Mambo 5 yanayoelezea mizizi ya kihistoria ya mgogoro wa Haiti

x

Chanzo cha picha, Getty Images

Ikiwa imezama katika umaskini, kutikiswa mara kwa mara na majanga ya asili, kuzama kwa deni lake la kihistoria na ukosefu wa utulivu wa serikali zake, Haiti inaonekana kuishi katika shida ya kudumu.

Mauaji ya Rais Jovenel Moïse mwaka wa 2021 na kuongezeka kwa ghasia na magenge ya wahalifu kumesababisha maelfu ya vifo na kuipeleka nchi ukingoni.

Lakini maovu yake yana mizizi mirefu zaidi, ambayo baadhi yake ni ya tangu kuanza kwa Haiti kama taifa huru, na ambayo imekita mizizi kwa karne nyingi.

Hapa tunakueleza baadhi ya mambo ya kihistoria yanayosaidia kuonyensha hali ambayo nchi inapitia kwa sasa.

1. Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa

Haiti imetikiswa na msukosuko wa kisiasa tangu kuzaliwa kwake kama taifa huru mnamo 1804.

Katika kipindi chote cha zaidi ya karne mbili, Haiti imekuwa na mfuatano wa udikteta na mabadilishano ya kidemokrasia na hata uingiliaji kati wa kigeni.

Mtawala wake wa kwanza, Jean-Jacques Dessalines, aliharamisha utumwa lakini alijipa mamlaka yote kwa kujitangaza kuwa gavana mkuu wa maisha ya nchi hiyo na, miezi michache baadaye, Emperor Jacques I wa Haiti. Aliuawa, hatima ambayo imefuata zaidi ya viongozi wachache wa Haiti.

Urithi wake ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na karne ya 19 ilishuhudia mlolongo wa watawala, wengi wao kwa maisha, ambao walidumu miaka michache tu madarakani, waliopinduliwa na uasi, kuuawa au kufukuzwa.

Marekani iliivamia nchi hiyo mwaka wa 1915, ikiwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa Wajerumani nchini Haiti na kulinda maslahi ya Marekani kwenye kisiwa hicho.

Hawakuiacha hadi 1943, ingawa wakati huo walikuwa wameweza kubadilisha sheria kuruhusu, kwa mfano, ununuzi wa ardhi na wageni, jambo ambalo lilikuwa marufuku hadi wakati huo, na ambalo lilisisitiza ushawishi wa makampuni ya Marekani katika uchumi na siasa ya nchi.

Utawala katili wa François "Papa Doc" Duvalier na mwanawe Jean Claude "Baby Doc" ulitisha nchi na kuhimiza kuundwa kwa magenge ya uhalifu, kama vile "toton macoutes" ya kijeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Utawala katili wa François "Papa Doc" Duvalier na mwanawe Jean Claude "Baby Doc" ulitisha nchi na kuhimiza kuundwa kwa magenge ya uhalifu, kama vile "toton macoutes" ya kijeshi.

Sehemu kubwa ya karne ya 20 iliwekwa alama, na serikali za kikatili za François "Papa Doc" Duvalier na mwanawe, Jean-Claude, aliyeitwa "Baby Doc."

Katika kipindi cha miaka 29 ambayo udikteta wa Duvalier ulidumu, ufisadi ulimaliza hazina ya nchi, na sera za ukandamizaji ziliacha karibu watu 30,000 wakiwa wamekufa au kupotea.

Baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoshindwa mnamo 1958, François Duvalier alijaribu kukwepa vikosi vya jeshi kwa kuunda wanamgambo wa kibinafsi, "tonton macoutes" , iliyolenga kutisha watu, kulinda mtawala na kuwatesa wapinzani wake.

Mwanawe, Jean-Claude, alishikilia mamlaka hadi uasi ulipomlazimisha kukimbilia uhamishoni nchini Ufaransa mnamo 1986.

Baada ya mapinduzi kadhaa, Haiti ilimchagua rais kidemokrasia mwaka 1990 kwa mara ya kwanza, Jean-Bertrand Aristide, kasisi wa zamani, ambaye aliungwa mkono na watu wasiojiweza zaidi. Muda wake ulidumu kwa miezi 7 tu, alipopinduliwa na mapinduzi mengine ya kijeshi na kulazimika kwenda uhamishoni.

Aristide aliweza kurejea Haiti mwaka wa 1994 kutokana na uingiliaji kati wa kijeshi wa Marekani na kuvunja jeshi.

Miaka miwili baadaye, René Preval alishinda uchaguzi na kumrithi Aristide kama rais, lakini Aristide alichaguliwa tena Novemba 2000.

Tangu kuuawa kwa Jovenel Moïse mwaka wa 2021, Haiti haina mtawala aliyechaguliwa kwenye uchaguzi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Tangu kuuawa kwa Jovenel Moïse mwaka wa 2021, Haiti haina mtawala aliyechaguliwa kwenye uchaguzi.

Kufuatia kuendelea kwa migogoro ya kisiasa na kiuchumi, Aristide alilazimika kustaafu mwaka wa 2004 huku upinzani ukizidi kuwa na vurugu.

Kulikuwa na shutuma za udanganyifu katika uchaguzi, vifo vya kiholela, mateso na ukatili. Mwaka huo huo Umoja wa Mataifa ulituma ujumbe wa amani nchini Haiti, ambao ulitumia miaka 13 nchini humo.

Preval alishinda tena mwaka wa 2006 na aliweza kumaliza muhula wake wa miaka 5, lakini tetemeko la ardhi la 2010 ambalo liliharibu sehemu kubwa ya nchi lilizidisha matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Haiti.

Kufuatia serikali ya Michel Martelly, mfanyabiashara Jovenel Moïse alishinda uchaguzi wa 2016. Uongozi wake ulikuwa na maandamano dhidi ya serikali, mara nyingi ya vurugu, na shutuma za ufisadi.

Mnamo Julai 7, 2021, Moïse aliuawa kwa kupigwa risasi na kundi la mamluki wa Colombia nyumbani kwake nje kidogo ya Port-au-Prince, ingawa hadi sasa haijawezekana kubaini ni nani aliyeamuru mauaji hayo.

Kifo chake kiliacha pengo la madaraka ambapo makundi yenye silaha yalichukua udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi.

Waziri mkuu wake wa zamani, Ariel Henry, alichukua madaraka kwa muda mfupi, lakini kuongezeka kwa maandamano kulimlazimu kujiuzulu wiki hii.

2. Ukatili uliokithiri

Haiti ni nchi iliyozama katika ghasia kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za karibu magenge 200 yanayodhibiti maeneo makubwa ya nchi, hasa katika mji mkuu, Port-au-Prince.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, ghasia hizo zimesababisha takriban watu 314,000 kuwa wakimbizi wa ndani.

Tangu yale ya kikatili "tonton macoute" yaliyoanzishwa na "Papa Doc" mwaka wa 1958, magenge ya wahalifu yameongeza tu uwepo wao, hasa wakati ombwe za nguvu zimeundwa.

Aristide alipovunja jeshi, jeshi ambalo wakati huo lilikuwa fisadi sana, Serikali iliachwa bila uwezo wa kupambana na uhalifu uliopangwa.

Wakati huo, walanguzi wa dawa za kulevya wa Haiti walifanya kazi kwa karibu na magendo ya Medellín ya Colombia, kulingana na Nicolas Forsans, mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Mafunzo ya Amerika Kusini na Karibea katika Chuo Kikuu cha Essex.

Tetemeko la ardhi la 2010 liliruhusu wanachama wengi wa genge kutoroka kutoka gerezani, jambo ambalo limechochea magenge, ambayo yametekeleza utekaji nyara, mashambulizi dhidi ya polisi, vyombo vya habari, wanasiasa na ambayo yamegeuza maisha ya kila siku ya Wahaiti wengi kuwa kuzimu.

Magenge hayo sasa yanaelekea kuwa na uhusiano na makundi mawili makuu : G-9 and Family, wakiongozwa na Jimmy Chérizier, anayejulikana kama "Barbecue" na G-Pep, wakiongozwa na Gabriel Jean-Pierre.

G-9 iliyoanzishwa mwaka wa 2020, imehusishwa na Chama cha Haiti cha Tèt Kale (PHTK) cha Moïse na Henry, ambao inadaiwa shirikisho hilo lilitumia kupata kura zao.

Genge hilo linadhibiti shughuli muhimu za kiuchumi kama vile bandari ya mji mkuu, vituo vya mafuta na sehemu za kuingilia na kutoka za Port-au-Prince.

Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, idadi ya vifo kutokana na ghasia za magenge iliongezeka maradufu mwaka jana, na kuzidi mauaji 5,000.

Polisi hawana uwezo wa kukabiliana nao, na maafisa wengi wameondoka kwenye jeshi katika mwaka uliopita, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Hivi sasa nchini Haiti kuna maafisa wa polisi 1.3 kwa kila wakaaji 1,000, wakati kiwango cha kimataifa ni 2.2.

Ghasia pia zimeenea kutoka mijini hadi maeneo ya vijijini, ambayo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ni "sababu nyingine ya hofu kubwa."

3. Madeni na uingiliaji wa kigeni

Haiti ilikuwa taifa la kwanza la Amerika Kusini kuwa huru, jamhuri kongwe zaidi ya watu weusi duniani, na jamhuri ya pili katika Ulimwengu wa Magharibi baada ya Marekani.

Uasi ambao watumwa walianza mnamo 1791 dhidi ya wakoloni wao wa Ufaransa ulifikia kilele mnamo 1804 kwa tangazo la uhuru.

Lakini uhuru ulikuja na ghrama.

Mapambano ya ukombozi kutoka kwa nira ya Ufaransa yaliharibu mashamba na miundombinu mingi ya nchi, na kuiingiza nchi katika matatizo makubwa ya kiuchumi.

Hakuna nchi iliyotaka kuitambua Haiti kidiplomasia hadi Ufaransa, mnamo 1825, ilikubali kufanya hivyo, lakini kwa masharti: walipe fidia kwa mashamba na watumwa waliopotea au wakabiliane na vita.

Kwa njia hii, Haiti ilikubali kulipa fidia ya faranga milioni 150 (kama dola bilioni 21 hivi leo), ambayo ilipaswa kulipa kwa awamu tano.

x

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa kuwa hawakuwa na fedha hizo, kwa kuwa mapato ya kila mwaka ya serikali ya Haiti yalikuwa sehemu ya kumi ya yale ambayo Ufaransa ilidai, Haiti ililazimika kuomba mkopo.

Hivi ndivyo kile kinachojulikana kama deni la Uhuru kilianza rasmi.

Tume za kidhalimu zilizotumiwa na Crédit Industriel et Commercial (leo inajulikana kama CIC) zilibadilisha deni hilo hadi Ufaransa kuwa linalojulikana kama "deni mara mbili."

Haiti ililazimika kuchukua mikopo mikubwa kutoka kwa benki za Marekani, Ufaransa na Ujerumani zenye viwango vya juu vya riba ambavyo viliilazimisha kutumia sehemu kubwa ya bajeti ya taifa kulipa.

Ilikuwa hadi 1947 ambapo Haiti ilimaliza kuwalipa fidia wamiliki wa mashamba ya koloni hiyo ya Ufaransa ambayo ilikuwa lulu ya Antilles.

Lakini Ufaransa haikuwa nchi pekee iliyochukua na kuondoa hazina ya Haiti.

Mnamo 1915, Wanajeshi 330 wa Majini wa Amerika walitua Port-au-Prince kutetea masilahi ya kampuni za Amerika nchini, ambayo iligubikwa na machafuko ya kisiasa.

4. Umaskini

Machafuko haya yote ya kisiasa, ghasia na uporaji vimekuwa na matokeo ya wazi kwa nchi na wakazi wake: Haiti ni nchi maskini zaidi katika Amerika ya Kusini na Karibiani, na mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.

Pato la Taifa kwa kila mtu (katika usawa wa uwezo wa kununua) lilikuwa Dola za Marekani 3,306 pekee mwaka 2022, kulingana na Benki ya Dunia (wakati wastani wa Amerika ya Kusini na Karibiani ulikuwa Dola za Marekani 19,269), takwimu ambayo haizingatii usawa wa mapato ya nchi ya wakazi wake.

Pia inachukuwa nafasi ya 163 kati ya 191 katika Fahirisi ya Maendeleo ya Binadamu iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya nusu ya watu wanaishi chini ya mstari wa umaskini na umri wa kuishi hauzidi miaka 64, hasa kutokana na hali mbaya ya maisha katika sehemu kubwa ya nchi na udhaifu wa mfumo wake wa afya.

Njaa na utapiamlo vimefikia viwango ambavyo havijawahi kushuhudiwa nchini humo na athari zinazoweza kuua, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Mnamo 2023, watoto milioni 3, idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa, walihitaji msaada wa kibinadamu nchini Haiti, ambapo karibu mtoto mmoja kati ya wanne ana utapiamlo sugu.

Hali ni mbaya hasa katika vitongoji vilivyotikiswa na ghasia kama vile Cité Soleil, huko Port-au-Prince, ambayo ina rekodi ya kusikitisha: kwa miaka mingi imekuwa kitongoji maskini zaidi katika mji mkuu maskini zaidi wa nchi maskini zaidi ya Amerika.

Hali mbaya ya usafi ambayo sehemu kubwa ya watu wanaishi inamaanisha kuwa magonjwa fulani ya kuambukiza husababisha uharibifu.

Haiti, kwa mfano, ina moja ya viwango vya juu zaidi vya ugonjwa wa kifua kikuu katika eneo hilo, na kipindupindu, ambacho baada ya tetemeko kubwa la ardhi la 2010 kilisababisha vifo vya karibu 10,000, kimeibuka tena katika sehemu fulani za nchi. Zaidi ya hayo, asilimia 1.7 ya watu wazima wanaishi na VVU/UKIMWI, kulingana na takwimu za UNAIDS.

Hii ni pamoja na ukweli kwamba karibu asilimia 40 ya watu hawajui kusoma na kuandika, kulingana na takwimu za Benki ya Dunia, na nusu tu ya watoto wanaenda shule, kulingana na takwimu zinazosimamiwa na Unicef.

PICHA

5. Majanga ya asili

Haiti iko katika hatari kubwa ya majanga ya asili kutokana na jiografia yake yenyewe. Nchi hiyo iko kwenye njia ya vimbunga vya Atlantiki, na iko kwenye maeneo mawili ambayo yanaifanya kuwa eneo la tetemeko la juu.

Hata hivyo, baadhi ya matokeo mabaya zaidi ya majanga haya ya asili yamezidishwa na binadamu.

Umaskini na kukaribia kutoweka kwa taifa kumesababisha ukataji miti na uharibifu wa mazingira, ambayo huongeza athari za vimbunga, wakati ugumu wa ujenzi hufanya idadi ya wahasiriwa na uharibifu kutoka kwa tetemeko la ardhi kuwa kubwa zaidi.

Asilimia 96 ya wakaazi karibu milioni 12 wa Haiti wanakabiliwa na maafa ya aina hii.

Haiti iko katika mwisho wa magharibi wa kisiwa cha Hispaniola, ambayo inakaribia na Jamhuri ya Dominika. Mandhari yake ni magumu, yenye mabonde, na idadi kubwa ya watu wamejikusanya pwani.

z

Chanzo cha picha, Getty Images

Benki ya Dunia inakadiria kuwa asilimia 98 ya misitu yake imekatwa, hasa kwa ajili ya kutengeneza kuni na mkaa, ambayo imesababisha mmomonyoko wa udongo na uhaba mkubwa wa maji ya kunywa.

Mmomonyoko huu hauathiri kilimo tu, bali unaifanya Haiti kuwa katika hatari zaidi ya vimbunga na dhoruba za kitropiki ambazo mara kwa mara huikumba nchi, na kusababisha mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi. Mwaka wa 2016, kwa mfano, Kimbunga Matthew kilisababisha uharibifu wa thamani ya asilimia 32 ya Pato la Taifa (GDP).

Haiti pia iko katikati ya mfumo mkubwa wa hitilafu za kijiolojia zinazotokana na kusogea kwa bamba la Karibea na bamba kubwa la Amerika Kaskazini.

Hitilafu ya Bustani ya Enriquillo-Plantain inapita kusini mwa nchi, huku ile ya Kaskazini Magharibi ikipitia kaskazini.

Hii imesababisha baadhi ya matetemeko makubwa zaidi katika siku za hivi karibuni, kama vile ukubwa wa 7 moja ambayo ilitikisa nchi mwaka 2010, ambayo iliua watu 250,000 na ambayo, kulingana na Benki ya Dunia, iliharibu asilimia 120 ya Pato la Taifa la Haiti.

Wakati katika nchi zingine za ulimwengu kama Chile au Japani, matetemeko ya ardhi yenye ukubwa sawa au makubwa zaidi hutokea bila kutoa idadi sawa ya wahasiriwa, miundo rahisi ya saruji ya miji ya Haiti, bila mto wowote, ilianguka kama nyumba ya kadi. .

Mnamo 2021, majanga ya asili yalitaokea mara mbili: baada ya tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.2 ambalo liliua karibu watu 2,000 na kuharibu asilimia 30 ya peninsula ya kusini mwa nchi, Tropical Storm Grace ilizidisha hali hiyo siku chache baadaye, na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Matokeo ya mzozo wa hali ya hewa, wataalam wanaonya, yatazidisha hali ya nchi iliyokumbwa na maovu mengi.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi