Fuvu la miaka 4,000 lafichua jinsi Wamisri walivyojaribu upasuaji wa saratani

xc

Chanzo cha picha, FRONTIER/TATIANA TONDINI, ALBERT ISIDRO, EDGAR CAMARÓS

Maelezo ya picha, Fuvu hilo lilikuwa la mwanaume aliyefariki akiwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35.

Ugunduzi wa hivi karibuni wa mafuvu mawili na kundi la wanasayansi, unaweza kubadilisha uelewa wetu wa historia ya matibabu.

Hii ni mifupa ya Wamisri ya maelfu ya miaka katika makumbusho ya Duckworth Collection ya Chuo Kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza, na inaonyesha vidonda vinavyosababishwa na uvimbe wa saratani.

Wataalamu wanadokeza kwamba moja ya fuvu hilo ambalo ni la miaka 4,000 iliyopita, lilifanyiwa upasuaji, ama kwa nia ya kuondoa uvimbe aliokuwa nao mtu huyo au uchunguzi wa maiti yake ili kuelewa uvimbe huo.

Edgard Camarós, mtaalamu wa magonjwa ya kale katika Chuo Kikuu cha Santiago de Compostela nchini Uhispania na mwandishi wa utafiti huo uliochapishwa Jumatano katika jarida la Frontiers, alisema ni jambo jipya kuwa tuna ushahidi Wamisri walijaribu kuelewa ugonjwa huo.

"Inafurahisha kuelewa kuwa kuna maana kwanini upasuaji huu ulifanyika; na hiyo ndiyo tiba ya hali ya juu ya Misri ya kale," Camarós aliambia BBC.

Fuvu lililofanyiwa upasuaji lilikuwa la mwanaume ambaye alikuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35 alipofariki, watafiti waliliambia shirika la habari la Press Association.

Pia waligundua vidonda vidogo vidogo 30, na kupendekeza kuwa saratani ilikuwa imeenea.

Pia unaweza kusoma

Fuvu la pili

ki

Chanzo cha picha, FRONTIER/TATIANA TONDINI, ALBERT ISIDRO, EDGAR CAMARÓS

Maelezo ya picha, Wamisri walijaribu kuitafiti saratani.

Katika makumbusho hayo, wanasayansi pia walipata fuvu la umri wa miaka 2,000, ambalo lilikuwa la mwanamke mwenye umri wa miaka 50.

Fuvu hilo linaonyesha vidonda vya saratani iliyoharibu fuvu, lakini wakati huo huo inaonyesha mtu huyo alikuwa amepona jeraha la kukatwa.

Kulingana na Camarós, jambo hili si la kawaida, kutokana na ukweli kuwa majeraha yanayohusiana na matukio ya vurugu - mara nyingi yapo katika mabaki ya wanaume.

Fuvu hilo lilichambuliwa na kompyuta na kulingana na wanasayansi, ishara za saratani zilikuwa wazi sana.

"Tunajua ilikuwa saratani kwa sababu ya aina ya vidonda kwenye mifupa, ambavyo huharibu mifupa," mwanasayansi huyo wa Uhispania anasema.

Ugonjwa wa zamani

k

Chanzo cha picha, FRONTIER/TATIANA TONDINI, ALBERT ISIDRO, EDGAR CAMARÓS

Maelezo ya picha, Vidonda vya saratani katika fuvu

Saratani ni ugonjwa ambao kwa sasa unaonekana kama ugonjwa wa zama hizi, hasa kutokana na uchafuzi wa mazingira, pamoja na chakula na vinasaba.

Lakini utafiti unaonyesha ni ugonjwa huo upo tangu nyakati za zamani.

"Saratani imekuwa nasi tangu kale na hata dinosau (dinosaur) waliugua saratani," anasema Camarós.

Mwanasayansi huyo anafafanua kuwa bado utafiti zaidi unahitajika ili kuelewa jinsi mababu zetu walivyokabiliana na ugonjwa huo.

“Lengo ni kukamilisha historia ya saratani tangu mwanzo wa historia ya mwanadamu," aliliambia shirika la Habari la Press Association.