Kwa nini ubongo wa Lenin ulikatwa vipande zaidi ya 30,000?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ubongo wa Lenin ulitolewa na madaktari waliomfanyia uchunguzi baada ya kifo chake.

Na Juan Francisco Alonso

BBC Mundo

Baada ya mwanzilishi wa Muungano wa Kisovieti, Vladimir Ilyich Ulyanov, anayejulikana zaidi kama Lenin, kufa mnamo Januari 1924, baadhi ya madaktari waliomtibu walipendekeza kuondoa ubongo wake ili 'kuufanyia utafiti.

Miaka mia moja iliyopita, lengo la wanasayansi hawa na washirika wao wa kisiasa lilikuwa ni kugundua uwezo mkubwa wa kiakili ambao ulitambuliwa kama ‘’uwezo mkubwa wa kiakili’’ wa Lenin.

Wazo hilo liliidhinishwa na uongozi wa Usoviet, ambao uliunda taasisi ya kufanya utafiti huu.

Karne moja baadaye, ubongo wa Lenin uko wapi na ni matokeo gani ya uchambuzi? Ili kujibu maswali haya na mengine, BBC News Mundo, idhaa ya BBC ya Kihispania, ilizungumza na wanahistoria na madaktari wa upasuaji wa neva ambao wamechunguza kisa hicho.

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Daktari wa Ujerumani Oskar Vogt, mmoja wa wataalamu wakubwa katika utafiti wa ubongo mwanzoni mwa karne ya 20, aliitwa na Muungano wa Usovieti kuchambua ubongo wa Lenin.

Mgeni asiye na raha

Hadithi ya ubongo wa Lenin lilianza na pendekezo lililotolewa kwa Politburo (kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Muungano wa Kisovieti uliokufa) na Waziri wa Afya Nikolai Semashko na msaidizi wa kibinafsi wa Stalin Ivan Tovstukha.

Lengo lilikuwa ni "kusafirisha" ubongo huo Berlin (Ujerumani) kwaajili ya kujifunza zaidi kuhusu uwezo wake,” mwanahistoria Mmarekani Paul Roderick Gregory alisema.

Mtaalamu huyo, mwandishi wa kitabu kuhusu ubongo wa Lenin- Lenin's Brain na vitabu vingine kuhusiana na siri za usovieti - Secret Soviet, anaeleza kwamba wakati wa kifo cha kiongozi huyo, Urusi haikuwa na wataalamu wa neva.

Kwa hiyo mamlaka ya Usoviti ilimwalika daktari wa Ujerumani Oskar Vogt (1870-1959) kuchambua kiungo hicho, baada ya kuondolewa wakati wa uchunguzi wa maiti.

Daktari mashuhuri wa ubongo , Vogt alianzisha na kuelekeza Taasisi ya Utafiti wa Ubongo ya Kaiser Wilhelm (leo Max Planck Society, shirika la kifahari linaunganisha pamoja vituo kadhaa vya kisayansi vya Ujerumani).

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ubongo wa Lenin ulikatwa katika vipande zaidi ya 30,000 ambavyo viliwekwa kwenye sahani za kioo na vingine vilioshwa kwa rangi kwa ajili ya utafiti. Katika miaka ya 1990, sampuli zilionyeshwa kwa waandishi wa habari

"Ujerumani ilikuwa na kiwango bora zaidi kisayansi wakati huo na idadi kubwa zaidi ya Tuzo za Nobel," José Ramón Alonso, profesa wa baiolojia ya ubongo katika Chuo Kikuu cha Salamanca (Hispania), anaelezea BBC News Mundo.

"Na ingawa Vogt alisita kukubali kazi hii, serikali ya Ujerumani ilimsukuma kufanya hivyo. Wakati huo, Ujerumani ilitaka kudumisha uhusiano mzuri na Muungano wa Usoviet i- USSR, ili kushinda, kupitia nchi hii, vikwazo vilivyoizonga. kutengeneza silaha baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia", anaongeza mtaalamu huyo, ambaye alichunguza ubongo huo kulingana na kitabu chake cha Historia del Cerebro ("Historia ya Ubongo").

Mpango wa kuchukua ubongo wa Lenin hadi Berlin, hata hivyo, haukutimia.

"Stalin hakupenda wazo la mgeni kushiriki katika mchakato huu, kwa sababu hangeweza kuudhibiti," anasema Gregory, ambaye ni mshiriki katika Taasisi ya Hoover katika Chuo Kikuu cha Stanford nchini Marekani.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Stalin hakupenda wazo la kumwachia mtu wa nje kuamua kama Lenin alikuwa fikra au la, asema mtafiti mmoja.

‘Kama jibini la Uswizi’

Licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa wa Usovieti, hatimaye Vogt alialikwa kushiriki katika utafiti huo na akapewa mojawapo ya sehemu 30,953 za ubongo wa marehemu zilizokuwa zimagawanywa, ambayo aliweza kuirejesha kwenye maabara yake Ujerumani.

Kwa kufanya hivyo Moscow ilimwomba mtaalamu wa Ujerumani kuwafundisha madaktari wa Kirusi wa ubongo na kusimamia kuundwa kwa Taasisi ya Ubongo ya Urusi (sasa kikiwa ni Chuo cha Urusi cha Sayansi ya Matibabu).

Lakini miaka kadhaa baadaye, uhasama kati yqa Vogt na serikali ya Nazi sio tu vilimgharimu nyadhifa zake nchini Ujerumani, lakini pia kulimpa Stalin kisingizio cha kumfukuza, mwanahistoria wa Amerika anaongeza.

Mashaka ya Muungano wa Usovieti juu ya uingiliaji wa kigeni basi yalionekana yanayofaa. Katika miaka ya 1930, Third Reich alidai kuwa Lenin alikuwa mgonjwa na kwamba ubongo wake ulionekana kama "jibini la gruyere," Bwana Alonso anakumbuka.

Ndiyo maana, karibu mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moscow ilianzisha operesheni ya siri ya kuokoa sampuli iliyokuwa mikononi mwa Vogt, wanaeleza watafiti wa Ubelgiji L. van Bogaert na A. Dewulf.

“Wasovieti waliogopa kwamba sampuli ya Vogt ingeangukia mikononi mwa Wamarekani na kwamba wangeweza kuitumia kumchafua Lenin, wakisema kwamba alikuwa na kaswende au kwamba hakuwa mtaalamu,” anaeleza mwalimu huyo wa Kihispania.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanazi walimwonyesha Lenin kama mgonjwa na mhalifu na kudai ubongo wake ulionekana kama "jibini la Uswizi" kwa sababu ulikuwa umejaa mashimo.

Kufeli kwa lengo la kufurahisha

Mwishoni mwa miaka ya 1920, Vogt aliwasilisha matokeo ya awali ya uchunguzi wake katika mfululizo wa mikutano iliyofanyika Ulaya. Hapo anasema kwamba "ubongo wa Lenin ulikuwa mkubwa sana ."

Kwa daktari wa neva wa Ujerumani, hii inaelezea "utendaji wa haraka kazi " wa ubongo wa kiongozi na uwezo wake wa "kuunganisha mawazo kwa haraka sana, pamoja na hali yake ya ukweli", sababu iliyomfanya kumuelezea Lenin kama "mwanariadha wa uratibu wa fikra".

Ingawa kwa juu juu mtaalam huyo alikuwa ameipa Moscow kile ilichokuwa ikitafuta, viongozi wengine wa Soviet hawakuridhika…Sababu? Wataalamu wengine wakati huo walibishana kuwa ubongo mwingi mkubwa pia uliashiria ulemavu wa akili, kiongozi wa kikomunisti alionya katika ripoti.

"Maamuzi ya Vogt yamekosolewa sana kwa sababu inaaminika kwamba aliwaambia Warusi kile walichotaka kusikia: kwamba ubongo wa Lenin ulikuwa wa kipekee ," anasema Alonso.

"Mamlaka za Muungano wa Usovieti zilishikilia kwamba Lenin ndiye aliyekuwa na fikra kuu zaidi na walitumaini kwamba ubongo wake ulikuwa na sifa za pekee na kwamba kulikuwa na jambo fulani la pekee ambalo lingewaruhusu kusema kwamba haukuwa kama ubongo wa mtu mwingine yeyote ule.

Vogt aliamini kuwa kuna viungo vya moja kwa moja kati ya muundo (ukubwa na sura) ya ubongo na akili ya watu.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Viongozi wa Kisovieti wanashikilia kuwa Lenin alikuwa gwiji na kujaribu kuthibitisha hilo kisayansi kwa kusoma ubongo wake.

Je, tunaweza kumchukulia kuwa mtu bora kiakili ambaye alitetea matumizi yya vitisho kuwadhibiti watu wengi au ambaye aliishi kwa kumtegemea mama yake hadi kifo chake?

Waandishi wa wasifu wa Muungano wa Usovieti walipuuza hili na kusema kwamba kumbukumbu kubwa ya Lenin ilimruhusu kusoma lugha saba na kuandika nakala za magazeti kwa saa moja tu.

Utafutaji wa mzizi wa "uwezo wa juu wa kiakili " wa kiongozi wa Bolshevik ulidumu zaidi ya muongo mmoja, kwani ilikuwa ni lazima kuanza kukusanya ubongo mwingine wa watu mbali mbali wengine ili wataalamu waweze kuwafananisha na wa marehemu huyo mwanamapinduzi, wataalam wa utafiti huo wanasema.

