Jinsi mwanamke wa Urusi anavyowasaidia mamluki wa zamani wa Wagner

Olga Antipina

Chanzo cha picha, BBC

  • Author, Nina Nazarova
  • Nafasi, BBC News Russian

Mwanaume mwenye umri wa miaka hamsini alikuwa amesimama kando ya barabara kuu ya Trans-Siberian karibu na jiji la Krasnoyarsk, zaidi ya maili 2,000 mashariki mwa Moscow, wakati gari jeupe liliposimama.

Alikuwa amevalia mavazi ya kujificha, akivalia kiraka cheusi na chekundu, ambacho kilikuwa alama ya 'Wagner', kikundi binafsi cha mamluki cha Urusi kinachotambuliwa kama shirika la kigaidi nchini Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine. Alikuwa na mkoba tu.

Katika gari hilo alikuwa Olga Antipina, mkazi wa umri wa miaka 48 wa mji mdogo wa Siberia wa Sosnovoborsk ambaye aliamua kuwasaidia mamluki wa zamani wa Wagner kuwa na maisha ya amani baada ya kurudi kutoka mstari wa mbele katika vita vya Urusi nchini Ukraine.

Kabla ya kumchukua kwenye barabara kuu, Olga hakuwahi kukutana na Valeriy Molokov, lakini alijua maisha yake ya nyuma, kwamba kabla ya kuajiriwa na 'Wagner' kupigana huko Ukraine, mzee huyo wa miaka 54 alikuwa akitumikia kifungo kwa mauaji.

Hata hivyo, alikubali kumsaidia.

Kuwaandikisha wafungwa

Urusi ilikuwa imeanza kuandikisha wafungwa kwa wingi miezi minne baada ya uvamizi wake huko Ukraine mnamo mwaka 2022.

Takribani wafungwa 50,000 wa Urusi walikwenda kupigana vitani, kwani waliahidiwa kusamehewa ndani ya miezi sita na malipo makubwa ya pesa taslimu baada ya kurejea.

Maelfu walikufa, lakini wengi waliweza kuishi na kurudi nyumbani.

Maoni ya umma ya Urusi yamegawanyika kuhusu kurejeshwa kwa mamluki wa zamani wa ‘Wagner’ kwani watu wengi wanawaogopa na kufikiria kuwa ni kinyume cha maadili kuwasamehe wafungwa na kuwaacha wakipigana vitani.

Pia, baadhi ya waajiri wa zamani wa ‘Wagner’ wameshutumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine na kutekeleza hukumu ya kunyonga.

Picha ya Valeriy Molokov

Kumeripotiwa zaidi ya kesi 200 mpya za mahakama kuhusu makosa yaliyotendwa na wafungwa wa zamani waliosamehewa na Rais Putin.

Valeriy Molokov alihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela mnamo Julai 2022 kwa mauaji ya dada yake mkubwa miezi sita nyuma.

Alisemekana kuwa alikunywa pombe wakati wawili hao walipogombana usiku wa kuamkia mwaka mpya.

Akampiga usoni, saa chache baadaye akampiga tena ngumi ya kichwa na kuendelea kumpiga hata baada ya kuanguka chini.

Gari ya kubeba wagonjwa iliitwa saa chache baadaye, kwani mdogo wao ambaye alishuhudia ugomvi huo alisema Valeriy alimzuia kupiga simu, akisema wanywe vodka badala yake.

Dada mkubwa alikufa hospitalini kutokana na kiwewe wiki moja baadaye.

Kumeripotiwa zaidi ya kesi 200 mpya za mahakama kuhusu makosa yaliyotendwa na wafungwa wa zamani waliosamehewa na Rais Putin.

Licha ya hali ya kutisha ya uhalifu huo, Molokov alikuwa amehudumu kwa miezi michache tu ambapo mnamo 2023 aliajiriwa na Wagner na kupelekwa mstari wa mbele.

Alipigana huko Bakhmut, jiji lililo katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine, na akarejea Urusi mnamo Agosti 2023 baada ya kupata jeraha.

Hakuwa na mahali popote pa kuishi au hakuna maisha yanayofaa ya kumfanya kurudi wakati mtu mmoja alimpa nambari ya Olga, akisema angeweza kumsaidia.

'Jambo pekee la manufaa '

Valeriy Molokov hakuwa mamluki wa kwanza wa Wagner au mhalifu wa kwanza aliyepatikana na hatia katika maisha ya Olga.

Mwenzi wake wa zamani pia aliajiriwa na 'Wagner', alikuwa ametoka gerezani kupigana vita na akauawa.

Walikutana alipokuwa gerezani na kuanza kuandikiana barua.

Baada ya kutoka gerezani, walikaa pamoja kwa miaka 13 na kupata watoto watatu, lakini marehemu mume wake alikuwa akinywa pombe kupita kiasi na kumpiga yeye na watoto wao mara kwa mara.

Mwaka 2015 alihukumiwa tena kwa uuzaji wa dawa za kulevya. Mnamo Machi 2023, bila kujua Olga, aliajiriwa na 'Wagner' wakati alipokuwa gerezani.

Olga alikiita kifo chake ‘jambo la pekee lenye manufaa ambalo amewahi kufanya kwa familia yake’ alipomnunulia mtoto wao mkubwa nyumba ikiwa ni fidia ambayo alipokea kutoka kwa ‘Wagner’ baada ya kuuawa vitani.

Kufuatia uzoefu wake mwenyewe, aliamua kusaidia mamluki wengine wa zamani wa 'Wagner' wanaorudi kutoka mstari wa mbele.

Olga Antipina

Baada ya kukutana na Valeriy, Olga alimtafutia makazi ya muda na akashauri afanye nini na fidia aliyopokea kutoka kwa ‘Wagner’.

"Alikuwa kama mtoto [akisema] nataka hiki, nataka kile. Nilimwambia: Hapana,” Olga alikumbuka, akizungumza na BBC News idhaa ya Kirusi.

"Kitu cha kwanza unachohitaji ni mali yako mwenyewe, kwa hivyo tunakununulia moja. Halafu, je, unataka gari? Sawa, tutakununulia gari,” alimwambia Valeriy.

Olga alisema hakuwa na nia ya kifedha ya kumsaidia, na kwamba hakuwa na wasiwasi kuhusu maisha yake ya zamani.

Amekuwa mshiriki wa Kanisa la Pentekoste, kanisa la kiinjilisti nchini Urusi, na alipoulizwa maoni yake kuhusu vita vya Ukraine alisema;

“Biblia inasema kwamba nyakati za mwisho zinskuja, na ndugu angempinga ndugu, na hili ndilo linalotokea.”

Valeriy pia alianza kwenda kwenye Kanisa la Pentekoste kila Jumapili na alishukuru sana msaada wa Olga hivi kwamba hata akapendekeza kumuoa wakati fulani. Alikataa pendekezo lake.

Alifanya kazi kwa muda katika kampuni ya ulinzi kwa zaidi ya mwezi mmoja, lakini hakuweza kuendelea.

Alipoulizwa juu ya nini kingekuwa kwake ikiwa Olga hangemsaidia, Valeriy alisema kwamba labda angerudi kwenye mstari wa mbele.

"Kusema ukweli, sina hamu kubwa [ya kurudi]," alisema. “Lakini inanivutia sana. Hapo nikajua ni nani adui yangu. Hapa sipo.”

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga.