Martine Moïse: Kwa nini Mjane wa rais wa zamani wa Haiti Jovenel Moïse anashutumiwa kuhusika katika mauaji yake?

Martine Moïse

Chanzo cha picha, Getty Images

Martine Moïse, ambaye alijeruhiwa katika shambulio ambalo mumewe, rais wa wakati huo wa Haiti Jovenel Moïse, aliuawa, sasa ni sehemu ya orodha ya makumi ya washtakiwa baada ya miaka miwili ya uchunguzi.

Anashtakiwa kwa "kuhusika na uhalifu na ushirika," kulingana na hati ya kisheria iliyofichuliwa na tovuti ya habari ya Haiti.

Mke wa rais wa zamani na wakili wake hawajatoa kauli yoyote kuhusiana na tuhuma hizo.

Moïse, ambaye hajulikani aliko, ametumia mitandao ya kijamii katika siku za hivi karibuni kushutumu "kukamatwa kwa dhuluma" na kile alichoelezea kama "mateso yasiyo na mwisho."

Mashtaka mapya

Vyombo vya habari vya Haiti viliangazia kwamba, wakati waraka huo mkubwa wa kisheria unawatuhumu watu 51, hautambui ni nani aliyeamuru na kufadhili mauaji ya Rais Moïse.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 53 aliuawa kwa kupigwa risasi Julai 7, 2021 katika makazi yake ya kibinafsi nje kidogo ya mji mkuu, Port-au-Prince, na kundi la mamluki, wengi wao wakiwa raia wa Colombia.

Mashtaka ya hivi punde yaliwekwa wazi siku ya Jumatatu, wakati tovuti ya habari ya Haiti Ayibo Post ilipofichua mashtaka hayo, na kuwasilishwa na Walther Wesser Voltaire, hakimu wa tano anayeongoza uchunguzi wa mauaji.

Katika hati ya kisheria yenye kurasa 122, hakimu anaweka wazi shutuma dhidi ya Martine Moïse na washukiwa wengine 50.

Anashikilia kuwa kauli za mke wa rais wa zamani baada ya kuuawa kwa mumewe "zilikuwa na utata kiasi kwamba zinaacha kutamanika na kumkosea heshima."

Mama wa taifa wa zamani

''

Chanzo cha picha, Getty Images

Martine Moïse, 49, alijeruhiwa vibaya katika shambulio dhidi ya makazi yake huko Pétion-Ville ambalo lilisababisha kifo cha mumewe.

Alipata majeraha ya risasi kwenye mikono na paja, pamoja na majeraha mabaya ya mkono na tumbo.

Baada ya tukio hilo, alitibiwa haraka katika Hospitali Kuu ya Port-au-Prince, huku kukiwa na mkanganyiko mkubwa na uvumi wa uongo kuhusu kifo chake.

Baadaye alihamishwa hadi Miami, Marekani, ambako alielezea mauaji ya mume wake kama shambulio la watu "waliofunzwa sana na waliokuwa na silaha nyingi" wakitaka kuhujumu mabadiliko ya kidemokrasia nchini Haiti.

Mnamo Julai 2021, alirejea nchini mwake ghafla, na utetezi wake wa kisheria unahakikisha kwamba kwa sasa amefichwa katika eneo lisilojulikana kwa sababu za usalama.

Martine Moïse amekosoa uchunguzi wa mauaji ya mumewe mara kadhaa, ikizingatiwa kwamba mahakimu wanaosimamia kesi hiyo hawana nia ya kufichua ukweli.

Mama wa taifa wa zamani, ambaye alikutana na Jovenel Moïse wakati wa siku zake za chuo kikuu, alijitokeza wakati wa mamlaka yake ya kusaidia masuala ya kiraia na kibinadamu.

Aliongoza Fondasyon Klere Ayiti, Shirika lisilo la Serikali la maendeleo ya jamii kuhusu elimu na masuala ya wanawake, na pia alikuwa rais mratibu wa Mfuko wa Kimataifa wa Haiti, ambao unalenga kupambana na VVU/UKIMWI, malaria na magonjwa mengine katika nchi hiyo ya Caribbean.

Kauli ya ushahidi

Kama ushahidi dhidi ya Martine Moïse, hati hiyo inanukuu taarifa ya Lyonel Valbrun, ambaye alikuwa katibu mkuu katika Ikulu ya Kitaifa ya Haiti wakati rais alipouawa.

Valbrun anadai kuwa Jovenel Moïse alifika katika Ikulu ya Kitaifa ya Haiti, makazi rasmi ya rais, siku mbili kabla ya mauaji.

Kulingana na katibu mkuu, Martine Moïse alitumia saa tano kuondoa "mambo mengi" kutoka kwa ikulu.

Haijabainika ni vitu gani anadaiwa kuchukua, lakini taarifa hiyo inapendekeza kwamba hatua za mke wa rais wa zamani hazikutokana na "intuition" au "nafasi," bali alikuwa na ujuzi wa mapema wa matukio ambayo yangekuja.

Valbrun pia anadai kwamba siku hiyo hiyo alimpigia simu na kumwambia: "Jovenel (Moïse) hajatufanyia chochote" kama rais.

Hati ya mashtaka pia inamtaja mshukiwa mwingine, afisa wa zamani wa Wizara ya Sheria ya Haiti Joseph Felix Badio, ambaye anamtuhumu Martine Moïse kwa kupanga njama ya kumpindua mumewe kutoka mamlaka.

Kulingana na Badio, mke wa rais wa zamani alikula njama na waziri mkuu wa wakati huo, Claude Joseph, kumwondoa Moïse.

Tuhuma juu ya rais wa sasa

Katika taarifa yake kwa gazeti la Miami Herald, Joseph alidai kuwa yeye na mke wa rais wa zamani wanashambuliwa na rais wa sasa na kaimu waziri mkuu wa Haiti, Ariel Henry.

Yule ambaye alikuwa waziri mkuu hadi kuuawa kwa Moïse anashikilia kuwa Henry alikuwa "mnufaika mkuu" wa uhalifu huu, tangu alipoingia madarakani wiki mbili baadaye na amebaki madarakani tangu wakati huo.

Wito wa kujiuzulu umeongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku raia wengi wa Haiti wakilaani kwamba hajatimiza ahadi yake ya kufanya uchaguzi.

Claude Joseph

Chanzo cha picha, Getty Images

Henry anashikilia kuwa uchaguzi hauwezi kuitishwa wakati nchi hiyo inakumbwa na ghasia za magenge, ambayo hayawezi kudhibitiwa tangu kuuawa kwa Rais Moïse.

Claude anamshutumu Henry kwa "kuvuruga mfumo wa haki wa Haiti, kuwashtaki wapinzani wa kisiasa kama mimi."

"Walishindwa kuniua mimi na Martine Moïse mnamo Julai 7, 2021, na sasa wanatumia mfumo wa haki wa Haiti kukuza ajenda yao," aliandika.

Henry hayumo kwenye orodha ya washtakiwa wa Jaji Walther Wesser Voltaire, ingawa rekodi za simu zilionyesha kuwa alipokea simu kadhaa kutoka kwa mmoja wa washukiwa saa moja baada ya mauaji hayo.

Mshukiwa anayedaiwa kumpigia simu rais wa sasa ni Joseph Felix Badio, mwanamume huyohuyo anayetajwa kumshutumu Martine Moïse kwa kupanga njama ya kumpindua mumewe.

Henry amekuwa akishikilia kuwa hakumbuki kupokea simu kutoka kwa Badio usiku wa mauaji hayo.

Hata hivyo, ukweli kwamba mwendesha mashtaka aliyejaribu kumhoji kwa njia ya simu alitimuliwa ulizua ukosoaji na kuchelewesha uchunguzi zaidi.

Waziri mkuu pia alipuuzilia mbali shutuma za kuhusishwa kwa njia yoyote na mauaji ya Moïse kama "habari za uwongo."

Mamlaka za Haiti sio pekee zinazochunguza mauaji ya Moïse.

Watu wanne wamehukumiwa kifungo cha maisha nchini Marekani, ambapo sehemu ya njama ya kumpindua Rais Moïse ilidaiwa kupangwa.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Jaison Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi