kukimbia mzozo huo.

Wanaweza kutuma maombi ya visa ya Misri katika maeneo mawili nchini Sudan Wadi Halfa kaskazini na Port Sudan mashariki. Wengi wanaelekea Wadi Halfa kwa kuwa ni karibu na Argeen, mpaka mkuu wa nchi kavu kati ya Sudan na Misri. Lakini karibu hakuna miundombinu katika Wadi Halfa.

Watu wanaokaa foleni ya visa kwa saa ili kushughulikiwa. Baada ya kutuma ombi, inaweza kuchukua miezi kadhaa ili kujua ikiwa wamefaulu. Wakiwa wamehama na wakiwa na pesa kidogo, wengi husubiri Wadi Halfa ili kusikia habari kuhusu ombi lao, wakilala mahali popote wanapoweza, katika shule zilizo karibu au barabarani.

Akiwa bado amedhamiria kutoka nje ya Sudan, Om Salma aliamua kujaribu njia ya kisheria katika jaribio lake la pili. Alisafiri hadi Port Sudan kuomba visa katika ubalozi mdogo wa Misri huko.

Lakini baada ya kungoja kwa miezi miwili, alikata tamaa na akachagua tena njia hiyo haramu. Watu wengi wananyimwa visa na hawawezi kumudu kusubiri, mara nyingi wakiamua kutumia pesa kidogo walizobakiza kwa mlanguzi ili kuwatoa nje ya nchi.

Om Salma anasema alijifunza somo lake kutokana na hofu ya jaribio lake la kwanza na kumwendea mlanguzi mwingine tofauti. "Safari hii tulijiandaa kwa safari," anaeleza, akipakia vyakula zaidi na maji.

"Tulitumia takribani siku sita jangwani," anasema, kabla ya kuvuka mpaka na kuelekea kusini mwa Misri.

Wahamiaji wa Sudan wakiwa kwenye foleni mjini Cairo kupata hadhi ya ukimbizi
Maelezo ya picha,

Mara wanapowasili nchini Misri, masaibu ya wahamiaji wa Sudan yanakuwa hayajaisha. Ikiwa hawana hadhi ya mkimbizi au hawawezi kuthibitisha kuwa wana miadi ya kuiomba, wanaweza kufukuzwa nchini.

Ili kupanga miadi lazima wasafiri hadi Cairo au Alexandria.

Katika kituo cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) mjini Cairo, maelfu ya wahamiaji wa Sudan, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wanasimama kwenye misururu mirefu wakisubiri kuandikisha majina yao na kupata kile kinachojulikana kama kadi ya njano.

Halima anasema "atasimama kwenye hali ya hewa ya baridi kwa saa nyingi, na kupanga tu mkutano kwa miezi minne baadaye".

"Kupata kadi ya njano, ambayo unapata mara tu unapokuwa mkimbizi aliyesajiliwa wa Umoja wa Mataifa, inakuwezesha kupata kazi kihalali na kupokea fedha za kila mwezi kutoka kwa UN," anaelezea.

Ingawa mkimbizi mwingine aliyesajiliwa wa Umoja wa Mataifa, Ibtessam, ananiambia si rahisi hivyo.

Ibtessam alisafirishwa kwa magendo kutoka Sudan hadi Misri msimu wa joto uliopita akiwa na vizazi vitatu vya familia yake, 17 kati yao kwa jumla, wakiwemo wazazi wake na watoto.

Lakini anasema licha ya kuwa na kadi ya njano, hajapokea fedha zozote tangu alipowasili mwezi Juni. "Sijui ni jinsi gani naweza kutunza familia yangu. Mume wangu amefariki, nina kodi ya nyumba na ada ya shule ya kulipa kila mwezi, na hakuna anayetusaidia."

Msemaji wa UNHCR Christin Bishay anakiri kufadhaika na mateso wanayopata wahamiaji wa Sudan nchini Misri lakini anasema shirika hilo "linakabiliwa na uhaba wa fedha".

"Tumepanua uwezo wetu kwa asilimia 900. Kwa hiyo inatubidi kuweka vipaumbele na kufikiria: 'Nani anahitaji msaada kwanza?'" anafafanua, na kuongeza: "Tumeanzisha huduma za matibabu katika mpaka kwa usaidizi wa shirika la kutoa huduma za dharura za matibabu na misaada ya kibinadamu nchini Misri."

Maisha si rahisi kwa wahamiaji wa Sudan nchini Misri, kama Om Salma, ambaye analazimika kutafuta mahali pa kuishi bila msaada au pesa kidogo.

Ananiambia ana wasiwasi kuhusu siku zijazo. Kwa hakika, anataka kurejea nchini mwake siku moja, lakini kwa sababu ya mzozo wa Sudan, anahofia hili haliwezi kutokea kamwe.

Majina yamebadilishwa kwa ajili ya usalama wa wazungumzaji

imetafsiriwa na Lizzy Masinga.