Watanzania wanaosaka mafuvu ya babu zao Ujerumani

Ujerumani imesema iko tayari kuomba msamaha

Ujerumani imesema iko tayari kuomba msamaha kwa kunyongwa kwa wanaume 19 katika eneo ambalo sasa ni kaskazini mwa Tanzania miaka 123 iliyopita.

Maiti nyingi zilikatwa vichwa na mafuvu yalitumwa Berlin.

Vizazi vyao wametumia miongo kadhaa kutafuta mabaki hayo na hivi majuzi, katika kile kinachoitwa ugunduzi wa miujiza, mafuvu mawili ya watu waliouawa yametambuliwa kati ya mkusanyiko wa maelfu ya vitu vya kale.

Ugunduzi wao unaunganisha pamoja hadithi ya ukatili wa kikoloni, kampeni kali na matumizi yasiyokuwa ya kawaida ya utafiti wa DNA.

_________

Ni nadra kupata mti wa mshita kwenye miteremko ya chini ya Mlima Kilimanjaro.

Matawi yake yanayopinda-pinda hufika juu ya barabara yenye mwinuko na kusimama nje kati ya mimea minene yenye rutuba.

Wakati fulani, ilifunika soko la wanakijiji wa Tsudunyi, sehemu ya kule ambako sasa kunajulikana kama Old Moshi, walikofurahia hali ya baridi kali iliyotokana na eneo la juu zaidi.

Lakini eneo hilo muhimu katika jamii likawa janga kubwa na licha ya amani kutokana na mazingira asilia, sasa athari zake zimerejea miongo kadhaa baadaye.

Ilikuwa hapa tarehe 2 Machi 1900 ambapo, kama wazao wanavyosema, mmoja-mmoja wale watu 19, wote wakuu au washauri, walinyongwa.

Walikuwa wamehukumiwa kwa haraka siku moja kabla, wakituhumiwa kupanga njama ya kushambulia majeshi ya Ujerumani.

Madai ya Ujerumani kwa sehemu hii ya bara yalirasimishwa katika Mkutano wa Berlin wa 1884-1885.

Mataifa ya Ulaya yaligawanya Afrika kabla watu wanaoishi huko kutoa maoni yoyote juu ya kile kilichotokea.

Mangi Meli, au chifu mashuhuri zaidi kati ya wale waliouawa, mwaka 1892 alifanikiwa kuwashinda wanajeshi wa Ujerumani.

Mafanikio hayo yalibadilishwa baadaye na kufikia mwisho wa Karne ya 19 Ulaya ilikuwa na nia ya kuleta ushawishi katika sehemu hii iliyojulikana kama Ujerumani ya Afrika Mashariki.

Walitaka kutoa mfano wa Mangi Meli na viongozi wengine wa eneo hilo ambao huenda walikuwa wakitafakari kuhusu uasi.

Picha hii ya 1910 inaaminika kuonyesha mti wa mshita ambapo wanaume hao walinyongwa mwaka wa 1900.

Chanzo cha picha, LEIBNIZ-INSTITUT FÜR LÄNDERKUNDE E.V.

Mateso hayakuishia hapo

Wakati viwiliwili vingi vinaaminika kuzikwa kwenye kaburi la pamoja mahali fulani karibu na mti, vichwa vyao viliondolewa, vikafungashwa na kutumwa kilomita 6,600 (maili 4,100) hadi mji mkuu wa Ujerumani.

Katika baadhi ya matukio mifupa ilisafirishwa. Ndani ya ngome ya Ujerumani mita 250 tu kutoka kwenye mti unaoning'inia kuna makaburi manne, yaliyowekwa vizuri karibu na msalaba, ya wanajeshi wa Ujerumani waliofariki wakipigana na vikosi vya mitaa - wanaume 19 walionyongwa hawakupewa heshima sawa.

Akizungumzia kilichotokea, Isaria Anael Meli, mjukuu wa Mangi Meli, hasikiki kuwa na hasira, lakini kuna huzuni katika sauti yake na hali ya kuchanganyikiwa juu ya jinsi hii iliruhusiwa kutokea.

Mzee huyo mashuhuri mwenye umri wa miaka 92 alielezwa kuhusu mauaji ya Mangi Meli na bibi yake ambaye anasema alilazimishwa kutazama mauaji hayo na anaeleza kuwa chifu huyo alimjia katika ndoto miongo kadhaa iliyopita akimwambia kuwa angerejea siku moja.

"Kila siku nilipoenda kulala, niliwaza bibi na babu yangu. Siku zote, alikuwa akinijia katika ndoto zangu," anasema.

Kofia yake ya jua iliyopeperuka na macho yanayopepesa anapotabasamu huficha utu wake wa ukakamavu.

Tangu takriban miaka ya 1960, Bw Meli amekuwa akiandikia mamlaka ya Ujerumani na Tanzania akiwataka watafute mabaki ya babu yake.

Anasema maafisa walijaribu kumkatisha tamaa kwa kumwambia kwamba rekodi zinazohusiana na mabaki ya binadamu ziliharibiwa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Lakini Bw Meli hakukatishwa tamaa.

"Siyo tu familia yangu ambayo ilikuwa ikitafuta fuvu hilo, lakini nchi nzima imekuwa ikilingojea.

"Wageni daima wanalia: 'Waambie watu wote wa Ujerumani warudishe fuvu la kichwa.'

"Waliiweka mahali fulani kwa sababu tu walidhani familia ya Mangi Meli ni watu wadogo - wakiamini kwamba wanaweza kufanya wanachotaka. Lakini kumbuka kuwa fuvu hili linahitajika na nchi nzima - sio mimi mwenyewe, peke yangu."

Kuna hisia ya hasara kubwa ambayo ni zaidi ya wazo kwamba hii ilikuwa dhuluma ya kihistoria.

Mangi Meli alikuwa chifu kutoka kabila la Wachaga. - moja ya kabila mashuhuri katika Tanzania ya sasa.

Kwa Wachagga, pamoja na watu wengine wa mkoa huo, wazo la kwamba kichwa kilitenganishwa na mwili na kisha kuchukuliwa kutoka kwa ardhi linasumbua mno.

 Mafanikio ya mapema ya Mangi Meli kuwapinga Wajerumani yalibadilishwa baadaye

Chanzo cha picha, DEUTSCHE FOTOTHEK/HANS MEYER

Katika utamaduni wa Wachaga wafu wanatakiwa kuzikwa nyumbani ili waendelee kuwaangalia walio hai.

Inaaminika kuwa kushindwa kufanya hivyo kunaweza kuwa na athari kwa vizazi.

“Tukiacha mafuvu huko Ujerumani mizimu itakuwa inatesa familia hizi,” anaeleza Gabriel Mzei Orio, ambaye alianzisha kampuni ya Old Moshi Cultural Tourism Enterprise kama sehemu ya kuangazia utamaduni wa Wachagga duniani kote.

Amesimama chini ya mti wa mshita huko Tsudunyi, karibu na ukumbusho wa waliouawa huko.

"Mizimu inasema: ‘Unajua tulipo na hutuleti kwenye nchi yetu na unajua tulichukuliwa kikatili.’”

Simulango Molelia, mjukuu wa mwingine wa waathiriwa wa kunyongwa – Mangi Molelia - anaamini familia yake inaandamwa na roho ya chifu.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 69 anakaa katika boma lake lenye kivuli lililozungukwa na ndizi, chakula kikuu katika eneo hilo na chanzo cha pombe ya kitamaduni ambayo familia hiyo hutengeneza.

Yuko mita chache tu kutoka kwenye makaburi ya mama na baba yake.

Simulango Molelia anaamini kuwa familia yake imeteseka kutokana na kilichotokea kwenye mabaki ya babu yake.

“Mambo mengi yaliathiriwa na mauaji hayo,” anasema kwa sauti nyororo na kuongeza kuwa ilikuwa kama mizizi ya mti ikishambuliwa.

"Mangi Molelia alipouawa, familia ilipoteza utajiri wake. Hadi sasa mambo si mazuri."

Lakini kwa wale ambao walichukua viungo vya mwili zaidi ya miaka 120 iliyopita hili kwao halikuwa jambo la kuwatia wasiwasi.

Mwanaanthropolojia wa Ujerumani Felix von Luschan, ambaye aliongoza idara ya Afrika na Oceania ya Jumba la Makumbusho ya Kifalme ya Ethnology ya Berlin, alikuwa na nia ya kupata mabaki kutoka kwa himaya ya Ujerumani na makoloni mengine ya Ulaya.

Mnamo Machi 1901 - mwaka mmoja baada ya kunyongwa - Von Luschan aliandika moja kwa moja kwa Lt First Moritz Merker, ambaye alikuwa mmoja wa wale waliokuwa wanasimamia majeshi ya Ujerumani huko Kilimanjaro.

Barua hiyo ilihusu baadhi ya sanaa za kitamaduni lakini katika aya ya mwisho aliandika: "Ninatumia fursa hii kuuliza kama itawezekana kwako kuwauliza wenyeji kwa njia ya amani kutukabidhi baadhi ya mifupa ya Wamasai na Wachaga."

Merker alijibu mwezi uliofuata akisema kuwa baadhi ya mabaki ya binadamu yalikuwa njiani na barua kutoka bandari ya Dar es Salaam inasema kwamba masanduku mawili ya mafuvu ya Wachagga na Wamasai yametumwa Berlin.

Haijabainika iwapo fuvu la kichwa la Mangi Meli lilikuwa miongoni mwa shehena hizo, lakini inaonekana huenda wakati huo ndipo baadhi ya mabaki ya watu waliouawa yaliposafirishwa, kwa mujibu wa mtafiti wa Ujerumani Konradin Kunze, ambaye amekuwa akijihusisha pakubwa katika kampeni ya kuwatafuta.

Mifupa hiyo kisha ikaingia kwenye hifadhi kubwa ya Von Luschan, ikijumuisha mkusanyiko ambao katika miongo minne hadi kifo chake mwaka wa 1924, ulikua na sampuli 6,300.

Baadhi ya mkusanyiko wake wa kibinafsi uliuzwa na mjane wake kwenye Jumba la Makumbusho la Marekani la Historia ya Asili huko New York. Hii ilijumuisha mifupa yote ya mmoja wa wale walionyongwa mnamo 1900.

“Walichokifanya Wajerumani hakikuwa kitu kizuri,” anasema Zablon Ndesamburo Kiwelu, ambaye babu yake, Mchili Sindato Kiutesha Kiwelu, aliwahi kuwa mshauri wa Mangi Meli na pia naye alinyongwa.

Kaka yake marehemu, pamoja na Isaria Meli, walianza utafutaji wa mabaki miongo kadhaa iliyopita na kisha akachukua hatua hiyo.

“Ni damu ya babu yangu,” anasema akieleza kwa nini utafutaji huo ulikuwa muhimu sana kwake.

"Tunasubiri mafuvu hayo yarudishwe katika nchi hii ili tufurahi, maana hatuna furaha."

Lakini ili kurudi tena, mafuvu yalihitaji kutambuliwa.

Hii ilikuwa kazi inayoonekana kutowezekana kutokana na ukubwa wa mkusanyiko wa Von Luschan na ukosefu wa nyaraka.

Dk Janine Mazanec ni mwanaanthropolojia wa kibaolojia katika Chuo Kikuu cha Göttingen na mara nyingi hufanya kazi na wanaakiolojia kwenye maeneo ya mazishi ya kihistoria ili kubaini uhusiano wa kifamilia kati ya wale waliozikwa.

Pia amefanya kazi na polisi kusaidia kutambua waathiriwa wa uhalifu.

Ili kugundua DNA, Dk Mazanec alilazimika kuchukua gego (molar) kutoka kwenye taya, kuondoa mzizi na kurudisha jino kwa uangalifu.

Aligundua fuvu linalolingana kabisa na fuvu la kichwa na uwezekano mkubwa wa kupata fuvu la pili.

Fuvu la babu ya Bwana Kiwelu lilikuwa limepatikana - na vile vile kwa Bw Molelia.

Lakini mabaki ya Mangi Meli hayakutambuliwa.

Mazungumzo kati ya mamlaka ya Ujerumani na Tanzania sasa yanafanyika ili kuwezesha uhamishaji wa mafuvu hayo, ambayo inaweza kuwa mchakato mgumu.

Lakini nadhari sasa pia unageukia serikali ya Ujerumani na ukoloni wake wa zamani.

"Ujerumani inakabiliwa na kuwajibika kutokana na masuala ya kihistoria... [na] imejitolea kuendeleza mchakato wa kukabiliana na dhuluma iliyofanywa wakati wa ukoloni wa Ujerumani," Katja Keul, waziri wa mambo ya nje katika wizara ya mambo ya nje aliandika katika jibu la barua pepe kwa orodha ya maswali.

Kunyongwa kwa wanaume hao 19 miaka 123 iliyopita ni moja ya "makosa mengi" ambayo alirejelea.

Alipoulizwa moja kwa moja kama Ujerumani iko tayari kuomba msamaha kwa mauaji hayo, alisema "ndio", lakini hakutoa maelezo yoyote kuhusu namna hili litatekelezwa.

Lakini Bw Meli - mjukuu wa Mangi Meli, ambaye fuvu lake halijapatikana - amechanganyikiwa baada ya miongo kadhaa ya kutafuta.

Ana hakika kwamba bado liko kwenye mkusanyiko wa makumbusho mahali fulani.

"Ninateseka kwa sababu nimetumia pesa kupambana na hili lakini sijafanikiwa? Kwa miaka mingi sana kile ambacho Wajerumani wote wanauliza ni: 'Ni nani aliyekusaidia?', na mimi husema, 'hakuna mtu isipokuwa mimi mwenyewe."

Lakini hajakata tamaa.

"Nataka kumuona babu yangu kabla sijafariki."