'Watu wengi hufikiri najitesa-lakini natimiza ndoto yangu'

TH

Chanzo cha picha, Nelly Makena

Na Yusuf Jumah

BBC Swahili , Nairobi

Kujiamini ni kama ‘vazi’ ambalo Nelly Makena amelivalia kwa muda sasa na ni ‘vazi’ ambalo limempa nguvu ya kupata mafanikio makubwa akiwa na umri mdogo . Amejikita katika ujasiriamali wa kutengeza na kupamba keki.

Makena ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 22 na alianzisha kampuni yake ya kutengeza keki akiwa na umri wa miaka 18 tu.

Simulizi yake inavutia kwa sababu inasheheni uchu mkubwa wa msichana anayetumia elimu na ujuzi anaopata kujiendeleza bila kujali dhana ambazo wakati mwingi huwafifisha vijana wa umri mdogo kufanya makubwa .

Makena anayesomea Shahada katika Usimamizi wa Masuala ya Hoteli katika chuo kikuu cha Kiufundi cha Kenya (TUK) anasema mvuto wake wa kutengeza keki ulianza akiwa mdogo wakati wazazi wake ambao ni walimu walipomsaidia pia kukuuza maarifa yake katika hilo.

Alikulia katika mazingira yaliyodhamini sana nidhamu na hilo anasema lilichangia msukumo wake wa kutaka kufanikiwa .

Bahati yake pia ilipigwa jeki na sifa yake ya kuwa mbunifu na kila alichofunzwa pale nyumbani ,alikiboresha kwa ubunifu wake na ndio maana haikuwa kazi ngumu Makena kujua kutengeneza keki na kuzipamba kwa njia iliyowavutia wengi .

Mwanzo wa safari ya kuwa mjasiriamali

th

Chanzo cha picha, Nelly Makena

Maelezo ya picha, Makena anasema alikulia katika mazingira yaliyodhamini sana nidhamu na hilo anasema lilichangia msukumo wake wa kutaka kufanikiwa .
Unaweza pia kusoma

Alipojiunga na Chuo Kikuu cha TUK alikutana na mwalimu wake aliyegundua ujuzi na mapenzi ya Makena kwa utengenezaji wa keki naupambaji.Haichukua zaidi ya miezi mitatu akiwa chuoni kwa Makena kuanza kuzitengeza keki na kuziuza.

Mapokezi mazuri ya bidhaa zake sokoni na mapato mazuri yalimpa moyo na muda si mrefu alianzisha kampuni yake ya Triple C Treats mwaka wa 2020.

Hadi sasa Makena amewaajiri vijana wenzake watano na kando na masomo yake chuoni ,anasimamia biashara yake hii ambayo imemfanya kuwatengezea watu wengi keki za hafla zao kubwa kubwa kama vile harusi na maadhimisho ya kuzaliwa .

Kuhusu jinsi alivyopata mtaji wa kuanzisha biashara yake Makena anasema kuanzisha biashara yake sio jambo lililompa kibarua kuhusu mtaji kwani alianza na kiasi kidogo cha hela zake na mtaji huo umezidi kadri anavyoendelea kutanua shughuli zake na pia imani ambayo ameijenga kwa wateja wake .

‘Nilianza kwa hatua ndogo sana na muda unaposonga ,ukubwa wa ninachofanya umezidi’.

Makena anasema kauli anayitegemea katika kuboresha biashara yake ni ile ‘kuanza safari ndefu kwa hatua moja’ na hiyo ni falsafa ambayo vijana wengi wa rika lake wanaonekana kuipuuzilia mbali.

‘Vijana wa rika langu wanataka vitu vya haraka,pesa za haraka bila kutoa jasho-huo ni mkondo ambao mimi kamwe sikutaka kuufuata’ anasema Makena.

Nidhamu na kuboresha ujuzi wangu

TH

Chanzo cha picha, Nelly Makena

Mafanikio ya Makena hayajatokana na uwezekano wa mtu kugonja sadfa kukutana na bahati,ila yamekuwa matokeo ya nidhamu iliyokuzwa na wazazi wake na kulelewa na sifa zake mwenyewe.

Anasema mara nyingi wanafunzi wa vyuo vikuu na hasa wa kike hujipata katika mitihani ya kimaisha ambayo inawavutia kutafuta njia za mkato kufaulu katika maisha.

Makena anasema njia kama hizo kwa mfano za kutumia ujana wake au mwili wake kufanya maovu ili kujipa pesa sio mtindo wa maisha ambao amewahi kufikiria na ndio maana kwake yeye ,mkondo wake wa kujipa ujuzi na kuuboresha ili kuutumia kuanzisha kampuni na biashara yake ndio njia yake ya kuwa kielelezo kwa vijana wa rika lake .

‘Wakati mwingi watu wananishangaa,na umri wangu mdogo pamoja na urembo wangu,kwa nini najitesa na kazi hii wakati ambapo ningekuwa kilabuni nikifanya starehe’ anasema huku akitabasamu .

TH

Chanzo cha picha, NELLY MAKENA

Maelezo ya picha, ‘Ikiwa una ndoto ya kufanya lolote, usisite kuifuata! Chukua hatua za kuboresha ujuzi wako'

Hilo ni swali ambalo hata wenzake chuoni wanaishi wakiimuuliza ,iwapo anahisi kuna sehemu ya ujana wake inampita akiendelea na ‘kazi za utu ukubwa’.Makena hajali kuhusu hofu hizo kwani anasema msingi aliotayarisha sasa utampa kila fursa ya kuishi maisha yake ya baadaye bila majuto .

Changamoto nyingine kwake imekuwa kucheza ngoma mbili kwa wakati mmoja.Ni kazi kubwa kuwa mwanafunzi na mjasiriamali kwa wakati mmoja kwa sababu anajipata wakati mwingine akihitajika kote .

Imemlazimu kuboresha uwezo wa wfanyakazi wake kushughulikia biashara yake wakati anapojipata na majukumu ya darasani na hilo limempa afueni kwani baada ya muda ,mambo yote mawili yanakwenda vizuri bila kumpa matatizo .

Pia anaongeza kuwa kwa sababu ya umri wake mdogo mara ya kwanza baadhi ya wateja wake walikuwa na shaka iwapo angeweza kutekeleza kazi walizompa lakini kujiamini ,ujuzi wake ,uwezo wake wa kuwasiliana na kujifunza mengi yamemfanya kuwaridhisha na kuondoa hofu zao kabisa kuhusu uwezo wake .

‘Zawadi yangu kwenu’

TH

Chanzo cha picha, Nelly Makena

Maelezo ya picha, Mafanikio ya Makena hayajatokana na uwezekano wa mtu kugonja sadfa kukutana na bahati,ila yamekuwa matokeo ya nidhamu iliyokuzwa na wazazi wake na kulelewa na sifa zake mwenyewe.

‘Ikiwa una ndoto ya kufanya lolote, usisite kuifuata! Chukua hatua za kuboresha ujuzi wako, jifunze kutoka kwa walio bora zaidi kwenye uwanja na ulitambulishe jina lako. Usikatishwe tamaa na vikwazo - kila safari huanza na hatua moja. Kama mtu aliyejenga biashara yenye mafanikio kutokana na ndoto yangu ya kutengeneza keki, ninaamini mtu yeyote anaweza kutimiza ndoto zake kwa bidii na uvumilivu’.