Euro 2024 : Timu zinahitaji nini kufuzu hatua ya 16 bora?

Uingereza inaongoza Kundi C ikiwa na alama nne na itafuzu iwapo itaepuka kushindwa dhidi ya Slovenia siku ya Jumanne

Chanzo cha picha, Getty Images

Kila upande sasa umecheza angalau mara mbili kwenye michuano ya Euro 2024 na mataifa manne yamejihakikishia nafasi zao za kufuzu.

Hiyo ina maana kwamba nafasi 12 kati ya 16 bado zinaendelea kunyakuliwa.

Timu mbili za juu katika makundi yote sita hufuzu moja kwa moja, zikiunganishwa na timu nne bora zilizo katika nafasi ya tatu.

Ratiba ya mwisho inapoendelea, BBC Sport inakuambia ni nani anahitaji nini ili kutinga hatua ya 16 bora.

Unaweza pia kusoma

Kundi A Ujerumani na Uswizi Zimefunzu

.

Chanzo cha picha, BBCSport

Scotland wametoka katika michuano ya Euro 2024 baada ya kumaliza mkiani mwa Kundi A kufuatia kushindwa kwa dakika za mwisho na Hungary katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi.

Ujerumani wameongoza kundi hilo, huku Uswizi wakifuzu kwa mtoano katika nafasi ya pili.

Hungary bado inaweza kufika hatua ya 16 bora kama moja ya timu nne bora zilizo katika nafasi ya tatu, lakini itahitaji kusubiri hadi michezo iliyosalia ya hatua ya makundi kukamilika ili hatima yao ithibitishwe.

Uhispania yafuzu raundi ya timu 16 bora

.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Uhispania wametinga hatua ya 16 bora wakiwa washindi wa makundi.

Itali itafuzu kwa mtoano kama washindi wa pili ikiwa wataepuka kushindwa dhidi ya Croatia. Mabingwa hao watetezi wataondolewa iwapo watapoteza na Albania kuifunga Uhispania.

Albania inaweza kushika nafasi ya pili ikiwa itaishinda Uhispania na Croatia kuifunga Italia. Ingawa, ikiwa tofauti ya ushindi wa Croatia ni mabao mawili zaidi ya Albania, wataruka juu ya wapinzani wao wa Kundi B.

Croatia pia itamaliza nafasi ya pili ikiwa itaifunga Itali na Albania isiifunge Uhispania.

Kundi C - England ina kazi ya ziada

.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, England ina kibarua cha ziara kufuzu

England inahitaji kuepuka kushindwa dhidi ya Slovenia katika mchezo wao wa mwisho Jumanne ili kujihakikishia kusonga mbele katika Kundi C.

Ushindi utawahakikishia vijana wa Gareth Southgate kusonga mbele kama washindi wa kundi.

Ikiwa Denmark itashindwa kuifunga Serbia, basi Uingereza itafuzu bila kujali matokeo yao dhidi ya Slovenia.

Denmark na Slovenia zitafuzu moja kwa moja zikipata ushindi. Serbia itamaliza katika nafasi mbili za juu ikiwa itaifunga Denmark na Slovenia isiifunge Uingereza.

Kundi D - Hali ni tete

.

Chanzo cha picha, BBC Sport

Maelezo ya picha, Hali ni tete katika kundi hili

Timu tatu za juu katika Kundi D zimetenganishwa kwa pointi moja pekee na kila moja inaweza kumaliza hatua ya makundi katika nafasi ya kwanza, ya pili au ya tatu.

Uholanzi itamaliza katika nafasi mbili za juu na kutinga hatua ya mtoano ikiwa itaepuka kushindwa na Austria.

Ufaransa watajihakikishia kutinga hatua ya 16 bora iwapo hawatapoteza dhidi ya Poland.

Austria itamaliza katika nafasi mbili za juu ikiwa itaifunga Uholanzi.

Poland imekuwa timu ya kwanza kuondolewa katika michuano hiyo kufuatia sare ya Ufaransa na Uholanzi siku ya Ijumaa.

Kundi E - Kila mtu ana pointi tatu

.

Chanzo cha picha, BBCSPORT

Kundi E liko katika hali isiyo ya kawaida ya kila mtu kuwa na pointi tatu baada ya michezo miwili.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Euro timu zote nne kuwa na pointi sawa baada ya michezo miwili.

Timu zote nne zinajua ushindi siku ya Jumatano utawapeleka katika hatua ya 16 bora - lakini hakuna timu ambayo itakuwa na uhakika wa kutinga kileleni kwa ushindi.

Pointi itatosha kwa Ubelgiji - ambao wanacheza na Ukraine - na Romania - ambao wanakabiliana na Slovakia.

Iwapo michezo yote miwili itatoka sare basi tofauti ya mabao itahitajika ili kuamua nani atamalizia wapi (kwa sababu kila timu itakuwa na pointi sawa za ana kwa ana.

Ubelgiji na Romania zingepitia katika hali hiyo, huku Slovakia ikitarajia kupita kama moja ya timu bora zilizoshika nafasi ya tatu. Hilo likifanyika Ukraine itakuwa nje.

Kundi F - Ureno yafuzu kama washindi wa kundi

.

Chanzo cha picha, BBCSPORT

Maelezo ya picha, Ureno tayari imefuzi nafasi ya 16 bora kama washindi wa kundi hilo

Ureno wametinga hatua ya 16 bora wakiwa washindi wa makundi.

Uturuki itafuzu kwa mtoano ikiwa itaepuka kushindwa dhidi ya Jamhuri ya Czech, bila kujali matokeo ya Georgia dhidi ya Ureno.

Wacheki lazima waifunge Uturuki na kutumaini Georgia itashindwa kushinda dhidi ya Ureno. Wakifanya hivyo itaamuliwa kwa tofauti ya mabao.

Washiriki wa michuano ya Euro kwa mara ya kwanza Georgia wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuifunga Ureno basi lazima wawe na matumaini kuwa Jamhuri ya Czech itaifunga Uturuki ikiwa wanataka kusonga mbele. Katika mfano huo, itaamuliwa kwa tofauti ya mabao yao ikilinganishwa na Wacheki.

Vipi kuhusu timu zinazoshika nafasi ya tatu?

.

Chanzo cha picha, BBCSPORT

Timu nne bora zilizo katika nafasi ya tatu zitaingia hatua ya 16 bora, huku zile mbili za chini zikitoka.

Katika Euro 2016 na 2020, kila timu iliyomaliza kwa pointi nne au tatu kwa tofauti ya mabao ambayo haikuwa mbaya ilifuzu

Je, timu mbili zinazomaliza sawa kwa pointi zinagawanywa vipi?

  • Matokeo ya ana kwa ana kati ya timu moja au nyingi
  • Tofauti ya mabao ya ana kwa ana
  • Mabao ya ana kwa ana yaliyofungwa
  • Tofauti ya jumla ya magoli yaliofungwa l
  • Jumla ya mabao yaliofungwa
  • Jumla ya pointi za chini za kinidhamu mfano (kadi nyekundu = pointi 3, kadi ya njano = pointi 1, kadi mbili za njano katika mechi moja = pointi 3)
  • Orodha ya kufuzu
Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah