Jinsi uchafuzi wa hewa unavyosababisha wasichana kupata hedhi mapema

SC
Maelezo ya picha, Utafiti umegundua wasichana wa Marekani wana uwezekano mkubwa wa kupata hedhi yao ya kwanza katika umri mdogo.
  • Author, David Cox
  • Nafasi, BBC

Utafiti mpya unaonyesha wasichana nchini Marekani wanapata ukubwa, yaani hedhi yao ya kwanza mapema. Hewa yenye sumu ni chanzo cha hilo.

Kwa miongo kadhaa, wanasayansi ulimwenguni wamekuwa na wasiwasi kwamba wasichana wanaingia kwenye ukubwa katika umri mdogo zaidi ikilinganishwa na vizazi vilivyopita.

Wasichana wa Marekani wanakadiriwa kuanza kupata hedhi miaka minne mapema, ikilinganishwa na wasichana walioishi karne moja iliyopita.

Ripoti mpya iliyotoka Mei mwaka huu, inaonyesha watoto waliozaliwa kati ya 1950 na 1969, walianza kupata hedhi wakiwa na miaka 12.5. Lakini mapema miaka 2000 - wastani wa wasichana kuanza hedhi ikawa ni miaka 11.9.

Mabadiliko hayo pia yametokea duniani kote. Wanasayansi wa Korea Kusini wameelezea jinsi wasichana wanavyo balehe mapema, kwa kukuwa matiti au kupata hedhi.

"Pia tunaona umri huu unaopungua katika balehe hutokea zaidi katika jamii za watu wa hali ya chini kiuchumi, na jamii za makabila madogo," anasema Audrey Gaskins, profesa wa Chuo Kikuu cha Emory huko Atlanta, Marekani.

Pia unaweza kusoma

Athari kwa Wasichana

fgv
Maelezo ya picha, Inakadiriwa wasichana nchini Marekani huanza kupata hedhi miaka minne mapema ikilinganishwa na wasichana walioishi karne moja iliyopita

Gaskins anasema kubalehe mapema kunaweza kusababisha msururu wa matukio baadaye katika utu uzima.

Takwimu zinaonyesha kupata hedhi mapema kunaweza kupunguza uwezo wa kuzaa, haswa ikiwa wanawake hawa wataingia kwenye kukoma hedhi mapema, vilevile kufupisha maisha yao.

Kubalehe mapema kumehusishwa na hatari ya magonjwa ya saratani ya matiti na ovari, vilevile kunenepa sana na kisukari cha aina ya 2, na ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu.

Wanasayansi bado wanajaribu kutafiti ni kwa nini hali iko hivyo.

Brenda Eskenazi, profesa wa afya ya umma katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, anasema: “Wasichana wanaobalehe mapema wana uwezekano mkubwa wa kuanza kujamiiana mapema. Na hilo litasababisha mimba nyingi za utotoni zisizohitajika."

Unene na uchafuzi wa hewa

Profesa Gaskins anasema, hadi miaka 10 na 20 iliyopita, wanasayansi walidhani sababu pekee ya kubalehe mapema ilikuwa unene wa utotoni, na protini zinazozalishwa na seli za mafuta ndio chanzo cha hilo.

Lakini idadi ya tafiti katika miaka mitatu iliyopita zimeelezea sababu nyingine, ya kushangaza zaidi – nayo ni uchafuzi wa hewa.

Utafiti wa hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha Ewha Womens huko Seoul unabainisha juu ya uhusiano kati ya vichafuzi na kubalehe mapema.

Baadhi ya vichafuzi hivyo ni gesi zenye sumu kama vile sulfuri dioksidi, nitrojeni dioksidi, kaboni monoksidi na ozoni, ambazo zote huingia angani kupitia magari au moshi unaozalishwa na viwanda.

Mwaka 2022, utafiti kutoka wanasayansi nchini Poland, nchi inayojulikana kwa hewa chafu kutokana na kuenea kwa viwanda vinavyochoma makaa ya mawe, ulichunguza wanawake 1,257 na athari za gesi za nitrojeni na kupata uhusiano na hedhi ya kabla ya umri wa miaka 11.

Gaskins anasema, "unazivuta sumu kwenye mapafu yako, na hazichujwa na zinaweza kufikia viungo tofauti - kwenye (kondo) plasenta, tishu za mtoto tumboni na ovari."

Uchunguzi uliotumia sampuli kutoka katika hewa, umeonyesha kemikali zilizomo ndani ya hewa, zinaweza kuingiliana homoni mbalimbali zinazohusika katika maendeleo ya mtoto – hasa homoni za androjeni na oestrogen. Na hilo linaweza kusababisha kuanza kwa balehe mapema.

TFG
Maelezo ya picha, Wanasayansi wanasema wasichana wanaoanza kubalehe mapema wanaweza kupata madhara makubwa baadaye katika utu uzima.

Lakini kuna uwezekano wa kuwepo sababu nyingine tofauti zinazohusika katika kubalehe kabla ya wakati. Gaskins anasema ushahidi unaojitokeza unaohusiana na sumu kutoka katika hewa na uchafuzi mwingine ni mfano mmoja tu wa jinsi kemikali hatari za mazingira zinavyoweza kupenya mwilini, na kuchochea mabadiliko makubwa ya homoni.

"Sababu nyingine kuu ya kuathiriwa na kemikali ambazo huharibu michakato ya homoni ni bidhaa binafsi za vipodozi," anasema Gaskins.

"Na sasa kuna kampuni nyingi zinazouza bidhaa hizo kwa idadi kubwa ya watu.

Eskenazi anasema bado kuna mengi ambayo hatujui kuhusu uhusiano kati ya ulimwengu wetu unaobadilika na jinsi mabadiliko haya yanavyoathiri ukuaji wa mtoto, huku athari ya vitu kama vile plastiki na mabadiliko ya hali ya hewa bado hatuzijui sana.

"Nadhani bado hatujui mengi," anasema. "Hatujui jinsi hali ya hewa ya joto inavyoathiri mzunguko wa hedhi au sababu nyingine za kijamii, na kuwafanya wasichana kukua mapema.

Lakini wasichana kupata ukubwa mapema, ni jambo la kweli, na kunaweza kuwepo na mchanganyiko wa mambo yanayohusu kemikali katika mazingira, unene na masuala ya kisaikolojia."

Pia unaweza kusoma

Imetafsriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah