Mwiba katika BBC: Waandishi wa habari wanaofanya kazi uhamishoni waelezea

Shazia Haya alikuwa akizunguka Afghanistan kama ripota

Idadi ya wanahabari wa BBC World Service wanaofanya kazi uhamishoni inakadiriwa kuwa karibu mara mbili, hadi 310, tangu 2020.

Takwimu hizo, zilizotolewa kwa mara ya kwanza kabla ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, zinaonesha ukandamizaji wa vyombo vya habari nchini Urusi, Afghanistan na Ethiopia.

Waandishi wa habari kutoka nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Iran, wameishi nje ya nchi kwa zaidi ya muongo mmoja.

Wengi wanakabiliwa na hukumu za jela, vitisho vya kifo ndani na nje.

“Njia pekee wanayoweza kuendelea kuripoti ni kulazimishwa kutoka nyumbani kwao,” asema mkurugenzi wa BBC World Service, Liliane Landor. "Ongezeko tunaloliona la idadi ya waandishi wa habari walio uhamishoni linahusu sana uhuru wa vyombo vya habari."

Wakati Taliban walipochukua udhibiti nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021, BBC iliwaondoa wengi wa timu yake nje ya nchi. Wafanyakazi wa kike hawakuruhusiwa tena kufanya kazi, huku wenzao wa kiume pia wakikabiliwa na vitisho.

Mnamo 2022, baada ya uvamizi wake Ukraine, Urusi ilianzisha sheria mpya ya udhibiti, ikimaanisha kuwa yeyote anayekosoa vita hivyo anaweza kufunguliwa mashtaka. "Ninaita vita, na kwa ajili hiyo ninaweza kufungwa kwa urahisi," anasema Nina Nazarova, mwandishi wa BBC idhaa ya Kirusi, ambaye amehamishia timu yake ya Moscow kwenda Latvia.

Mnamo Aprili mwaka huu, mfanyakazi mwenzake Nina, mwandishi wa BBC Idhaa ya Kirusi Ilya Barabanov, aliitwa "wakala wa kigeni", akishutumiwa "kueneza habari za uongo" na kupinga vita. Yeye na BBC wanakataa hili na wanalipinga mahakamani.

Waandishi wa habari nchini Myanmar na Ethiopia pia wameshuhudia kuongezeka kwa shinikizo, jambo ambalo limewafanya washindwe kuripoti kwa uhuru.

Jodie Ginsburg, kutoka Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari, anasema idadi ya waandishi wa habari waliohamishwa inatoa msaada wa kifedha na kisheria imeongezeka kwa 225% katika miaka mitatu iliyopita.

"Tumekaribia rekodi ya idadi ya waandishi wa habari walioko jela, mauaji ya waandishi wa habari yamefikia kiwango cha juu ambacho hakijaonekana tangu 2015," anaongeza.

Nina Nazarova aliondoka Urusi mnamo 2022 na mumewe na mtoto wa miezi 16

"Mimi huwa makini sana," anasema mwandishi wa BBC Kiajemi Jiyar Gol. Anasema anatafuta njia ya kutoroka. "Nina kamera nyingi za usalama nyumbani kwangu. Nilionywa itakuwa busara kumuhamisha shule ya binti yangu."

Jiyar hajakwenda Iran tangu 2007. Mama yake alipofariki hakuweza kwenda kwenye mazishi yake. Amefaulu kuvuka mpaka kutembelea kaburi lake.

Lakini tangu mke wake alipofariki kwa saratani miaka minne iliyopita, amekuwa mwangalifu zaidi. "Kikitokea kitu kwangu, nini kitatokea kwa binti yangu? Hilo ni jambo ambalo huwa kwenye akili yangu kila wakati," anasema.

"Utawala wa Iran umekua na ujasiri," anaongeza. "Wako chini ya vikwazo vikali, hawajali jumuiya ya kimataifa inafikiria nini juu yao kwa sababu wametengwa."

Mwezi Machi, mtangazaji wa shirika la utangazaji huru la Iran International alidungwa kisu mguuni nje ya nyumba yake ya London, na hivi karibuni polisi wa Uingereza wa kukabiliana na ugaidi walionya juu ya ongezeko la tishio kwa wafanyakazi wa BBC wa Kiajemi wanaoishi Uingereza.

Wafanyakazi kumi wa BBC wa Kiajemi walifahamu hivi karibuni walikuwa wamehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela bila wao kuwepo. Waligundua baada ya wadukuzi kuvujisha taarifa kutoka kwenye mahakama ya Iran.

Hapo awali, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliwashutumu wafanyakazi wa BBC wa Uajemi kwa kuchochea ghasia, matamshi ya chuki na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mwandishi wa habari mmoja wa shirika la World Service barani Afrika, ambaye hakutajwa jina kwa hofu ya kuwachokoza viongozi katika nchi yake, anasema hofu yake kubwa ni kutokuwa na utaifa iwapo serikali yake itakataa kuhuisha paspoti yake.

Kwa Shazia Haya, kutoka BBC Pashto, maisha ya uhamishoni yamejaa hatia. Alihamishwa hadi Uingereza peke yake mnamo 2022 wakati Taliban walipochukua udhibiti nchini Afghanistan, wakiwaacha wazazi na kaka yake huko Kabul.

"Usiku nilioondoka nyumbani, mwendo wa saa 02:00, sijui kwa nini lakini sikuweza kumkumbatia mdogo wangu. Na ninajutia hilo," anasema. "Niko huru hapa, lakini wako katika aina fulani ya gereza."

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi