Wachawi wa Usiku: Kikosi cha marubani wa kike wa Kisovieti walioogopwa na Wanazi

k

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wengi wa waliojitolea katika Kikosi cha 588 walikuwa vijana wa kike waliotaka kupigania nchi yao.

Wengi wao walikuwa bado ni vijana wadogo. Walilazimika kukabiliana na sio tu ukatili wa vita, lakini pia mawazo ya wanaume ambao walitilia shaka uwezo wa kundi la marubani wa kike na ikiwa wangefanikiwa katika vita.

Lakini marubani hao wa Kikosi cha 588, walifanikiwa kuangusha tani 23,000 za mabomu kwenye maeneo ya Wajerumani.

Wakawa sehemu muhimu katika ushindi wa Umoja wa Kisovieti dhidi ya jeshi la Wanazi katika Vita vya Pili vya Dunia.

“Mwanzoni, wanaume walitucheka,” anasema mwanahisabati na mwanafizikia Mrusi, Irina Rakovólskaya katika mahojiano ya 1993. Irina alikuwa kiongozi wa kikosi hicho.

“Walituona jinsi tulivyokuwa wajuzi wa kurusha ndege. Wanaume wa kikosi cha anga walianza kutuita 'dada' na askari wa miguu wakatuita 'viumbe wa mbinguni.' Lakini Wajerumani walituita 'wachawi wa usiku',” anaelezea Irina Rakovólskaya.

“Sera ya Muungano wa Sovieti wakati huo ilitoa fursa sawa za elimu kwa wanaume na wanawake. Kwa sababu hiyo, wasichana wengi waliweza kwenda katika shule za urubani,” anasema mtaalamu wa masuala ya anga Debbie Land katika mahojiano na BBC.

Land ni mtafiti wa masuala ya urubani kutoka Shuttleworth Collection, jumba la makumbusho ya usafiri wa anga na magari nchini Uingereza.

“Kulikuwa na shirika katika Muungano wa Sovieti lililosaidia vijana wa kiume na wa kike kujifunza kuendesha ndege. Programu hiyo ilikuwa ni bure kabisa,” anasema Land.

Kwa hiyo, "Wajerumani waliposhambulia na kuharibu majeshi ya Urusi, marubani wa kike walikuwa wako tayari."

Pia unaweza kusoma

Jeshi la mashujaa wa kike

K

Chanzo cha picha, WIKIMEDIA COMMONS

Maelezo ya picha, Kamanda Yevdokia Bershánskaia.

Wanawake wengi ambao baadae walikuwa marubani walikuwa wakisoma fizikia, angaza za juu, jiografia, hisabati na kemia katika vyuo vikikuu wakati Ujerumani iliposhambulia Umoja wa Kisovieti Juni 22, 1941.

Wakati huo, serikali mpya ya Sovieti ilihitaji wanaume kupigana vita. Lakini, wanawake pia walitaka kupigana.

Wanawake kadhaa vijana walimwandikia barua Marina Raskova, rubani maarufu wa kike katika Muungano wa Sovieti. Baadaye ndiye akawa na jukumu kubwa katika uundaji wa kikosi cha wanawake.

M

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Marina Raskova alikuwa mwanamke wa kwanza wa Soviet kupata diploma ya urubani wa kitaalamu.

Marina Raskova alikuwa mwanamke wa kwanza katika Umoja wa Kisovieti kupokea diploma ya urubani. Raskova alionekana kama shujaa baada ya kuvunja rekodi ya safari ya ndege ya masafa marefu bila kusimama mnamo 1938.

Katika safari hiyo ya kihistoria, Raskova hakutumika kama rubani bali kama mtaalamu wa safari, katika kikosi kilichojumuisha wanawake wengine wawili.

Safari hiyo ilikuwa hatari sana, na mtaalamu wa safari alilazimika kuruka kwa miamvuli kabla ya ndege kutua kwa dharura.

Raskova alitumia siku 10 peke yake katika msitu baridi wa Siberia bila chakula na maji kidogo tu akiitafuta ndege hiyo.

Ameandika matukio ya maisha yake kwenye kitabu. Shukrani kwa kitabu hicho, Raskova alikua maarufu katika Umoja wa Soviet.

Shukrani kwa umaarufu wa Raskova, wanawake wengi wa Kisovieti waliomba waweze kupigania nchi - sio tu kuteuliwa kama wachapaji au wauguzi.

Hatimaye, Raskova alifika kwa kiongozi wa Umoja wa Kisoeti, Josef Stalin. Alimwomba Stalin ruhusa ya kuunda jeshi lake, linalojumuisha tu marubani wa kike.

Stalin alikubali, na Raskova aliunda vikosi vitatu vya wanawake watupu: Kikosi cha 568, Kikosi cha 587 na Kikosi cha 588, ambacho kilijulikana kama "Wachawi wa Usiku."

Umoja wa Kisovieti ukawa nchi ya kwanza kuruhusu wanawake kupigana. Wakati huo kulikuwa na marubani wengi wa kike, lakini hawakuwa wataalamu au mafundi.

"Kwa hiyo waliwafunza wanawake ili kuweza kumudu stadi hizo," anasema Reina Pennington, mwalimu wa historia katika Chuo Kikuu cha Kijeshi cha Norwich, Marekani.

Operesheni hatari

K

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Ndege iliyotumiwa na marubani wa kike wa Kikosi cha 588 ilikuwa Polikarpov PO-2. Ndege ya zamani iliyotengenezwa kwa mbao na bila ulinzi.

Wanawake katika vikosi hivi walianza kujifunza ndege aina ya Polikarpov Po-2. Ndege hii ya zamani, iliyoundwa 1928, kawaida ilitumiwa kwa mafunzo na kunyunyizia dawa katika kilimo.

Polikarpov Po-2 huufanya mwili kuwa dhaifu na mwepesi. Chumba cha marubani kiko wazi, hivyo marubani hawana ulinzi dhidi ya baridi ya usiku.

"Huwezi kushambulia na ndege hiyo wakati wa mchana kwa sababu ni hatari sana.”

"Ndege haikuwa na silaha au bunduki, na haikuweza kukabiliana na ndege za Ujerumani. Kwa hivyo ndege hizi zinaweza kutumika usiku tu, na zinaweza kubeba mabomu machache," anasema Pennington.

Kwa sababu hawakuwa na zana za kuwasaidia kulenga shabaha kwa uhakika, marubani wa kikosi cha 588 walifanya operesheni hatari. Walipokaribia eneo la kushambulia, walizima injini zao ili waweze kupaa kimya kimya.

Kwa wakati ufaao, waliwasha moto ili kutoa ishara kwa rubani mwenzake ni wapi wanapaswa kurusha bomu. Na moto huo pia ulifichua mahali walipo askari wa Nazi.

Misheni zao zilikuwa ngumu kwa sababu Wanazi walitumia taa kubwa za kung'aa kutatiza shabaha zao, na vile vile silaha za kuzuia ndege.

Kwa kuwa ndege za Polikarpov Po-2 hazikuwa na ulinzi, mara nyingi zilishika moto.

Jukumu la wachawi wa usiku sio tu kutupa mabomu na kusababisha vifo na uharibifu. Jukumu lao lilikuwa pia kuwavuruga wanajeshi wa Ujerumani ambao walikuwa wakifanya mazoezi siku nzima," anaeleza Debbie Land.

"Kwa hiyo kazi yao ilikuwa ni kuwaondolea Wajerumani usingizi, kwa kuwalazimisha kufanya kazi usiku kucha ili kesho yake wawe wamechoka."

Tofauti na wenzao wa kiume, kikosi hakipumziki kuvuta sigara au kunywa chai. Wanapotua tu, wanajaza mabomu na kuruka tena.

Marubani wa kike wakati mwingine wanaweza kuruka hadi mara 15 usiku, wakiwazidi marubani wanaume, kulingana na ripoti.

Kama alama ya heshima kwa huduma yao, Kikosi cha 588 cha Wachawi wa Usiku kilipandishwa cheo na Jeshi la Anga. Kikosi hicho kilijulikana kama 46 Guards Night Bomber Regiment.

Bershánskaia pia alipewa tuzo na wachawi wengine wa usiku pia walipokea tuzo hiyo ya kifahari. Marubani 23 wa kike walipokea tuzo ya "mashujaa wa Umoja wa Kisoveti," tuzo ya juu zaidi ya nchi.