Ukraine-Urusi: Kupungua misaada ya Magharibi tayari kunaiathiri Ukraine

dxc

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais Zelensky akiwa na Rais wa Marekani, Joe Biden
  • Author, Jonathan Beale
  • Nafasi, BBC

Bila msaada wa kijeshi kutoka Marekani kuna hatari Ukraine inaweza kupoteza vita dhidi ya Urusi.

Rais Volodymyr Zelensky yuko Washington kueleza hilo, akitumai anaweza kulishawishi Bunge la Congress kupitisha msaada wa dola bilioni 60 ambao umekwama huku kukiwa na mzozo kuhusu usalama wa mpaka wa Marekani.

Siku ya Jumapili, mke wa rais wa Ukraine, Olena Zelenska, alionya Ukraine iko katika hatari bila msaada wa Marekani.

Ni Marekani, sio Ulaya, ambayo imetoa sehemu kubwa ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Ulaya sasa iko njiani kuipita Marekani katika suala la msaada wa kiuchumi kwa Ukraine. Lakini Marekani iko mbele sana katika suala la msaada wa kijeshi.

Kulingana na Taasisi ya Kiel, ambayo inafuatilia misaaada hiyo - Marekani imetoa vifaa vya kijeshi vya pauni bilioni 44. Ujerumani, mfadhili mkubwa zaidi wa Ulaya, imechangia pauni bilioni 18.

Marekani sio tu imekuwa muhimu katika kuunga mkono juhudi za vita vya Ukraine, pia imewajibika kwa kiasi kikubwa kuratibu msaada huo.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius hivi majuzi alikiri Umoja wa Ulaya hautafikia lengo lake la kuipatia Ukraine makombora milioni moja kufikia Machi mwaka ujao.

Badala yake Ulaya itatuma nchini Ukraine nusu ya kile ilichoahidi. Kwa wakati huu Ukraine inahitaji angalau makombora milioni 2.4 kwa mwaka ili kuwa na uwezo wa kuendelea na vita.

Wengi wa wanachama wa Nato barani Ulaya bado hawafikii lengo la kutumia 2% ya mapato yao ya kitaifa (Pato la Taifa) katika ulinzi, kiwango kilichowekwa karibu muongo mmoja uliopita.

Wiki hii, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Grant Shapps alisema Ulaya lazima ifanye zaidi: "Hatuwezi kuendelea kuitarajia Marekani kila mara kuiokoa Ulaya."

Pia Unaweza Kusoma

Uchumi wa vita wa Urusi

FD

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi, Vladimir Putin

Maafisa wa nchi za Magharibi wanakadiria kuwa karibu 40% ya matumizi ya serikali ya Urusi mwaka ujao yatakuwa katika ulinzi na usalama - zaidi ya bajeti yake ya afya na elimu kwa pamoja.

Wakati kama huu mwaka jana, Urusi ilipokea takribani ndege 40 zisizo na rubani za Shahed kutoka Iran. Sasa inaaminika inatengeneza hadi ya ndege 300 kwa mwezi.

Mwishoni mwa 2022, Urusi iliweza kutengeneza karibu makombora 40 ya masafa marefu kwa mwezi. Sasa inakadiriwa kufikia makombora mia moja kwa mwezi, licha ya vikwazo vya magharibi.

Pia imeongeza uzalishaji wake wa mizinga, na kujaza ghala lake kwa usaidizi wa Korea Kaskazini.

Maafisa wa nchi za Magharibi wanakadiria Urusi ilikuwa ikipata hasara kubwa katika kipindi cha mwezi wa Novemba katika mashambulizi yake ya Avdiivka pekee mashariki mwa Ukraine.

Msaada kwa Ukraine Wapungua

YGF

Matumaini ya nchi za Magharibi ya mwaka mmoja uliopita, kufuatia mafanikio ya awali ya mashambulizi ya Ukraine, yamepungua mno.

Mashambulizi ya Ukraine ya majira ya kiangazi hayakufikia malengo ya kuvunja safu za ulinzi za Urusi upande wa kusini.

Mtaalamu wa masuala ya ulinzi kutoka Taasisi ya Royal United Service, Jack Watling, anasema, “hivi vitakuwa vita vya muda mrefu ambavyo vitaleta uchovu na kubadilisha hesabu za vita."

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kiel, ahadi za msaada mpya kwa Ukraine kati ya Agosti na Oktoba mwaka huu zilishuka hadi kiwango cha chini kabisa tangu Januari 2022.

Kati ya mataifa 42 wafadhili yaliyofuatiliwa, ni 20 pekee ambayo yametoa msaada mpya katika kipindi hicho – msaada umeshuka hadi 90% kutoka mwaka uliopita.

Wengi wa wanaounga mkono Ukraine, angalau hadharani, wanasema msaada wao haujapungua. Lakini baadhi ya mataifa yanajitahidi kuendana na kiwango cha michango ya kijeshi ya awali - huku akiba yao ikiwa tayari imepungua.

Slovakia, chini ya serikali mpya, imeondoa uungaji mkono wake kabisa.

Bado haijafahamika ni kiasi gani cha msaada kwa Ukraine kitakwenda kutoka Uholanzi katika siku zijazo, kufuatia mafanikio ya uchaguzi ya chama cha mrengo wa kulia cha Geert Wilders. Waholanzi, hadi sasa, wamekuwa sehemu muhimu ya muungano unaoahidi kuipatia Ukraine ndege za F-16.

Athari kwa za siku zijazo

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Makombora ya ulinzi wa anga ya Ukraine

Afisa mmoja wa magharibi anasema kuna matarajio madogo ya aina yoyote ya mafanikio makubwa kati ya pande zote mbili kwa miezi ijayo.

Urusi na Ukraine zimejikita zaidi kujilinda – ni aina ya operesheni ambazo hutumia rasilimali nyingi sana. Kutokana na uwezekano wa Ukraine kuwa na kiwango kisichotosha cha silaha katika miezi ijayo - kuna huenda nguvu za vikosi vyake itazidi kumomonyoka.

Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa White House, aliiambia gazeti la New York Times, “Marekani haitaweza tena kutuma mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine kama vile betri za Patriot na makombora.”

Kauli hiyo inakuja huku Urusi ikitarajiwa kuongeza ulengaji wake wa miundombinu muhimu nchini Ukraine katika wiki zijazo.

Watling, ambaye amerejea kutoka Ukraine, anasema kutokuwa na uhakika juu ya misaada - tayari kunaathiri sana uwezo wa Ukraine wa kutengeneza mipango.

Anasema mkwamo wa sasa wa bunge la Marekani unazuia uwezo wa Ukraine sio tu kuweza kupanga mipango yake inayofuata kwenye uwanja wa vita, lakini pia kueleza mipango hiyo ili kupata uungwaji mkono zaidi kutoka nchi za magharibi.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Munira Hussein.