Wakalimani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali wanahofia kuadhibiwa kwa mtindo wa Taliban

UN MUNISMA peacekeepers patrol the streets of Gao, Mali

Chanzo cha picha, Getty Images

  • Author, Na Esther Kahumbi
  • Nafasi, BBC News

Mwezi Juni mwaka huu, Hachimi Dicko, alikuwa akisafiri kwa lori kutoka Niamey, mji mkuu wa Niger, kwenda Gao nchini Mali wakati alipotekwa na wanamgambo wa Islamic wanaohudumu katika eneo la Sahara.

Watu waliokuwa wakisafiri naye walisimulia kilichofanyika baadaye.

Wanasema Dicko mwenye umri wa miaka 32 alitengwa na wanamgambo kwa sababu ya viatu vya kijeshi alivyokuwa amevaa. Watekaji wake awali walidai fidia.

Lakini wapiganaji hao walipoangalia simu ya Dicko, walipata picha zake akiwa amesimama karibu na wanajeshi wa Ujerumani kutoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Mali.

Picha hizo zilifunga hatima yake. Wanamgambo hao walimteka nyara Dicko, wakimwita msaliti, jasusi na msaidizi wa adui. Miezi miwili baadaye aliuawa. Picha za mauaji yake ya kikatili zilisambazwa mtandaoni.

Picha za Dicko karibu na wanajeshi wa Ujerumani zilipigwa alipoajiriwa kama msimamizi wa kusafisha nguo wa Ecolog, mkandarasi mdogo katika Camp Castor, kituo cha uendeshaji cha Ujerumani huko Gao.

Umoja wa Mataifa kujiondoa

Kwa mujibu wa ripoti ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Dola ya Kiislamu katika eneo la Sahara imeongeza maradufu maeneo inayodhibiti katika mwaka uliopita.

Makundi yenye itikadi kali nchini Mali yameelezea chuki yao dhidi ya wenyeji wanaoshirikiana na mashirika ya kigeni, hususan kikosi cha kimataifa cha Umoja wa Mataifa kilichoko nchini humo.

"Magaidi wamekuwa wakisema waziwazi kwamba mtu yeyote anayefanya kazi na vikosi vya kimataifa anachukuliwa kuwa adui," anasema mtafsiri wa kikosi cha kijeshi cha Ujerumani ambaye hakutaja jina lake kwa sababu za kiusalama.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MINUSMA, umekuwa ukifanya kazi nchini Mali tangu mwaka 2013 kwa lengo la kuleta utulivu na kuunga mkono kurejea kwa nchi hiyo katika utawala wa kikatiba. Inaundwa na wanajeshi kutoka karibu nchi 60, na Chad, Senegal, Misri, Ujerumani na Bangladesh miongoni mwa wachangiaji wakuu.

Operesheni hiyo ilipangwa kumalizika mnamo 2024 lakini tarehe hiyo ilisogezwa mbele hadi Desemba 31 mwaka huu. Hii ilitokana na shinikizo kutoka kwa serikali ya kijeshi ya Mali ambayo ilichukua udhibiti baada ya mapinduzi mwaka wa 2021. Wengi wa majeshi ya kimataifa tayari wameondoka au kuanza kuondoka.

Makana City, Mali

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mji wa Menaka unajulikana kuwa ngome ya Islamic State katika eneo la Sahel

Kuachwa nyuma

Takriban raia 900 wa Mali wameajiriwa kufanya kazi na MINUSMA kama watafsiri, madereva, na majukumu mengine ya usaidizi katika kambi 12 za Umoja wa Mataifa zilizoenea kote nchini.

“Tunapoenda uwanjani, kazi yetu ni kwenda kukusanya taarifa za vikosi. Nimetembelea vijiji vingi, na wananiita Kufur (kafiri). Wananiambia peupe kwamba mtu yeyote anayefanya kazi kwa makafiri pia ni kafiri,” mtafsiri anayefanya kazi katika vikosi vya Ujerumani anasema.

Mtafsiri huyo amekuwa na MINUSMA kwa miaka saba. Sasa vikosi vya kimataifa vinaondoka, anaogopa kwamba yeye na wenzake 18 wataachwa na watu ambao wametumia miaka kusaidia.

"Wanatujua sisi ni akina nani, nyuso zetu ziko nje, wanasubiri tu vikosi vya kimataifa kuondoka nchini ili washambulie," anasema.

"Tunafanya kazi na wanajeshi, kila mahali wanapoenda, tupo kwa sababu sisi ni midomo yao, (watafsiri) na watu wengi waovu wanatuona kuwa wapelelezi."

"Nilitamka shahada ili kuthibitisha kuwa mimi ni Muislamu, lakini walisema haitoshi, kwa sababu ninachukua pesa za kafiri. Nimewaambia wakuu wangu, (kuhusu vitisho) lakini hawajafanya chochote. Sasa Ujerumani inaondoka hivi karibuni lakini hawajapanga chochote kwa ajili yetu, "anasema.

Ulinzi

Wakati kuondoka nchini Mali kukikaribia, makundi ya wapiganaji wenye mafungamano na Islamic State yanakaribia.

Mwezi Agosti, kundi la watafsiri wa Mali liliiandikia serikali ya Ujerumani na vikosi vyao vilivyoko Mali kuomba ulinzi.

“Kuondoka kwako kutaleta pengo kubwa la usalama, haswa kwa wakalimani ambao wamekuwa na jukumu nyeti sana tangu kuanza kwa misheni. Tumeona jumbe hapa Mali ambapo magaidi wanatishia kuwashambulia watu wote ambao wamefanya kazi kwa vikosi vya kitaifa na kimataifa. Tunahofia hatari ya kulipizwa kisasi baada ya kuondolewa kwa misheni hii,” barua hiyo ilisema.

Mwezi mmoja baada ya kutuma barua hii, video za kunyongwa kwa Dicko na wanamgambo wa Islamic State zilionekana mtandaoni.

Mashirika yanayofanya kazi na watafsiri katika maeneo yenye mizozo pia yametoa tahadhari.

Linda Fitchett, kiongozi wa mradi wa Wakalimani katika Maeneo yenye Migogoro katika Chama cha Kimataifa cha Wakalimani wa Mikutano (AIIC) anasema kuwa tangu mwaka 2009, mashirika kama yake yamejaribu kupata Umoja wa Mataifa kupitisha azimio ambalo lingewapa ulinzi wa kisheria watafsiri walio katika hatari.

"Kama hatuwezi kuishinikiza Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la ulinzi, ni nani atawalinda wakalimani hawa? Je, ni UN, ni nchi moja moja? Kwa kweli hatujui kitakachotokea,” asema Bi Fitchett.

Kama Afghanistan

Makubaliano ya Umoja wa Mataifa na nchi zinazoshiriki yanatoa ulinzi tu kwa wafanyikazi wa kiraia ambao tayari wameajiriwa na vikosi vya jeshi kabla ya kuanza kwa misheni. Lakini baadhi ya wakalimani na wafanyikazi wa usaidizi wana mikataba ya muda ambayo inaisha kabla ya operesheni kumalizika.

Kwa kuwa Umoja wa Mataifa kwa sasa hautoi suluhu, wakalimani wanaagazia nchi moja moja zinazoshiriki kwenye operesheni hiyo.

Mnamo mwaka wa 2022, AIIC, pamoja na mashirika mengine 21 ya lugha na misaada ya kiutu, yaliwaandikia Mawaziri wa Ujerumani wakihimiza kuondolewa kwa wakalimani hao na familia zao "kabla ya kuondoka kabisa".

"Tuna wasiwasi kwamba kwa kuondolewa kwa wanajeshi nchini Mali, jambo lile lile litatokea nchini Mali kama ilivyokuwa nchini Afghanistan," anasema Bi Fitchett.

Baada ya kuondoka kwa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan, maelfu ya wakalimani waliachwa nyuma. Baadhi wameuawa na Taliban na wengine wengi wako mafichoni.

Msemaji wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Ujerumani aliiambia BBC kwamba wamekubali kuchukua hatua za ulinzi ili kuhakikisha usalama wa wafanyikazi wa ndani ikiwa shida itatokea.

"Hizi zinaweza kujumuisha, kwa mfano, kutoa likizo kwa malipo kamili, usaidizi wa kifedha au wa vifaa kwa ajili ya kuhamia maeneo mengine, ambayo ni salama zaidi ya nchi na - kwa upande wa Mali - majimbo mengine katika eneo la ECOWAS ambako raia wa Mali wanafurahia uhuru. ya harakati,” alisema msemaji huyo.

Hata hivyo, haijulikani ni nini kinajumuisha mgogoro.

Camp Castor, UN Peacekeeping base in Gao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Camp Castor, kambi ya Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani huko Gao

Kamandi ya Operesheni ya Pamoja ya Kikosi cha Ulinzi cha Ujerumani nchini Mali inasema inaendelea kutathmini hali ya usalama. Hata hivyo, katika taarifa kwa BBC, inasema kwa sasa haiwezi kupata ushahidi wa kuaminika wa tishio la kimfumo au la mtu binafsi kwa wafanyikazi wa ndani.

"Ilikuwa wazi kwamba hoja zilizotolewa na wafanyikazi wa ndani hazikuwa na msingi maalum. Hata walipoulizwa, wafanyakazi wa ndani hawakuweza kutoa ushahidi wowote wa hatari inayotokana moja kwa moja na kazi zao, "inasema taarifa hiyo.

Lakini raia wa Mali walioajiriwa na vikosi vya Ujerumani wanasema vitisho dhidi yao ni vya kweli.

“Ushahidi wanaoutaka ni upi? ama wanasubiri mmoja wetu atekwe na kuuawa ndio wajiridhishe? Ikiwa hakungekuwa na hofu ya usalama, tungekuwa tunalala kwenye kambi ya Wajerumani?" anauliza mfasiri mmoja ambaye amekuwa akiishi katika kambi hiyo tangu kuanza kazi kwa sababu za usalama.

“Hali inazidi kuwa mbaya. Sio haki; tuliona kilichotokea Afghanistan baada ya kuondoka kwa Wamarekani na kinaweza kutokea hapa”, anasema mfasiri mwingine ambaye aliomba kutotajwa jina.

Mtu huyu ameshiriki katika misheni na vikosi vya Ujerumani inayohusisha unyakuzi wa silaha kutoka kwa makundi ya wapiganaji.

"Mmoja wa watu ambao tumeshughulika nao alisema anajua mimi ni nani. Watu wanadhani ni kusini pekee ambayo si salama, lakini wako kila mahali,” anasema.

"Tuko sawa kwenda hata katika nchi nyingine ya Kiafrika, sio lazima watupeleke Ujerumani."