Ni nini huifanya Canada kuwavutia watu wengi kutaka kuishi huko?

.

Chanzo cha picha, Muddymari/Getty Images

Ikiwa na Vancouver, Calgary na Toronto zote zimeorodheshwa kwenye kundi la 10 bora katika kipimo cha ‘Global Liveability Index 2023’, tunazungumza na wakazi katika kila jiji ili kujua ni nini hufanya maisha kuwa mazuri zaidi maeneo hayo.

Ingawa maeneo ya Ulaya na Skandinavia mara kwa mara hujikuta yakiwa juu ya viwango vya dunia - kama vile nchi zenye afya bora zaidi duniani, au nchi bora zaidi za kulea watoto - Canada imekuwa ikipanda daraja kimya kimya kama nchi yenye ushindani.

Hilo limedhihirika haswa katika viwango vya hivi karibuni zaidi vya miji inayopendwa na wengi, iliyofanywa na Kitengo cha ‘Economist Intelligence’, ambacho kilitaja miji mitatu ya Canada katika 10 bora, zaidi ya nchi nyingine yoyote iliyowakilishwa.

Miji mitatu iliyoongoza ya Canada kwenye orodha hiyo ilijumuisha Vancouver (iliyoorodheshwa ya 5), Calgary (iliyoshika nambari 7 na Geneva) na Toronto (iliyoshika nafasi ya 9), kila moja ikiwa na alama bora za afya na elimu.

Mambo hayo yanawavutia Wakanada, wanaosifu sera chanya za serikali zinazoboresha maisha ya maeneo hayo.

"Siasa zetu zinazoendelea na huduma ya afya kwa wote hufanya Canada kuwa mahali pazuri pa kuishi," mkazi wa Vancouver Samantha Falk alisema.

"Siwezi kufikiria kuishi katika nchi ambayo ni lazima uwe na wasiwasi juu ya kumudu kuona daktari au kumpeleka mtoto wangu hospitalini, au kuwa katika hatari ya kufilisika kwa kuwa na saratani."

Hisia hii ya kujali inaenea zaidi hata kuliko wanasiasa, na kusababisha hisia ya jumuiya ambayo inaboresha maisha kazini na nyumbani pia.

"Kuanzia kusaidia shuleni hadi wamiliki wa biashara, Wakanada wanajulikana kwa urafiki wao na kutoa ushirikiano," alisema Jane Stoller, mkazi wa Vancouver na mwanzilishi wa Organized Jane, huduma ya kuandaa biashara ya muda mrefu.

"Hisia hii ya urafiki inakuza mazingira mazuri ambapo watu wanaweza kustawi na kupata mafanikio katika maisha yao ya kibinafsi na ya kitaaluma."

.

Chanzo cha picha, Credit: Orchidpoet/Getty Images

Uwekezaji wa Kanada katika usafiri wa umma na mifumo ya usafiri pia hurahisisha urambazaji katika miji yake mikubwa.

Falk, ambaye ameishi Montreal, Calgary na Toronto, hakupata leseni yake ya udereva hadi alipokuwa na umri wa miaka 24, na rafiki yake hatimaye anapata yake akiwa na miaka 53, kwa sababu tu hawajahitaji gari kwa ajili ya usafiri.

Hata hivyo, kile ambacho wakaazi hupenda zaidi ni uhusiano thabiti ambao taifa linao nje ya nchi.

"Miji yote mitatu [ambayo watu wangependa kuishi zaidi] - kama miji mingi nchini Canada - iko karibu na maeneo ya asili, na pia imejumuisha hilo katika muundo wao wa jiji," Falk alisema.

"Kuna mfumo wa mifereji ya maji na fukwe huko Toronto; Mont Royal na mitaa yenye miti mingi huko Montreal; Vancouver ina bustani ya Stanley, mojawapo ya mifano bora zaidi duniani ya asili ya mijini."

Lakini hata nje ya miji mikubwa, zingatio la mazingira ya asili bado ni kipengele cha msingi, kuakisi umuhimu wa nyika kwa wakazi.

"Sisi ni watu wa kupenda kutokatoka!" Falk alisema.

.

Chanzo cha picha, Laughingmango/Getty Images

Vancouver

Ipo kwenye pwani ya magharibi ya nchi yenye mandhari nzuri, Vancouver ilionekana kama jiji linalopendwa zaidi kutokana na alama za juu zaidi katika taswira ya utamaduni na mazingira, likishindwa na Auckland pekee katika orodha ya 10 bora.

Hayo ni maoni ambayo wakaazi wanayaunga mkono, ambao wamependezwa zaidi na asili ya mazingira ya eneo hilo.

"Mchanganyiko wa kipekee na mzuri wa milima na bahari Vancouver, hulifanya kuwa jiji yenye kupendwa mno," alisema Falk, ambaye anaendesha kampuni yake ya mawasiliano inayojulikana nje ya jiji.

"Hata baada ya kuishi Vancouver kwa miaka 20, jiji bado linanivuta."

Ili kupata mazuri zaidi na kujihisi uko nyumbani katika eneo hili, anasema lazima utoke nje – hata (na hasa) wakati wa mvua.

Sehemu moja rahisi ya kufanya hivyo ni bustani ya Stanley, mbuga ya umma ya hekta 405 katikati mwa jiji ambalo lina msitu wa mvua wenye miti ya karne nyingi iliyopita, ikiwa ni pamoja na kisiki cha mwerezi mwekundu wenye umri wa miaka 700-800 unaoitwa ‘Hollow Tree’.

