Kenya yaondoa marufuku ya ukataji miti

Ashley Lime

.

Rais wa Kenya William Ruto ameondosha marufuku ya miaka sita ya ukataji miti - na hivyo kuzua hasira kutoka kwa wanamazingira.

Kiongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki alisema, haja ya kufungua uchumi wa kanda zinazotegemea mazao ya misitu ilichochea uamuzi wake.

Kwa nini marufuku hiyo imeondolewa?

Rais Ruto alieleza ajabu ya miti iliyokomaa kuoza katika misitu ya Kenya huku nchi ikiagiza mbao kutoka nje ya nchi.

Anataka kufufua uvunaji wa mbao ili kutengeneza ajira kwa vijana na kufungua njia ya biashara ya mabilioni ya dola.

Waagizaji wa mbao na samani sasa watatozwa ushuru huku Ruto akitaka zitengenezwe nchini.

Kwanini marufuku hiyo iliwekwa?

.

Malalamiko ya umma juu ya athari mbaya za ukataji miti kinyume cha sheria, kama vile kupungua kwa viwango vya maji katika mito mikuu ya Kenya, ilisababisha kutangazwa kwa marufuku ya kukata miti katika misitu ya umma mnamo Februari 2018.

Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta alisema hatua hiyo itasaidia kuhuisha misitu iliyopotea na kuongeza kasi ya upandaji miti.

Shirika la Huduma ya Misitu nchini humo (KFS), lililokuwa na jukumu la kulinda misitu, pia lilifanyiwa marekebisho ili kukabiliana na ufisadi na kuimarisha ufanisi.

Marufuku hiyo ilikuwa na athari gani?

.

Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha hasara ya Shilingi za Kenya 4 bilioni ( dola za kimarekani 28,300,000) katika mapato na ajira 44,000 wakati wa marufuku ya miaka sita. Misitu inachangia asilimia 3.6 ya pato la taifa la Kenya.

Ripoti ya Utafiti wa Kiuchumi ya 2020 inaonyesha – wingi wa misitu uliongezeka kutoka hekta 141,600 mwaka 2018 hadi hekta 147,600 mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia nne.

.

Serikali ina mpango gani wa kuhifadhi misitu?

Utawala wa Ruto umetangaza mpango kabambe wa kupanda miti bilioni 15 katika muda wa miaka 10 ili kukuza msitu wa taifa.

Sekta ya mbao mara nyingi huelezwa kama mojawapo ya sekta zenye faida kubwa zaidi nchini Kenya, ikiajiri maelfu ya vijana wasio na kazi na wasio na elimu. Mikoa inayotegemea mbao kujikimu kimaisha iko katika Bonde la Ufa, haswa Kusini.

.

Wanamazingira wanasemaje?

Wanamazingira wameelezea wasiwasi wao kwenye Twitter kuhusu hatua hiyo ya Ruto, huku baadhi wakidai rais anakiuka baadhi ya ahadi alizotoa kupambana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi.

"Siku ya huzuni kwa miti nchini Kenya huku marufuku ya kukata miti ikiondolewa. Wakenya wanaelezea wasiwasi wao - jinsi misitu itakavyolindwa?

‘Miti itakayo pandwa haitakuwa sawa kiikolojia, kijamii, kitamaduni na kijeni na misitu iliyokuwa zamani. William Ruto ameweka mkono wake kwenye kitufe cha kusitisha,” alisema mwanaikolojia Dkt. Paula Kahumbu.

Mwanamazingira Elizabeth Wathuti alisema, "kudhani kwamba wakataji miti watachagua miti mizee na kuacha miti michanga ni uongo unaotumiwa vibaya".

Shirika la kampeni ya mazingira Greenpeace Africa limemwomba Rais Ruto kurejesha marufuku ya ukataji miti katika misitu yote ya umma na iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali. Shirika hilo pia linataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuruhusiwa kusimamia misitu ili kutunza miti iliyo hatarini.

Ni masomo gani tunaweza kujifunza?

.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, Gabon imetunza msitu wake wa mvua tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000 ili kuunda mbuga 13 za kitaifa, moja wapo imeorodheshwa kwenye Tovuti ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.

Misitu ya nchi hiyo inafyonza tani milioni 140 za hewa chafu kila mwaka, sawa na kuondoa magari milioni 30 kutoka barabarani ulimwenguni kote.

Wakati wa mkutano wa COP26 viongozi wa dunia waliahidi kukomesha ukataji miti ifikapo 2030.