Jinsi silaha za Korea Kaskazini zinavyoua raia wa Ukraine

.

Chanzo cha picha, Reuters

Tarehe 2 Januari, mkaguzi wa silaha wa Ukraine, Krystyna Kimachuk, alipata habari kwamba kombora la sura isiyo ya kawaida lilianguka kwenye jengo katika jiji la Kharkiv.

Alianza kuwapigia simu anaowasiliana nao katika jeshi la Ukraine, akitamani kuanza kulifanyia ukaguzi. Ndani ya wiki moja, uchafu huo ulitawanywa mbele yake katika eneo salama katika mji mkuu wa Kyiv.

Alianza kulipasua na kupiga picha kila kipande, ikiwa ni pamoja na skrubu na chip za kompyuta ndogo kuliko kucha zake. Angeweza kusema mara moja kwamba hili halikuwa kombora la Urusi, lakini changamoto yake ilikuwa kuthibitisha hilo.

Akiwa katikati ya vyuma na waya za kombora hilo Bi Kimachuk aliona herufi ndogo kutoka kwa alfabeti ya Kikorea. Kisha akakutana na maelezo zaidi. Nambari 112 ilikuwa imegongwa kwenye sehemu za ganda. Hii inalingana na mwaka wa 2023 katika kalenda ya Korea Kaskazini.

Aligundua kuwa alikuwa akiangalia sehemu ya kwanza ya ushahidi mgumu kwamba silaha za Korea Kaskazini zilitumiwa kushambulia nchi yake.

"Tulisikia kwamba walikuwa wamewasilisha silaha kwa Urusi, lakini niliweza kuiona, kuigusa, kuichunguza, kwa njia ambayo hakuna mtu aliyeweza kufanya hapo awali. Hii ilisisimua sana", aliniambia kupitia simu kutoka mjini Kyiv.

Tangu wakati huo, jeshi la Ukraine linasema makumi ya makombora ya Korea Kaskazini yamerushwa na Urusi katika ardhi yake.

Wamewauwa watu wasiopungua 24 na kujeruhi zaidi ya 70.

Kwa mazungumzo yote ya hivi karibuni ya Kim Jong Un akijiandaa kuanzisha vita vya nyuklia, tishio la haraka zaidi sasa ni uwezo wa Korea Kaskazini kuchochea vita vilivyopo na kupeana silaha na kusababisa ukosefu wa utulivu duniani.

Bi Kimachuk anafanya kazi katika shirika la Utafiti wa Silaha za Migogoro (CAR), ambalo hutafuta silaha zinazotumiwa vitani, ili kufahamu jinsi zilivyotengenezwa.

Lakini haikuwa hadi baada ya kumaliza kupiga picha mabaki ya kombora hilo na timu yake ikachambua mamia ya vipengele vyake, ndipo ufunuo mkubwa zaidi wa kudondosha taya ulijitokeza.

Ilikuwa na teknolojia ya hivi karibuni ya kigeni.

Sehemu nyingi za elektroniki zilikuwa zimetengenezwa Marekani na Ulaya katika miaka michache iliyopita. Kulikuwa na hata chip ya kompyuta ya Marekani iliyotengenezwa hivi majuzi Machi 2023.

Hii ilimaanisha kwamba Korea Kaskazini ilikuwa imenunua kwa njia isiyo halali vifaa muhimu vya silaha, na kuviingiza nchini humo, kukusanya kombora, na kulisafirisha hadi Urusi kwa siri, ambako lilikuwa limesafirishwa kwa mstari wa mbele na kutumika - yote katika suala la miezi kadhaa.

"Huu ulikuwa mshangao mkubwa, kwamba licha ya kuwa chini ya vikwazo vikali kwa karibu miongo miwili, Korea Kaskazini inaweza kupata chochote inachohitaji kutengeneza silaha zake, na kwa kasi ya ajabu," alisema Damien Spleeters, naibu mkurugenzi wa shirika hilo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong un na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin

Huko London, Joseph Byrne, mtaalamu wa Korea Kaskazini katika taasisi ya utetezi ya Taasisi ya Royal United Services (RUSI), alipigwa na butwaa vile vile.