Anapendekeza kupanda urefu wa 2.9km kwenye uso wa mlima Grouse.

"Mara nyingi hujulikana kama 'stairmaster', kupanda mlima huo wakati mwingi itakufanya uhisi kama kutapika, lakini utakapofika juu kileleni utaona thamani yake," alisema.

"Kunywa kahawa au glasi ya divai kwenye mgahawa ulio juu ya mlima na kupata mwonekano wa kipekee - na urahisi uliopo wakati wa kushuka mlima."

.

Chanzo cha picha, AJ_Watt/Getty Images

Calgary

Ikiwa karibu na Milima ya Rocky katika mkoa wa magharibi wa Alberta, Calgary ilipita miji mingine miwili ya Canada kwa matokeo yake kwenye (kipimo cha kuangazia machafuko ya kiraia na ufisadi wa serikali).

Wakazi wanaelezea Calgary kama kuwa na mji mdogo na kujisikia kupata huduma za miji mikubwa, wakati pia kuna gharama ya chini ya maisha kulinganishwa na miji mingine ya Canada.

"Licha ya kuwa mojawapo ya miji mikubwa zaidi nchini Canada, Calgary imeweza kuendeleza haiba ya kipekee, inayotoka kwa wenyeji ambao ni marafiki, mawazo yanayozingatia jamii na masoko ya wakulima yanayozingatia ujirani," alisema mwanablogu ambaye pia ni mkazi Lora Pope.

"Bado haikosekani linapokuja suala la mikahawa ya kisasa, sherehe za kitamaduni na maisha ya usiku ya kushangaza."

Jiji pia ni la tatu kwa kuwa anuwai zaidi nchini Canada lenye asili zaidi ya 240 za makabila na lugha 165.

Jiji pia lina sekta ya mafuta na gesi yenye faida kubwa, jumuia ya wafanyabiashara iliyoajiri watu wengi na lenye gharama nafuu ya maisha.

"Wakalgaria wana pesa na wanapenda kuzitumia," alisema Jessie P Cayabo, mtaalamu wa mawasiliano ambaye alihamia jiji hilo kutoka Edmonton miaka mitatu iliyopita.

Kila mwaka kuna tamasha la Calgary Stampede (ambalo huanza Ijumaa ya kwanza ya Julai) na kuendelea kwa siku 10 ni tamasha ambapo kila mtu huvaa gia za magharibi na kuvutia watu kutoka kote ulimwenguni.

"Watu huudhuria sana tamasha hili. Mahala pa kuegesha magari hujaa huku mikahawa ikiwa na shughuli nyingi," aliungwa mkono na mkazi Shannon Hughes, mmiliki wa kampuni ya ushauri ya Captivate Benefits iliyoko Calgary.

Anapendekeza kupiga simu mapema ili uwezeke kujiwekea nafasi katika mkahawa wa Major Tom wakati wa machweo upate sehemu ya kutazama vizuri milima ya jiji.

.

Chanzo cha picha, Rubens Alarcon/Alamy

Toronto

Kama jiji lenye watu wengi zaidi nchini Canada, Toronto inachanganya midundo ya miji mikubwa na bustani zaidi ya 1,500 ambazo hufanya wakaazi kutoka nje na kuzitembelea.

Limepata alama nzuri katika uthabiti, Toronto hudumisha hali ya usalama ambayo huwawezesha watu kujisikia vizuri iwe wanatembea, kuchukua usafiri wa umma au kuendesha baiskeli.

Hasa, miundombinu inayozingatia binadamu inamaanisha kuwa maisha ni rahisi zaidi kuliko katika miji mikubwa.

Wakazi hasa hufurahia PATH, njia ya waenda kwa miguu chini ya ardhi ambayo hufanya majira ya baridi ya Canada kuwa yenye kuvumilika.

"Kutoka ofisini kwangu hadi uwanja wa ndege kwa [treni], kula, kufanya manunuzi na hata miadi ya daktari, kila kitu kinafikiwa kwa urahisi bila hitaji la kuvaa koti msimu wa baridi," alisema mkazi Hoang Anh Le, ambaye ni mwanablogu.

Mkazi Kyra Marskell anakubali, alisema wakati Tume ya Usafiri ya Toronto (TTC) haikosi dosari zake, kuwa na usafiri wa treni uliopangwa vizuri – unaopatikana ndani ya dakika nne - huleta tofauti kubwa wakati unatoka kwenye kitongoji ambapo kuendesha gari ndilo chaguo pekee.

"Pia tuna baiskeli za kukodisha kuzunguka jiji ambalo ni chaguo bora la kusafiri na nimefurahia huduma hiyo hivi majuzi," aliongeza.

Jiji pia linajulikana kwa utofauti wake, zaidi ya 51% ya wakaazi wake wakizaliwa nje ya Canada.

"Ndio mji mkuu pekee wa Magharibi ambapo [wasio wazungu] ni wengi," alisema Marcus Räder, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza katika kampuni ya programu ya Hostaway.

"Kuna fursa za kupata tamaduni na lugha nyingi hapa, na Canada inakumbatia tamaduni nyingi badala ya kushinikiza kuiga."

Utofauti huu wa kitamaduni huboresha jamii kupitia sherehe mbalimbali, vyakula kwa kila bei na heshima ya kubadilishana mawazo na njia mpya za kuishi.