Kwa nini bahari za dunia zinabadilika rangi?

fdcv

Chanzo cha picha, ESA

Maelezo ya picha, Utafiti unaonyesha viwango vikubwa vya klorofili katika maji yenye joto kali huko Ulaya
  • Author, Frankie Adkins
  • Nafasi, BBC

Utafiti wa hivi karibuni unaeleza kuwa bahari za ulimwengu wetu zinabadilika kuwa kijani kibichi. Na hilo huenda linachangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Phytoplankton ni viumbe vya baharini, vinavyofanana na koya la kijani vinavyotengeneza tabaka la chakula cha baharini.

Ingawa baadhi ya maji yanazidi kuwa ya kijani kibichi, hasa karibu na ikweta, mengine yanakua bluu zaidi huku halijoto duniani likiongezeka.

Ingawa mabadiliko haya ya rangi hayaonekani kwa macho, tafiti za setilaiti zinaweza kuonyesha mabadiliko hayo.

Ripoti ya hivi karibuni ya Hali ya Hewa huko Ulaya, iliyochapishwa Aprili 2024 na European Union's Copernicus Climate Service, ilifichua mabadiliko katika bahari; rangi ya kijani iko kwa 200-500% kuliko kawaida katika bahari ya Norway na Bahari ya Altantic kaskazini mwa Uingereza mwezi Aprili 2023.

Lakini rangi hiyo ilikuwa chini kwa 60-80% katika bahari ya magharibi ya Peninsula ya Iberia. Bahari ya Mediterania kiwango cha rangi ya kijani ni 50-100% juu kuliko ilivyokuwa awali. Vipimo hivyo vilichukuliwa kuanzia 1998-2020.

Uchambuzi wa BBC News wa halijoto ya bahari iliokusanywa na taasisi ya Copernicus - umefichua kuwa bahari duniani zinakabiliwa na ongezeko la joto. Ilionyesha kuwa joto baharini lilizidi kila siku katika mwaka uliopita.

Pia unaweza kusoma
fdc

Chanzo cha picha, esa

Maelezo ya picha, Maua ya planktoni nchini Ugiriki katika Bahari ya Barents kaskazini mwa Ulaya

Miongo miwili ya kutumia satelaiti za Nasa pamoja na wanasayansi kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT), waligundua kuwa zaidi ya nusu ya eneo la bahari duniani - 56% - limebadilika rangi. Eneo hili ni kubwa kuliko ardhi yote ya dunia.

"Tunaona mabadiliko katika mabonde yote makubwa ya bahari - kwenye Pasifiki, Atlantiki na [bahari] za Hindi. Haya ni mabadiliko makubwa ya kimataifa ambayo tunaona," anasema B B Cael, mwanasayansi kutoka National Oceanography Centre huko Southampton, Uingereza.

Hii inathibitisha nadharia katika ripoti ya awali ya Stephanie Dutkiewicz, mwanasayansi wa bahari kutoka taasisi ya MIT na Kituo cha Global Change Science..

Mwaka 2019, Dutkiewicz alitumia kompyuta kutabiri mabadiliko ya baadaye katika rangi ya bahari. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kubainisha ikiwa hilo lilitokana na mabadiliko ya hali ya hewa au mifumo ya kawaida ya bahari.

cv

Chanzo cha picha, getty images

Maelezo ya picha, Maji ya kijani kibichi husababishwa mimea ya klorofili

"Ni vigumu kusema ikiwa mabdiliko haya yanatokana na mabadiliko ya hali ya hewa au la," anasema Dutkiewicz.

Utafiti wa Cael, ambao uliongeza data ya setilaiti, ulipanua wigo zaidi. Dutkiewicz, ambaye pia alifanya kazi katika utafiti wa Cael, anasema ripoti ya hivi karibuni inathibitisha utabiri wake.

"Vipimo vya satelaiti vinaendana na kile kinachoonekana kwenye taarifa yake," anasema. "Kwa hivyo, mabadiliko tunayoyaona katika ulimwengu yana uwezekano ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na binadamu."

Athari za mabadiliko haya kwenye bahari zinaweza kuwa kubwa. Watafiti wengine wametabiri mabadiliko ya rangi yatahamia kaskazini kwa kasi ya karibu 35km (maili 21) kila muongo wakati joto linapoendelea kupanda.

Hii itasababisha mabadiliko kwa viumbe vidogo vya baharini wanaokula phytoplankton, huku utajiri wa spishi ukitarajiwa kupungua na kuongezeka kwa joto la bahari, na kusababisha athari zaidi katika chakula na samaki wanaotegemea viumbe hawa.

Rangi ya bahari haitobadilika kwa usiku moja ama ghafla. Lakini mabadiliko haya yanafichua mwelekeo ambao unaonyesha mabadiliko kadiri halijoto inavyoongezeka.

"Sio rangi yenyewe ambayo inatia wasiwasi," anasema Cael. "Kilicho muhimu ni kuwa mabadiliko ya rangi yanaakisi mabadiliko katika mfumo wa ikolojia ya bahari."