"Sikuwahi kufikiria ningeona makombora ya balistiki ya Korea Kaskazini yakitumiwa kuua watu katika ardhi ya Ulaya," alisema. Yeye na timu yake katika RUSI wamekuwa wakifuatilia shehena ya silaha za Korea Kaskazini hadi Urusi tangu Bw Kim alipokutana na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin nchini Urusi mnamo Septemba mwaka jana ili kufanya makubaliano yanayoshukiwa kuwa ya silaha.

Kwa kutumia picha za satelaiti, wameweza kuona meli nne za mizigo za Urusi zikisafiri kwenda na kurudi kati ya Korea Kaskazini na bandari ya kijeshi ya Urusi, zikiwa zimesheheni mamia ya makontena kwa wakati mmoja.

Kwa jumla RUSI inakadiria kuwa kontena 7,000 zimetumwa, zikiwa na zaidi ya makombora ya risasi milioni moja na roketi ambazo zinaweza kurushwa kutoka kwa malori .

Tathmini zao zimeungwa mkono kijasusi kutoka Marekani, Uingereza na Korea Kusini, ingawa Urusi na Korea Kaskazini zimekanusha biashara hiyo.

Makombora na roketi hizi ni baadhi ya vitu vinavyotafutwa sana duniani hivi sasa na vinairuhusu Urusi kuendelea kushambulia miji ya Ukraine wakati ambapo Marekani na Ulaya zimekuwa zikiyumba juu ya silaha za kuchangia," Bw Byrne alisema.

Kununua na kurusha risasi

Lakini ni kuwasili kwa makombora ya balestiki kwenye uwanja wa vita ndiko kumemtia wasiwasi Bw Byrne na wenzake zaidi, kwa sababu ya kile wanachofichua kuhusu mpango wa silaha wa Korea Kaskazini.

Tangu miaka ya 1980 Korea Kaskazini imeuza silaha zake nje ya nchi, kwa kiasi kikubwa kwa nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, zikiwemo Libya, Syria na Iran.

Yameonekana kuwa makombora ya zamani, ya Soviet yenye sifa mbaya.

.

Chanzo cha picha, reuters

Kuna ushahidi kwamba wapiganaji wa Hamas wana uwezekano wa kutumia baadhi ya mabomu ya zamani ya roketi ya Pyongyang katika mashambulizi yao ya Oktoba 7 iliyopita.

Lakini kombora lililorushwa tarehe 2 Januari, ambalo Bi Kimachuk alilitenganisha, lilikuwa kombora la kisasa zaidi la masafa mafupi la Pyongyang - Hwasong 11 - lenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 700 (maili 435).

Ingawa Waukraine wamepuuza usahihi wao, Dk Jeffrey Lewis, mtaalam wa silaha za Korea Kaskazini na kutoeneza silaha katika Taasisi ya Mafunzo ya Kimataifa ya Middlebury, anasema zinaonekana kuwa mbaya zaidi kuliko makombora ya Urusi.

Faida ya makombora haya ni kwamba ni ya bei nafuu sana, alieleza Dk Lewis. Hii ina maana unaweza kununua zaidi na kufyatua mengi zaidi, kwa matumaini ya ulinzi mkubwa wa angani, kitu ambacho Warusi wanaonekana kufanya.

Hii inazua swali la ni makombora mangapi kati ya haya ambayo Wakorea Kaskazini wanaweza kutengeneza.

Hivi majuzi serikali ya Korea Kusini iliona kwamba Korea Kaskazini imetuma makontena 6,700 ya silaha nchini Urusi, inasema kwamba viwanda vya kutengeneza silaha vya Pyongyang vilikuwa vinafanya kazi kwa kiwango kamili, na Dk Lewis, ambaye amekuwa akichunguza viwanda hivyo kupitia satelaiti, vinaweza kutenegenza mamia ya makombora kwa mwaka.

Wakiwa bado wanahangaika kutokana na ugunduzi wao, Bw Spleeters na timu yake sasa wanajaribu kutafakari jinsi hii inavyowezekana, ikizingatiwa kwamba makampuni yamepigwa marufuku kuuza vipuri kwa Korea Kaskazini.