Jinsi magenge yalivyoibuka na kuitawala Haiti

A man drives past a burning barricade during a protest against Prime Minister Ariel Henry's government and insecurity, in Port-au-Prince, Haiti on 1 March 2024

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Maandamano dhidi ya Waziri Mkuu, Ariel Henry yamekuwa yakiongezeka wiki za hivi karibuni
  • Author, By Vanessa Buschschlüter
  • Nafasi, BBC News Online Latin America and Caribbean editor

Maelfu ya wafungwa wamekuwa huru baada ya magenge kuvamia jela na kuwaachia huru, katika nchi yenye serikali isiyo na afisa hata mmoja aliyechaguliwa na raia na kiongozi wa genge ambaye anamtishia waziri mkuu waziwazi.

Matukio yanayoendelea nchini Haiti yanawashtua hata wale wanaofuatilia kuongezeka kwa makundi yenye silaha nchini humo katika miaka ya hivi karibuni.

Hapa tunaangalia kwa undani jinsi magenge yalivyoibuka na kutawala maeneo makubwa ya mji mkuu na maeneo ya vijijini ya nchi hiyo ya Caribbean.

Makundi yenye silaha kwa muda mrefu yamekuwa yakihusika na umwagaji damu katika historia ya Haiti.

Wakati wa miaka 29 ya udikteta wa François Duvalier, anayejulikana kama Papa Doc, na mwanawe Jean Claude "Baby Doc" Duvalier, kikosi cha kijeshi kilichoitwa Tonton Macouse kilitumia vurugu kali kukomesha upinzani wowote kwa utawala wa Duvalier.

Duvalier mdogo alilazimishwa kwenda uhamishoni mwaka 1986, lakini magenge yamekuwa yakipata nguvu kila uchao na wakati mwingine yakilindwa na kuhamasishwa na wanasiasa wanaoshirikiana nao.

Jovenel Moise, Haiti's then president, speaks during an interview in Port-Au-Prince, Haiti, on Monday 29 January 2018

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Jovenel Moïse alipigwa risasi Julai 2021

Mauaji ya Rais Moïse

Mlipuko wa sasa wa ghasia za magenge umechochewa na mauaji ya Rais Jovenel Moïse tarehe 7 Julai 2021.

Rais huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na kundi la mamluki wa Colombia nyumbani kwake nje ya Port-or-Prince.

Wakati raia hao wa Colombia na washukiwa wengine kadhaa wakikamatwa, uchunguzi wa mauaji yake bado haujabaini ni nani aliamuru kuuawa kwa rais huyo.

Vurugu za magenge tayari zilikuwa zimekithiri chini ya Rais Moïse, lakini ombwe la mamlaka lililotokana na mauaji yake liliruhusu magenge kuteka maeneo zaidi na kuwa na ushawishi zaidi.

Na sio tu nafasi ya rais ambayo iko wazi: Kufuatia kucheleweshwa mara kwa mara kwa uchaguzi wa wabunge, mihula ya viongozi wote waliochaguliwa yameisha, na kuacha taasisi za nchi zikiwa hazina usukani.

Tangu mauaji ya Jovenel Moïse, nchi hiyo imetawaliwa na Ariel Henry.

Henry alikuwa ameteuliwa na Rais Moïse kama waziri mkuu wake muda mfupi kabla ya kuuawa, lakini hajachaguliwa na raia na kwa hiyo baadhi wanatilia shaka uhalali wake.

Upinzani dhidi ya uongozi wa Ariel Henry umekuwa ukiongezeka huku chaguzi alizoahidi kufanya zikishindwa kutekelezwa.

Isitoshe, ukosefu wa usalama umeongezeka, na kuwalazimu maelfu ya raia wa Haiti kukimbia makazi yao.

Haitian prime minister Ariel Henry addresses world leaders during the United Nations (UN) General Assembly on 22 September 22 2023 in New York City

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ariel Henry amekuwa waziri mkuu wa Haiti tangu 2021 - wakati nafasi ya rais ikiwa tupu

Magenge ya Haiti

Mmoja wa wapinzani wakuu wa Henry ni Jimmy Chérizier, afisa wa zamani wa polisi ambaye amekuwa kiongozi wa genge baada ya kutimuliwa na jeshi la polisi.

Anajulikana kwa lakabu ya Barbecue, askari huyo wa zamani anaongoza genge la G9, muungano wa magenge tisa yaliyoanzishwa mwaka 2020 ambayo yanaripotiwa kuwa na uhusiano na Chama cha marehemu Rais Moïse cha Tèt Kale.

Barbeque amempinga Waziri Mkuu Henry tangu mwanzo.

Kiongozi wa genge hilo alitumia mauaji ya Moïse, ambapo anawalaumu mabwanyenye kwa mauaji hayo na kuwahimiza wafuasi wake kushiriki katika kile alichokiita "vurugu halali."

Mashambulizi ya kikatili na uporaji yameenea, haswa katika mji mkuu, Port-or-Prince, ambapo Barbeque ana ngome zake.