Ndio maana leo, sio ubongo wa Lenin tu unaowekwa unaowekwa kwenye maabara za Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Moscow, lakini pia ule wa mwanafizikia Ivan Pavlov, mhandisi wa anga Konstantin Tsiolkovsky na mwandishi Maxim Gorky.

Lakini , vipande vya ubongo vya mwanzilishi wa USSR vililinganishwa sio tu na vile vya wenzao mahiri, bali pia na ubongo wa raia wengine kumi wa kawaida.

Matokeo hayakuwekwa wazi na yaliwasilishwa kwa mamlaka ya juu tu.

"Katika Taasisi ya Hoover kuna nakala ya ripoti ambayo Politburo ilipokea, yenye kurasa 63. Ripoti hiyo iko katika hali mbaya na ina lugha nyingi za kisayansi na upuuzi, lakini inahitimisha wazi kuwa Lenin alikuwa gwiji katika maisha yake yote, licha ya kwamba alipata kiharusi mara nne maishani mwake," anasema Gregory.

"Kusoma hati hii ilikuwa ni jambo la kuchekesha, kwa sababu mtu alikuwa na hisia kwamba (waandishi wake) walikuwa wakibuni vitu ili kufikia hitimisho walilotaka," anaongeza.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tangu 1922, Lenin alipata kiharusi angala mara nne maishani mwake ambavyo vilimfanya asiweze kuzungumza, kuandika na kutembea, lakini viongozi wa Usovieti wakati huo walisisitiza kuwa akili yake ilifanya kazi kama mashine.

Ingawa ubongo wake ulikuwa na uzito wa kilo 1.3 tu, ukilinganishwa na zaidi ya kilo 2 kwa waandishi fulani mashuhuri wa wakati huo, watafiti wa Usovieti walihakikisha kwamba ubongo wa Lenin ulionyesha "utata wa misaada na mambo maalum katika usanidi wa mifereji na mizunguko, haswa katika sehemu yake ya mbele" jambo linalodhihirisha kuwa anastahili kuitwa mtu mwenye "uwezo wa juu wa kiakili".

Alonso anakataa hitimisho la Vogt na warithi wake. “Hakuna anayeamini kuwa ukubwa au umbo la ubongo lina uhusiano wowote na akili (...) Kuna watu wenye akili kubwa waliacha kazi kubwa za kisanii au kisayansi, lakini pia wapo ubongo mdogo waolifanya hivyo hatujapata mtu ambaye anayetuwezesha kusema fikra iko wapi," anaeleza.

Na Alonso anasisitiza kuwa "leo bado tunajadili kile tunachokiita akili".

"Mchoraji Vincent Van Gogh anachukuliwa kuwa mtaalamu wa kisanii, lakini alikuwa na matatizo mengi. Vivyo hivyo kwa (mwanafizikia Isaac) Newton, ambaye anachukuliwa kuwa mwanasayansi bora zaidi katika historia, lakini hakuwa na marafiki na aliishi katika umaskini, hata, ingawa alikuwa na pesa,” anamalizia mtaalamu huyo.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chuo cha Urusi cha Sayansi ya Matibabu kina mfano wa nta ya ubongo wa Lenin, ambayo inatuwezesha sisi kuuona kama ilivyokuwa wakati wa kifo chake.

Silaha ya kisiasa

Baada ya kuvunjika kwa Muungano wa Usovieti (USSR) mnamo 1991, wanasayansi wengine ambao walikuwa wamehifadhi au kuchunguza ubongo wa Lenin walianza kupendekeza matoleo mengine isipokuwa toleo rasmi.

Utafiti wa ubongo wa Lenin pia ulikuwa moja ya silaha ambazo Stalin alitaka kujitambulisha kama mrithi wa mwanzilishi wa USSR.

"Stalin alitaka si tu kuthibitisha kipaji cha Lenin, lakini pia kuwa mkalimani wake ili kuimarisha nafasi yake katika mapambano ya mamlaka ambayo yalianza baada ya kifo cha Lenin," anaongeza Gregory.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kutofariki kwa Lenin kulikuwa sehemu ya mkakati wa Stalin kuchukua udhibiti wa USSR mpya.

Lakini ubongo wa Lenin sio kitu pekee ambacho Stalin alitumia katika vita vyake vya madaraka. Alipuuza matakwa ya mtangulizi wake na familia yake na akaamua kuuhifadhi mwili wa Lenin na kuuonyesha hadharani kama ule wa mtakatifu katika kaburi lililojengwa chini ya kuta za Kremlin, ambapo bado upo hadi leo.

Lakini wataalam kama vile mwanahistoria wa Cuba Armando Chaguaceda wanaamini kwamba ni Lenin mwenyewe aliyeanzisha mchakato wa u mungu uliofuata.

"Lenin ndiye muundaji wa serikali ya kiimla ya Usovieti, moja ya nguzo ambazo ni propaganda," anaeleza.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah