Kwa nini bahari ya Pasifiki iko juu kuliko ya Atlantiki?

K

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

  • Author, Christina J. Arcas
  • Nafasi, BBC

Kuna tofauti ya mwinuko wa karibu sentimita 20 kati ya Bahari ya Pasifiki na Bahari ya Atlantiki. Ni kama ukubwa wa penseli.

Inaweza kuonekana kama tofauti ndogo, lakini ina athari kwa mzunguko wa bahari na hali ya hewa ya kimataifa. Pia ina athari kwa miradi mikubwa ya uhandisi kama vile Mfereji wa Panama.

Tofauti hiyo huzingatiwa katika uanzishwa wa njia za meli, biashara ya mafuta ya baharini, shughuli za uvuvi, utafutaji na uokoaji, njia za kuzuia umwagikaji wa mafuta na shughuli za baharini.

Je, unajua kwamba bahari za Chile, Peru, Ecuador au Colombia ziko juu kuliko Argentina, Brazili au Uruguay? Maana yake, Bahari ya Pasifiki iko juu kuliko Bahari ya Atlantiki.

Bahari hizi mbili zinakutana na hutengeneza mtiririko wa maji ya chumvi yanayofunika zaidi ya 71% ya uso wa Dunia.

Pia unaweza kusoma

Urefu wa bahari hupimwaje?

DFC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

"Urefu wa bahari ni kipimo ambacho kinaweza kuchunguzwa kutoka angani," anasema Susanna Buchan, mtaalamu wa masuala ya bahari na profesa katika Chuo Kikuu cha Concepcion nchini Chile.

"Kupitia satelaiti, unaweza kujua joto la bahari na rangi ya bahari. Hayo hutusaidia kujua mambo mbalimbali kuhusu bahari, na athari zake kwa viumbe hai," anafafanua.

Kifaa cha kupimia mawimbi hutumiwa kupima usawa wa bahari. Wnasayansi hutumia vipimo vya satelaiti ili kuamua pembe kamili ya bahari na sakafu ya bahari.

Satalaiti hupima usawa wa bahari kwa usahihi. Taarifa zinazokusanywa kwa miaka mingi husaidia kuelewa kina cha uso wa bahari. Na ndivyo tofauti za mwinuko ndani ya bahari kwa kiwango cha kimataifa hujuulikana.

Shughuli fulani baharini zinaweza kusababisha tofauti ya mwinuko. Na baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha mabadiliko ya usawa wa bahari kwa muda mfupi, ni mawimbi au volkeno chini ya bahari.

Yapo mambo mengine yanayosababisha tofauti ya usawa kati ya bahari moja na nyingine kwa muda mrefu:

Uzito

FG

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Maji yenye joto yanapoteza uwezo wake wa kushikilia oksijeni na wanasayansi wanasema kuwa kati ya 1960 na 2010, okyjini imepungua kwa 2%.

Mfano mzuri ambao wataalamu wanaelezea kuhusu uzito, ni kama tofauti kati ya maji na mafuta. Ikiwa mafuta na maji yatawekwa kwenye glasi – mafuta ambayo ni mepesi yataonekana yakiwa juu.

Uzito wa maji husababisha tofauti katika usawa wa maji, na hilo hutokana na chumvi: Bahari ya Atlantiki ina chumvi zaidi kuliko Pasifiki.

Osvaldo Ulloa, mkurugenzi wa Taasisi ya masuala ya baharini, (Millennium Institute of Oceanography), kutoka Chile na mtaalamu katika Chuo Kikuu cha Concepcion, anasema:

"Watu wengi wanafikiri kwa sababu bahari zinaungana, manake ziko kwenye kiwango sawa. Kwa sababu ya uzito, urefu wa Atlantiki uko chini kidogo, Atlantiki ni nzito kuliko Pasifiki.”

Safu za milima huko Marekani Kusini na Kaskazini huathiri mtiririko wa maji. Chumvi kidogo ya Bahari ya Pasifiki huongeza urefu wa Bahari hiyo.

"Safu za milima ya Andes na safu ya milima ya Rockies hutoa mvua nyingi katika Bahari ya Pasifiki na kupunguza chumvi yake," anasema.

"Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha mvua katika ukanda wa Pasifiki ni nyingi, na chumvi hupungua. Mvua zikiwa nyingi, chumvi itapungua," anasema.

Hali ya Hewa

Sababu nyingine inayochangia tofauti ya urefu kati ya bahari ni hali ya hewa ya maji. Maji ya joto ni mepesi kidogo kuliko maji baridi. Joto na baridi kati ya bahari huunda tofauti katika ya usawa wa bahari moja na nyingine.

Bahari ya Pasifiki ina joto la juu kidogo kuliko Atlantiki na hivyo maji ni mepesi kidogo. Kwa hivyo tunachohitaji kukumbuka ni kwamba uzito mdogo huongeza urefu.

Mazingira ya bahari

MJ

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mito ya chini ya maji, tambarare na mabonde, mifereji ya baharini huathiri mzunguko wa bahari.

Ardhi iliyo chini ya bahari pia ina jukumu katika namna maji yanavyokaa baharini. Ardhi pia inaathiri usawa wa bahari.

Katika sehemu za ndani kabisa za bahari, mifereji ya baharini kama vile Mariana Trench hushuka kwa zaidi ya kilomita 11. Pia sakafu za bahari na safu za milima zinazopatikana baharini huwa ni kama vizuizi katika njia ya mtiririko wa maji.

"Kuna mambo mingi ya asili ndani ya bahari ambayo hubadilisha urefu wa bahari. Mabadiliko haya katika usawa wa bahari husababisha mambo tofauti kutokea," anasema Susanna Buchan.

Kwa hivyo matuta ya chini ya maji, mabonde na mifereji ya bahari huathiri mzunguko wa bahari na huathiri usawa wa bahari.