Je, kutumia silaha za Magharibi dhidi ya Urusi kutasaidia Ukraine kuvibadili vita?

Majengo yaliyoharibika

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukraine sasa inaruhusiwa kutumia silaha za Magharibi kulenga shabaha ndani ya Urusi. Je, uamuzi huu utabadilikaje na utaathiri vipi mstari wa mbele nchini Ukraine?

Hadi sasa, nchi za Magharibi zilizuia matumizi ya silaha zao kwa malengo ya kijeshi yaliyo ndani ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na Crimea na maeneo yaliyokaliwa.

Walikuwa na wasiwasi kwamba kushambulia katika mpaka unaotambulika kimataifa kwa silaha zinazotolewa na nchi za Nato kungezidisha mzozo huo.

Lakini hatua ya hivi punde ya Urusi katika eneo la kaskazini mashariki la Kharkiv yaliwashawishi washirika wa Kyiv kwamba ili kujilinda, Ukraine lazima iweze kuharibu maeneo ya kijeshi katika upande mwingine wa mpaka pia.

Mwezi uliopita, Urusi ilianzisha mashambulizi makubwa ya ardhini katika eneo hilo, na kufungua njia mpya na kuteka vijiji kadhaa.

Hatua hiyo ya Urusi ilileta tishio kubwa kwa Kharkiv, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ukraine, ambalo liko umbali wa kilomita 30 tu kutoka mpakani.

Mpaka katika eneo hili ni mstari wa mbele pia, kwa hivyo marufuku ya kutumia silaha za Magharibi kulenga shabaha zaidi ya Ukraine iliwezesha wanajeshi wa Urusi kujiandaa kwa operesheni hiyo katika mazingira salama.

Kutokana na shinikizo la kuongezeka kutoka kwa Ukraine na mataifa mengine ya Ulaya, Marekani ilikubali kubadili sera yake na kuruhusu Kyiv kuishambulia Urusi kwa silaha za Magharibi.

"Ili kukidhi kile kinachoendelea kwenye uwanja wa vita, tunahakikisha kuwa Ukraine ina kile inachohitaji, wakati inapohitaji," Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Nato mjini Prague siku ya Ijumaa.

Maeneo mengi ya makazi yalipigwa na shambulio la hivi karibuni la Urusi huko Kharkiv

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku chache tu kabla ya tangazo hili, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitishia kupanua "maeneo ya usafi" ikiwa silaha za masafa marefu za Magharibi zitatumika kupiga eneo la Urusi.

Alisema kuwa nchi za Nato barani Ulaya lazima zikumbuke kuwa zina "majimbo yenye maeneo madogo na idadi kubwa ya watu".

"Lazima wazingatie jambo hili kabla ya kujadili kuhusu shambulizi ndani ya eneo la Urusi," aliongeza.

Kuepuka kuongezeka pengine ndiyo sababu iliyofanya Marekani kutojumuisha silaha za masafa marefu kama vile ATACMS (Mifumo ya Mbinu ya Kijeshi ya Kombora) katika idhini yake ya kushambulia Urusi.

Makombora haya yana umbali wa kilomita 300 na yanaweza kutumika kupiga kambi za kijeshi na viwanja vya ndege hadi katika ardhi ya Urusi.

Vizuizi kama hivyo vinaiacha Ukraine ikiwa na chaguo pekee la kuzingatia maeneo karibu na mpaka wake. Lakini hii bado ni mabadiliko makubwa ya sera na washirika wakuu wa Kyiv.

Hata ikiwa na masafa mafupi, hadi 70km, virusha roketi nyingi kama vile HIMARS vinaweza kutatiza kwa kiasi kikubwa shughuli za usafirishaji wa Urusi na harakati za askari, ambayo hatimaye itapunguza kasi ya mipango yoyote ya kushambulia.

Sasa, Ukraine inaweza "kushambulia maeneo ambayo adui walijilimbikizia wanajeshi wake, vifaa vya kuhifadhia vitu ambavyo vinatumika kushambulia Ukraine," anasema Yuriy Povkh kutoka kundi la mbinu la Kharkiv ambalo linaratibu operesheni za kijeshi kaskazini mashariki.

Mapema wiki hii, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kuwa Urusi ilikuwa inakusanya wanajeshi wake kilomita 90 tu kutoka Kharkiv kwa ajili ya mashambulizi mengine.

Na Taasisi ya Uchunguzi wa Vita ilizitathimini picha za setilaiti na kuthibitisha kwamba kulikuwa na "shughuli zilizopanuliwa kwenye bohari na maghala" katika eneo hilo.

Kwa hivyo uwezo wa kulenga vituo hivyo utaimarisha sana uwezo wa vikosi vya Ukraine kuzima mashambulizi mapya katika eneo hilo.

Kuondoa marufuku ya silaha za Magharibi, hata hivyo, hakuna uwezekano wa kusaidia kulinda Ukraine dhidi ya mabomu ya Kirusi ya kuteleza yanayojulikana kama KAB. Yana athari mbaya na hutumiwa mara kwa mara kupiga mabomu Kharkiv na miji mingine ya mpaka.

Lakini ili kukomesha mashambulizi hayo, vikosi vya Ukraine lazima vilenge ndege zinazoangusha hizo KAB hatari.

Ukraine ilipokea HIMARS kama sehemu ya usaidizi wao wa kijeshi wa kimataifa

Chanzo cha picha, Getty Images

Silaha pekee yenye uwezo wa kunasa ndege hizo ambazo Ukraine inayo kwa sasa ni mfumo wa ulinzi wa anga wa Marekani wa Patriot.

Hata hivyo, kupata silaha hii karibu na Kharkiv ni hatari kubwa. Ndege zisizo na rubani za kupeleleza zinaweza kuiona kwa haraka na Moscow inaweza kurusha makombora kama vile Iskander kuharibu mfumo huu ghali.

Jambo la kufurahisha ni kwamba, Uingereza na Ufaransa, ambazo zinaipatia Ukraine makombora ya safari ya anga ya Storm Shadow (au Scalp kama yanavyoitwa Ufaransa), hazijazuia matumizi yao kwa njia ya wazi.

Na safu yao inaweza kwenda hadi 250km. Kwa hakika, Rais wa Ufaransa Emanuel Macron aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita: "Tunapaswa kuruhusu [Ukraine] kugeuza maeneo ya kijeshi ambayo makombora yanarushwa na kimsingi, maeneo ya kijeshi ambayo Ukraine inashambuliwa."

Na matamshi kama hayo yanaonekana kama ruhusa ya kutumia Storm Shadows/Scalps, afisa wa jeshi la anga ambaye anapendelea kutotajwa jina, aliiambia BBC. Kwa hivyo, anasema, Ukraine sasa inaweza kushambulia viwanja vya ndege katika mikoa ya Kursk na Belgorod inayopakana na Ukraine.

Hatahivyo, shughuli kama hizo zitakuwa na kikomo kulingana na kile wanaweza kufikia. Ndege za Kiukreni za Su-24 ambazo zina makombora haya ya kusafiri zitalazimika kufika karibu na mpaka wa Urusi ili kuzirusha, jambo ambalo linawafanya kuwa hatarini kwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi.

Jeti za F-16 zinazotarajiwa kufikia mwisho wa mwaka huu zina vifaa bora zaidi kwa kazi kama hizo. Lakini Rais Zelensky anakiri kwamba bado haijabainika ikiwa washirika wa Ukraine wataruhusu jeti hizi kutumika kushambulia nchini Urusi.

"Nadhani kutumia silaha yoyote, aina ya Magharibi, katika eneo la Urusi ni suala la wakati," alisema katika mkutano wa kilele wa Nordic huko Stockholm siku ya Ijumaa.

Baadhi ya ndege zao zisizo na rubani zimeshambulia maghala ya mafuta na vituo vya kijeshi vilivyo umbali wa mamia ya kilomita kutoka mpakani.

Shambulizi la hivi punde lilikuwa kwenye kituo cha masafa marefu cha rada katika mji wa Orsk, ulio umbali wa kilomita 1800 kutoka mpaka wa Ukraine.