Jimmy "Barbecue" Chérizier, kiongozi wa magenge ya uhalifu ya Haiti ni nani?

sd

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Jimmy Barbeque Chérizier amekuwa kiongozi mkuu wa genge linalojulikana kama G-9 and Family.

Huku machafuko yakiongezeka nchini Haiti na serikali kutangaza hali ya hatari, viongozi wa magenge yanayodhibiti sehemu ya nchi hiyo wanatoa wito wa kujiuzulu Waziri Mkuu Ariel Henry.

Mmoja wa viongozi hao ni Jimmy Chérizier, anayejulikana kama "Barbecue" na kiongozi wa moja ya magenge yenye nguvu zaidi la G-9 and Family.

Ghasia hizi zilizoanza 2020 zilifikia kiwango kibaya baada ya watu wenye silaha kuingia katika gereza kuu siku ya Jumamosi na kuwaachilia huru zaidi ya wafungwa 3,700. Katika uvamizi huo, watu 12 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Vurugu zimesabaisha maelfu ya vifo na hali mbaya ya ukosefu wa utulivu wa kijamii. Mojawapo ya nyakati mbaya zaidi ilikuwa ni mauaji ya Rais Jovenel Moïse Julai 7, 2021.

Magenge yanadhibiti karibu 80% ya eneo la Port-or-Prince, yanamtaka Waziri Mkuu Henry ajiuzulu, ambaye alichukua nafasi Moïse aliyetawala nchi bila kuitisha uchaguzi ulioahidiwa.

Pia Unaweza Kusoma

Chérizier ni nani?

SD

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Chérizier alikuwa afisa wa polisi kabla ya kuwa mhalifu.

"Tunaomba Polisi wa Kitaifa wa Haiti na jeshi kuchukua jukumu la kumkamata Ariel Henry. Kwa mara nyingine tunasema, raia sio maadui zetu, makundi yenye silaha sio maadui zetu," alisema Chérizier katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.

Kiongozi huyo wa uhalifu siku za nyuma aliomba msamaha kutoka kwa serikali ya Henry na aliomba wanachama wote wa kundi lake waachiliwe huru.

Chérizier, ni afisa wa polisi wa zamani ambaye sasa amegeuka kuwa mkuu wa uhalifu, amejidhihirisha kuwa mmoja wa watu wakuu katika wimbi la vurugu za magenge.

Kwa mujibu wa Marekani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, anahusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Haiti. Kwa sababu hiyo, Washington na Umoja wa Mataifa zimemuwekea vikwazo.

Tangu kifo cha Moïse, Chérizier amechukua usukani kuhimiza mapinduzi dhidi ya wanasiasa mafisadi. Hutumia mitandao ya kijamii pia kuvutia wafuasi wapya kujiunga na genge lake.

Kutoka Polisi hadi Mkuu wa Magenge

SD

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Hali nchini Haiti haijadhibitiwa baada ya uvamizi wa watu wenye silaha katika gereza kuu la Port-or-Prince mwishoni mwa wiki.

Swali la kwanza ni kuhusu sababu ya jina lake la utani. Alisema katika mahojiano ni kwa sababu mama yake aliuza kuku mitaani.

Lakini kulingana na baadhi ya mashahidi wa vurugu za Haiti, ni kwa sababu yeye huchoma nyumba na miili ya waathiriwa wake.

Alizaliwa katika mji mkuu wa Haiti takriban miaka 47 iliyopita, si vikwazo ambavyo Marekani imemwekea wala mamlaka yoyote katika nchi yake - havijaweza kudhibiti vitendo vyake.

Kazi ya uhalifu ya Chérizier ilianza alipokuwa afisa wa polisi na alihusika katika vifo vya raia tisa, katika operesheni dhidi ya magenge huko Grand Ravine, kitongoji cha Port-or-Prince, mwezi Novemba 2017.

Kuanzia wakati huo na kuendelea, uhusiano wake na magenge pia ulianza. Alianza kwa kujiunga na genge la Delmas 6, ambapo alikua mmoja wa wasemaji wakuu.

Umoja wa Mataifa na Marekani zinasema alikuwa mmoja wa maafisa waliohusika katika mauaji ya La Saline, katika kitongoji cha Port-or-Prince.

Katika tukio hilo lililoratibiwa na polisi na vikundi vya uhalifu dhidi ya wakazi wa eneo hilo, makumi ya watu waliuawa - ili kukandamiza upinzani wa kisiasa, kama Marekani inavyosema.

Uhalifu wa Cherizier

SD

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Inakadiriwa kuwa magenge yanadhibiti 80% ya mji mkuu wa Haiti.

Cherizier amekuwa akikana madai ya kuhusika na mauaji.

"Mimi sio jambazi, sitokuwa jambazi," aliiambia Al Jazeera katika mahojiano ya mwaka 2021.

"Napigana na mfumo. Mfumo huo una pesa nyingi na una udhibiti wa vyombo vya habari. Wanafanya nionekane kama jambazi," alisema.

Mwaka 2018 na 2019, Chérizier alidaiwa kuhusika katika mashambulizi mengine ya kikatili huko Port-or-Prince.

"Magenge ya wahalifu yana vifaa bora kuliko polisi na yana ulinzi wa mamlaka," Pierre Esperance, mkurugenzi wa Mtandao wa Kitaifa wa Kutetea Haki za Kibinadamu wa Haiti, aliiambia BBC katika mahojiano ya 2021, akielezea muktadha wa magenge kutochukuliwa hatua.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Kulinda Haki za Kibinadamu nchini Haiti, vitendo vya Chérizier na kundi lake lenye silaha havikulenga tu kuuwa watu, bali pia kuchoma moto makazi ya wale ambao walikuwa walengwa wa mashambulio hayo.

Kuelekea Juni 2020, akitumia fursa ya machafuko - Chérizier aliunganisha magenge tisa katika kundi ambalo hatimaye aliliita G-9 and Family. Tangazo hilo lilitolewa kupitia chaneli yake ya YouTube.

Kulingana na tovuti ya InSight Crime, kabla ya mauaji ya Moïse, 50% ya ufadhili wa G-9 ulikuwa ni pesa za serikali, 30% zikitoka katika utekaji nyara na 20% iliyobaki ilipatikana kwa ulaghai.

Lakini baada ya mauaji hayo Moise, ufadhili wa serikali ulipungua kwa 30%. Hilo lilimchochea kiongozi huyo kuelekeza vita vyake dhidi ya watu waliorithi utawala wa kisiasa wa nchi hiyo.

Oktoba 2021, Waziri Mkuu Henry, ambaye alichukua madarakani baada ya mauaji ya Moïse, alizuiwa kuweka shada la maua kwenye mnara kwa sababu wanachama waliokuwa na silaha wa genge la Chérizier walitokea ghafla na kupiga risasi hewani.

Akiwa amevalia suti nyeupe akiwa na watu wake, kiongozi wa genge hilo aliweka shada la maua kwenye mnara huo, katika tukio la ajabu la kuonyesha nguvu zake.

Chérizier pia anatuhumiwa kuongoza vitendo vya hujuma dhidi ya usambazaji wa mafuta nchini humo, watu wake walizuia shehena za petroli kama shinikizo dhidi ya serikali ya Henry.

Uhaba wa petroli ulizidisha hali mbaya ya kibinadamu nchini Haiti.

Genge lake la G-9 pia limekuwa likiendesha vita vya umwagaji damu na genge la G-Pèp. Genge linaloripotiwa kuwa na uhusiano na vyama vilivyompinga Rais Moïse.

Mapigano kati ya vikundi hivyo viwili ni ya mara kwa mara na hutokea katika vitongoji masikini katikati ya Port-or-Prince.

Mapigano hayo ni kwa lengo la kupanua himaya zao na kuvutia wafuasi zaidi kwenye makundi yao.

Maagizo na vitisho YouTube

DSX

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hali mbaya nchini Haiti imechangiwa na usambazaji wa fikra za magenge kupitia mitandao ya kijamii.

Kile ambacho kinatokea katika mitaa ya Port-or-Prince pia kimehamishiwa kwenye uwanja wa mitandao ya kijamii.

"Majambazi wasingekuwa na nguvu kama walizo nazo nchini Haiti bila mitandao ya kijamii. Tumewahi kuwa na wahalifu, lakini bila majukwaa hayo hawakuwa maarufu," Yvens Rumbold, wa taasisi ya utafiti ya Policité, aliiambia The Washington Post.

Mitandao imetumiwa na Chérizier kutekeleza mpango wake. Hakutumia tu akaunti yake ya YouTube kueleza kuundwa kundi la G-9, lakini pia kuomba polisi wamkamate waziri mkuu wa sasa wa Haiti.

Kwenye X (zamani wa Twitter) pia ametoa wito wa kuichukua nchi na kuondoa tabaka tawala la sasa.

Mitandao imetumika pia kueneza picha za miili baada ya mauaji kupitia WhatsApp au kuomba kuungwa mkono kupitia ujumbe kwenye Instagram au TikTok.

Chérizier alizungumza juu ya umuhimu wa mitandao ya kijamii katika mahojiano kwenye chaneli yake ya YouTube.

"Nawashukuru wanaounda teknolojia hizi. Teknolojia leo inatupa fursa ya kujisogeza na kujitangaza kwa umma, siuzi uongo," alisema alipoulizwa na mfuatiliaji.

"Mimi ndiye ninayesema. Asilimia 99 ya kile walichosema nimefanya mimi sijafanya. Teknolojia ilinipa fursa ya kujitetea," aliongeza.

Pia Unaweza Kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuharirirwa na Dinah Gahamanyi