Mwezi Oktoba 2021, Ariel Henry alizuiwa kuweka shada la maua kwenye mnara wa Moise, wakati wanachama waliokuwa wamejihami na silaha wa genge la Barbeque walipojitokeza ghafla na kufyatua risasi hewani.

Akiwa amevalia suti nyeupe na pembeni yake akiwa na watu wake, Barbeque aliweka shada la maua kwenye mnara huo – katika tukio la kuonyesha nguvu zake.

Genge lake la G9 pia limekuwa likipigana vita vya umwagaji damu na G-Pèp, genge pinzani ambalo linahusishwa na vyama vilivyompinga Rais Moïse.

Former police officer Jimmy "Barbecue" Cherizier, leader of the 'G9' coalition, speaks during a press tour of the La Saline shanty area of Port-au-Prince, Haiti 3 November 3 2021.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jimmy "Barbecue" Chérizier ni kiongozi wa genge anayejionyesha kama mwanamapinduzi

Shule na hospitali zimelazimika kufungwa na zaidi ya watu 100,000 walikimbia makazi yao mwaka 2023, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu iliiambia BBC wafanyakazi wake walilazimika kuzungumza na mamia ya magenge ili kuweza kutoa misaada ya kibinadamu.

Katika kunyoosha misuli yake, genge la G9 pia lilizuia usafirishaji wa mafuta mwaka 2022, na kusababisha uhaba wa mafuta na pia kutatiza usafirishaji wa dawa na maji ya kunywa.

Jeshi la polisi la taifa la Haiti - ambalo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023 lina maafisa 9,000 pekee katika nchi hiyo yenye wakazi milioni 11 - limejitahidi kukabiliana na magenge hayo, ambayo yamejihami kwa silaha zinazoingizwa kinyemela kutoka Marekani.

Asilimia 80 ya mji mkuu uko chini ya udhibiti wa magenge na watu wanaoishi katika maeneo haya wanakabiliwa na ukatili mbaya, kulingana na mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Ulrika Richardson.

Bi Richardson anasema kumekuwa na ongezeko la 50% la unyanyasaji wa kingono kati ya 2022 na 2023, huku wanawake na wasichana wakilengwa na magenge hayo.

Uingiliaji kati kutoka Nje

Jimmy Cherizer

Chanzo cha picha, PIERRE MICHEL JEAN

Maelezo ya picha, Jimmy "Barbecue" Chérizier alipendekeza mpango wake mwenyewe wa amani

Henry amerudia wito wa kuungwa mkono kimataifa ili kukabiliana na ghasia hizo, lakini hadi sasa ni Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad pekee ambazo zimeuambia rasmi Umoja wa Mataifa kwamba wanapanga kutuma maafisa wa usalama.

Lakini hakuna afisa aliyefika hadi sasa.

Wakati wa ongezeko la ghasia za sasa, Henry alikwenda Kenya kushawishi maafisa ili kutimiza ahadi yao ya kupeleka maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti.

Wakati raia wa Haiti wanatamani usalama, kutumwa kwa maafisa wa kigeni wa usalama kunatazamwa kwa wasiwasi na baadhi ya watu.

Haiti, ambayo ilipata uhuru kutoka kwa Ufaransa baada ya mafanikio ya uasi wa watumwa 1791, ilitawaliwa na Marekani kutoka 1915 hadi 1934. Uingiliaji kati wa kijeshi wa Marekani kati ya 1994 na 2004 pia umewafanya wengi kuwa na wasiwasi kuhusu uingiliaji kati kutoka nje.

Baadhi ya wakosoaji wa Henry wanadhani anataka kuwatumia polisi wa Kenya kuimarisha mamlaka yake, huku maandamano ya kumtaka ajiuzulu yanazidi kuongezeka.

Barbeque ni mmoja wa wale ambao wamemshutumu Ariel Henry kwa kujaribu kuimarisha mamlaka yake kwa kuwaalika maafisa wa usalama wa kigeni.

Mwaka 2022, kiongozi huyo wa genge aliweka mpango wake mwenyewe wa "amani," akipendekeza wanachama wa genge lake wapewe msamaha na baraza la wazee liundwe na wawakilishi kutoka mikoa 10 ya Haiti.

Pia alipendekeza genge lake lipewe nyadhifa katika baraza la mawaziri.

Tangu wakati huo, amekuwa akiongeza shinikizo, akijaribu kujidhihirisha kama "mwanamapinduzi" anayelenga kupindua anachosema ni kiongozi "haramu."

Tarehe 1 Machi, Chérizier alisema ataendelea kupigana na Ariel Henry. "Vita vitadumu kadri inavyohitajika," aliongeza.

Haijulikani kwa sasa Henry yuko wapi, wakati huu maelfu ya wafungwa wakitoroka gereza na kiongozi mwenye nguvu wa G9 akitoa wito waziwazi kumtaka aachie ngazi.

Uwezekano wa waziri mkuu kurudisha tena utawala wa sheria umezidi kuwa mgumu.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi