Jinsi mwezi unavyorefusha siku duniani

D

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Mabilioni ya miaka iliyopita, wastani wa siku ya duniani ilikuwa ni chini ya saa 13. Tangu wakati huo ukubwa wa siku umekuwa ukirefuka polepole, kwa sababu ya mwezi na bahari zetu.

Baadhi ya watu kwa karne, hutumia mienendo ya mwezi kwa ajili ya kalenda zao – kutokana na mwanga wa jua unaoakisiwa kwenye uso wa mwezi.

Muhimu zaidi, mwezi husaidia kuunda mazingira ambayo hufanya maisha kwenye sayari yetu yawezekane na mwezi unaweza kuathiri mifumo ya hali ya hewa inayounda maisha yetu leo.

Pia unaweza kusoma

Kwanini siku zinakuwa ndefu?

D

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Kwa kila mwaka unaopita, mwezi husogea mbali zaidi na dunia na wastani wa urefu wa siku unakuwa mrefu kidogo.

Mwezi unasogea mbele – kwenda mbali zaidi kutoka dunia yetu. Wanasayansi hivi karibuni wameweza kupima kwa usahihi wa milimita jinsi mwezi unavyosogea mbali zaidi.

Walithibitisha kuwa mwezi husogea kwa kasi ya sentimita 3.8 kila mwaka. Na hilo linapotokea, siku zetu zinakuwa ndefu kidogo.

David Waltham, profesa wa jiofizikia kutoka Chuo Kikuu cha Royal Holloway, London, ambaye anasoma uhusiano kati ya dunia na mwezi, anasema:

"Mawimbi ya bahari hupunguza kasi ya mzunguko wa dunia. Dunia inapozunguka, mvuto wa mwezi huvuta bahari na kuunda mawimbi ya juu na ya chini.

Dunia inazunguka kwenye mhimili wake kwa kasi zaidi kuliko mzunguko wa wezi, ikimaanisha maji husonga mbele kidogo ya mwezi, lakini mwezi unajaribu kuyarudisha nyuma.

Hii hupunguza polepole mzunguko wa sayari yetu, ikipunguza kasi yake huku mwezi ukipata nishati na urefu katika mzunguko wake.

Kupungua huko kwa mzunguko wa sayari yetu kunafanya ongezeko la wastani wa siku ya dunia kwa milisekunde 1.09 kwa karne tangu mwisho wa karne ya 17.

Zamani na Sasa

SD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Umbali kati ya Dunia na Mwezi umeongezeka sana kwa mamilioni ya miaka.

Inaaminika kuwa Mwezi uliundwa katika miaka milioni 50 ya kwanza baada ya kuzaliwa kwa mfumo wa Jua. Mwezi kwa sasa uko kilomita 384,400 kutoka duniani.

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha karibu miaka bilioni 3.2 iliyopita, mwezi ulikuwa umbali wa kilomita 270,000.

"Dunia, ambayo inazunguka kwa kasi, ilikuwa na siku fupi, kwa hiyo katika kipindi cha saa 24 jua lilichomoza mara mbili na kuzama mara mbili," anasema Tom Eulenfeld, mtaalamu wa jiofizikia ambaye aliongoza utafiti huo katika Chuo Kikuu cha Friedrich Schiller huko Jena, Ujerumani.

Anaongeza kwa kusema, "hilo linaweza kuwa limepunguza tofauti ya hali ya hewa kati ya mchana na usiku na kuathiri biokemia ya viumbe."

Tafiti zao zinaonyesha kasi ya mzunguzo wa mwezi haijabadilika pia; huongezeka na kisha hupungua kwa muda.

Utafiti wa Vanina López de Azarevich, mwanajiolojia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Salta nchini Argentia, unasema karibu miaka milioni 550-625 iliyopita mwezi ulikuwa unasogea hadi inchi 2.8 (sentimita 7) kwa mwaka.

"Kasi ambayo mwezi ulikuwa ukienda mbali na dunia kwa hakika ilibadilika baada ya muda na itabadilika tena katika siku zijazo," anasema Eulenfeld.

Kwa sasa tunaishi katika kipindi ambacho kasi ya kusogea mwezi ni ya juu isivyo kawaida: Mwezi ungelazimika tu kuondoka kwa kasi ya sasa kwa miaka bilioni 1.5 ili kufikia nafasi uliyopo leo.

Mchakato huu umekuwa ukitokea tangu mwezi ulipoundwa miaka bilioni 4.5 iliyopita, ambayo inaonyesha kwamba wakati fulani huko nyuma ulikuwa ukisogea polepole.

Mawimbi

Kwa sasa mawimbi ni makubwa mara tatu kuliko tunavyotarajia," anasema Waltham. Hii inahusishwa na Bahari ya Atlantiki.

Bonde la Atlantiki ya Kaskazini lina athari kubwa, kwa hiyo maji yaliyomo hutembea na kurudi kwa kasi sawa na ile ya mawimbi. Hii ina maana mawimbi ni makubwa zaidi.

Fikiria kama kumsukuma mtoto kwenye bembea: anaenda juu na kurudi. Na hurudi zaidi kutokana na msukumo wa kwenda.

"Mifano hiyo inaonyesha ikiwa tutarudi nyuma miaka milioni, nguvu ya mawimbi ilikuwa ndogo kwa sababu mabara yalikuwa katika nafasi tofauti."

Nini kitatokea siku zijazo?

SD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwezi utaendelea kusonga mbali na dunia.

Kwa hivyo kunaweza kuwa na wakati ambapo dunia haina tena mwezi?

Hata kwa kiwango chake cha juu cha kusogea, mwezi hauwezekani kuondoka kabisa duniani.

Kuangamia kwa jua kunaweza kutokea kabla ya mwezi kutoweka, takribani miaka bilioni 5 hadi 10 ijayo, na kuna uwezekano wanadamu watatoweka muda mrefu kabla ya hapo.

Binaadamu wenyewe wanaweza kuchangia katika kurefusha siku zaidi kidogo, kwa kupunguza kiasi cha maji yaliyonaswa kwenye barafu na kuyeyuka kunakosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

"Barafu kimsingi hukandamiza mawimbi," Waltham anasema, akibainisha kuwa takriban miaka milioni 600-900 iliyopita, wakati sayari yetu inafikiriwa kuingia katika kipindi cha barafu, kulikuwa na kushuka kwa kasi ya mwezi kusogea.

Kinadharia, kizazi kijacho cha wanaanga ambao wataruka hadi mwezini kwa mpango wa NASA wa Artemis wataweza kusema waliona sayari yao kutoka mbali zaidi kuliko watangulizi wao wa Apollo walivyofanya miaka 60 iliyopita.

Kwa sisi wengine, maisha yetu yatakuwa mafupi sana kuona mabilioni ya sekunde ambayo huongezeka kila siku inayopita.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi